Stefano Analikemea Baraza la Wayahudi
Stefano, baada ya kukatizwa alipokuwa akijitetea, analikemea Baraza la Wayahudi kuwa wao ndio wauaji wa Masiya wao.
33 au 34 BK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
51 “Enyi watu wenye shingo ngumu, msiotahiriwa mioyo wala masikio, daima hamwachi kumpinga Roho Mtakatifu, kama walivyofanya baba zenu. 52 Je, kuna nabii gani ambaye baba zenu hawakumtesa? Waliwaua wale waliotabiri habari za kuja kwake yule Mwenye Haki. Nanyi sasa mmekuwa wasaliti wake na wauaji. 53 Ninyi ndio mlipokea sheria zilizoletwa kwenu na malaika, lakini hamkuzitii.”
Stefano Anapigwa Mawe Hadi Kufa 34 BK
Stefano anapigwa mawe hadi kufa, akiwaombea wauaji wake.
54 Waliposikia haya wakaghadhibika, wakamsagia meno. 55 Lakini yeye Stefano, akiwa amejaa Roho Mtakatifu, alikaza macho mbinguni, akaona utukufu wa Mungu, na Yesu akiwa amesimama mkono wa kuume wa Mungu. 56 Akasema, “Tazameni! Naona mbingu zimefunguka, na Mwana wa Adamu amesimama upande wa kuume wa Mungu.”
57 Lakini wao wakapiga kelele kwa sauti kubwa, wakaziba masikio yao, wakamrukia kwa nia moja. 58 Wakamtupa nje ya mji, wakampiga kwa mawe. Nao mashahidi wakaweka mavazi yao miguuni mwa kijana mmoja ambaye jina lake aliitwa Sauli.
59 Walipokuwa wakimpiga mawe, Stefano aliomba, “Bwana Yesu, pokea roho yangu.” 60 Kisha akapiga magoti, akalia kwa sauti kubwa akasema, “Bwana usiwahesabie dhambi hii.” Baada ya kusema hayo, akalala.
8:1 Naye Sauli alikuwepo pale, akiridhia kuuawa kwa Stefano.
Siku ile kukatukia mateso makuu dhidi ya kanisa huko Yerusalemu, waumini wote isipokuwa mitume wakatawanyika, wakakimbilia Uyahudi na Samaria. 2 Watu wacha Mungu wakamzika Stefano na kumwombolezea sana.
Mateso ya Jumla Dhidi ya Wakristo
Mateso ya jumla dhidi ya Wakristo, ambayo Sauli (baadaye Paulo) anashiriki kwa kuchukua nafasi ya kuongoza.
3 Lakini kwa habari ya Sauli alikuwa analiharibu kanisa, akiingia nyumba kwa nyumba, akiwaburuta wanawake na wanaume na kuwatupa gerezani.
Filipo Anahubiri Samaria
Filipo, shemasi, baada ya kuondoka Yerusalemu kwa sababu ya mateso, anaenda Samaria, ambako anahubiri na kufanya miujiza.
5 Filipo akateremkia mji mmoja wa Samaria akawahubiria habari za Kristo 6 Watu walipomsikia Filipo na kuona ishara na miujiza aliyofanya, wakasikiliza kwa bidii yale aliyosema. 7 Pepo wachafu wakawa wakiwatoka watu wengi huku wakipiga kelele na wengi waliopooza na viwete wakaponywa. 8 Hivyo pakawa na furaha kuu katika mji huo.
9 Basi mtu mmoja jina lake Simoni alikuwa amefanya uchawi kwa muda mrefu katika mji huo akiwashangaza watu wote wa Samaria. Alijitapa kwamba yeye ni mtu mkuu, 10 nao watu wote wakubwa kwa wadogo wakamsikiliza na kumaka, wakisema “Mtu huyu ndiye uweza wa Mungu ujulikanao kama ‘Uweza Mkuu.’ ” 11 Wakamfuata kwa sababu kwa muda mrefu alikuwa amewashangaza kwa uchawi wake. 12 Lakini watu walipomwamini Filipo alipohubiri habari njema za Ufalme wa Mungu na jina la Yesu Kristo, wakabatizwa wanaume na wanawake. 13 Simoni naye akaamini na akabatizwa. Akamfuata Filipo kila mahali, akistaajabishwa na ishara kuu na miujiza aliyoiona.
Petro na Yohana Wanashuka Kwenda Samaria
Petro na Yohana wanashuka kutoka Yerusalemu kwenda Samaria ili kuwapa waongofu wapya karama za Roho Mtakatifu.
14 Basi mitume waliokuwa Yerusalemu waliposikia kuwa Samaria wamelipokea neno la Mungu, wakawatuma Petro na Yohana waende huko. 15 Nao walipofika wakawaombea ili wampokee Roho Mtakatifu, 16 kwa sababu Roho Mtakatifu alikuwa bado hajawashukia hata mmoja ila wamebatizwa tu katika jina la Bwana Yesu. 17 Ndipo Petro na Yohana wakaweka mikono yao juu ya wale waliobatizwa, nao wakapokea Roho Mtakatifu.
Petro Anamkemea Simoni Mchawi
18 Simoni alipoona kuwa watu wanapokea Roho Mtakatifu mitume walipoweka mikono juu yao, akataka kuwapa fedha 19 akisema, “Nipeni na mimi uwezo huu ili kila mtu nitakayeweka mikono yangu juu yake apate kupokea Roho Mtakatifu.”
20 Petro akamjibu, “Fedha yako na iangamie pamoja nawe, kwa sababu ulidhani unaweza kununua karama ya Mungu kwa fedha! 21 Wewe huna sehemu wala fungu katika huduma hii kwa kuwa moyo wako si mnyofu mbele za Mungu. 22 Kwa hiyo tubu kwa uovu huu wako na umwombe Bwana. Yamkini aweza kukusamehe mawazo uliyo nayo moyoni mwako. 23 Kwa maana ninaona kwamba wewe umejawa na uchungu na ni mfungwa wa dhambi.”
24 Ndipo Simoni akajibu, “Niombeeni kwa Bwana, ili hayo mliyosema lolote yasinitukie.”