Mose Arudia Sheria ya Mahakama (continued)
1451 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Asiingie mtu yeyote aliyehasiwa kwa kupondwa makende au kwa kukatwa uume wake katika kusanyiko la Bwana.
2 Mtu yeyote ambaye amezaliwa kwenye ndoa isiyo halali au wazao wake wasiingie kwenye kusanyiko la Bwana, hata mpaka kizazi cha kumi.
3 Hapatakuwa na Mwamoni au Mmoabu au yeyote wa wazao wao atakayeruhusiwa kuingia katika kusanyiko la Bwana, hata mpaka kizazi cha kumi. 4 Kwa kuwa hawakuja kuwalaki wakiwa na mkate na maji mlipokuwa njiani mlipotoka Misri, tena walimwajiri Balaamu mwana wa Beori kutoka Pethori iliyoko Aramu-Naharaimu ili kuwalaani ninyi. 5 Hata hivyo, Bwana Mungu wenu hakumsikiliza Balaamu bali aligeuza laana kuwa baraka kwenu kwa sababu Bwana Mungu wenu anawapenda. 6 Msitafute mapatano ya urafiki nao maisha yenu yote.
7 Usimchukie Mwedomu, kwa kuwa yeye ni ndugu yako. Usimchukie Mmisri, kwa sababu uliishi kama mgeni katika nchi yake. 8 Kizazi cha tatu cha watoto watakaozaliwa nao wanaweza kuingia katika kusanyiko la Bwana.
9 Unapokuwa umepiga kambi dhidi ya adui zako, jitenge na kitu chochote kisicho safi. 10 Ikiwa mtu amechafuka kwa sababu ya kutokwa na shahawa usiku, inampasa atoke nje ya kambi na kukaa huko. 11 Lakini jioni ikikaribia ataoga, na baada ya jua kuzama ataingia tena kambini.
12 Tengeni mahali nje ya kambi ambapo mnaweza kwenda kujisaidia. 13 Kama sehemu ya vifaa vyenu kuweni na kitu cha kulimia, nanyi mnapojisaidia, chimba shimo na kisha funika kile kikutokacho. 14 Kwa kuwa Bwana Mungu wenu hutembea katika kambi yenu ili kuwalinda na kuwaweka adui zenu mikononi mwenu. Kambi yenu ni lazima iwe takatifu, ili asione kitu chochote miongoni mwenu kilicho kichafu akageuka na kuwaacha.
15 Ikiwa mtumwa amekimbilia kwako, usimrudishe kwa bwana wake. 16 Mwache aishi miongoni mwenu mahali popote anapopapenda na katika mji wowote anaochagua. Usimwonee.
17 Asiwepo Mwisraeli mwanamke kahaba au mwanaume hanithi wa mahali pa kuabudia miungu. 18 Kamwe usilete mapato ya ukahaba ikiwa ni ya mwanamke au ni ya mwanaume katika nyumba ya Bwana Mungu wako kwa ajili ya nadhiri yoyote, kwa sababu Bwana Mungu wako anachukizwa na yote mawili.
19 Usimtoze ndugu yako riba, iwe ni fedha ama chakula ama kitu kingine chochote ambacho waweza kupata riba juu yake. 20 Unaweza kumtoza mgeni riba, lakini siyo nduguyo Mwisraeli, ili kwamba Bwana Mungu wako akubariki katika kila kitu unachoweka mkono katika nchi unayoingia kuimiliki.
21 Ukiweka nadhiri kwa Bwana Mungu wako, usichelewe kuitimiza, kwa kuwa Bwana Mungu wako atakudai, nawe utakuwa na hatia ya dhambi. 22 Lakini ukijizuia kuweka nadhiri, hutakuwa na hatia. 23 Chochote kitakachotamkwa kwa midomo yako ni lazima uhakikishe umekifanya, kwa sababu uliweka nadhiri yako kwa hiari mbele za Bwana Mungu wako kwa kinywa chako mwenyewe.
24 Kama ukiingia katika shamba la mizabibu la jirani yako, unaweza kula zabibu kadiri utakavyo, lakini usiweke chochote kwenye kikapu chako. 25 Kama ukiingia katika shamba la nafaka la jirani yako, unaweza kukwanyua kwa mikono yako, lakini usikate kwa mundu nafaka iliyosimama.
