Wito wa Kuhitimisha wa Mose kwa Watu

1451 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Kumbukumbu 29–30

1 Haya ndiyo maneno ya Agano Bwana aliyomwagiza Mose kufanya na Waisraeli huko Moabu, kuwa nyongeza ya Agano alilofanya nao huko Horebu.

2 Mose akawaita Waisraeli wote akawaambia:

Macho yenu yameona yale yote Bwana aliyofanya kwa Mfalme Farao huko Misri, kwa maafisa wake wote na kwa nchi yake yote. 3 Kwa macho yenu wenyewe mliona yale majaribu makubwa, ishara zile za miujiza na maajabu makubwa. 4 Lakini mpaka leo Bwana hajawapa akili ya kuelewa au macho yanayoona au masikio yanayosikia. 5 Kwa muda wa miaka arobaini niliyowaongoza jangwani, nguo zenu hazikuchakaa, wala viatu miguuni mwenu. 6 Hamkula mkate na hamkunywa divai wala kileo chochote. Nilifanya hivi ili mpate kujua kuwa mimi ndimi Bwana Mungu wenu.

7 Wakati mlipofika mahali hapa, Sihoni mfalme wa Heshboni na Ogu mfalme wa Bashani walikuja kupigana dhidi yetu, lakini tuliwashinda. 8 Tuliichukua nchi yao na kuwapa Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase kama urithi wao.

9 Fuateni kwa bidii masharti ya Agano hili, ili kwamba mweze kustawi katika kila kitu mnachofanya. 10 Ninyi nyote leo mnasimama mbele za Bwana Mungu wenu; mkiwa viongozi na wakuu wenu, wazee na maafisa wenu, na wanaume wengine wote wa Israeli, 11 pamoja na watoto wenu, wake zenu na pia wageni waishio katika kambi zenu wanaowapasulia kuni na kuwachotea maji. 12 Mnasimama hapa ili kufanya Agano na Bwana Mungu wenu, Agano ambalo Mungu analifanya nanyi siku hii ya leo na kulitia muhuri kwa kiapo, 13 kuwathibitisha ninyi siku hii ya leo kama taifa lake, ili aweze kuwa Mungu wenu kama alivyowaahidi na kama alivyowaapia baba zenu Abrahamu, Isaki na Yakobo. 14 Ninafanya Agano hili pamoja na kiapo chake, sio na ninyi tu 15 mnaosimama hapa na sisi leo mbele za Bwana Mungu wetu, bali pia pamoja na wale ambao hawapo hapa leo.

16 Ninyi wenyewe mnajua jinsi tulivyoishi nchini Misri na jinsi tulivyopita katikati ya nchi mpaka tukafika hapa. 17 Mliona miongoni mwao vinyago vyao vya kuchukiza na sanamu za miti na mawe, za fedha na dhahabu. 18 Hakikisheni kwamba hakuna mwanaume au mwanamke, ukoo au kabila miongoni mwenu leo ambalo moyo wake utamwacha Bwana Mungu wetu, kwenda kuabudu miungu ya mataifa hayo. Hakikisheni hakuna mzizi miongoni mwenu unaotoa sumu chungu ya namna hii.

19 Wakati mtu wa namna hii asikiapo maneno ya kiapo hiki, hujibariki mwenyewe na kisha hufikiri, “Nitakuwa salama, hata kama nikiendelea kuifuata njia yangu mwenyewe.” Hili litaleta maafa juu ya nchi iliyonyeshewa sawasawa na nchi kame. 20 Bwana kamwe hatakuwa radhi kumsamehe, ghadhabu na wivu wa Mungu vitawaka dhidi ya mtu huyo. Laana zote zilizoandikwa katika kitabu hiki zitamwangukia na Bwana atafuta jina lake chini ya mbingu. 21 Bwana atamtwaa peke yake kutoka makabila ya Israeli kwa maangamizo, kulingana na laana zote za Agano zilizoandikwa kwenye Kitabu hiki cha Sheria.

22 Watoto wako watakaofuata baada yako katika vizazi vya baadaye na wageni ambao watakuja kutoka nchi za mbali, wataona maafa, yaliyoipata nchi na magonjwa ambayo Bwana aliyaleta juu yake. 23 Nchi yote itakuwa jaa linaloungua la chumvi na kiberiti: hakutakuwa kilichopandwa, hakutakuwa kinachochipua, wala hakutakuwa mimea inayoota juu yake. Itakuwa kama maangamizo ya Sodoma na Gomora, Adma na Seboimu, ambazo Bwana aliangamiza kwa hasira kali. 24 Mataifa yote yatauliza: “Kwa nini Bwana amefanya hivi juu ya nchi hii? Kwa nini hasira hii kali ikawaka?”

