Sehemu ya 7: Safari ya Mwisho ya Paulo na Kukamilika kwa Kanoni

Tangu mwanzo wa safari ya tano na ya mwisho ya Paulo hadi kukamilishwa kwa kanoni ya Andiko lote, pamoja na muhtasari wa historia ya kanisa la Mkristo hadi wakati wa sasa.

Paulo Anawaandikia Waebrania

Paulo, akiwa Italia akimngojea Timotheo, anaandika ufunguo wa Agano la Kale, yaani barua kwa Waebrania. Anaiandika ili kuwathibitishia Wayahudi, kutokana na Maandiko yao wenyewe, ubinadamu, uungu, upatanisho na maombezi ya Kristo, ubora wa injili kuliko Sheria, na kusudi na mpango halisi wa taratibu zilizowekwa na Mose.

62 BK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Mafunuo Yote Mawili Yanatoka kwa Mungu Mmoja

Paulo anaanza kwa kusisitiza kwamba mafunuo ya Kiyahudi na ya Kikristo yalitolewa na Mungu yuleyule, na anahitimisha kwamba kwa hiyo lazima yapatane na kufafanua kila moja jingine. Injili inatangazwa kuwa bora zaidi, kwa sababu ilitolewa na Mwana wa Mungu aliyeahidiwa, aliyewekwa kuwa mrithi wa vitu vyote. Yeye ndiye utukufu uliofunuliwa na mfano uliotwaa mwili wa Baba Mwenyezi asiyeonekana, naye anautegemeza ulimwengu kwa nguvu zake. Baada ya kujitoa mwenyewe kuwa dhabihu ya upatanisho kwa ajili ya dhambi za wanadamu, alikuwa amerudi katika hali yake ya kibinadamu kwenye utukufu mkuu pamoja na Baba, ambao ulikuwa wake katika hali yake ya kimungu kabla ya ulimwengu kuumbwa.

Waebrania 1:1–3

1 Zamani Mungu alisema na baba zetu kwa njia ya manabii mara nyingi na kwa njia mbalimbali, 2 lakini katika siku hizi za mwisho anasema nasi kwa njia ya Mwanawe, ambaye amemweka kuwa mrithi wa vitu vyote, na ambaye kupitia kwake aliuumba ulimwengu. 3 Mwana ni mngʼao wa utukufu wa Mungu na mfano halisi wa nafsi yake, akivihifadhi vitu vyote kwa neno lake lenye uweza. Akiisha kufanya utakaso kwa ajili ya dhambi, aliketi mkono wa kuume wa Aliye Mkuu huko mbinguni.

Mwana Ni Mkuu Kuliko Malaika

Ili kuthibitisha hoja yake kwamba Kristo ni mkuu kuliko viumbe vyote, Paulo anasisitiza asili ya uungu ya Mwana wa Mungu, ambayo ni tofauti na asili ya malaika na iko juu yake. Jina lake ni kuu kuliko majina yao kwa urithi, au kwa haki yake ya asili (Zaburi 2:2). Anaabudiwa na malaika (Zaburi 97:7), ambao ni wahudumu na watumishi wake wa kiroho (Zaburi 104:4). Utawala wake unaenea katika malimwengu yote mawili na unadumu milele. Kwa sababu ya kupenda kwake haki, kulikodhihirishwa kwa kufanyika kwake mwanadamu na kwa kifo chake, ametiwa mafuta katika asili yake ya kibinadamu kwa karama za Roho Mtakatifu kuliko manabii, makuhani na wafalme wote waliomtangulia, naye anaunganisha nyadhifa hizo tatu katika nafsi yake mwenyewe. Ili kuthibitisha zaidi ukuu wa Kristo, na kuondoa dhana potovu kwamba malaika walisaidia kuumba ulimwengu, Paulo anathibitisha kwa maneno ya Daudi (Zaburi 102:25–27) kwamba Kristo aliumba mbingu na dunia. Ataziondoa na kuweka mbingu mpya na dunia mpya mahali pake, lakini yeye atabaki bila kubadilika na kuwa yuleyule katika asili yake milele yote. Kristo ni mkuu kuliko malaika, kwa maana Baba mwenyewe hajampa yeyote kati yao hadhi ya Mwana (Zaburi 110:1) na mamlaka juu ya vyote: wao ni roho watumikao, walio chini yake na anaowatumia kwa manufaa ya wanadamu.

