Akishi Anampa Daudi Siklagi
Daudi anakimbilia kwa Akishi, mfalme wa Gathi, ambaye anampa Siklagi ili aishi humo. Kifo cha Sauli.
1056 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Daudi akasema moyoni mwake, “Katika mojawapo ya siku hizi nitaangamizwa kwa mkono wa Sauli. Jambo lililo bora ni kutorokea kwenye nchi ya Wafilisti. Hivyo Sauli atakata tamaa ya kunisaka popote katika Israeli, nami nitakuwa nimeponyoka mkononi mwake.”
Zaburi ya Daudi.
1 Ee Bwana, ninakuita wewe, uje kwangu hima.
Sikia sauti yangu ninapokuita.
2 Maombi yangu na yafike mbele zako kama uvumba;
kuinua mikono yangu juu na kuwe kama dhabihu ya jioni.
3 Ee Bwana, weka mlinzi kinywani mwangu,
weka ulinzi mlangoni mwa midomo yangu.
4 Usiuache moyo wangu uvutwe katika jambo baya,
nisije nikashiriki katika matendo maovu
pamoja na watu watendao mabaya,
wala nisije nikala vyakula vyao vya anasa.
5 Mtu mwenye haki na anipige: ni jambo la huruma;
na anikemee: ni mafuta kichwani mwangu.
Kichwa changu hakitalikataa.
Hata hivyo, maombi yangu daima
ni kinyume cha watenda mabaya,
6 watawala wao watatupwa chini
kutoka kwenye majabali,
waovu watajifunza kwamba maneno yangu
yalikuwa kweli.
7 Watasema, “Kama mtu anavyolima na kuvunja ardhi,
ndivyo mifupa yetu imetawanywa kwenye mlango wa kaburi.”
8 Lakini nimekaza macho yangu kwako, Ee Bwana Mwenyezi,
ndani yako nimekimbilia, usiniache nife.
9 Niepushe na mitego waliyonitegea,
kutokana na mitego iliyotegwa na watenda mabaya.
10 Waovu na waanguke kwenye nyavu zao wenyewe,
wakati mimi ninapita salama.
2 Hivyo Daudi akaondoka na hao watu mia sita waliokuwa pamoja naye na kwenda kwa Akishi mwana wa Maoki mfalme wa Gathi. 3 Daudi na watu wake wakakaa huko Gathi pamoja na Akishi. Kila mtu alikuwa pamoja na jamaa yake, naye Daudi pamoja na wakeze wawili: yaani Ahinoamu wa Yezreeli, na Abigaili wa Karmeli, mjane wa Nabali. 4 Sauli alipokuwa ameambiwa kwamba Daudi alikuwa amekimbilia Gathi, hakuendelea kumsaka tena.
5 Ndipo Daudi akamwambia Akishi, “Kama nimepata kibali machoni pako, unipe sehemu katika mojawapo ya miji katika nchi nikae huko. Kwa nini mtumwa wako akae pamoja nawe katika mji huu wa kifalme?”
6 Hivyo siku hiyo Akishi akampa Daudi mji wa Siklagi, nao Siklagi umekuwa mali ya wafalme wa Yuda tangu wakati huo. 7 Daudi akaishi katika nchi ya Wafilisti muda wa mwaka mmoja na miezi minne.
1 Hawa ndio watu waliomjia Daudi huko Siklagi, wakati alikuwa amefukuzwa mbele ya Sauli mwana wa Kishi (walikuwa miongoni mwa mashujaa waliomsaidia Daudi vitani, 2 walikuwa na pinde na walikuwa na uwezo wa kupiga mishale au kutupa mawe kwa kombeo wakitumia mkono wa kushoto au wa kulia; hawa walikuwa ndugu zake Sauli kutoka kabila la Benyamini):
3 Mkuu wao alikuwa Ahiezeri, na wa pili Yoashi, wote wana wa Shemaa Mgibeathi; pia Yezieli na Peleti wana wa Azmawethi; Beraka, Yehu Mwanathothi, 4 na Ishmaya Mgibeoni, shujaa miongoni mwa wale Thelathini, ambaye alikuwa kiongozi wa wale Thelathini; Yeremia, Yahazieli, Yohanani, Yozabadi, Mgederathi, 5 Eluzai, Yeremothi, Bealia, Shemaria, Shefatia, Mharufi; 6 Elikana, Ishia, Azareli, Yoezeri na Yashobeamu, wana wa Kora; 7 Yoela na Zebadia, wana wa Yerohamu, kutoka Gedori.
8 Basi Daudi na watu wake wakapanda na kuwashambulia Wageshuri, Wagirizi na Waamaleki. (Tangu zamani haya mataifa yalikuwa yameishi kwenye eneo lililotanda kuanzia Telemu katika njia iteremkayo Shuri hadi kufikia nchi ya Misri.) 9 Kila mara Daudi aliposhambulia eneo, hakubakiza hai mwanaume wala mwanamke, lakini alichukua kondoo na ngʼombe, punda na ngamia, na nguo. Kisha akarudi kwa Akishi.
10 Akishi alipomuuliza, “Je leo umeshambulia wapi?” Daudi humjibu, “Dhidi ya Negebu ya Yuda,” au wakati mwingine husema, “Dhidi ya Negebu ya Yerameeli,” au “Dhidi ya Negebu ya Wakeni.” 11 Daudi hakumwacha hai mwanaume au mwanamke ili apate kuletwa Gathi, kwa maana Daudi aliwaza, “Wanaweza kujulisha habari zetu na kusema, ‘Hivi ndivyo alivyofanya Daudi.’ ” Hii ndiyo ilikuwa desturi yake wakati wote aliishi katika nchi ya Wafilisti. 12 Akishi akamsadiki Daudi na kuwaza moyoni mwake, akasema, “Daudi amekuwa kitu cha kuchukiza kabisa kwa watu wake, Waisraeli, hivi kwamba atakuwa mtumishi wangu milele.”
