Petro Analiambia Baraza la Wayahudi Kwamba Kristo Ndiye Masiya

Baraza la Wayahudi linakutana tena. Mbele yao Petro anatangaza kwamba Kristo ndiye Masiya.

32 BK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Matendo 5:22–33

22 Lakini wale walinzi wa Hekalu walipokwenda gerezani hawakuwakuta mitume mle. Kwa hiyo wakarudi na kutoa habari. 23 Wakasema, “Tumekuta milango ya gereza imefungwa sawasawa na askari wa gereza wamesimama nje ya mlango, lakini tulipofungua milango hakuwepo mtu yeyote ndani.” 24 Basi mkuu wa walinzi wa Hekalu na viongozi wa makuhani waliposikia haya, wakafadhaika na kushangaa sana kwa ajili yao kwamba jambo hili litakuwaje.

25 Ndipo mtu mmoja akaja akawaambia, “Tazameni watu mliowatia gerezani wako Hekaluni wakiwafundisha watu.” 26 Ndipo yule mkuu wa walinzi wa Hekalu wakaenda pamoja na askari wakawaleta wale mitume, lakini bila ghasia kwa sababu waliogopa kupigwa mawe na watu.

27 Wakiisha kuwaleta mitume wakawaamuru kusimama mbele ya baraza ili kuhani mkuu awahoji. 28 “Tuliwaonya kwa nguvu msifundishe kwa jina hili, lakini ninyi mmeijaza Yerusalemu yote mafundisho yenu na tena mmekusudia kuleta damu ya mtu huyu juu yetu.”

29 Petro na wale mitume wengine wakajibu, “Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu. 30 Mungu wa baba zetu alimfufua Yesu kutoka kwa wafu, ambaye ninyi mlimuua kwa kumtundika kwenye msalaba. 31 Mungu alimtukuza, akamweka mkono wake wa kuume kuwa Kiongozi na Mwokozi ili awape Israeli toba na msamaha wa dhambi. 32 Nasi tu mashahidi wa mambo haya, vivyo hivyo na Roho Mtakatifu ambaye Mungu amewapa wale wanaomtii.”

33 Wale wajumbe wa baraza la wazee waliposikia haya, walijawa na ghadhabu, wakataka kuwaua mitume.

Ushauri wa Gamalieli Unawafanya Mitume Waachiliwe Huru

Matendo 5:34–42

34 Lakini Farisayo mmoja, jina lake Gamalieli, aliyekuwa mwalimu wa sheria, aliyeheshimiwa na watu wote, akasimama mbele ya baraza akaamuru mitume watolewe nje kwa muda. 35 Ndipo alipowaambia wajumbe wa baraza, “Enyi watu wa Israeli, fikirini kwa uangalifu mnayotaka kuwatendea watu hawa. 36 Kwa maana wakati uliopita, aliinuka mtu mmoja jina lake Theuda, alijidai kuwa yeye ni mtu maarufu, akapata wafuasi wapatao 400 walioambatana naye. Lakini aliuawa, na wafuasi wake wote wakatawanyika, wakawa si kitu. 37 Baada yake, alitokea Yuda Mgalilaya wakati wa kuorodhesha watu, naye akaongoza kundi la watu kuasi. Yeye pia aliuawa, nao wafuasi wake wakatawanyika. 38 Kwa hiyo, kwa habari ya jambo hili nawashauri, jiepusheni na watu hawa. Waacheni waende zao! Kwa maana kama kusudi lao na shughuli yao imetokana na mwanadamu, haitafanikiwa. 39 Lakini ikiwa imetoka kwa Mungu, hamtaweza kuwazuia watu hawa. Badala yake mtajikuta mnapigana na Mungu.”

40 Wakapokea ushauri wa Gamalieli. Wakawaita mitume ndani, wakaamuru wachapwe mijeledi, kisha wakawaagiza wasinene tena kwa jina la Yesu, wakawaachia waende zao.

41 Nao mitume wakatoka nje ya baraza, wakiwa wamejaa furaha kwa sababu wamehesabiwa kustahili kupata aibu kwa ajili ya jina la Yesu. 42 Kila siku, Hekaluni na nyumba kwa nyumba, hawakuacha kufundisha na kuhubiri habari njema kwamba Yesu ndiye Kristo.

Kuteuliwa kwa Mashemasi Saba

Matendo 6:1–6

1 Basi ikawa katika siku hizo, wakati idadi ya wanafunzi ilipokuwa ikiongezeka sana, palitokea manungʼuniko kati ya Wayahudi wa Kiyunani, dhidi ya Waebrania kwa sababu wajane wao walisahaulika katika mgawanyo wa chakula wa kila siku. 2 Wale mitume kumi na wawili wakakusanya wanafunzi wote pamoja wakasema, “Haitakuwa vyema sisi kuacha huduma ya neno la Mungu ili kuhudumu mezani. 3 Kwa hiyo ndugu, chagueni watu saba miongoni mwenu, watu wenye sifa njema, waliojawa na Roho Mtakatifu na hekima, ambao tunaweza kuwakabidhi kazi hii, 4 nasi tutatumia muda wetu kuomba na huduma ya neno.”

5 Yale waliyosema yakawapendeza watu wote, nao wakamchagua Stefano (mtu aliyejawa na imani na Roho Mtakatifu) pamoja na Filipo, Prokoro, Nikanori, Timoni, Parmena na Nikolao, mwongofu kutoka Antiokia. 6 Wakawaleta watu hawa mbele ya mitume, nao wakawaombea na kuwawekea mikono juu yao.

Kanisa Linaendelea Kuongezeka kwa Idadi 33 BK

Matendo 6:7

7 Neno la Mungu likazidi kuenea. Idadi ya wanafunzi ikazidi kuongezeka sana katika Yerusalemu hata makuhani wengi wakaitii ile imani.

Stefano Anashtakiwa kwa Kukufuru 33 au 34 BK

Stefano, baada ya kutangaza kwa ujasiri kwamba Kristo ndiye Masiya, anashtakiwa kwa kukufuru mbele ya Baraza la Wayahudi.

Matendo 6:8–14

8 Stefano, akiwa amejaa neema na nguvu za Mungu, alifanya ishara na miujiza mikubwa miongoni mwa watu. 9 Hata hivyo, ukainuka upinzani wa watu wa Sinagogi la Watu Huru (kama lilivyokuwa linaitwa), la Wayahudi wa Kirene na wa Iskanderia, na wengine kutoka Kilikia na Asia. Watu hawa wakaanza kupingana na Stefano. 10 Lakini hawakuweza kushindana na hekima yake wala huyo Roho ambaye alisema kwake.

11 Ndipo kwa siri wakawashawishi watu fulani waseme, “Tumemsikia Stefano akisema maneno ya kufuru dhidi ya Mose na dhidi ya Mungu.”

12 Wakawachochea watu, wazee na walimu wa Sheria, nao wakamkamata Stefano wakamfikisha mbele ya baraza. 13 Wakaweka mashahidi wa uongo ambao walishuhudia wakisema, “Mtu huyu kamwe haachi kusema dhidi ya mahali hapa patakatifu na dhidi ya Sheria. 14 Kwa maana tumemsikia akisema kwamba Yesu wa Nazareti atapaharibu mahali patakatifu na kubadili desturi zote tulizopewa na Mose.”