Waebrania 1:4–14

4 Kwa hiyo alifanyika bora kuliko malaika, kama jina alilorithi lilivyo bora kuliko lao.

5 Kwa maana ni malaika yupi ambaye wakati wowote Mungu alipata kumwambia,

“Wewe ni Mwanangu;

leo mimi nimekuzaa?”

Au tena,

“Mimi nitakuwa Baba yake,

naye atakuwa Mwanangu?”

6 Tena, Mungu amletapo mzaliwa wake wa kwanza ulimwenguni, anasema,

“Malaika wote wa Mungu na wamsujudu.”

7 Anenapo kuhusu malaika asema,

“Huwafanya malaika wake kuwa pepo,

watumishi wake kuwa miali ya moto.”

8 Lakini kwa habari za Mwana asema,

“Kiti chako cha enzi, Ee Mungu,

kitadumu milele na milele,

nayo haki itakuwa fimbo ya utawala

ya ufalme wako.

9 Umependa haki na kuchukia uovu;

kwa hiyo Mungu, Mungu wako,

amekuweka juu ya wenzako

kwa kukupaka mafuta ya furaha.”

10 Pia asema,

“Hapo mwanzo, Ee Bwana, uliweka misingi ya dunia,

nazo mbingu ni kazi ya mikono yako.

11 Hizo zitatoweka, lakini wewe utadumu;

zote zitachakaa kama vazi.

12 Utazikungʼutakungʼuta kama joho,

nazo zitachakaa kama vazi.

Lakini wewe hubadiliki,

nayo miaka yako haikomi kamwe.”

13 Je, ni kwa malaika yupi ambaye Mungu amepata kumwambia wakati wowote,

“Keti mkono wangu wa kuume,

hadi nitakapowaweka adui zako

chini ya miguu yako”?

14 Je, malaika wote si roho watumikao, waliotumwa kuwahudumia wale watakaourithi wokovu?

Onyo la Kuitii Injili

Akitumia hoja iliyotangulia, Paulo anaonyesha kwamba injili ya Kristo inadai usikivu na utii wa hali ya juu kabisa. Kutokana na adhabu zilizowapata wana wa Israeli wa kale walioiacha imani, anahitimisha kwamba wale wanaoiacha injili wanakabiliwa na hukumu kubwa zaidi. Kwa maana injili ilitoa matumaini makubwa zaidi ya wokovu. Ilifunuliwa kwanza na Kristo mwenyewe, kisha ikathibitishwa kwa wanadamu na mitume waliokuwa wameipokea kutoka kwake, huku Mungu mwenyewe akiushuhudia ukweli wake kwa miujiza na kwa karama za Roho Mtakatifu wake. Ushuhuda huu ni mkuu kuliko ule wa malaika, kwa maana ulimwengu ujao, ambao injili inaahidi, haukuwekwa chini ya mamlaka ya malaika bali ya Kristo.

Waebrania 2:1–5

1 Kwa hiyo, imetupasa kuwa waangalifu sana kuhusu kile tulichosikia, ili tusije tukakiacha. 2 Kwa kuwa kama ujumbe ulionenwa na malaika ulikuwa imara, na kila uasi na kutokutii kulipata adhabu ya haki, 3 je, sisi tutapaje kupona kama tusipojali wokovu mkuu namna hii? Wokovu huu, ambao mwanzo ulitangazwa na Bwana, ulithibitishwa kwetu na wale waliomsikia. 4 Pia Mungu aliushuhudia kwa ishara, maajabu na kwa miujiza mbalimbali, na karama za Roho Mtakatifu alizozigawa kulingana na mapenzi yake.

