Mithali za Solomoni

984 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Mithali 10–11

1 Mithali za Solomoni:

Mwana mwenye hekima

huleta furaha kwa baba yake,

lakini mwana mpumbavu

huleta huzuni kwa mama yake.

2 Hazina zilizopatikana kwa njia mbaya hazifai,

lakini uadilifu huokoa kutoka mautini.

3 Bwana hawaachi waadilifu kukaa njaa,

lakini hupinga tamaa ya mtu mwovu.

4 Mikono mivivu hufanya mtu kuwa maskini

lakini mikono yenye bidii huleta utajiri.

5 Yeye akusanyaye mazao wakati wa kiangazi

ni mwana mwenye hekima,

lakini yeye alalaye wakati wa mavuno

ni mwana mwenye kuaibisha.

6 Baraka huwa taji kichwani mwa mwenye haki,

lakini jeuri hufunika kinywa cha mwovu.

7 Kumbukumbu ya mwenye haki itakuwa baraka,

lakini jina la mwovu litaoza.

8 Mwenye hekima moyoni hupokea maagizo,

lakini mpumbavu apayukaye huangamia.

9 Mtu mwadilifu hutembea salama,

lakini mtu aendaye katika njia zilizopotoka atagunduliwa.

10 Yeye akonyezaye kwa nia mbaya husababisha huzuni,

naye mpumbavu apayukaye huangamia.

11 Kinywa cha mwenye haki ni chemchemi ya uzima,

lakini jeuri hufunika kinywa cha mwovu.

12 Chuki huchochea faraka,

lakini upendo husitiri mabaya yote.

13 Hekima hupatikana katika midomo ya wenye kupambanua,

lakini fimbo ni kwa ajili ya mgongo wake asiye na ufahamu.

14 Wenye hekima huhifadhi maarifa,

bali kinywa cha mpumbavu hualika maangamizi.

15 Mali ya tajiri ni mji wake wenye ngome,

bali ufukara ni maangamizi ya maskini.

16 Ujira wa wenye haki huwaletea uzima,

lakini mapato ya waovu huwaletea adhabu.

17 Anayekubali kuadibishwa yuko katika njia ya uzima,

lakini yeyote anayepuuza maonyo hupotosha wengine.

18 Yeye afichaye chuki yake ana midomo ya uongo,

na yeyote anayeeneza uchonganishi ni mpumbavu.

19 Wakati maneno ni mengi, dhambi haikosekani,

lakini yeye ambaye huzuia ulimi wake ni mwenye busara.

20 Ulimi wa mwenye haki ni fedha iliyo bora,

bali moyo wa mwovu una thamani ndogo.

21 Midomo ya mwenye haki hulisha wengi,

lakini wapumbavu hufa kwa kukosa ufahamu.

22 Baraka ya Bwana hutajirisha,

wala haichanganyi huzuni.

23 Mpumbavu hufurahia tabia mbaya,

lakini mtu mwenye ufahamu hupendezwa na hekima.

24 Kile anachoogopa mwovu ndicho kitakachompata;

kile anachoonea shauku mwenye haki atapewa.

25 Tufani inapopita, waovu hutoweka,

lakini wenye haki husimama imara milele.

26 Kama siki ilivyo kwa meno na moshi kwa macho,

ndivyo alivyo mvivu kwa wale waliomtuma.

27 Kumcha Bwana huongeza urefu wa maisha,

lakini miaka ya mwovu inafupishwa.

28 Tarajio la mwenye haki ni furaha,

bali matumaini ya mwovu huwa si kitu.

29 Njia ya Bwana ni kimbilio kwa wenye haki,

lakini ni maangamizi ya wale watendao mabaya.

30 Kamwe wenye haki hawataondolewa,

bali waovu hawatasalia katika nchi.

31 Kinywa cha mwenye haki hutoa hekima,

bali ulimi wa upotovu utakatwa.

32 Midomo ya wenye haki inajua kile kinachofaa,

bali kinywa cha mwovu hujua kile kilichopotoka tu.

