Petro na Yohana Wanahubiri katika Vijiji Vingi vya Samaria

34 BK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Matendo 8:25

25 Nao walipokwisha kutoa ushuhuda na kuhubiri neno la Bwana, wakarudi Yerusalemu wakihubiri Injili katika vijiji vingi vya Samaria.

Filipo Anambatiza Mweka Hazina wa Malkia Kandake

Mweka hazina wa Malkia Kandake, mwongofu wa haki, anaongoka na kubatizwa na Filipo, ambaye sasa anahubiri katika miji ya Uyahudi.

Matendo 8:26–40

26 Basi malaika wa Bwana akamwambia Filipo, “Nenda upande wa kusini kwenye ile barabara itokayo Yerusalemu kuelekea Gaza ambayo ni jangwa.” 27 Hivyo akaondoka. Akiwa njiani akakutana na towashi wa Kushi, aliyekuwa afisa mkuu, mwenye mamlaka juu ya hazina zote za Kandake, Malkia wa Kushi. Huyu towashi alikuwa amekwenda Yerusalemu ili kuabudu, 28 naye akiwa njiani kurudi nyumbani alikuwa ameketi garini mwake akisoma kitabu cha nabii Isaya. 29 Roho Mtakatifu akamwambia Filipo, “Nenda kwenye lile gari ukae karibu nalo.”

30 Ndipo Filipo akakimbilia lile gari na kumsikia yule mtu anasoma kitabu cha nabii Isaya. Filipo akamuuliza, “Je, unaelewa hayo usomayo?”

31 Yule towashi akasema, “Nitawezaje kuelewa mtu asiponifafanulia?” Hivyo akamkaribisha Filipo ili apande na kuketi pamoja naye.

32 Huyu towashi alikuwa anasoma fungu hili la Maandiko:

“Aliongozwa kama kondoo aendaye machinjoni,

kama mwana-kondoo anyamazavyo

mbele yake yule amkataye manyoya,

hivyo hakufungua kinywa chake.

33 Katika kufedheheshwa kwake alinyimwa haki yake.

Nani awezaye kueleza juu ya kizazi chake?

Kwa maana maisha yake yaliondolewa

kutoka duniani.”

34 Yule towashi akamuuliza Filipo, “Tafadhali niambie, nabii huyu anena habari zake mwenyewe au habari za mtu mwingine?” 35 Ndipo Filipo akaanza kutumia fungu lile la Maandiko, akamweleza habari njema za Yesu.

36 Walipokuwa wakiendelea na safari wakafika mahali palipokuwa na maji, yule towashi akamuuliza Filipo, “Tazama, hapa kuna maji. Kitu gani kitanizuia nisibatizwe?” [ 37 Filipo akamwambia, “Kama ukiamini kwa moyo wako wote unaweza kubatizwa.” Akajibu, “Naamini kuwa Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu.”] 38 Naye akaamuru lile gari lisimamishwe. Wakateremka kwenye maji wote wawili, yule towashi na Filipo, naye Filipo akambatiza. 39 Nao walipopanda kutoka kwenye maji, ghafula Roho wa Bwana akamnyakua Filipo, naye towashi hakumwona tena, lakini akaenda zake akifurahi. 40 Filipo akajikuta yuko Azoto, akasafiri akihubiri Injili katika miji yote mpaka alipofika Kaisaria.

Waongofu Waliotawanyika Wanawahubiria Wayahudi

Waongofu wengi waliokuwa wamekimbia kutoka Yerusalemu kwa sababu ya mateso huko wanawahubiria Wayahudi injili katika majimbo.

Matendo 8:4

4 Kwa hiyo wale waliotawanyika wakalihubiri neno la Mungu kila mahali walipokwenda.

Sauli Anaongoka Akiwa Njiani Kwenda Dameski 35 BK

Akiwa njiani kwenda Dameski, Sauli anaongoka na kuikubali imani aliyokuwa akiipinga, anaposikia sauti ya Mungu kutoka mbinguni na kuona utukufu wa uwepo wa Mungu.

Matendo 9:1–9

1 Wakati ule ule, Sauli alikuwa bado anazidisha vitisho vya kuua wanafunzi wa Bwana, akamwendea kuhani mkuu, 2 naye akamwomba kuhani mkuu ampe barua za kwenda kwenye masinagogi huko Dameski, ili akimkuta mtu yeyote wa Njia Ile, akiwa mwanaume au mwanamke, aweze kuwafunga na kuwaleta Yerusalemu. 3 Basi akiwa katika safari yake, alipokaribia Dameski, ghafula nuru kutoka mbinguni ikamwangaza kotekote. 4 Akaanguka chini, akasikia sauti ikimwambia, “Sauli, Sauli, mbona unanitesa?”

5 Sauli akajibu, “U nani wewe, Bwana?”

Ile sauti ikajibu, “Mimi ni Yesu unayemtesa. 6 Sasa inuka uingie mjini, nawe utaambiwa yakupasayo kutenda.”

7 Watu waliokuwa wakisafiri pamoja na Sauli wakasimama bila kuwa na la kusema, kwa sababu walisikia sauti lakini hawakumwona aliyekuwa akizungumza. 8 Sauli akainuka kutoka pale chini na alipojaribu kufungua macho yake hakuweza kuona kitu chochote. Basi wakamshika mkono wakamwongoza mpaka Dameski. 9 Naye kwa muda wa siku tatu alikuwa kipofu naye hakula wala kunywa chochote.