Kifo cha Sauli (continued)
1055 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Wafilisti wakakusanya majeshi yao yote huko Afeki, nao Waisraeli wakapiga kambi karibu na chemchemi iliyoko Yezreeli. 2 Watawala wa Wafilisti walipokuwa wakipita pamoja na vikosi vyao vya mamia na vya maelfu, Daudi na watu wake walikuwa wakitembea huko nyuma pamoja na Akishi. 3 Majemadari wa Wafilisti wakauliza, “Vipi kuhusu hawa Waebrania?”
Akishi akajibu, “Huyu si Daudi, aliyekuwa afisa wa Sauli mfalme wa Israeli? Ameshakuwa pamoja nami kwa zaidi ya mwaka, naye tangu alipomwacha Sauli hadi sasa, sikuona kosa lolote kwake.”
4 Lakini majemadari wa Wafilisti wakamkasirikia na kusema, “Mrudishe mtu huyu, apate kurudi mahali pale ulipompangia. Haimpasi kufuatana pamoja nasi vitani, asije akageuka, akawa kinyume chetu vitani. Ni kwa njia ipi bora zaidi angeweza kujipatia tena kibali kwa bwana wake, isipokuwa kwa vichwa vya watu wetu wenyewe? 5 Je, huyu si ndiye Daudi walioimba kumhusu katika ngoma zao, wakisema:
“ ‘Sauli amewaua elfu zake,
naye Daudi makumi elfu yake’?”
6 Basi Akishi akamwita Daudi na kumwambia, “Kama vile Bwana aishivyo, wewe umekuwa mtu mwaminifu, nami ningependa utumike pamoja nami katika jeshi. Tangu siku ile uliyofika kwangu hadi sasa, sijaona kosa lolote kwako, lakini hao watawala hawakukubali. 7 Rudi na uende kwa amani; usifanye chochote cha kuwakasirisha watawala wa Kifilisti.”
8 Daudi akamuuliza Akishi, “Lakini mimi nimefanya nini? Je, umeona nini kibaya juu ya mtumishi wako tangu siku ile niliyokuja kwako hadi leo? Kwa nini nisirudi na kupigana na adui za bwana wangu mfalme?”
9 Akishi akamjibu Daudi, “Mimi ninajua ya kuwa wewe umekuwa wa kupendeza machoni pangu kama vile malaika wa Mungu. Lakini hao majemadari wa Wafilisti wamesema, ‘Huyu haimpasi kwenda vitani pamoja nasi.’ 10 Sasa amka mapema, pamoja na watumishi wa bwana wako waliofuatana nawe, nanyi ondokeni asubuhi mara kutakapopambazuka.”
11 Hivyo Daudi na watu wake wakaamka asubuhi na mapema, wakaenda zao kurudi katika nchi ya Wafilisti, nao Wafilisti wakapanda kwenda Yezreeli.
19 Baadhi ya watu kutoka kabila la Manase wakajiunga na Daudi wakati alikwenda pamoja na Wafilisti, kupigana na Sauli. (Daudi na watu wake hawakuwasaidia Wafilisti kwa sababu, baada ya ushauri, watawala wao walimrudisha. Wakasema, “Itatugharimu vichwa vyetu kama Daudi atatuasi na kurudi kwa Sauli bwana wake.”) 20 Daudi alipokwenda Siklagi, hawa ndio watu wa kabila la Manase waliojiunga naye: Adna, Yozabadi, Yediaeli, Mikaeli, Yozabadi, Elihu na Silethai, viongozi wa vikosi vya watu 1,000 katika kabila la Manase. 21 Walimsaidia Daudi dhidi ya makundi ya uvamizi, kwa kuwa wote walikuwa mashujaa hodari na walikuwa majemadari katika jeshi lake. 22 Siku baada ya siku watu walikuja kumsaidia Daudi, mpaka akawa na jeshi kubwa, kama jeshi la Mungu.
1 Daudi na watu wake wakafika Siklagi siku ya tatu. Basi Waamaleki walikuwa wamevamia Negebu na Siklagi. Wakawa wameshambulia mji wa Siklagi na kuuteketeza kwa moto, 2 nao wakawa wamewachukua mateka wanawake pamoja na wote waliokuwamo humo, vijana na wazee. Hawakuua yeyote, bali waliwachukua wakaenda zao.
