Waliochaguliwa Wameipata, Wengine Wamepofushwa

Paulo anaendelea kusisitiza kwamba ingawa Israeli kama taifa walishindwa kupata kuhesabiwa haki na haki waliyotafuta katika matendo ya Sheria, mabaki waliochaguliwa ambao waliipokea injili walikuwa wameipata, na wengine walipofushwa, macho yao yakafungwa wasiione kweli. Hilo lilitimiza utabiri wa Isaya, na pia wa Daudi, aliyetabiri hali ya kusikitisha waliyokuwa wamefikia sasa kwa sababu ya kuendelea kuwa na mioyo migumu. Ugumu huo uligeuza baraka zao bora kuwa laana na mitego na njia za kuadhibiwa kwao, kwa kuwafanya wamtarajie Masiya wa kidunia. Daudi pia alitabiri kwamba kutokuamini kwao kungewafikisha katika hali ya utumwa wa kudhalilisha sana na fedheha.

58 BK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Warumi 11:7–10

7 Tuseme nini basi? Kile kitu ambacho Israeli alikitafuta kwa bidii hakukipata. Lakini waliochaguliwa walikipata. Waliobaki walifanywa wagumu, 8 kama ilivyoandikwa:

“Mungu aliwapa bumbuazi la mioyo,

macho ili wasiweze kuona,

na masikio ili wasiweze kusikia,

hadi leo.”

9 Naye Daudi anasema:

“Karamu zao na ziwe tanzi na mtego wa kuwanasa,

kitu cha kuwakwaza waanguke, na adhabu kwao.

10 Macho yao yatiwe giza ili wasiweze kuona,

nayo migongo yao iinamishwe daima.”

Wayahudi Hawajaanguka Kiasi cha Kushindwa Kuinuka Tena

Kwa swali la kama Wayahudi wamejikwaa hata wakaanguka wasiweze kuinuka tena, Paulo anajibu, “La hasha!” Kwa kumkataa Kristo waliharakisha kuitwa kwa watu wa Mataifa, na kupokelewa huko kwa watu wa Mataifa katika agano na Mungu kulikusudiwa kuwanufaisha Wayahudi, ili kuwachochea watamani pia kushiriki baraka za injili. Anatabiri kurejeshwa kwao hatimaye, na anatoa hoja kwamba ikiwa kwa kutokuamini kwao utajiri wa neema ya Mungu unaonyeshwa kwa ulimwengu wa watu wa Mataifa, basi neema na utukufu wake vitatukuzwa zaidi sana kwa kurudi kwao! Anajivunia huduma aliyokabidhiwa ya kuhubiri miongoni mwa watu wa Mataifa, akitumaini kwamba kupitia kwake Wayahudi watachochewa kushindana na watu wa Mataifa, na watu wa Mataifa wataongozwa kuwaheshimu Wayahudi. Anarudia kwamba ikiwa kuanguka kwao kulitoa nafasi ya ulimwengu wa wapagani kupatanishwa na Mungu, kurejeshwa kwa taifa la Wayahudi kutafanya mengi zaidi kuthibitisha ukweli wa Ukristo, na kutauletea ulimwengu furaha kubwa kana kwamba wamefufuka kutoka kwa wafu. Kwa maana ikiwa mabaki ya Wayahudi, malimbuko ambao wameamini, wamekubaliwa na Mungu, taifa lote la Wayahudi litakubaliwa wakati wao pia watakapoamini. Na ikiwa Abrahamu, mzizi wa taifa hilo, alihesabiwa haki kwa njia ya imani, matawi yake pia yatahesabiwa haki kwa masharti hayohayo.

Warumi 11:11–16

11 Hivyo nauliza tena: Je, Waisraeli walijikwaa ili waanguke na kuangamia kabisa? La, hasha! Lakini kwa sababu ya makosa yao, wokovu umewafikia watu wa Mataifa, ili kuwafanya Waisraeli waone wivu. 12 Basi ikiwa kukosa kwao kumekuwa utajiri mkubwa kwa ulimwengu, tena kama kuangamia kwao kumeleta utajiri kwa watu wa Mataifa, kurudishwa kwao kutaleta utajiri mkuu zaidi.

