Mithali za Solomoni (continued)

984 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Mithali 17–18

1 Afadhali kula ukoko mkavu ukiwa na amani na utulivu

kuliko kukaa kwenye nyumba ya karamu kukiwa na magomvi.

2 Mtumishi mwenye hekima atatawala juu ya mwana aaibishaye,

naye atashirikiana katika urithi kama mmoja wa hao ndugu.

3 Kalibu ni kwa ajili ya fedha na tanuru ni kwa ajili ya dhahabu,

bali Bwana huujaribu moyo.

4 Mtu mwovu husikiliza midomo mibaya;

mwongo husikiliza kwa makini ulimi wa madhara.

5 Yeye anaye mdhihaki maskini huonyesha dharau kwa Muumba wake;

yeyote afurahiaye maafa hataepuka kuadhibiwa.

6 Wana wa wana ni taji la wazee,

nao wazazi ni fahari ya watoto wao.

7 Midomo yenye uwezo wa ushawishi haimfai mpumbavu:

je, ni mibaya kiasi gani zaidi midomo ya uongo kwa mtawala!

8 Kipawa ni kama kito cha thamani machoni pake yeye aliye nacho;

kokote kigeukiapo, hufanikiwa.

9 Yeye anayesamehe kosa hudumisha upendo,

bali yeyote arudiaye jambo hutenganisha marafiki wa karibu.

10 Karipio humwingia sana mtu mwenye kutambua

kuliko mapigo mia kwa mpumbavu.

11 Mtu mbaya hupenda kuasi tu;

mjumbe asiye na huruma atatumwa dhidi yake.

12 Ni afadhali ukutane na dubu aliyenyangʼanywa watoto wake,

kuliko mpumbavu katika upumbavu wake.

13 Ikiwa mtu atalipa baya kwa jema,

kamwe ubaya hautaondoka katika nyumba yake.

14 Kuanzisha ugomvi ni kama kutoboa bwawa la maji;

kwa hiyo acha jambo hilo kabla mabishano hayajaanza.

15 Yeye asemaye kuwa asiye na haki ana haki,

naye asemaye kuwa mwenye haki hana haki:

Bwana huwachukia sana wote wawili.

16 Fedha ina faida gani mikononi mwa mpumbavu,

wakati yeye hana haja ya kupata hekima?

17 Rafiki hupenda wakati wote

naye ndugu amezaliwa kwa ajili ya wakati wa shida.

18 Mtu mjinga hupana mkono ili kuweka rehani,

naye huweka dhamana kwa jirani yake.

19 Yeye apendaye ugomvi apenda dhambi;

naye ainuaye sana lango lake hutafuta uharibifu.

20 Mtu mwenye moyo mpotovu hawezi kufanikiwa;

naye ambaye ulimi wake ni mdanganyifu huanguka kwenye taabu.

21 Kuwa na mwana mpumbavu huleta huzuni;

hakuna furaha kwa baba wa mpumbavu.

22 Moyo wenye furaha ni dawa nzuri,

bali roho iliyopondeka hukausha mifupa.

23 Mtu mwovu hukubali rushwa kwa siri

ili kupotosha njia ya haki.

24 Mtu wa ufahamu huitazama hekima,

lakini macho ya mpumbavu huhangaika

hadi kwenye miisho ya dunia.

25 Mwana mpumbavu huleta huzuni kwa baba yake

na uchungu kwa yeye aliyemzaa.

26 Si vizuri kumwadhibu mtu asiye na hatia,

au kuwapiga sana maafisa kwa ajili ya uadilifu wao.

27 Mtu mwenye maarifa hutumia maneno kwa kujizuia,

naye mtu mwenye ufahamu ana moyo wa utulivu.

28 Hata mtu mpumbavu hudhaniwa kuwa na hekima kama akinyamaza,

na mwenye ufahamu kama akiuzuia ulimi wake.

18:1 Mtu ajitengaye na wengine

hufuata matakwa yake mwenyewe;

hupiga vita kila shauri jema.

2 Mpumbavu hafurahii ufahamu,

bali hufurahia kutangaza

maoni yake mwenyewe.

3 Wakati uovu unapokuja, dharau huja pia,

pamoja na aibu huja lawama.

4 Maneno ya kinywa cha mwanadamu ni kina cha maji,

bali chemchemi ya hekima ni kijito kinachobubujika.

5 Sio vizuri kumpendelea mtu mwovu,

au kumnyima haki asiye na hatia.

6 Midomo ya mpumbavu humletea ugomvi

na kinywa chake hualika kipigo.

7 Kinywa cha mpumbavu ni uharibifu wake

na midomo yake ni mtego kwa nafsi yake.

8 Maneno ya mchongezi ni kama chakula kitamu;

huingia sehemu za ndani sana za mtu.

9 Mtu aliye mlegevu katika kazi yake

ni ndugu na yule anayeharibu.

10 Jina la Bwana ni ngome imara,

wenye haki huikimbilia na kuwa salama.

11 Mali ya tajiri ni mji wake wenye ngome,

wanaudhania kuwa ukuta usioweza kurukwa.

12 Kabla ya anguko moyo wa mtu hujaa kiburi,

bali unyenyekevu hutangulia heshima.

13 Yeye ajibuye kabla ya kusikiliza,

huo ni upumbavu wake na aibu yake.

14 Roho ya mtu itastahimili katika ugonjwa

bali roho iliyovunjika ni nani awezaye kuistahimili?

15 Moyo wa mwenye ufahamu hujipatia maarifa,

masikio ya mwenye hekima huyatafuta maarifa.

16 Zawadi humfungulia njia mtoaji,

nayo humleta mbele ya wakuu.

17 Yeye aliye wa kwanza kuleta mashtaka huonekana sahihi,

hadi mwingine ajitokezapo na kumuuliza maswali.

18 Kupiga kura hukomesha mashindano

na kutenganisha wapinzani wakuu wanaopingana.

19 Ndugu aliyechukizwa ni mgumu kuridhika

kuliko mji uliozungushiwa ngome,

nayo mabishano ni kama malango

ya ngome yenye makomeo.

20 Tumbo la mtu litajaa kutokana na tunda la kinywa chake,

atashibishwa mavuno yanayotokana na midomo yake.

21 Mauti na uzima viko katika uwezo wa ulimi,

nao waupendao watakula matunda yake.

22 Apataye mke apata kitu chema

naye ajipatia kibali kwa Bwana.

23 Mtu maskini huomba kuhurumiwa

bali tajiri hujibu kwa ukali.

24 Mtu mwenye marafiki wengi wanaweza kumharibu,

bali yuko rafiki aambatanaye na mtu kwa karibu kuliko ndugu.