3 Daudi na watu wake walipofika Siklagi, wakakuta mji umeangamizwa kwa moto na wake zao pamoja na wana wao na binti zao wamechukuliwa mateka. 4 Hivyo Daudi na watu wake wakapiga yowe mpaka wakaishiwa na nguvu za kulia. 5 Wake wawili wa Daudi walikuwa wametekwa: yaani Ahinoamu wa Yezreeli, na Abigaili, mjane wa Nabali wa Karmeli. 6 Daudi alihuzunika sana kwa sababu watu walikuwa wakisemezana juu ya kumpiga kwa mawe. Kila mmoja alikuwa na uchungu rohoni kwa sababu ya wanawe na binti zake. Lakini Daudi akajitia nguvu katika Bwana, Mungu wake.
7 Kisha Daudi akamwambia kuhani Abiathari mwana wa Ahimeleki, “Niletee kisibau.” Abiathari akamletea, 8 naye Daudi akamuuliza Bwana, “Je, nifuatie kundi hili la wavamizi? Je, nitawapata?”
Bwana akajibu, “Wafuatie. Hakika utawapata na utafanikiwa kuwaokoa.”
9 Daudi pamoja na watu wake 600 wakafika kwenye Bonde la Besori, mahali ambapo wengine waliachwa nyuma, 10 kwa kuwa watu 200 walikuwa wamechoka sana kuweza kuvuka hilo bonde. Lakini Daudi pamoja na watu 400 wakaendelea kufuatia.
11 Wakamkuta Mmisri katika shamba fulani, nao wakamleta kwa Daudi. Wakampa huyo Mmisri maji ya kunywa na chakula; 12 kipande cha andazi la tini na andazi la zabibu zilizokaushwa. Akala naye akapata nguvu, kwa kuwa hakuwa amekula chakula chochote wala kunywa maji kwa siku tatu usiku na mchana.
13 Daudi akamuuliza, “Wewe ni wa nani, na umetoka wapi?”
Akajibu, “Mimi ni Mmisri, mtumwa wa Mwamaleki. Bwana wangu alinitelekeza nilipougua siku tatu zilizopita. 14 Tulivamia Negebu ya Wakerethi, na nchi ya Yuda, na Negebu ya Kalebu. Nasi tulichoma moto Siklagi.”
15 Daudi akamuuliza, “Je, unaweza kuniongoza kufikia kundi hili la uvamizi?”
Akajibu, “Niapie mbele ya Mungu kwamba hutaniua wala kunikabidhi mikononi mwa bwana wangu, nami nitakupeleka hadi waliko.”
16 Akamwongoza Daudi mpaka mahali walipokuwa, nao walikuwa wametawanyika eneo lote, wakila, wakinywa na wakifanya karamu kwa sababu ya nyara nyingi walizochukua kutoka nchi ya Wafilisti na kutoka Yuda. 17 Daudi akapigana nao kuanzia machweo ya jua hadi kesho yake jioni, na hakuna yeyote miongoni mwao aliyetoroka, isipokuwa vijana wanaume 400 waliopanda ngamia na kutoroka. 18 Daudi akarudisha kila kitu Waamaleki walikuwa wamechukua, pamoja na wake zake wawili. 19 Hakuna chochote kilichopotea: kijana au mzee, mvulana au msichana, nyara au kitu kingine chochote walichokuwa wamechukua. Daudi akarudisha kila kitu. 20 Akachukua makundi yote ya kondoo, mbuzi na ngʼombe, nao watu wake wakawaswaga wanyama hao mbele ya wanyama wengine wa kufugwa, wakisema, “Hizi ni nyara za Daudi.”
21 Kisha Daudi akafika kwa wale watu 200 waliokuwa wamechoka sana kumfuata na ambao waliachwa nyuma kwenye Bonde la Besori. Wakatoka kwenda kumlaki Daudi na wale watu aliokuwa nao. Daudi na watu wake walipowakaribia, akawasalimu. 22 Lakini watu wote waovu na wakorofi miongoni mwa wafuasi wa Daudi wakasema, “Kwa sababu hawakwenda pamoja nasi, hatutagawana nao nyara tulizorudisha. Lakini, kila mtu aweza kuchukua mkewe na watoto wake na kuondoka.”
