Mithali za Solomoni (continued)

984 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Mithali 12–13

1 Yeyote apendaye kuadibishwa hupenda maarifa,

bali yeye achukiaye kuonywa ni mpumbavu.

2 Mtu mwema hupata kibali kutoka kwa Bwana,

bali Bwana humhukumu mwenye hila.

3 Mtu hathibitiki kutokana na uovu,

bali mwenye haki hataondolewa.

4 Mke mwenye tabia nzuri ni taji ya mumewe,

bali aaibishaye ni kama uozo

katika mifupa ya mumewe.

5 Mipango ya mtu mwadilifu ni ya haki,

bali ushauri wa mwovu ni udanganyifu.

6 Maneno ya waovu huotea kumwaga damu,

bali maneno ya waadilifu huwaokoa.

7 Watu waovu huondolewa na kutoweka,

bali nyumba ya mwenye haki husimama imara.

8 Mtu husifiwa kulingana na hekima yake,

bali watu wenye akili zilizopotoka hudharauliwa.

9 Heri mtu wa hali ya chini mwenye mtumishi,

kuliko kujifanya mtu wa hali ya juu nawe huna chakula.

10 Mtu mwenye haki hujali mahitaji ya mnyama wake,

bali matendo ya huruma ya mwovu ni ukatili.

11 Yeye alimaye shamba lake atakuwa na chakula tele,

bali yeye afuataye mambo ya upuzi hana akili.

12 Waovu hutamani mateka ya watu wabaya,

bali shina la mwenye haki hustawi.

13 Mtu mwovu hunaswa kwa mazungumzo yake ya dhambi,

bali mwenye haki huepuka taabu.

14 Kutokana na tunda la midomo yake

mtu hujazwa na mambo mema,

hakika kama ilivyo kazi ya mikono yake humtunza.

15 Njia ya mpumbavu huonekana sawa

machoni pake mwenyewe,

bali mtu mwenye hekima husikiliza ushauri.

16 Mpumbavu huonyesha kuudhika kwake mara moja,

bali mtu wa busara hupuuza matukano.

17 Shahidi wa kweli hutoa ushuhuda wa kuaminika,

bali shahidi wa uongo husema uongo.

18 Maneno ya kipumbavu huchoma kama upanga,

bali ulimi wa mwenye hekima huleta uponyaji.

19 Midomo isemayo kweli hudumu milele,

bali ulimi wa uongo hudumu kwa muda mfupi tu.

20 Upo udanganyifu katika mioyo

ya wale ambao hupanga mabaya,

bali kuna furaha kwa wale wanaoleta amani.

21 Hakuna dhara linalompata mwenye haki,

bali waovu wana taabu nyingi.

22 Bwana anachukia sana midomo idanganyayo,

bali hufurahia watu ambao ni wa kweli.

23 Mtu mwenye busara hujihifadhia maarifa yeye mwenyewe,

bali moyo wa wapumbavu hububujika upumbavu.

24 Mikono yenye bidii itatawala,

bali uvivu huishia katika kazi za utumwa.

25 Moyo wa wasiwasi humlemea mtu,

bali neno la huruma humfurahisha.

26 Mtu mwenye haki ni mwangalifu katika urafiki,

bali njia ya waovu huwapotosha.

27 Mtu mvivu haoki mawindo yake,

bali mtu mwenye bidii ana mali za thamani.

28 Katika njia ya haki kuna uzima;

katika mapito hayo kuna maisha ya milele.

13:1 Mwana mwenye hekima husikia mafundisho ya babaye,

bali mwenye dharau hasikilizi maonyo.

2 Kutoka tunda la midomo yake mtu hufurahia mambo mema,

bali wasio waaminifu wanatamani sana jeuri.

3 Yeye alindaye midomo yake hulinda nafsi yake,

bali yeye asemaye kwa haraka ataangamia.

4 Mvivu hutamani sana na hapati kitu,

bali nafsi ya mwenye bidii

hutoshelezwa kikamilifu.

5 Mwenye haki huchukia uongo,

bali waovu huleta aibu na fedheha.

6 Haki humlinda mtu mwadilifu,

bali uovu humwangusha mwenye dhambi.

7 Mtu mmoja hujifanya tajiri, kumbe hana chochote;

mwingine hujifanya maskini, kumbe ana utajiri mwingi.

8 Utajiri wa mtu waweza kukomboa maisha yake,

bali mtu maskini hasikii kitisho.

9 Nuru ya mwenye haki hungʼaa sana,

bali taa ya mwovu itazimwa.

10 Kiburi huzalisha magomvi tu,

bali hekima hupatikana kwa wale wanaozingatia ushauri.

11 Fedha isiyo ya halali hupungua,

bali yeye akusanyaye fedha kidogo kidogo huongezeka.

12 Kilichotarajiwa kikikawia kuja moyo huugua,

bali tumaini lililotimizwa ni mti wa uzima.

13 Yeye anayedharau mafundisho anajiletea maangamizi,

bali yeye anayeheshimu agizo hupewa tuzo.

14 Mafundisho ya mwenye busara ni chemchemi ya uzima,

ili kumwepusha mtu na mitego ya mauti.

15 Ufahamu mzuri hupata upendeleo,

bali njia ya asiye mwaminifu ni ngumu.

16 Kila mwenye busara hutenda kwa maarifa,

bali mpumbavu hudhihirisha upumbavu wake.

17 Mjumbe mwovu huanguka kwenye taabu,

bali mjumbe mwaminifu huleta uponyaji.

18 Yeye anayedharau maonyo hupata umaskini na aibu,

bali yeye anayekubali maonyo huheshimiwa.

19 Tarajio lililotimizwa ni tamu kwa nafsi,

bali wapumbavu huchukia sana kuacha ubaya.

20 Yeye atembeaye na mwenye hekima atapata hekima,

bali rafiki wa mpumbavu hupata madhara.

21 Balaa humwandama mtenda dhambi,

bali mafanikio ni thawabu kwa mwenye haki.

22 Mtu mwema huwaachia wana wa wanawe urithi,

bali mali ya wenye dhambi imehifadhiwa

kwa ajili ya wenye haki.

23 Shamba la mtu maskini laweza kuzalisha chakula kingi,

bali dhuluma hukifutilia mbali.

24 Yeye aizuiaye fimbo yake hampendi mwanawe,

bali yeye ampendaye

huwa mwangalifu kumwadibisha.

25 Mwenye haki hula mpaka akaridhisha moyo wake,

bali tumbo la mwovu hutaabika kwa njaa.