25 Na jibu litakuwa: “Ni kwa sababu watu hawa waliacha Agano la Bwana, Mungu wa baba zao, Agano alilofanya nao wakati alipowatoa katika nchi ya Misri. 26 Walienda zao na kuabudu miungu mingine na kuisujudia, miungu wasioijua, miungu ambayo Mungu hakuwapa. 27 Kwa hiyo hasira ya Bwana ikawaka dhidi ya nchi hii, hivyo Mungu akaleta juu yake laana zote zilizoandikwa katika kitabu hiki. 28 Katika hasira kali na katika ghadhabu kuu Bwana aliwangʼoa kutoka nchi yao na kuwasukumia katika nchi nyingine, kama ilivyo sasa.”

29 Mambo ya siri ni ya Bwana Mungu wetu, bali yaliyofunuliwa ni yetu na watoto wetu milele, ili tuweze kuyafanya maneno yote ya sheria hii.

30:1 Wakati baraka hizi zote pamoja na laana nilizoziweka mbele yako zitakapokujia, nawe ukazitafakari moyoni popote Bwana Mungu wako atakapokutawanya miongoni mwa mataifa, 2 hapo wewe na watoto wako mtakapomrudia Bwana Mungu wako, na kumtii kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote kulingana na kila kitu ninachokuamuru leo, 3 ndipo Bwana Mungu wako atakapokurudisha kutoka utumwani na kukuhurumia, naye atakukusanya tena kutoka mataifa yote kule alikutawanya. 4 Hata kama umefukuziwa katika nchi ya mbali kiasi gani chini ya mbingu, kutoka huko Bwana Mungu wako atakukusanya na kukurudisha. 5 Yeye Bwana atakurudisha katika nchi iliyokuwa mali ya baba zako, nawe utaimiliki. Naye atakufanya ufanikiwe sana na kukuzidisha kwa idadi kuliko baba zako. 6 Bwana Mungu wako ataitahiri mioyo yenu na mioyo ya wazao wenu ili mweze kumpenda kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote ukaishi. 7 Bwana Mungu wako ataweka laana hizi zote juu ya adui zako ambao wanakuchukia na kukutesa. 8 Utamtii tena Bwana na kuzishika amri zake zote ninazokupa leo. 9 Ndipo Bwana Mungu wako atakapokufanikisha sana katika kazi zote za mikono yako na katika uzao wa tumbo lako, wadogo wa mifugo yako na mazao ya nchi yako. Bwana atakufurahia tena na kukufanikisha, kama alivyowafurahia baba zako, 10 kama ukimtii Bwana Mungu wako, na kuzishika amri zake na maagizo yake ambayo yameandikwa katika Kitabu hiki cha Sheria, na kumgeukia Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote.

11 Ninachokuagiza leo sio kigumu sana kwako au usichokiweza. 12 Hakiko juu mbinguni, ili uulize, “Ni nani atakayepanda mbinguni kukileta na kututangazia ili tuweze kutii?” 13 Wala hakiko ngʼambo ya bahari, ili uulize, “Ni nani atakayevuka bahari kwenda kukichukua na kututangazia ili tupate kutii?” 14 La hasha! Lile neno liko karibu sana nawe; liko kinywani mwako na ndani ya moyo wako ili uweze kulitii.

15 Tazama, naweka mbele yako leo uzima na mafanikio, mauti na maangamizo. 16 Ninakuamuru leo kwamba umpende Bwana Mungu wako, utembee katika njia zake, na kutunza maagizo yake, amri na sheria zake; ndipo utakapoishi na kuongezeka, naye Bwana Mungu wako atakubariki katika nchi unayoingia kuimiliki.

17 Lakini kama moyo wako ukigeukia mbali ukawa huna utii, kama umevutwa kuisujudia miungu mingine na kuiabudu, 18 nakutangazia leo hii kwamba hakika utaangamizwa. Hutaishi maisha marefu katika nchi unayovuka Yordani kuiingia na kuimiliki.

19 Leo ninaziita mbingu na nchi kama mashahidi dhidi yako kwamba nimeweka mbele yako uzima na mauti, baraka na laana. Basi sasa chagueni uzima, ili wewe na watoto wako mpate kuishi, 20 na ili upate kumpenda Bwana Mungu wako, uisikilize sauti yake na kuambatana naye. Kwa kuwa Bwana ndiye uzima wako, na atakupa wingi wa siku ili upate kuishi katika nchi aliyoapa kuwapa baba zako Abrahamu, Isaki na Yakobo.

Hesabu 36:13

13 Haya ndiyo maagizo na masharti ambayo Bwana aliwapa Waisraeli kupitia Mose katika tambarare za Moabu, karibu na Yordani ngʼambo ya Yeriko.