Mose Arudia Sheria ya Mahakama (continued)
1451 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Watu wanapokuwa na ugomvi, wapeleke mahakamani na waamuzi wataamua shauri hilo; watawaachia wasio na kosa na kuwahukumu wenye hatia. 2 Kama mtu mwenye hatia anastahili kuchapwa, mwamuzi atamwamuru alale chini ili achapwe mbele yake idadi ya viboko kulingana na kosa lake, 3 lakini kamwe asichapwe zaidi ya viboko arobaini. Ikiwa atachapwa zaidi ya viboko arobaini, nduguyo atadhalilika machoni pako.
4 Usimfunge maksai kinywa anapopura nafaka.
5 Ikiwa ndugu wanaishi pamoja na mmoja wao akafa bila kuacha mwana, kamwe mjane wake asiolewe nje ya jamaa hiyo. Ndugu wa mumewe atamchukua, amwoe na kutimiza wajibu wa shemeji kwake. 6 Mwana wa kwanza atakayemzaa atapewa jina la ndugu aliyekufa ili jina lake lisifutike katika Israeli.
7 Hata hivyo, ikiwa ndugu huyo wa mume hataki kuoa huyo mke wa nduguye, mjane atawaendea wazee kwenye lango la mji na kusema, “Ndugu wa mume wangu anakataa kuendeleza jina la nduguye katika Israeli. Hataki kutimiza wajibu wa shemeji kwangu.” 8 Ndipo wazee wa mji wake watamwita na kuzungumza naye. Kama atashikilia kukataa akisema, “Sitaki kumwoa,” 9 mjane wa nduguye atamwendea mbele ya wazee, atamvua kiatu kimoja na kumtemea mate usoni, na kusema, “Hivi ndivyo ambavyo hufanywa kwa mtu ambaye atakataa kuendeleza jamaa ya ndugu yake.” 10 Jamaa ya mtu huyo itafahamika katika Israeli kama Jamaa ya Aliyevuliwa Kiatu.
11 Ikiwa watu wawili wanapigana na mke wa mmoja wao akaja kumwokoa mumewe na yule anayemshambulia, naye mke huyo akifika na kumkamata sehemu za siri, 12 huyo mwanamke utamkata mkono wake. Usimhurumie.
13 Usiwe na mawe ya kupimia ya aina mbili katika mkoba wako, moja zito na jingine jepesi. 14 Usiwe na vipimo viwili tofauti katika nyumba yako, kimoja kikubwa, kingine kidogo. 15 Ni lazima uwe na uzito na vipimo sahihi na vya haki, ili upate kuishi maisha marefu katika nchi anayokupa Bwana Mungu wako. 16 Kwa maana Bwana Mungu wako humchukia yeyote ambaye hufanya mambo kama haya, yeyote anayetenda kwa udanganyifu.
17 Kumbuka kile Waamaleki walichowatendea mlipokuwa njiani mkitoka Misri. 18 Wakati mlipokuwa mmechoka na kuishiwa nguvu kwa safari yenu, wakawapiga wale wote waliokuja nyuma. Waamaleki hawakumwogopa Mungu. 19 Bwana Mungu wako atakapokupa pumziko mbali na adui zako wote wanaokuzunguka katika nchi akupayo kuimiliki kuwa urithi, utafutilia mbali kumbukumbu lote la Waamaleki chini ya mbingu. Usisahau!
26:1 Mtakapokuwa mmeingia nchi ile ambayo Bwana Mungu wenu anawapa kama urithi na mtakapokuwa mmeimiliki na kukaa ndani yake, 2 chukueni baadhi ya mavuno ya kwanza ya yale yote mtakayozalisha kutoka udongo wa nchi ambayo Bwana Mungu wenu anawapa na mweke kwenye kapu. Kisha uende mahali ambapo Bwana Mungu wako atapachagua kuwa makao kwa ajili ya Jina lake 3 na umwambie kuhani atakayekuwepo kwa wakati huo, “Ninatangaza leo kwa Bwana Mungu wako kwamba nimekuja katika nchi ambayo Bwana aliwaapia baba zetu kwamba atatupa.” 4 Kuhani atapokea lile kapu mikononi mwako na kuliweka chini mbele ya madhabahu ya Bwana Mungu wako. 5 Kisha utatangaza mbele za Bwana Mungu wako: “Baba yangu alikuwa Mwaramu aliyekuwa anatangatanga, akaenda Misri pamoja na watu wachache, akaishi huko hadi akawa taifa kubwa, lenye nguvu na watu wengi. 6 Lakini Wamisri walituonea na kututaabisha, wakitufanyisha kazi ngumu. 7 Kisha tulimlilia Bwana, Mungu wa baba zetu, naye Bwana akasikia sauti yetu na akaona huzuni yetu, taabu yetu na mateso yetu. 8 Kwa hiyo Bwana akatutoa nchi ya Misri kwa mkono wenye nguvu na ulionyooshwa, pamoja na utisho mkuu, ishara za miujiza na maajabu. 9 Akatuleta mahali hapa akatupa nchi hii, nchi inayotiririka maziwa na asali; 10 nami sasa ninaleta malimbuko ya ardhi ambayo wewe, Ee Bwana, umenipa.” Weka kapu mbele za Bwana Mungu wako na usujudu mbele zake. 11 Kisha wewe pamoja na Walawi na wageni wote walioko miongoni mwenu mtafurahi katika vitu vyote vizuri ambavyo Bwana Mungu wenu amewapa pamoja na wa nyumbani mwenu.
12 Wakati utakapokuwa umeshatoa zaka zote za mazao yako katika mwaka wa tatu, ambao ni mwaka wa zaka, utampa Mlawi, mgeni, yatima na mjane, ili waweze kula katika miji yenu na kushiba. 13 Kisha umwambie Bwana Mungu wako: “Nimeondoa katika nyumba yangu ile sehemu iliyowekwa wakfu na nimempa Mlawi, mgeni, yatima na mjane, kulingana na yote uliyoamuru. Sijazihalifu amri zako wala kusahau hata mojawapo. 14 Sijala sehemu iliyowekwa wakfu wakati nilipokuwa nikiomboleza, wala sijaondoa mojawapo wakati nilipokuwa najisi, wala sijatoa sehemu yake yoyote kwa wafu. Nimemtii Bwana Mungu wangu; nimefanya kila kitu ulichoniamuru. 15 Angalia chini kutoka mbinguni, maskani yako matakatifu, uwabariki watu wako Israeli pamoja na nchi uliyotupa kama ulivyoahidi kwa kiapo kwa baba zetu, nchi inayotiririka maziwa na asali.”
16 Bwana Mungu wako anakuagiza leo kufuata amri hizi na sheria; zishike kwa bidii kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote. 17 Umetangaza leo kwamba Bwana ndiye Mungu wako na kwamba utafuata njia zake, kwamba utayashika maagizo yake, amri zake na sheria zake nawe utamtii. 18 Naye Bwana ametangaza leo kwamba ninyi ni taifa lake, hazina yake ya thamani kama alivyoahidi, ili kwamba mpate kuyashika maagizo yake yote. 19 Ametangaza kwamba atawaweka juu kuliko mataifa mengine aliyoyafanya katika sifa, kuwa fahari na heshima, na kwamba mtakuwa taifa takatifu kwa Bwana Mungu wenu, kama alivyoahidi.