Kuvamiwa kwa Uyahudi na Kuangamizwa kwa Babeli Vyatabiriwa

713 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Isaya 22:1–14

1 Neno kuhusu Bonde la Maono:

Nini kinachokutaabisha sasa,

kwamba ninyi nyote mmepanda juu ya mapaa?

2 Ewe mji uliojaa ghasia,

ewe mji wa makelele na sherehe!

Watu wenu waliokufa hawakuuawa kwa upanga,

wala hawakufa vitani.

3 Viongozi wako wote wamekimbia pamoja,

wamekamatwa bila kutumia upinde.

Ninyi nyote mliokamatwa mlichukuliwa wafungwa pamoja,

mlikimbia wakati adui alipokuwa bado mbali.

4 Kwa hiyo nilisema, “Geukia mbali nami,

niache nilie kwa uchungu.

Usijaribu kunifariji

juu ya maangamizi ya watu wangu.”

5 Bwana, Bwana Mwenye Nguvu Zote, anayo siku

ya ghasia, ya kukanyaga, na ya kuogofya

katika Bonde la Maono,

siku ya kuangusha kuta

na ya kupiga kelele mpaka milimani.

6 Elamu analichukua podo,

pamoja na waendesha magari ya vita na farasi.

Kiri anaifungua ngao.

7 Mabonde yako yaliyo mazuri sana yamejaa magari ya vita,

nao wapanda farasi wamewekwa kwenye malango ya mji;

8 ulinzi wa Yuda umeondolewa.

Nawe ulitazama siku ile

silaha katika Jumba la Kifalme la Mwituni,

9 mkaona kuwa Mji wa Daudi

una matundu mengi katika ulinzi wake,

mkaweka akiba ya maji

kwenye Bwawa la Chini.

10 Mlihesabu majengo katika Yerusalemu

nanyi mkabomoa nyumba ili kuimarisha ukuta.

11 Mlijenga bwawa la maji katikati ya kuta mbili

kwa ajili ya maji ya Bwawa la Zamani,

lakini hamkumtazama Yule aliyelitengeneza,

au kuwa na heshima kwa Yule aliyeubuni tangu zamani za kale.

12 Bwana, Bwana Mwenye Nguvu Zote,

aliwaita siku ile

ili kulia na kuomboleza,

kungʼoa nywele zenu na kuvaa nguo ya gunia.

13 Lakini tazama, kuna furaha na sherehe,

kuchinja ngʼombe na kuchinja kondoo,

kula nyama na kunywa mvinyo!

Mnasema, “Tuleni na kunywa,

kwa kuwa kesho tutakufa!”

14 Bwana Mwenye Nguvu Zote amelifunua hili nikiwa ninasikia: Bwana, Bwana Mwenye Nguvu Zote, asema: “Mpaka siku ya kufa kwenu, dhambi hii haitafanyiwa upatanisho.”

Isaya 21

1 Neno kuhusu Jangwa kando ya Bahari:

Kama upepo wa kisulisuli unaopita katika nchi hadi kusini,

mshambuliaji anakuja kutoka jangwani,

kutoka nchi inayotisha.

2 Nimeonyeshwa maono ya kutisha:

Msaliti anasaliti, mteka nyara anateka nyara.

Elamu, shambulia! Umedi, izunguke kwa jeshi!

Nitakomesha huzuni zote alizosababisha.

3 Katika hili mwili wangu umeteswa na maumivu,

maumivu makali ya ghafula yamenishika,

kama yale ya mwanamke mwenye utungu wa kuzaa.

Nimeduwazwa na lile ninalolisikia,

nimeshangazwa na lile ninaloliona.

4 Moyo wangu unababaika,

woga unanifanya nitetemeke,

gizagiza la jioni nililolitamani sana,

limekuwa hofu kuu kwangu.

5 Wanaandaa meza,

wanatandaza mazulia,

wanakula, wanakunywa!

Amkeni, enyi maafisa,

zitieni ngao mafuta!

6 Hili ndilo Bwana analoniambia:

“Nenda, weka mlinzi,

na atoe taarifa ya kile anachokiona.

7 Anapoona magari ya vita

pamoja na kundi la farasi,

wapanda punda au wapanda ngamia,

na awe macho, awe macho kikamilifu.”

8 Naye mlinzi alipaza sauti,

“Mchana baada ya mchana, bwana wangu, ninasimama katika mnara wa ulinzi,

kila usiku ninakaa mahali pangu nilipoamriwa.

9 Tazama, yuaja mtu anayepanda gari la vita

pamoja na kundi la farasi.

Naye anajibu:

‘Babeli umeanguka, umeanguka!

Vinyago vyote vya miungu yake

vimelala chini vikiwa vimevunjwa!’ ”

10 Ee watu wangu, mliopondwa kwenye sakafu ya kupuria,

ninawaambia kile nilichokisikia

kutoka kwa Bwana Mwenye Nguvu Zote,

kutoka kwa Mungu wa Israeli.

11 Neno kuhusu Duma:

Mtu fulani ananiita kutoka Seiri,

“Mlinzi, usiku utaisha lini?

Mlinzi, usiku utaisha lini?”

12 Mlinzi anajibu,

“Asubuhi inakuja, lakini pia usiku.

Kama ungeliuliza, basi uliza;

bado na urudi tena.”

13 Neno kuhusu Arabia:

Enyi misafara ya Wadedani,

mnaopiga kambi katika vichaka vya Arabia,

14 leteni maji kwa wenye kiu,

ninyi mnaoishi Tema,

leteni chakula kwa ajili ya wakimbizi.

15 Wanaukimbia upanga,

kutoka upanga uliochomolewa alani,

kutoka upinde uliopindwa,

na kutoka kwenye joto la vita.

16 Hili ndilo Bwana analoniambia: “Katika muda wa mwaka mmoja, kama vile mtumishi aliyefungwa na mkataba angeihesabu, majivuno yote ya Kedari yatafikia mwisho. 17 Wanaume wavutao pinde walionusurika, mashujaa wa Kedari, watakuwa wachache.” Bwana, Mungu wa Israeli, amesema.