24:1 Ikiwa mtu atamwoa mke na akamchukia kwa sababu ya kukosa adabu, naye akamwandikia hati ya talaka, akampa na kumfukuza kutoka nyumbani kwake, 2 ikiwa baada ya kuondoka nyumbani kwake atakuwa mke wa mtu mwingine, 3 ikiwa mume wake wa pili atachukizwa naye akamwandikia hati ya talaka, akampa na kumfukuza kutoka nyumbani kwake, au kama akifa, 4 basi yule mume wake wa kwanza, ambaye alimpa talaka, haruhusiwi kumwoa tena baada ya mwanamke huyo kuwa najisi. Hayo yatakuwa machukizo machoni pa Bwana. Usilete dhambi juu ya nchi ambayo Bwana Mungu wako anakupa kama urithi.
5 Kama mtu ameoa karibuni, kamwe asipelekwe vitani au kupewa wajibu mwingine wowote. Kwa mwaka mmoja atakuwa huru kubaki nyumbani ili amfurahishe mke aliyemwoa.
6 Usitoe jozi ya mawe ya kusagia, hata ikiwa lile la juu, kuweka rehani kwa ajili ya deni, kwa sababu itakuwa ni kuweka uhai wa mtu kama dhamana.
7 Kama mtu akikamatwa akiiba yeyote miongoni mwa ndugu zake wa Waisraeli na kumtenda kama mtumwa au akimuuza, mwizi huyo ni lazima auawe. Nawe utaondoa uovu kutoka miongoni mwenu.
8 Pakitokea magonjwa ya ngozi ya kuambukiza, mwe waangalifu sana kufanya sawasawa na maagizo ya makuhani, ambao ni Walawi. Ni lazima mfuate kwa uangalifu yale niliyowaamuru. 9 Kumbukeni kile Bwana Mungu wenu alichomfanyia Miriamu njiani baada ya ninyi kutoka Misri.
10 Unapomkopesha jirani yako chochote, usiingie nyumbani kwake kutwaa kile anachokitoa kama rehani. 11 Ukae nje na umwache huyo mtu uliyemkopesha akuletee hiyo rehani. 12 Ikiwa mtu huyo ni maskini, usiende kulala ukiwa na hiyo rehani yake katika milki yako. 13 Rudisha vazi lake kabla ya machweo ya jua ili apate kulilalia. Kisha atakushukuru na kitaonekana kama kitendo cha haki mbele za Bwana Mungu wako.
14 Usimwonee mtu maskini na mhitaji ambaye umemwajiri, akiwa ni nduguyo Mwisraeli au mgeni anayeishi katika mojawapo ya miji yenu. 15 Mlipe ujira wake kila siku kabla ya jua kutua, kwa sababu yeye ni maskini na anautegemea ujira huo. La sivyo, anaweza kumlilia Bwana dhidi yako, nawe ukapata hatia ya dhambi.
16 Baba wasiuawe kwa ajili ya watoto wao, wala watoto wasiuawe kwa ajili ya baba zao; kila mmoja atakufa kwa ajili ya dhambi yake mwenyewe.
17 Usipotoshe hukumu ya mgeni au yatima, au kuchukua vazi la mjane kama rehani. 18 Kumbukeni kwamba mlikuwa watumwa huko Misri, naye Bwana Mungu wenu akawakomboa kutoka huko. Hii ndiyo sababu ninawaamuru kutenda hili.
19 Unapovuna shamba lako na ukasahau mganda, usirudi kuuchukua. Acha kwa ajili ya mgeni, yatima na mjane, ili Bwana Mungu wako aweze kukubariki wewe katika kazi zote za mikono yako. 20 Unapovuna zeituni kutoka miti yako, usirudie matawi mara ya pili. Acha kilichobaki kwa ajili ya mgeni, yatima na mjane. 21 Unapochuma zabibu katika shamba lako la mizabibu usirudie tena. Acha zinazobaki kwa ajili ya mgeni, yatima na mjane. 22 Kumbuka kwamba mlikuwa watumwa katika nchi ya Misri. Ndiyo sababu ninawaamuru kufanya hili.