Mageuzi ya Dini ya Yosia

624 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

2 Wafalme 23:4–21

4 Mfalme akamwamuru Hilkia kuhani mkuu, makuhani waliomfuata kwa cheo, na mabawabu kuondoa kutoka kwenye Hekalu la Bwana vyombo vyote vilivyofanywa kwa ajili ya Baali na Ashera na jeshi lote la mianga ya angani! Akavichoma nje ya Yerusalemu katika mashamba ya Bonde la Kidroni, na kuyachukua hayo majivu mpaka Betheli. 5 Akawafukuza makuhani wa kipagani waliokuwa wameteuliwa na wafalme wa Yuda kufukiza uvumba katika mahali pa juu pa kuabudia miungu katika miji ya Yuda na ile iliyozunguka Yerusalemu, yaani wale waliofukiza uvumba kwa Baali, kwa jua na mwezi, kwa makundi ya nyota, na jeshi lote la angani. 6 Akaiondoa nguzo ya Ashera kutoka kwenye Hekalu la Bwana, na kuipeleka kwenye Bonde la Kidroni nje ya Yerusalemu, akaiteketeza huko. Akaisaga hadi ikawa unga na kusambaza hilo vumbi juu ya makaburi ya watu wa kawaida. 7 Akabomoa pia nyumba za mahanithi wa mahali pa ibada za miungu, zilizokuwa ndani ya Hekalu la Bwana na mahali wanawake walipofuma kwa ajili ya Ashera.

8 Yosia akawaleta makuhani wote wa Bwana kutoka miji yote ya Yuda, na kunajisi mahali pa juu pa kuabudia miungu, kuanzia Geba hadi Beer-Sheba, mahali pote ambapo hao makuhani wa miungu walifukiza uvumba. Akabomoa mahali pa kuwekea vitu vya ibada za miungu palipokuwa katika malango, kwenye ingilio la Lango la Yoshua, mtawala wa mji, lililoko upande wa kushoto wa lango la mji. 9 Ingawa makuhani wa mahali pa juu pa kuabudia miungu hawakuhudumu katika madhabahu ya Bwana katika Yerusalemu, walikula mikate isiyotiwa chachu miongoni mwa ndugu zao.

10 Kisha mfalme akanajisi Tofethi, palipokuwa katika Bonde la Ben-Hinomu, ili mtu yeyote asiweze kupatumia kumtoa kafara mwanawe au binti yake katika moto kwa mungu Moleki. 11 Akaondoa kutoka kwenye ingilio la Hekalu la Bwana wale farasi ambao wafalme wa Yuda walikuwa wamewaweka wakfu kwa ajili ya jua. Walikuwa kwenye ua karibu na chumba cha afisa aliyeitwa Nathan-Meleki. Basi Yosia akayachoma moto yale magari yaliyokuwa yamewekwa wakfu kwa jua.

12 Alizivunja madhabahu ambazo wafalme wa Yuda walikuwa wamezijenga kwenye paa la ghorofa ya Ahazi, pia madhabahu alizokuwa amezijenga Manase katika nyua mbili za Hekalu la Bwana. Akaziondoa huko, akazivunja vipande vipande, na kutupa hicho kifusi katika Bonde la Kidroni. 13 Mfalme pia akanajisi mahali pa juu pa kuabudia miungu, palipokuwa mashariki ya Yerusalemu upande wa kusini wa Kilima cha Uharibifu, pale ambapo Solomoni mfalme wa Israeli alikuwa amejenga kwa ajili ya Ashtorethi mungu mke chukizo la Wasidoni, kwa ajili ya Kemoshi mungu chukizo la Wamoabu, na kwa ajili ya Moleki mungu chukizo la watu wa Amoni. 14 Yosia akapasua yale mawe ya kuabudiwa na kuzikatakata nguzo za Ashera. Kisha akafunika hayo maeneo kwa mifupa ya wanadamu.

15 Hata madhabahu yaliyokuwa huko Betheli, mahali pa juu pa kuabudia miungu palipokuwa pamejengwa na Yeroboamu mwana wa Nebati, ambaye aliwafanya Israeli watende dhambi, alibomoa hata hayo madhabahu na mahali pa juu pa kuabudia miungu. Alipateketeza kwa moto hapo mahali pa juu pa kuabudia miungu na kupasaga hadi pakawa vumbi, na kuichoma hiyo nguzo ya Ashera pia. 16 Kisha Yosia akatazama huku na huko, naye alipoona makaburi yaliyokuwa huko kwenye kilima, akaamuru mifupa itolewe humo na akaichoma juu ya madhabahu ya Betheli ili kupanajisi. Hili lilitokea kulingana na neno la Bwana lililosemwa na mtu wa Mungu ambaye alitangulia kusema mambo haya.

17 Mfalme akauliza, “Lile kaburi lenye mnara wa ukumbusho ninaloliona ni kwa ajili gani?”

Watu wa mji wakasema, “Hii ni alama ya kaburi la mtu wa Mungu aliyekuja kutoka Yuda, naye akanena dhidi ya hii madhabahu ya Betheli mambo yale yale uliyoifanyia leo.”

18 Akasema, “Liacheni, msiliguse. Msimruhusu mtu yeyote kuiondoa mifupa yake.” Basi wakaiacha mifupa yake pamoja na ile ya yule nabii ambaye alikuwa amekuja kutoka Samaria.

19 Kama alivyokuwa amefanya huko Betheli, Yosia akabomoa na kunajisi mahali pa kuabudia miungu kwenye mahali pa juu ambapo wafalme wa Israeli walikuwa wamejenga ndani ya miji ya Samaria, ambayo ilikuwa imemghadhibisha Bwana. 20 Yosia akawachinja makuhani wote wa mahali pa juu pa kuabudia miungu katika madhabahu zao wenyewe, na kuchoma mifupa ya wanadamu juu yake. Kisha akarudi Yerusalemu.