13 Sasa ninasema nanyi watu wa Mataifa. Maadamu mimi ni mtume kwa watu wa Mataifa, naitukuza huduma yangu 14 ili kuwafanya watu wangu waone wivu na hivyo kuwaokoa baadhi yao. 15 Kwa kuwa ikiwa kukataliwa kwao ni kupatanishwa kwa ulimwengu, kukubaliwa kwao si kutakuwa ni uhai baada ya kufa? 16 Kama sehemu ya donge la unga uliotolewa kuwa limbuko ni mtakatifu, basi unga wote ni mtakatifu, nalo shina kama ni takatifu, vivyo hivyo na matawi nayo.

Watu wa Mataifa Waliopandikizwa Hawapaswi Kuwadharau Wayahudi

Paulo anawahimiza watu wa Mataifa wasiwadharau wala kuwabeza Wayahudi kwa sababu sasa wamekatwa na kutengwa na watu wa Mungu. Wanapaswa kukumbuka kwamba wao wenyewe, kama mzeituni wa mwituni, wamepandikizwa miongoni mwao na kufanywa washiriki pamoja nao katika mzizi na utajiri wa mzeituni mzuri, wakipata faida na mapendeleo yao yote ya kiroho kutoka katika mzizi wake, yaani, kutoka katika agano na Abrahamu. Wanaonywa wasijivunie upendeleo waliopewa sasa, kwa maana Wayahudi walianguka kwa kutokuamini, nao wanasimama kwa imani; kwa hiyo hawapaswi kuwa na kiburi, bali waogope. Kwa maana ikiwa Mungu hakuyahurumia matawi ya asili, hawawezi kutarajia kwamba atawahurumia wao. Wanaagizwa kukumbuka ukali wa Mungu kwa Wayahudi walioanguka, na rehema zake kuu kwao ikiwa watadumu katika imani yao kwake; la sivyo wao pia watakatwa. Na Wayahudi, ikiwa hawataendelea katika kutokuamini, watapandikizwa tena na kurudishiwa mapendeleo waliyopoteza, jambo ambalo Mungu katika rehema zake bado anaweza kufanya. Kwa maana ikiwa watu wa Mataifa, kama chipukizi la mwituni lisilozaa matunda, walipandikizwa kinyume na maumbile katika shina zuri, wakaletwa katika kumjua Mungu na kukubaliwa kuingia katika agano naye, si zaidi sana itawezekana kwamba matawi ya asili, ambayo tayari yamepokea Sheria na Manabii, yataletwa katika kuujua wokovu na kupandikizwa tena katika mzeituni wao wenyewe!

Warumi 11:17–24

17 Lakini kama baadhi ya matawi yalikatwa, nawe chipukizi la mzeituni mwitu ukapandikizwa mahali pao ili kushiriki unono pamoja na matawi mengine kutoka shina la mzeituni, 18 basi usijivune juu ya hayo matawi. Kama ukijivuna, kumbuka jambo hili: si wewe unayelishikilia shina, bali ni shina linalokushikilia wewe. 19 Basi utasema, “Matawi yale yalikatwa ili nipate kupandikizwa katika hilo shina.” 20 Hii ni kweli. Matawi hayo yalikatwa kwa sababu ya kutokuamini kwake, lakini wewe umesimama tu kwa sababu ya imani. Kwa hiyo usijivune, bali simama kwa kuogopa. 21 Kwa maana kama Mungu hakuyahurumia matawi ya asili, wala hatakuhurumia wewe.

22 Angalia basi wema na ukali wa Mungu: Kwa wale walioanguka, ukali, bali kwako wewe wema wa Mungu, kama utadumu katika wema wake. La sivyo, nawe utakatiliwa mbali. 23 Wao nao wasipodumu katika kutokuamini kwao, watapandikizwa tena kwenye shina, kwa maana Mungu anao uwezo wa kuwapandikiza tena kwenye hilo shina. 24 Ikiwa wewe ulikatwa kutoka kile ambacho kwa asili ni mzeituni mwitu na kupandikizwa kinyume cha asili kwenye mzeituni uliopandwa, si rahisi zaidi matawi haya ya asili kupandikizwa tena kwenye shina lake la mzeituni!