5 Mungu hakuuweka ulimwengu ujao ambao tunanena habari zake chini ya malaika.

Kristo Afanywa Mdogo Kuliko Malaika

Akigusia pingamizi ambazo walimu wa Kiyahudi walitoa dhidi ya uungu wa Kristo, Paulo anathibitisha kutokana na maneno ya ufunuo wa Mungu (Zaburi 8:4–6) kwamba ilikuwa imetabiriwa kuwa yeye aliyekuwa Mungu angewatembelea wanadamu na kufanywa kuwa mdogo kuliko malaika, ili vitu vyote viwekwe chini ya mamlaka yake. Kwa sasa si vitu vyote vilivyo chini ya mamlaka yake, kwa kuwa wanadamu waovu na malaika waovu bado hawajatiishwa kwa nguvu zake. Lakini Yesu, akiwa katika umbo la mwanadamu, ameonja mauti kwa ajili ya kila mtu na amevikwa taji la utukufu na heshima, na mambo haya ni uthibitisho wa kutosha kwamba hatimaye nguvu zake zitashinda.

Waebrania 2:6–9

6 Lakini kuna mahali mtu fulani ameshuhudia akisema:

“Mwanadamu ni kitu gani hata unamfikiria,

binadamu ni nani hata unamjali?

7 Umemfanya chini kidogo kuliko malaika;

ukamvika taji ya utukufu na heshima,

8 nawe umeweka vitu vyote chini ya miguu yake.”

Kwa kuweka vitu vyote chini yake, Mungu hakuacha kitu chochote ambacho hakukiweka chini ya mwanadamu. Lakini kwa sasa, hatuoni kwamba kila kitu kiko chini yake. 9 Lakini twamwona Yesu, aliyefanywa chini kidogo kuliko malaika, sasa akiwa amevikwa taji ya utukufu na heshima kwa sababu alistahimili mauti, ili kwamba kwa neema ya Mungu apate kuonja mauti kwa ajili ya kila mtu.

Kwa Nini Kristo Alitwaa Asili Yetu

Paulo anaonyesha manufaa yaliyoletwa na Kristo kufanyika mwanadamu na kufa. Hii ndiyo njia ambayo Mungu aliweka kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu, ili yeye atakasaye, au afanyaye upatanisho, na wale wanaotakaswa wawe na asili moja. Kwa sababu hiyo, kama Daudi alivyotabiri (Zaburi 22:22, 26), haoni aibu kuwaita ndugu. Kwa kufanyika kwake mwanadamu, ndugu zake wanaingizwa katika uhusiano mpya na Baba yuleyule wa mbinguni, kama Isaya alivyotabiri (Isaya 8:18). Kwa kuwa watoto ambao Kristo angewaokoa walikuwa wanadamu wenye kufa, Kristo, ambaye angewafia, alipaswa kushiriki asili hiyo hiyo. Akiwa mwakilishi wao, angemshinda ibilisi, aliyekuwa na uwezo wa kuwaletea wanadamu wote dhambi na mauti, na kuwaweka huru kutoka katika utumwa wake. Kwa maana hakuwashika malaika ili awakomboe, bali aliwaokoa wazao wa Abrahamu kutoka katika maangamizi. Ilifaa Kristo afanywe kama ndugu zake, ili awe kuhani mkuu mwaminifu katika mambo ya Mungu, akizidumisha sheria zake, ibada yake, haki yake na rehema zake, na wakati huohuo kufanya upatanisho kwa ajili ya wanadamu. Anawaweka huru kutoka katika uovu na nguvu za dhambi, na kwa damu yake anawapatia urithi wa mbinguni. Kwa kuwa yeye mwenyewe amevumilia majaribu na mateso ya hali ya kibinadamu, anaweza kuwasaidia vizuri zaidi wale wanaojaribiwa, na kutathmini udhaifu na mapungufu ya hali hiyo. Hitimisho ni kwamba kufanyika kwake mwanadamu na kufa kwake si hoja ya kuonyesha kwamba yeye ni mdogo kuliko manabii au malaika: alitwaa asili ya mwanadamu kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu, bila kupunguza uungu wake kwa namna yoyote.

