Hitimisho la Maisha ya Mose
Kifo cha Mose Chatangazwa
1451 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
12 Kisha Bwana akamwambia Mose, “Panda juu ya mlima huu katika kilele cha Abarimu uione nchi ambayo nimewapa Waisraeli. 13 Baada ya kuiona, wewe pia utakusanywa pamoja na watu wako kama ndugu yako Aroni alivyokusanywa, 14 kwa kuwa jumuiya ilipoasi amri yangu kwenye maji katika Jangwa la Sini, wakati jumuiya ilipogombana nami, nyote wawili mliacha kuitii amri yangu ya kuniheshimu kama mtakatifu mbele ya macho yao.” (Haya yalikuwa maji ya Meriba huko Kadeshi, katika Jangwa la Sini.)
Yoshua Ateuliwa Kuchukua Nafasi ya Mose
15 Mose akamwambia Bwana, 16 “Bwana, Mungu wa roho zote za wanadamu, na amteue mtu juu ya jumuiya hii 17 ili atoke na kuingia mbele yao, atakayewaongoza katika kutoka kwao na kuingia kwao, ili watu wa Bwana wasiwe kama kondoo wasio na mchungaji.”
18 Kwa hiyo Bwana akamwambia Mose, “Mchukue Yoshua mwana wa Nuni, mtu ambaye Roho yuko ndani yake, uweke mkono juu yake. 19 Msimamishe mbele ya kuhani Eleazari pamoja na kusanyiko lote, umpe maagizo mbele yao. 20 Mpe sehemu ya mamlaka yako ili jumuiya yote ya Waisraeli ipate kumtii. 21 Atasimama mbele ya kuhani Eleazari, ambaye atapokea maamuzi kwa ajili yake, kwa kuuliza mbele za Bwana kwa ile Urimu. Kwa amri yake, yeye na jumuiya yote ya Waisraeli watatoka, na kwa amri yake, wataingia.”
22 Mose akafanya kama Bwana alivyomwagiza. Akamtwaa Yoshua na kumsimamisha mbele ya kuhani Eleazari na kusanyiko lote. 23 Kisha akaweka mikono yake juu ya kichwa cha Yoshua na kumpa maagizo, kama vile Bwana alivyoelekeza kupitia kwa Mose.
Maagizo ya Mwisho ya Mose kwa Watu
1 Kisha Mose akaenda akasema maneno haya kwa Waisraeli wote: 2 “Sasa nina miaka mia moja na ishirini nami siwezi tena kuwaongoza. Bwana ameniambia, ‘Hutavuka Yordani.’ 3 Bwana Mungu wenu, yeye mwenyewe atavuka mbele yenu. Ataangamiza mataifa haya mbele yenu, nanyi mtaimiliki nchi yao. Pia Yoshua atavuka mbele yenu, kama Bwana alivyosema. 4 Naye Bwana atawafanyia watu hao kile alichowafanyia Sihoni na Ogu, wafalme wa Waamori, ambao aliwaangamiza pamoja na nchi yao. 5 Bwana atawakabidhi kwenu, nanyi lazima mwatendee yale yote niliyowaamuru. 6 Kuweni imara na moyo wa ushujaa. Msiogope wala msifadhaike kwa sababu yao, kwa kuwa Bwana Mungu wenu anakwenda pamoja nanyi; kamwe hatawaacha wala hatawatupa ninyi.”
Maagizo ya Mose kwa Yoshua
7 Kisha Mose akamwita Yoshua na akamwambia mbele ya Israeli wote, “Uwe imara na moyo wa ushujaa, kwa kuwa ni lazima uende na watu hawa katika nchi ile Bwana aliyowaapia baba zao kuwapa, nawe ni lazima uwagawie kama urithi wao. 8 Bwana mwenyewe atakutangulia naye atakuwa pamoja nawe; kamwe hatakuacha wala hatakutupa. Usiogope, wala usifadhaike.”
Mose Amaliza Kuandika Sheria
Mose amaliza kuandika Sheria na kuikabidhi kwa makuhani.