Siri ya Kurejeshwa kwa Israeli

Paulo anathibitisha kwamba hataki watu wa Mataifa wasijue siri ya kurejeshwa kwa Wayahudi wakati ujao, ili wasijione kuwa wanastahili kuliko ilivyo. Anathibitisha kwamba upofu umewapata baadhi ya Israeli mpaka kanisa la watu wa Mataifa litimie, na ndipo Wayahudi wenyewe watakapoletwa kwenye maarifa ya wokovu, kama manabii wao wenyewe walivyotabiri. Na Mungu, atakapoondoa dhambi zao, atawaingiza tena katika agano na kuwarejeshea haki walizokuwa wamepoteza (linganisha mstari wa 27; Isaya 59:20–21). Wayahudi wasioamini, wakiwa maadui wa injili, walikataliwa na Mungu kwa faida ya watu wa Mataifa. Lakini kwa habari ya uteule, ambao kwa huo Mungu aliwachagua kwanza wawe watu wake mwenyewe, wanapendwa kwa ajili ya mababu zao. Zawadi ya bure ya Mungu na mwito wa wazao wa Abrahamu havitabadilishwa. Kwa maana kama vile ilivyo hakika kwamba watu wa Mataifa sasa wamepata rehema kupitia kutokuamini kwa Wayahudi, vivyo hivyo ni hakika kwamba Wayahudi ambao hawajaamini wataonyeshwa rehema hiyo hiyo. Kwa maana Mungu amewafungia wote, Myahudi na mtu wa Mataifa, katika kutokuamini, kila mmoja kwa zamu yake akiwa ameiasi nuru aliyokuwa nayo, ili wote wapewe kwa usawa zawadi ya bure ya msamaha.

Warumi 11:25–32

25 Ndugu zangu, ili msije mkajidai kuwa wenye hekima kuliko mlivyo, nataka mfahamu siri hii: Ugumu umewapata Israeli kwa sehemu hadi idadi ya watu wa Mataifa watakaoingia itimie. 26 Hivyo Israeli wote wataokolewa. Kama ilivyoandikwa:

“Mkombozi atakuja kutoka Sayuni;

ataondoa kutokumcha Mungu katika Yakobo.

27 Hili ndilo agano langu nao

nitakapoziondoa dhambi zao.”

28 Kwa habari ya Injili, wao ni adui wa Mungu kwa ajili yenu, lakini kuhusu kule kuteuliwa kwao ni wapendwa, kwa ajili ya mababa zao wa zamani, 29 kwa maana akishawapa watu karama, Mungu haziondoi, wala wito wake. 30 Kama vile ninyi wakati fulani mlivyokuwa waasi kwa Mungu lakini sasa mmepata rehema kwa sababu ya kutokutii kwao, 31 hivyo nao Waisraeli wamekuwa waasi ili kwamba wao nao sasa waweze kupata rehema kwa ajili ya rehema za Mungu kwenu. 32 Kwa maana Mungu amewafunga wanadamu wote kwenye kuasi ili apate kuwarehemu wote.

Sifa za Paulo kwa Hekima ya Mungu Isiyochunguzika

Paulo anamalizia mjadala huu wote muhimu kwa maneno yaliyojaa shangwe, mshangao na sifa kwa hekima na wema wa Mungu katika kuwatendea wanadamu. Anasisitiza kwamba hakuna anayeweza kufahamu hukumu na mashauri ya siri ya Mungu, na kwamba kuchaguliwa kwa Wayahudi au kwa watu wa Mataifa kunapatana kabisa na haki yake, kwa kuwa hakuna anayeweza kudai chochote kutoka kwake, yeye aliye mwanzilishi na msababishaji wa vitu vyote, ambavyo vyote vipo kwa uwezo wake na kupitia yeye. Basi Mungu atukuzwe milele katika kazi zake zote.

Warumi 11:33–36

33 Tazama jinsi kilivyo kina cha utajiri

wa hekima na maarifa ya Mungu!

Tazama jinsi ambavyo hukumu zake hazichunguziki,

na ambavyo njia zake zisivyotafutikana!

34 “Ni nani aliyeyafahamu mawazo ya Bwana?

Au ni nani ambaye amekuwa mshauri wake?”

35 “Au ni nani aliyempa chochote

ili arudishiwe?”

36 Kwa maana vitu vyote vyatoka kwake, viko kwake na kwa ajili yake.

Utukufu ni wake milele! Amen.