21 Mfalme akatoa agizo hili kwa watu wote: “Adhimisheni Pasaka kwa Bwana Mungu wenu, kama ilivyoandikwa katika Kitabu hiki cha Agano.”

2 Nyakati 34:33

33 Yosia akaondoa machukizo yote ya sanamu kutoka nchi yote iliyokuwa mali ya Waisraeli na akawataka wale wote waliokuwako katika Israeli wamtumikie Bwana Mungu wao. Kwa muda wote alioishi, hawakushindwa kumfuata Bwana, Mungu wa baba zao.

Yosia Aadhimisha Pasaka 623 KK

Maadhimisho ya Pasaka.

2 Nyakati 35:1–19

1 Yosia akaadhimisha Pasaka kwa Bwana katika Yerusalemu, mwana-kondoo wa Pasaka akachinjwa siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza. 2 Akawaweka makuhani kwenye wajibu wao na kuwatia moyo katika utumishi wa Hekalu la Bwana. 3 Akawaambia Walawi, waliowafundisha Waisraeli wote na waliokuwa wamejiweka wakfu kwa ajili ya kazi ya Bwana, “Liwekeni hilo Sanduku takatifu katika Hekalu lile alilojenga Solomoni mwana wa Daudi mfalme wa Israeli. Halipaswi kubebwa huku na huko mabegani mwenu. Sasa mtumikieni Bwana Mungu wenu na watu wake Israeli. 4 Jiandaeni kwa kufuata jamaa zenu katika migawanyo yenu, kufuatana na maelezo yaliyoandikwa na Daudi mfalme wa Israeli na mwanawe Solomoni.

5 “Simameni mahali patakatifu kwa kufuata migawanyo ya jamaa za baba zenu kulingana na koo zenu na pawepo Walawi kwa ajili ya kila mgawanyo wa nyumba ya baba zenu. 6 Chinjeni mwana-kondoo wa Pasaka, jitakaseni, nanyi kwa niaba ya koo zenu fanyeni maandalizi, mkitenda sawasawa na neno la Bwana kwa mkono wa Mose.”

7 Ndipo Yosia akawapa watu wote wana-mbuzi waliokuwepo jumla ya kondoo wapatao 30,000 kwa ajili ya sadaka ya Pasaka, pia na ngʼombe 10,000, vyote hivi kutoka mali binafsi ya mfalme.

8 Pia maafisa wake, wakatoa kwa hiari yao wakawapa watu, makuhani na Walawi. Hilkia, Zekaria na Yehieli, waliokuwa maafisa wakuu wa Hekalu la Mungu, wakawapa makuhani sadaka za Pasaka wana-kondoo na wana-mbuzi 2,600 na mafahali 300. 9 Konania na nduguze wawili, Shemaya na Nethaneli, pamoja na Hashabia, Yeieli na Yozabadi waliokuwa viongozi wa Walawi, nao pia wakawapa Walawi wana-kondoo na wana-mbuzi 5,000 na mafahali 500, kwa ajili ya sadaka za Pasaka.

10 Huduma ilipomalizika kuandaliwa makuhani wakasimama mahali pao na Walawi katika migawanyo yao kama mfalme alivyokuwa ameamuru. 11 Wana-kondoo wa Pasaka wakachinjwa, nao makuhani wakanyunyiza ile damu waliyokabidhiwa, wakati Walawi wakiwa wanawachuna wale wanyama ngozi. 12 Wakatenga sadaka za kuteketezwa ili waweze kugawia ili migawanyo kwa kufuata jamaa za baba zao ili watoe sadaka kwa Bwana kama ilivyoandikwa katika Kitabu cha Mose. Wakafanya vivyo hivyo kwa wale mafahali. 13 Wakawaoka wale wanyama wa Pasaka kwenye moto kama ilivyoamriwa, wakachemsha zile sadaka takatifu kwenye vyungu, masufuria makubwa na vikaango na kuwagawia watu wote upesi. 14 Hatimaye wakafanya maandalizi kwa ajili yao wenyewe na kwa ajili ya makuhani, kwa sababu wale makuhani, yaani, wazao wa Aroni, walikuwa wanatoa sadaka za kuteketezwa pamoja na zile sehemu zilizonona mpaka usiku. Hivyo Walawi wakafanya maandalizi kwa ajili yao wenyewe na kwa ajili ya makuhani wa uzao wa Aroni.

15 Waimbaji, wazao wa Asafu, walikuwa katika nafasi zao, kama ilivyoagizwa na Mfalme Daudi, Asafu, Hemani na Yeduthuni mwonaji wa Mfalme. Mabawabu katika kila lango hawakuhitaji kuacha nafasi zao kwa sababu Walawi wenzao walifanya maandalizi kwa ajili yao.

16 Kwa hiyo wakati ule huduma yote ya Bwana ilifanyika katika kuadhimisha Pasaka, kutoa sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu ya Bwana kama alivyoamuru Mfalme Yosia. 17 Waisraeli waliokuwepo wakaadhimisha Pasaka wakati huo na Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu kwa siku saba. 18 Kulikuwa hakujafanyika Pasaka kama hii katika Israeli tangu siku za nabii Samweli wala hakukuwa na mfalme yeyote wa Israeli ambaye kamwe alishaadhimisha Pasaka kama ile aliyofanya Mfalme Yosia, akiwa na makuhani, Walawi na watu wote wa Yuda na watu wa Israeli waliokuwepo huko, pamoja na watu wa Yerusalemu. 19 Pasaka iliadhimishwa katika mwaka wa kumi na nane wa utawala wa Mfalme Yosia.