9 Kwa hiyo Mose akaandika sheria hii na kuwapa makuhani, wana wa Lawi, waliochukua Sanduku la Agano la Bwana na wazee wote wa Israeli. 10 Kisha Mose akawaamuru, akasema: “Mwishoni mwa kila miaka saba, katika mwaka wa kufuta madeni, wakati wa Sikukuu ya Vibanda, 11 Waisraeli wote wanapokuja mbele za Bwana Mungu wenu mahali atakapopachagua, utasoma sheria hii mbele yao masikioni mwao. 12 Kusanya watu wote, wanaume, wanawake, watoto na wageni wanaoishi katika miji yenu, ili waweze kusikia na kujifunza kumcha Bwana Mungu wenu na kufuata kwa bidii maneno yote ya sheria hii. 13 Watoto wao, ambao hawaijui sheria hii, lazima waisikie na kujifunza kumcha Bwana Mungu wenu kwa muda mtakaoishi katika nchi mnayovuka Yordani kuimiliki.”
14 Bwana akamwambia Mose, “Sasa siku ya kifo chako imekaribia. Mwite Yoshua, mkajihudhurishe katika Hema la Kukutania, mahali nitakapompa maagizo ya kazi.” Kwa hiyo Mose na Yoshua wakaja na kujihudhurisha kwenye Hema la Kukutania.
15 Kisha Bwana akatokea katika Hema katika nguzo ya wingu, nalo wingu likasimama juu ya ingilio la Hema. 16 Kisha Bwana akamwambia Mose: “Unakwenda kupumzika na baba zako, nao watu hawa hivi karibuni watazini na miungu migeni ya nchi wanayoingia. Wataniacha na kuvunja Agano nililofanya nao. 17 Siku hiyo nitawakasirikia na kuwaacha; nitawaficha uso wangu, nao wataangamizwa. Maafa mengi na shida nyingi zitakuja juu yao, nao siku hiyo watauliza, ‘Je, maafa haya hayakuja juu yetu kwa sababu Mungu wetu hayuko pamoja nasi?’ 18 Nami hakika nitauficha uso wangu siku hiyo kwa sababu ya maovu yao yote kwa kugeukia miungu mingine.
19 “Sasa ujiandikie wimbo huu, uwafundishe Waisraeli na uwaamuru wauimbe, ili upate kuwa ushahidi wangu dhidi yao. 20 Nitakapokwisha kuwaingiza katika nchi itiririkayo maziwa na asali, nchi niliyowaahidi baba zao kwa kiapo, nao watakapokula wakashiba na kufanikiwa, watageukia miungu mingine na kuiabudu, wakinikataa mimi na kuvunja Agano langu. 21 Maafa na shida zitakapokuja juu yao, wimbo huu utashuhudia dhidi yao, kwa sababu hautasahauliwa na wazao wao. Ninajua lile wanaloandaa kufanya, hata kabla sijawaingiza katika nchi niliyowaahidi kwa kiapo.”
Maagizo ya Pili kwa Yoshua
Maagizo ya pili kwa Yoshua, na kukabidhiwa kwa Sheria kwa Walawi.
23 Bwana akampa Yoshua mwana wa Nuni agizo hili: “Uwe hodari na shujaa, kwa kuwa utawaleta Waisraeli katika nchi niliyowaahidi kwa kiapo, nami mwenyewe nitakuwa pamoja nawe.”
24 Baada ya Mose kumaliza kuandika kwenye kitabu maneno ya sheria hii kutoka mwanzo hadi mwisho, 25 akawapa Walawi wale waliolibeba Sanduku la Agano la Bwana agizo hili, akawaambia: 26 “Chukueni Kitabu hiki cha Sheria mkakiweke kando ya Sanduku la Agano la Bwana Mungu wenu. Hapo ndipo kitakapokaa kama shahidi dhidi yenu. 27 Kwa kuwa ninajua jinsi mlivyo waasi na mlivyo na shingo ngumu. Kama mmekuwa mkiasi dhidi ya Bwana nikiwa bado niko hai na nikiwa pamoja nanyi, mtaasi mara ngapi baada ya kufa kwangu! 28 Kusanyeni mbele yangu wazee wote wa makabila yenu na maafisa wenu wote, ili nipate kusema maneno haya masikioni mwao na kuziita mbingu na nchi ili kushuhudia dhidi yao. 29 Kwa kuwa ninajua baada ya kifo changu hakika mtakuwa waovu kabisa na kugeuka kutoka njia niliyowaamuru ninyi. Katika siku zijazo, maafa yatawapata kwa sababu mtafanya maovu mbele ya macho ya Bwana, na kuchochea hasira yake kwa yale mikono yenu itakayokuwa imefanya.”