Kifo cha Sauli 1055 KK
1 Siku zile Wafilisti wakakusanya majeshi yao ili kupigana vita dhidi ya Israeli. Akishi akamwambia Daudi, “Lazima ujue kuwa wewe pamoja na watu wako mtafuatana nami kwenda vitani.”
2 Daudi akasema, “Ndipo wewe mwenyewe utakapojionea jambo ambalo mtumishi wako anaweza kufanya.”
Akishi akamjibu Daudi, “Vyema sana, mimi nitakufanya uwe mlinzi wangu daima.”
3 Wakati huo Samweli alikuwa amekufa, nao Israeli wote walikuwa wamemwombolezea na kumzika kwenye mji wake mwenyewe huko Rama. Sauli alikuwa amewafukuza waaguzi na wachawi.
4 Wafilisti wakakusanyika na kupiga kambi yao huko Shunemu, naye Sauli akawakusanya Waisraeli wote na kupiga kambi yao huko Gilboa. 5 Sauli alipoona jeshi la Wafilisti, akaogopa; moyo wake ukajawa na hofu kuu. 6 Ndipo Sauli akauliza ushauri kwa Bwana, lakini Bwana hakumjibu kwa ndoto, wala kwa Urimu, wala kwa njia ya manabii. 7 Basi Sauli akawaambia watumishi wake, “Nitafutieni mwanamke mwaguzi ili nimwendee, nipate kuuliza kwake.”
Watumishi wake wakamwambia, “Yuko mwanamke mmoja huko Endori.”
8 Hivyo Sauli akajigeuza kwa kuvaa mavazi mengine, naye usiku akiwa amefuatana na watu wawili wakaenda kwa huyo mwanamke. Akamwambia, “Nibashirie kwa uaguzi, unipandishie yule nitakayekutajia.”
9 Huyo mwanamke akamwambia, “Wewe unajua lile alilofanya Mfalme Sauli. Amewakatilia mbali waaguzi, wapiga ramli wote na wachawi katika nchi. Mbona umenitegea maisha yangu ili wapate kuniua?”
10 Sauli akamwapia huyo mwanamke kwa Jina la Bwana, akasema, “Kwa hakika kama Bwana aishivyo, hutaadhibiwa kwa ajili ya jambo hili.”
11 Ndipo yule mwanamke akauliza, “Je unataka nikupandishie nani?”
Sauli akasema, “Nipandishie Samweli.”
12 Yule mwanamke alipomwona Samweli, alipiga yowe kwa sauti kuu, naye akamuuliza Sauli, “Mbona umenidanganya? Wewe ndiwe Sauli.”
13 Mfalme akamwambia, “Usiogope. Unaona nini?”
Yule mwanamke akasema, “Naona mungu unapanda kutoka ardhini.”
14 Sauli akamuuliza, “Ni mfano wa nini?”
Yule mwanamke akasema, “Ni mwanaume mzee amevaa joho anayepanda.”
Ndipo Sauli akatambua kwamba ni Samweli. Sauli akasujudu kifudifudi, uso wake hadi ardhini.
15 Samweli akamuuliza Sauli, “Kwa nini unanitaabisha kwa kunipandisha juu?”
Sauli akasema, “Mimi ninasumbuka sana, kwa maana Wafilisti wanapigana vita dhidi yangu, naye Mungu ameniacha. Hanijibu tena wala kwa njia ya manabii wala kwa ndoto. Kwa hiyo nimekuita wewe ili unijulishe la kufanya.”
16 Samweli akamuuliza, “Kwa nini uniulize mimi, maadamu Bwana amekuacha na kuwa adui yako? 17 Bwana ametenda lile alilotangulia kusema kupitia kwangu. Bwana ameurarua ufalme kutoka mikononi mwako, naye amempa mmoja wa jirani zako, yaani Daudi. 18 Kwa sababu wewe hukumtii Bwana, wala hukumtimizia ghadhabu yake kali juu ya Waamaleki, Bwana amekutendea mambo haya leo. 19 Zaidi ya hayo, Bwana atawatia Israeli pamoja na wewe mikononi mwa Wafilisti, na kesho wewe na wanao mtakuwa pamoja nami. Bwana pia atalitia jeshi la Israeli mikononi mwa Wafilisti.”
20 Papo hapo Sauli akaanguka chini, akajinyoosha, akiwa amejawa na hofu kwa ajili ya maneno ya Samweli. Nguvu zake zikamwishia kwa maana alikuwa hajala chochote mchana ule wote na usiku.
21 Yule mwanamke alipomwendea Sauli na kumwona amepatwa na hofu, akamwambia, “Tazama, mimi mtumishi wako mwanamke nimekutii. Nimeweka maisha yangu hatarini kwa kufanya kile ulichoniagiza nifanye. 22 Sasa tafadhali isikilize sauti ya mtumishi wako, uniruhusu nikupatie chakula kidogo ule ili uwe na nguvu za kurejea ulikotoka.”
23 Akakataa, akisema, “Mimi sitaki kula.”
Lakini watumishi wake wakaungana na yule mwanamke wakamsihi ale, naye akakubali. Basi akainuka hapo chini, akaketi juu ya kitanda.
24 Yule mwanamke alikuwa na ndama aliyenona hapo nyumbani, akamchinja mara moja. Akachukua unga, akaukanda, akatengeneza mkate usio chachu. 25 Ndipo akamwandalia meza Sauli pamoja na watu wake, nao wakala. Usiku ule ule wakainuka na kwenda zao.