Uvamizi wa Kwanza wa Senakeribu

713 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

2 Nyakati 32:1–8

1 Baada ya yale yote aliyokuwa amefanya Hezekia kwa uaminifu mkubwa, Senakeribu mfalme wa Ashuru akaja na kuvamia Yuda. Akaizunguka miji yenye ngome kwa jeshi, akifikiri kuiteka iwe yake. 2 Hezekia alipoona kuwa Senakeribu amekuja na kwamba alikusudia kufanya vita juu ya Yerusalemu, 3 akafanya shauri na maafisa wake na mashujaa wake juu ya kuzuia maji kutoka chemchemi zilizo nje ya mji, nao wakamsaidia. 4 Umati mkubwa wa watu ukakusanyika na kuzuia chemchemi zote na vijito vilivyotiririka katika nchi yote, wakisema: “Kwa nini wafalme wa Ashuru waje na kukuta maji tele?” 5 Hezekia akafanya kazi kwa bidii kukarabati sehemu zote zilizokuwa zimebomoka za ukuta na kujenga minara juu yake. Akajenga ukuta mwingine nje ya ule uliokuwepo na kuimarisha Milo katika Mji wa Daudi. Akatengeneza pia silaha nyingi na ngao.

6 Akaweka maafisa wa jeshi juu ya watu, wakawakutanisha mbele yake katika uwanja kwenye lango la mji, naye akawatia moyo kwa maneno haya: 7 “Kuweni hodari na wenye moyo mkuu. Msiogope, msifadhaike wala msikate tamaa kwa sababu ya mfalme wa Ashuru na hili jeshi kubwa lililo pamoja naye, kwa kuwa aliye pamoja nasi ni mkuu kuliko aliye pamoja naye. 8 Kwake uko mkono wa mwili tu, bali kwetu yuko Bwana Mungu wetu kutusaidia na kutupigania vita vyetu.” Nao watu wakatiwa moyo kutokana na maneno aliyowaambia Hezekia mfalme wa Yuda.

Hezekia Anajisalimisha, na Ashdodi Inatekwa

2 Wafalme 18:13–16

13 Katika mwaka wa kumi na nne wa utawala wa Mfalme Hezekia, Senakeribu mfalme wa Ashuru akaishambulia miji yote ya Yuda yenye ngome na kuiteka. 14 Basi Hezekia mfalme wa Yuda akamtumia ujumbe mfalme wa Ashuru huko Lakishi akisema: “Nimefanya makosa. Ondoka katika nchi yangu, nami nitakulipa chochote unachokitaka kwangu.” Mfalme wa Ashuru akamtoza Hezekia mfalme wa Yuda talanta 300 za fedha, na talanta thelathini za dhahabu. 15 Basi Hezekia akampa fedha yote iliyopatikana ndani ya Hekalu la Bwana na katika hazina ya jumba la mfalme.

16 Wakati huu Hezekia mfalme wa Yuda akabandua dhahabu yote iliyokuwa imefunika milango na miimo ya Hekalu la Bwana, akampa mfalme wa Ashuru.

Isaya 20

1 Katika mwaka ule ambao jemadari mkuu alitumwa na Mfalme Sargoni wa Ashuru, naye akaja mpaka Ashdodi, akaushambulia na kuuteka, 2 wakati ule Bwana alisema kwa kinywa cha Isaya mwana wa Amozi. Akamwambia, “Vua nguo ya gunia kutoka mwilini mwako na viatu kutoka miguuni mwako.” Naye akafanya hivyo, akatembea huku na huko uchi, bila viatu.

3 Kisha Bwana akasema, “Kama vile mtumishi wangu Isaya alivyotembea uchi na bila viatu kwa miaka mitatu, kama ishara na dalili mbaya dhidi ya nchi ya Misri na Kushi, 4 vivyo hivyo mfalme wa Ashuru atawaongoza mateka wa Wamisri, na watu wa uhamisho wa Kushi, uchi na bila viatu, vijana hata wazee, wakiwa matako wazi, kwa aibu ya Wamisri. 5 Wale waliotegemea Kushi na kujivunia Misri wataogopa na kuaibika. 6 Katika siku ile watu wanaoishi katika pwani hii watasema, ‘Tazama lililowapata wale tuliowategemea, wale tuliowakimbilia kwa msaada na wokovu kutoka mikononi mwa mfalme wa Ashuru! Tutawezaje basi kupona?’ ”

Wito wa Kinabii kwa Yerusalemu

Wito wa kinabii kwa Yerusalemu wakati jeshi la Senakeribu liko nchini.

Isaya 29

1 Ole wako, wewe Arieli, Arieli,

mji alimokaa Daudi!

Ongezeni mwaka kwa mwaka,

na mzunguko wa sikukuu zenu uendelee.

2 Hata hivyo nitauzunguka Arieli kwa jeshi,

utalia na kuomboleza,

utakuwa kwangu kama mahali

pa kuwashia moto madhabahuni.