23 Daudi akajibu, “La hasha, ndugu zangu, kamwe hamwezi kufanya hivyo kwa kile ambacho Bwana ametupatia. Yeye ametulinda na kuweka mikononi mwetu majeshi yale yaliyokuja kupigana dhidi yetu. 24 Ni nani atasikiliza yale mnayosema? Fungu la mtu aliyekaa na vyombo litakuwa sawa na la yule aliyekwenda vitani. Wote watashiriki sawa.” 25 Daudi akafanya hili liwe amri na agizo kwa Israeli kutoka siku ile hata leo.
26 Daudi alipofika Siklagi, akatuma baadhi ya nyara kwa wazee wa Yuda, waliokuwa rafiki zake, akasema, “Tazama, hapa kuna zawadi kwa ajili yenu kutoka nyara za adui za Bwana.”
27 Akazituma kwa wale waliokuwa Betheli, Ramoth-Negebu na Yatiri; 28 kwa wale walioko Aroeri, Sifmothi, Eshtemoa 29 na Rakali; kwa wale waliokuwa katika miji ya Wayerameeli na ya Wakeni; 30 na kwa wale walioko Horma, Bori-Ashani, Athaki, 31 na kwa wakazi wa Hebroni; na kwa wale waliokuwa mahali pengine pote ambako Daudi na watu wake walitembelea.
31:1 Basi Wafilisti wakapigana na Israeli. Waisraeli wakawakimbia, na wengi wakauawa katika Mlima Gilboa. 2 Wafilisti wakawafuatia kwa bidii Sauli na wanawe, wakawaua Yonathani, Abinadabu na Malki-Shua. 3 Mapigano yakawa makali sana kumzunguka Sauli, nao wapiga upinde wakampata na kumjeruhi vibaya.
4 Sauli akamwambia mbeba silaha wake, “Futa upanga wako unichome nao, la sivyo hawa watu wasiotahiriwa watakuja wanichome na kunidhalilisha.”
Lakini mbeba silaha wake akaogopa sana wala hakuweza kufanya hivyo. Kwa hiyo Sauli akachukua upanga wake mwenyewe na kuuangukia. 5 Mchukua silaha wake alipoona Sauli amekufa, naye pia akaangukia upanga wake akafa pamoja naye. 6 Basi Sauli, wanawe watatu, mbeba silaha wake na watu wake wote wakafa pamoja siku ile ile.
7 Waisraeli waliokuwa kandokando ya bonde na wale waliokuwa ngʼambo ya Yordani walipoona kuwa jeshi la Waisraeli limekimbia na kwamba Sauli na wanawe wamekufa, wakaacha miji yao na kukimbia. Nao Wafilisti wakaja na kukaa humo.
8 Kesho yake Wafilisti walipokuja kuwavua maiti silaha, walimkuta Sauli na wanawe watatu wameanguka katika Mlima Gilboa. 9 Wakamkata Sauli kichwa na kumvua silaha zake, nao wakatuma wajumbe katika nchi yote ya Wafilisti kutangaza habari katika hekalu la sanamu zao na miongoni mwa watu wao. 10 Wakaweka silaha zake katika hekalu la Maashtorethi, na kukifunga kiwiliwili chake katika ukuta wa Beth-Shani.
11 Watu wa Yabeshi-Gileadi waliposikia yale Wafilisti walichomfanyia Sauli, 12 mashujaa wao wote wakaenda usiku hadi Beth-Shani. Wakauchukua mwili wa Sauli na miili ya wanawe kutoka kwenye ukuta wa Beth-Shani na kurudi hadi Yabeshi, mahali ambapo waliiteketeza kwa moto. 13 Kisha wakachukua mifupa yao na kuizika chini ya mti wa mkwaju huko Yabeshi, nao wakafunga siku saba.
13 Sauli alikufa kwa sababu hakuwa mwaminifu kwa Bwana. Hakulishika neno la Bwana, hata akataka shauri kwa mwaguzi kwa ajili ya uongozi, 14 hakumuuliza Bwana. Kwa hiyo Bwana alimuua, na ufalme akampa Daudi mwana wa Yese.