11:1 Bwana huchukia sana mizani za udanganyifu,

bali vipimo sahihi ni furaha yake.

2 Kiburi kinapokuja, ndipo huja aibu,

bali unyenyekevu huja na hekima.

3 Uadilifu wa wenye haki huwaongoza,

bali wasio waaminifu huharibiwa na hila yao.

4 Utajiri haufaidi kitu katika siku ya ghadhabu,

bali haki huokoa kutoka mautini.

5 Haki ya wasio na lawama, huwatengenezea njia iliyonyooka,

bali waovu huangushwa kwa uovu wao wenyewe.

6 Haki ya wanyofu huwaokoa,

bali wasio waaminifu hunaswa na tamaa mbaya.

7 Wakati mtu mwovu anapokufa, matumaini yake hutoweka;

yote aliyoyatazamia kutokana na nguvu zake huwa si kitu.

8 Mtu mwenye haki huokolewa kutoka taabu,

naye mtu mwovu huingia humo badala yake.

9 Kwa kinywa chake mtu asiyemwamini Mungu

humwangamiza jirani yake,

bali kwa maarifa mwenye haki huokolewa.

10 Wakati mwenye haki anapofanikiwa, mji hufurahi;

mwovu atowekapo, kuna kelele za furaha.

11 Kutokana na baraka ya mtu mnyofu mji hukwezwa,

bali kwa kinywa cha mwovu mji huharibiwa.

12 Mtu asiye na akili humdharau jirani yake,

bali mtu mwenye ufahamu huuzuia ulimi wake.

13 Masengenyo husaliti tumaini,

bali mtu mwaminifu hutunza siri.

14 Pasipo ushauri wa hekima taifa huanguka,

bali washauri wengi hufanya ushindi uwe wa hakika.

15 Yeye amdhaminiye mgeni hakika atateseka,

bali yeyote akataaye kuunga mkono dhamana ni salama.

16 Mwanamke mwenye moyo wa huruma hupata heshima,

bali wanaume wakorofi hupata mali tu.

17 Mwenye huruma hujinufaisha mwenyewe,

bali mkatili hujiletea taabu mwenyewe.

18 Mtu mwovu hupata ujira wa udanganyifu,

bali yeye apandaye haki huvuna tuzo ya uhakika.

19 Mtu mwenye haki kweli kweli hupata uzima,

bali yeye afuatiliaye ubaya huendea kifo chake.

20 Bwana huwachukia sana watu wenye moyo wa upotovu,

bali hupendezwa na wale ambao njia zao hazina lawama.

21 Uwe na hakika na hili: Waovu hawataepuka kuadhibiwa,

bali wenye haki watakuwa huru.

22 Kama pete ya dhahabu katika pua ya nguruwe

ndivyo alivyo mwanamke mzuri ambaye hana busara.

23 Shauku ya mwenye haki huishia tu kwenye mema,

bali tumaini la mwovu huishia tu kwenye ghadhabu.

24 Kuna mtu atoaye kwa ukarimu, hata hivyo hupata zaidi,

mwingine huzuia, lakini huwa maskini.

25 Mtu mkarimu atastawi;

yeye awaburudishaye wengine

ataburudishwa mwenyewe.

26 Watu humlaani mtu awanyimae watu nafaka,

bali baraka itamkalia kichwani kama taji

yeye aliye radhi kuiuza.

27 Yeye atafutaye mema hupata ukarimu,

bali ubaya huja kwake yeye autafutaye.

28 Yeyote ategemeaye utajiri wake ataanguka,

bali mwenye haki atastawi kama jani bichi.

29 Yeye aletaye taabu kwa jamaa yake atarithi tu upepo,

naye mpumbavu atakuwa mtumishi wa wenye hekima.

30 Tunda la mwenye haki ni mti wa uzima,

naye mwenye hekima huvuta roho za watu.

31 Kama wenye haki watapokea ujira wao duniani,

si zaidi sana yule asiyemcha Mungu na mwenye dhambi?