3 Nitapiga kambi pande zote dhidi yako,

nitakuzunguka kwa minara

na kupanga mazingirwa yangu dhidi yako.

4 Utakaposhushwa, utanena kutoka ardhini,

utamumunya maneno yako kutoka mavumbini.

Sauti yako itatoka katika nchi kama vile ya mzimu,

utanongʼona maneno yako toka mavumbini.

5 Lakini adui zako wengi watakuwa kama vumbi laini,

kundi la wakatili watakuwa

kama makapi yapeperushwayo.

Naam, ghafula, mara moja,

6 Bwana Mwenye Nguvu Zote atakuja

na ngurumo, tetemeko la ardhi, na kwa sauti kuu,

atakuja na dhoruba, tufani na miali ya moto iteketezayo.

7 Kisha makundi ya mataifa yote yale yapiganayo dhidi ya Arieli,

yale yanayomshambulia yeye na ngome zake, na kumzunguka kwa jeshi,

watakuwa kama ilivyo ndoto,

kama maono wakati wa usiku:

8 kama vile mtu aliye na njaa aotavyo kuwa anakula,

lakini huamka, bado njaa yake ingalipo,

kama vile mtu mwenye kiu aotavyo kuwa anakunywa maji,

lakini huamka akiwa anazimia, akiwa bado angali ana kiu.

Hivyo ndivyo itakavyokuwa kwa makundi yote ya mataifa

yanayopigana dhidi ya Mlima Sayuni.

9 Duwaeni na kushangaa,

jifanyeni vipofu wenyewe na msione,

leweni, lakini si kwa mvinyo,

pepesukeni lakini si kwa kileo.

10 Bwana amewaleteeni usingizi mzito:

Ameziba macho yenu (ninyi manabii);

amefunika vichwa vyenu (ninyi waonaji).

11 Kwa maana kwenu ninyi, maono haya yote si kitu ila maneno yaliyotiwa lakiri katika kitabu. Kama mkimpa mtu yeyote awezaye kusoma kitabu hiki, nanyi mkamwambia, “Tafadhali kisome,” yeye atajibu, “Mimi siwezi, kwa kuwa kimetiwa lakiri.” 12 Au kama mkimpa mtu yeyote kitabu hiki asiyeweza kusoma na kumwambia, “Tafadhali kisome,” atajibu, “Mimi sijui kusoma.”

13 Bwana anasema:

“Watu hawa hunikaribia kwa vinywa vyao

na kuniheshimu kwa midomo yao,

lakini mioyo yao iko mbali nami.

Ibada yao kwangu inatokana na maagizo

waliyofundishwa na wanadamu.

14 Kwa hiyo mara nyingine tena nitawashangaza watu hawa,

kwa ajabu juu ya ajabu.

Hekima ya wenye hekima itapotea,

nayo akili ya wenye akili itatoweka.”

15 Ole kwa wale wanaokwenda kwenye vilindi virefu

kumficha Bwana mipango yao,

wafanyao kazi zao gizani na kufikiri,

“Ni nani anayetuona? Ni nani atakayejua?”

16 Mnapindua mambo juu chini,

kana kwamba mfinyanzi aweza kufikiriwa kuwa kama udongo wa mfinyanzi!

Je, kile kilichofinyangwa chaweza kumwambia yule aliyekifinyanga,

“Wewe hukunifinyanga mimi?”

Je, chungu kinaweza kumwambia mfinyanzi,

“Wewe hujui chochote?”

17 Kwa muda mfupi sana, je, Lebanoni haitageuzwa kuwa shamba lenye rutuba,

na shamba lenye rutuba liwe kama msitu?

18 Katika siku ile viziwi watasikia maneno ya kitabu,

na katika utusitusi na giza

macho ya kipofu yataona.

19 Mara nyingine tena wanyenyekevu watafurahi katika Bwana,

wahitaji watafurahi katika yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli.

20 Wakatili watatoweka na wenye kudhihaki watatokomea,

nao wote wenye jicho la uovu watakatiliwa mbali,

21 wale ambao kwa neno humfanya mtu kuwa mwenye hatia,

wamtegeao mtego mtetezi katika mahakama,

na kwa ushuhuda wa uongo humnyima haki

yeye asiye na hatia.

22 Kwa hiyo hili ndilo Bwana, aliyemkomboa Abrahamu, analosema kwa nyumba ya Yakobo:

“Yakobo hataaibishwa tena,

wala nyuso zao hazitabadilika sura tena.

23 Wakati watakapoona watoto wao miongoni mwao,

kazi ya mikono yangu,

watalitakasa Jina langu takatifu;

wataukubali utakatifu wa yeye Aliye Mtakatifu wa Yakobo,

nao watamcha Mungu wa Israeli.

24 Wale wanaopotoka rohoni watapata ufahamu,

nao wale wanaolalamika watayakubali mafundisho.”