Waebrania 2:10–18

10 Ili kuwaleta wana wengi katika utukufu, ilifaa kwamba Mungu, ambaye ni kwa ajili yake na kupitia kwake kila kitu kimekuwepo, amkamilishe mwanzilishi wa wokovu wao kwa njia ya mateso. 11 Yeye awafanyaye watu kuwa watakatifu, pamoja na hao ambao hufanywa watakatifu, wote hutoka katika jamaa moja. Hivyo Yesu haoni aibu kuwaita ndugu zake. 12 Yeye husema,

“Nitalitangaza jina lako kwa ndugu zangu;

mbele ya kusanyiko nitaimba sifa zako.”

13 Tena,

“Nitaweka tumaini langu kwake.”

Tena anasema,

“Niko hapa, pamoja na watoto ambao Mungu amenipa.”

14 Basi kwa kuwa watoto wana nyama na damu, yeye pia alishiriki katika ubinadamu wao, ili kwa kifo chake, apate kumwangamiza huyo mwenye nguvu za mauti, yaani ibilisi, 15 na kuwaweka huru wale waliokuwa utumwani maisha yao yote kwa sababu ya kuogopa mauti. 16 Kwa kuwa ni dhahiri kwamba hakuja kusaidia malaika, bali uzao wa Abrahamu. 17 Kwa sababu hii ilibidi afanane na ndugu zake kwa kila hali, ili apate kuwa Kuhani Mkuu mwenye huruma na mwaminifu katika kumtumikia Mungu, ili pia apate kufanya upatanisho kwa ajili ya dhambi za watu. 18 Kwa kuwa yeye mwenyewe aliteswa alipojaribiwa, aweza kuwasaidia wale wanaojaribiwa.

Kristo Ni Mkuu Kuliko Mose

Baada ya kuthibitisha ukuu wa Kristo kuliko malaika, Paulo sasa anaonyesha kwamba, akiwa mtume na kuhani mkuu wa agano jipya, yeye ni mkuu kuliko Mose na Aroni, mitume na makuhani wakuu wa agano la kale. Mose alikuwa mwaminifu katika kuisimamia nyumba ya Mungu (Hesabu 12:7), yaani wana wa Israeli wa kale, akiwa mwalimu, mtoa sheria na nabii. Kupitia vielelezo na taratibu za ibada, alimshuhudia Yesu Kristo na injili yake. Kristo anastahili utukufu zaidi kuliko Mose, kwa sababu alikuwa Bwana na mjenzi wa nyumba ambayo Mose alikuwa mtumishi tu ndani yake. Wakristo sasa ni nyumba na familia ya Kristo, ikiwa wataendelea katika imani yake, kama vile Wayahudi watiifu walivyokuwa wanafunzi na nyumba ya Mose.

Waebrania 3:1–6

1 Kwa hiyo ndugu watakatifu, mnaoshiriki mwito wa mbinguni, mtafakarini Yesu, mtume na Kuhani Mkuu wa ukiri wetu. 2 Alikuwa mwaminifu kwa yeye aliyemweka, kama vile Mose alivyokuwa mwaminifu katika nyumba yote ya Mungu. 3 Yesu ameonekana anastahili heshima kubwa kuliko Mose, kama vile mjenzi wa nyumba alivyo wa heshima kubwa kuliko nyumba yenyewe. 4 Kwa kuwa kila nyumba hujengwa na mtu fulani, lakini Mungu ni mjenzi wa kila kitu. 5 Basi Mose kama mtumishi alikuwa mwaminifu katika nyumba yote ya Mungu, akishuhudia kwa yale ambayo yangetamkwa baadaye. 6 Lakini Kristo ni mwaminifu kama Mwana katika nyumba ya Mungu. Sisi ndio nyumba yake, kama tutashikilia sana ujasiri wetu na tumaini tunalojivunia.

Jihadharini na Moyo Usioamini

Paulo anatumia hoja hii kwa Waebrania kwa maneno ya Roho Mtakatifu (Zaburi 95:7–11), ambayo Daudi aliwaelekezea Wayahudi wa wakati wake. Kisha anawahimiza wajihadhari ili wao pia wasiwe na moyo mwovu wa kutokuamini, utakaowafanya waache injili ya Kristo. Wanapaswa kutiana moyo ili wasidanganywe na dhambi, wasije wakapendelea Misri kuliko Kanaani, na utumwa wa ulimwengu kuliko kumtumikia Mungu (Hesabu 14:3, 4). Ni wale tu wanaosimama imara katika imani wanaoweza kushiriki baraka za injili. Anaonyesha kutokana na maneno ya Roho Mtakatifu kwamba ni lazima wavumilie na kuyatii mara moja: Roho anawaita sasa kwa njia ya injili, kama alivyowaita wana wa Israeli wa zamani (Hesabu 13:26; 14:1–31), waingie katika pumziko. Wakati huo kulikuwa na mabaki walioamini, kama ilivyo sasa, na ahadi za Mungu zilitimizwa kwao. Wale walioasi na kutokuamini, baada ya kuona maonyesho ya nguvu za Mungu mara kwa mara, walizuiwa kwa kiapo wasiingie katika pumziko lililoahidiwa la Kanaani kwa sababu ya kutokuamini kwao (Yoshua 5:6), nao wakafa jangwani (Hesabu 14:29). Hapa Paulo anadokeza kwamba wazao wa Abrahamu kwa mwili walikuwa warithi wa agano lake kwa njia ya imani tu.

Waebrania 3:7–19

7 Kwa hiyo, kama Roho Mtakatifu asemavyo:

“Leo, kama mkiisikia sauti yake,

8 msiifanye mioyo yenu migumu,

kama mlivyofanya katika uasi,

wakati ule wa kujaribiwa jangwani,

9 ambapo baba zenu walinijaribu na kunipima

ingawa kwa miaka arobaini

walikuwa wameyaona matendo yangu.

10 Hiyo ndiyo sababu nilikasirikia kizazi kile,

nami nikasema, ‘Siku zote mioyo yao imepotoka,

nao hawajazijua njia zangu.’

11 Hivyo nikatangaza kwa kiapo katika hasira yangu,

‘Kamwe hawataingia rahani mwangu.’ ”

12 Ndugu zangu, angalieni, asiwepo miongoni mwenu mtu mwenye moyo mwovu usioamini, unaojitenga na Mungu aliye hai. 13 Lakini mtiane moyo mtu na mwenzake kila siku, maadamu iitwapo Leo, ili asiwepo hata mmoja wenu mwenye kufanywa mgumu kwa udanganyifu wa dhambi. 14 Kwa kuwa tumekuwa washiriki wa Kristo, kama tukishikamana tu kwa uthabiti na tumaini letu la kwanza hadi mwisho. 15 Kama ilivyonenwa:

“Leo, kama mkiisikia sauti yake,

msiifanye mioyo yenu migumu

kama mlivyofanya wakati wa kuasi.”

16 Basi ni nani waliosikia lakini bado wakaasi? Je, si wale wote waliotoka Misri wakiongozwa na Mose? 17 Lakini ni nani aliowakasirikia miaka arobaini? Je, si wale waliofanya dhambi ambao miili yao ilianguka jangwani? 18 Ni nani hao ambao Mungu aliapa kuwa kamwe hawataingia rahani mwake isipokuwa ni wale waliokataa kutii? 19 Hivyo tunaona kwamba hawakuweza kuingia kwa sababu ya kutokuamini kwao.