Mithali za Solomoni (continued)

984 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Mithali 19–20

1 Afadhali mtu maskini ambaye mwenendo wake hauna lawama,

kuliko mpumbavu ambaye midomo yake imepotoka.

2 Sio vizuri kuwa na juhudi bila maarifa,

wala kufanya haraka na kuikosa njia.

3 Upumbavu wa mtu mwenyewe huharibu maisha yake

hata hivyo moyo wake humkasirikia Bwana.

4 Mali huleta marafiki wengi,

bali rafiki wa mtu maskini humwacha.

5 Shahidi wa uongo hataacha kuadhibiwa,

naye amwagaye uongo hataachwa huru.

6 Wengi hujipendekeza kwa mtawala

na kila mmoja ni rafiki wa mtu atoaye zawadi.

7 Mtu maskini huepukwa na ndugu zake wote:

Je, marafiki zake watamkwepa kiasi gani!

Ingawa huwafuata kwa kuwasihi,

hawapatikani popote.

8 Yeye apataye hekima huipenda nafsi yake mwenyewe,

yeye ahifadhiye ufahamu hustawi.

9 Shahidi wa uongo hataacha kuadhibiwa,

naye amwagaye uongo ataangamia.

10 Haistahili mpumbavu kuishi katika anasa,

itakuwa vibaya kiasi gani

kwa mtumwa kuwatawala wakuu.

11 Hekima ya mtu humpa uvumilivu,

ni kwa utukufu wake kusamehe makosa.

12 Ghadhabu ya mfalme ni kama mngurumo wa simba,

bali wema wake ni kama umande juu ya nyasi.

13 Mwana mpumbavu ni maangamizi ya babaye,

naye mke mgomvi ni kama kutonatona kusikoisha.

14 Nyumba na mali hurithiwa kutoka kwa wazazi,

bali mke mwenye busara hutoka kwa Bwana.

15 Uvivu huleta usingizi mzito,

naye mtu mzembe huona njaa.

16 Yeye ambaye hutii mafundisho huulinda uhai wake,

bali yeye anayezidharau njia zake atakufa.

17 Yeye amhurumiaye maskini humkopesha Bwana,

naye atamtuza kwa aliyotenda.

18 Mrudi mwanao, kwa maana katika hiyo kuna tumaini,

usiwe mshirika katika mauti yake.

19 Mtu mwenye kukasirika haraka ni lazima atapata adhabu yake,

kama utamwokoa, itakubidi kufanya hivyo tena.

20 Sikiliza mashauri na ukubali mafundisho,

nawe mwishoni utakuwa na hekima.

21 Kuna mipango mingi ndani ya moyo wa mtu,

lakini kusudi la Bwana ndilo litakalosimama.

22 Lile mtu alionealo shauku ni upendo usio na mwisho,

afadhali kuwa maskini kuliko kuwa mwongo.

23 Kumcha Bwana huongoza kwenye uzima,

kisha mtu hupumzika akiwa ameridhika,

bila kuguswa na shida.

24 Mtu mvivu hutumbukiza mkono wake kwenye sahani,

lakini hawezi hata kuupeleka kwenye kinywa chake!

25 Mpige mwenye mzaha, naye mjinga atajifunza busara,

mkemee mwenye ufahamu naye atapata maarifa.

26 Yeye amwibiaye baba yake na kumfukuza mama yake

ni mwana aletaye aibu na fedheha.

27 Mwanangu, ukiacha kusikiliza mafundisho,

utatangatanga mbali na maneno ya maarifa.

28 Shahidi mla rushwa hudhihaki hukumu

na kinywa cha mtu mwovu humeza ubaya kwa upesi.

29 Adhabu zimeandaliwa kwa ajili ya wenye dhihaka

na mapigo kwa ajili ya migongo ya wapumbavu.

20:1 Mvinyo ni mdhihaki na kileo ni mgomvi;

yeyote apotoshwaye navyo hana hekima.

2 Ghadhabu ya mfalme ni kama ngurumo ya simba;

yeye amkasirishaye hupoteza uhai wake.

3 Ni kwa heshima ya mtu kujitenga ugomvi,

bali kila mpumbavu ni mwepesi kugombana.

4 Mvivu halimi kwa majira;

kwa hiyo wakati wa mavuno hutazama

lakini hapati chochote.

5 Makusudi ya moyo wa mwanadamu ni maji yenye kina,

lakini mtu mwenye ufahamu huyachota.

6 Watu wengi hujidai kuwa na upendo usiokoma,

bali mtu mwaminifu ni nani awezaye kumpata?

7 Mtu mwenye haki huishi maisha yasiyo na lawama,

wamebarikiwa watoto wake baada yake.

8 Wakati mfalme aketipo katika kiti chake cha enzi kuhukumu,

hupepeta ubaya wote kwa macho yake.

9 Ni nani awezaye kusema, “Nimeuweka moyo wangu safi;

mimi ni safi na sina dhambi?”

10 Mawe ya kupimia yaliyo tofauti na vipimo tofauti,

Bwana huchukia vyote viwili.

11 Hata mtoto hujulikana kwa matendo yake,

kama tabia yake ni safi na adili.

12 Masikio yasikiayo na macho yaonayo,

Bwana ndiye alivifanya vyote viwili.

13 Usiupende usingizi la sivyo utakuwa maskini,

uwe macho nawe utakuwa na chakula cha akiba.

14 “Haifai, haifai!” asema mnunuzi,

kisha huondoka akijisifia ununuzi wake.

15 Dhahabu kunayo, na marijani kwa wingi,

lakini midomo inenayo maarifa

ni kito cha thamani kilicho adimu.

16 Chukua vazi la yule awekaye dhamana

kwa ajili ya mgeni;

lishikilie iwe dhamana kama anafanya hivyo

kwa ajili ya mwanamke mpotovu.

17 Chakula kilichopatikana kwa hila ni kitamu kwa mwanadamu,

bali huishia na kinywa kilichojaa changarawe.

18 Fanya mipango kwa kutafuta mashauri,

ukipigana vita, tafuta maelekezo.

19 Maneno ya kusengenya husababisha kutokuaminika,

kwa hiyo mwepuke mtu anayezungumza kupita kiasi.

20 Ikiwa mtu atamlaani baba yake au mama yake,

taa yake itazimwa katika giza nene.

21 Urithi upatikanao haraka mwanzoni,

hautabarikiwa mwishoni.

22 Usiseme, “Nitakulipiza kwa ajili ya kosa hili!”

Mngojee Bwana, naye atakuokoa.

23 Bwana anachukia sana mawe ya kupimia ya udanganyifu,

nazo mizani zisizo halali hazimpendezi.

24 Hatua za mtu huongozwa na Bwana.

Anawezaje basi mtu yeyote kuelewa njia yake mwenyewe?

25 Ni mtego kwa mtu kuweka wakfu kitu kwa haraka

na baada ya kitambo kidogo kufikiria tena nadhiri zake.

26 Mfalme mwenye hekima hupepeta waovu,

hulipitisha gurudumu la kupuria juu yao.

27 Taa ya Bwana huchunguza roho ya mwanadamu,

huchunguza utu wake wa ndani.

28 Upendo na uaminifu humweka mfalme salama,

kwa njia ya upendo, kiti chake cha enzi huwa salama.

29 Utukufu wa vijana ni nguvu zao,

mvi ni fahari ya uzee.

30 Mapigo na majeraha huusafisha ubaya,

nayo michapo hutakasa utu wa ndani.