Warumi Wahimizwa Kuwa Dhabihu Zilizo Hai

Baada ya kumaliza sehemu ya barua yake inayohusu mafundisho ya imani, Paulo anasisitiza umuhimu wa maisha matakatifu ambayo mafundisho hayo yalikusudiwa kufundisha. Anawasihi Warumi waitoe miili yao wenyewe kwenye madhabahu ya kiroho ya Mungu kuwa dhabihu iliyo hai, badala ya wanyama waliotolewa kwa Mungu chini ya Sheria ya Mose, wakiweka miili yao wakfu kabisa kwa Mungu, jambo ambalo ni ibada inayokubalika na yenye maana kwa Mkristo. Anawahimiza wasifuate desturi na mitazamo ya ulimwengu huu, bali wabadilike katika mwelekeo na mtazamo wa akili zao, ili waweze kutimiza katika maisha yao wenyewe, na kuwathibitishia wengine, mapenzi ya Mungu yaliyo makamilifu na yanayokubalika. Kwa mamlaka ya cheo chake cha mtume, Paulo anawaonya wasijione kuwa wakuu kuliko walivyo kwa sababu ya karama zao za kiroho, kwa maana ingawa karama zao zinaweza kutofautiana, wao ni viungo vya mwili mmoja, na kila kiungo kinahitajika na vingine. Anawahimiza watumie kwa bidii na uaminifu karama alizokabidhiwa kila mmoja wao.

Warumi 12:1–8

1 Kwa hiyo, ndugu zangu, nawasihi kwa rehema zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu na inayompendeza Mungu, hii ndiyo ibada yenu yenye maana. 2 Msifuatishe tena mfano wa ulimwengu huu, bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu. Ndipo mtaweza kuonja na kuhakikisha ni nini mapenzi ya Mungu yaliyo mema, yanayopendeza machoni pake na ukamilifu.

3 Kwa ajili ya neema niliyopewa nawaambia kila mmoja miongoni mwenu, asijidhanie kuwa bora kuliko impasavyo, bali afikiri kwa busara kwa kulingana na kipimo cha imani Mungu aliyompa. 4 Kama vile katika mwili mmoja tulivyo na viungo vingi, navyo viungo vyote havina kazi moja, 5 vivyo hivyo na sisi tulio wengi, tu mwili mmoja katika Kristo, nasi kila mmoja ni kiungo cha mwenzake. 6 Tuna karama zilizotofautiana kila mmoja kutokana na neema tuliyopewa. Kama ni unabii na tutoe unabii kwa kadiri ya imani. 7 Kama ni kuhudumu na tuhudumu, mwenye kufundisha na afundishe, 8 kama ni kutia moyo na atie moyo, kama ni kuchangia kwa ajili ya mahitaji ya wengine na atoe kwa ukarimu, kama ni uongozi na aongoze kwa bidii, kama ni kuhurumia wengine na afanye hivyo kwa furaha.

Paulo Ahimiza Upendo, Unyenyekevu, na Kutojilipiza Kisasi

Paulo anaendelea na mafundisho yake ya vitendo, akiwahimiza wapendane na kuwatendea wote mema; wawe na unyenyekevu, bidii, moyo wa kujitoa, na kuhurumiana; na wasitafute kulipiza kisasi, bali waushinde uovu kwa wema, pamoja na wajibu mwingine muhimu wa kimaadili.

Warumi 12:9–21

9 Upendo lazima usiwe na unafiki. Chukieni lililo ovu, shikamaneni na lililo jema. 10 Pendaneni ninyi kwa ninyi kwa upendo wa ndugu. Waheshimuni na kuwatanguliza wengine. 11 Msiwe wavivu, bali mwe na bidii katika roho mkimtumikia Bwana. 12 Kuweni na furaha katika tumaini, katika dhiki kuweni na saburi, dumuni katika maombi. 13 Changieni katika mahitaji ya watakatifu, wakaribisheni wageni.

14 Wabarikini wale wanaowatesa, barikini wala msilaani. 15 Furahini pamoja na wenye kufurahi, lieni pamoja na wale waliao. 16 Kaeni kwa amani ninyi kwa ninyi. Msijivune, bali mwe tayari kushirikiana na wanyonge. Wala msiwe watu wenye kujivuna kwamba mnajua kila kitu.

17 Msimlipe mtu yeyote ovu kwa ovu. Jitahidini ili mtende yaliyo mema machoni pa watu wote. 18 Kama ikiwezekana, kwa upande wenu kaeni kwa amani na watu wote. 19 Wapendwa, msilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu, maana imeandikwa: “Ni juu yangu kulipiza kisasi, nitalipiza,” asema Bwana. 20 Badala yake:

“Kama adui yako ana njaa, mlishe;

kama ana kiu, mpe kinywaji.

Kwa kufanya hivyo,

unaweka makaa ya moto yanayowaka kichwani pake.”

21 Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema.