Yeremia Akemea Kurudi Nyuma kwa Watu

Yeremia anawakemea watu kwa kurudi kwao nyuma baada ya mageuzi ya Yosia.

612 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Yeremia 3:6–25

6 Wakati wa utawala wa Mfalme Yosia, Bwana aliniambia, “Umeona kile Israeli asiye mwaminifu amekifanya? Amepanda juu ya kila kilima kirefu, na chini ya kila mti uliotanda na amefanya uzinzi huko. 7 Mimi nilifikiri kuwa baada ya kuyafanya yote haya angelinirudia, lakini hakurudi, naye dada yake Yuda mdanganyifu aliona hili. 8 Nilimpa Israeli asiye mwaminifu hati yake ya talaka, na kumfukuza kwa ajili ya uzinzi wake wote. Hata hivyo nikaona kuwa Yuda dada yake mdanganyifu hakuogopa. Yeye pia alitoka na kufanya uzinzi. 9 Kwa sababu uasherati wa Israeli haukuwa kitu kwake, Yuda aliinajisi nchi kwa kuzini na mawe na miti. 10 Pamoja na hayo yote, Yuda dada yake mdanganyifu hakunirudia kwa moyo wake wote, bali kwa kujifanya tu,” asema Bwana.

11 Bwana akaniambia, “Israeli asiye mwaminifu ana haki kuliko Yuda mdanganyifu. 12 Nenda, ukatangaze ujumbe huu kuelekea kaskazini:

“ ‘Rudi, Israeli usiye mwaminifu,’ asema Bwana,

‘sitakutazama tena kwa uso uliokunjamana,

kwa kuwa mimi ni mwenye huruma,’ asema Bwana,

‘Sitashika hasira yangu milele.

13 Ungama dhambi zako tu:

kwamba umemwasi Bwana Mungu wako,

umetapanya wema wako kwa miungu ya kigeni

chini ya kila mti unaotanda,

nawe hukunitii mimi,’ ”

asema Bwana.

14 “Rudini, enyi watu msio waaminifu, kwa kuwa mimi ni mume wenu,” asema Bwana. “Nitawachagua ninyi, mmoja kutoka kwenye mji, na wawili kutoka kwenye ukoo, nami nitawaleta Sayuni. 15 Kisha nitawapeni wachungaji wanipendezao moyo wangu, ambao watawaongoza kwa maarifa na ufahamu. 16 Katika siku hizo, idadi yenu itakapokuwa imeongezeka sana katika nchi, watu hawatasema tena, ‘Sanduku la Agano la Bwana,’ ” asema Bwana. “Halitaingia tena kwenye mawazo yao wala kukumbukwa, hawatalihitaji wala halitatengenezwa jingine. 17 Wakati huo, wataita Yerusalemu kuwa Kiti cha Enzi cha Bwana, nayo mataifa yote watakusanyika Yerusalemu kuliheshimu jina la Bwana. Hawatafuata tena ukaidi wa mioyo yao miovu. 18 Katika siku hizo, nyumba ya Yuda itaungana na nyumba ya Israeli, wao kwa pamoja watakuja kutoka nchi ya kaskazini hadi nchi niliyowapa baba zenu kama urithi.

19 “Mimi mwenyewe nilisema,

“ ‘Tazama jinsi nitakavyowatunza kwa furaha kama wana

na kuwapa nchi nzuri,

urithi ulio mzuri kuliko wa taifa jingine lolote.’

Nilidhani mngeniita ‘Baba,’

na msingegeuka, mkaacha kunifuata.

20 Lakini kama mwanamke asiye mwaminifu kwa mumewe,

vivyo hivyo mmekosa uaminifu kwangu pia, ee nyumba ya Israeli,”

asema Bwana.

21 Kilio kinasikika juu ya miinuko iliyo kame,

kulia na kuomboleza kwa watu wa Israeli,

kwa sababu wamepotoka katika njia zao

na wamemsahau Bwana Mungu wao.

22 “Rudini, enyi watu msio waaminifu,

nami nitawaponya ukengeufu wenu.”

“Naam, tutakuja kwako,

kwa maana wewe ni Bwana Mungu wetu.

23 Hakika zile ghasia za kuabudu sanamu kwenye vilima

na milimani ni udanganyifu;

hakika katika Bwana, Mungu wetu,

uko wokovu wa Israeli.

24 Tangu ujana wetu miungu ya aibu imeyala

matunda ya kazi za baba zetu:

makundi yao ya kondoo na ngʼombe,

wana wao na binti zao.

25 Sisi na tulale chini katika aibu yetu,

na fedheha yetu itufunike.

Tumetenda dhambi dhidi ya Bwana Mungu wetu,

sisi na mababa zetu;

tangu ujana wetu hadi leo

hatukumtii Bwana Mungu wetu.”

Yeremia Aona Kimbele Huzuni za Utumwa

Yeremia anaeleza kimbele, akiwa nabii, huzuni za utumwa unaokuja.

Yeremia 4

1 “Ikiwa utataka kurudi, ee Israeli,

nirudie mimi,”

asema Bwana.

“Ikiwa utaondoa sanamu zako za kuchukiza mbele ya macho yangu

na usiendelee kutangatanga,

2 ikiwa kwa kweli, kwa haki na kwa unyofu utaapa,

‘Kwa hakika kama vile Bwana aishivyo,’

ndipo mataifa yatakapobarikiwa naye

na katika yeye watajitukuza.”

3 Hili ndilo asemalo Bwana kwa watu wa Yuda na kwa Yerusalemu:

“Vunjeni mabonge kwenye mashamba yenu,

wala msipande katikati ya miiba.

4 Jitahirini katika Bwana,

tahirini mioyo yenu,

enyi wanaume wa Yuda

na watu wa Yerusalemu,

la sivyo ghadhabu yangu itatoka kwa nguvu

na kuwaka kama moto

kwa sababu ya uovu mliotenda,

ikiwaka pasipo wa kuizima.

5 “Tangaza katika Yuda na upige mbiu katika Yerusalemu na kusema:

‘Piga tarumbeta katika nchi yote!’

Piga kelele na kusema:

‘Kusanyikeni pamoja!

Tukimbilie katika miji yenye maboma!’

6 Onyesheni ishara ili kwenda Sayuni!

Kimbilieni usalama pasipo kuchelewa!

Kwa kuwa ninaleta maafa kutoka kaskazini,

maangamizi ya kutisha.”

7 Simba ametoka nje ya pango lake,

mharabu wa mataifa amejipanga.

Ametoka mahali pake

ili aangamize nchi yenu.

Miji yenu itakuwa magofu

pasipo mtu wa kuishi humo.

8 Hivyo vaeni nguo za magunia,

ombolezeni na kulia kwa huzuni,

kwa kuwa hasira kali ya Bwana

haijaondolewa kwetu.

9 “Katika siku ile,” asema Bwana

“mfalme na maafisa watakata tamaa,

makuhani watafadhaika,

na manabii watashangazwa mno.”

10 Ndipo niliposema, “Aa, Bwana Mwenyezi, umewadanganyaje kabisa watu hawa na Yerusalemu kwa kusema, ‘Mtakuwa na amani,’ wakati upanga uko kwenye koo zetu!”

11 Wakati huo watu hawa na Yerusalemu wataambiwa, “Upepo wa moto kutoka miinuko iliyo kame katika jangwa unavuma kuelekea watu wangu, lakini sio kupepeta au kutakasa, 12 upepo wenye nguvu sana kuliko wa kupepeta na kutakasa utakuja kwa amri yangu. Sasa natangaza hukumu zangu dhidi yao.”

13 Tazama! Anakuja kama mawingu,

magari yake yanakuja kama upepo wa kisulisuli,

farasi wake wana mbio kuliko tai.

Ole wetu! Tunaangamia!

14 Ee Yerusalemu, usafishe uovu kutoka moyoni mwako na uokolewe.

Utaendelea kuficha mawazo mapotovu mpaka lini?

15 Sauti inatangaza kutoka Dani,

ikipiga mbiu ya maafa kutoka vilima vya Efraimu.

16 “Waambie mataifa jambo hili,

piga mbiu hii dhidi ya Yerusalemu:

‘Jeshi la kuzingira linakuja kutoka nchi ya mbali,

likipiga kelele ya vita dhidi ya miji ya Yuda.

17 Wamemzunguka kama watu walindao shamba,

kwa sababu amefanya uasi dhidi yangu,’ ”

asema Bwana.

18 “Mwenendo wako na matendo yako mwenyewe

yameleta haya juu yako.

Hii ndiyo adhabu yako.

Tazama jinsi ilivyo chungu!

Tazama jinsi inavyochoma moyo!”

19 Ee mtima wangu, mtima wangu!

Ninagaagaa kwa maumivu.

Ee maumivu makuu ya moyo wangu!

Moyo wangu umefadhaika ndani yangu,

siwezi kunyamaza.

Kwa sababu nimesikia sauti ya tarumbeta,

nimesikia kelele ya vita.

20 Maafa baada ya maafa,

nchi yote imekuwa magofu.

Kwa ghafula mahema yangu yameangamizwa,

makazi yangu kwa muda mfupi.

21 Hata lini nitaendelea kuona bendera ya vita

na kusikia sauti za tarumbeta?

22 “Watu wangu ni wapumbavu,

hawanijui mimi.

Ni watoto wasio na akili,

hawana ufahamu.

Ni hodari kutenda mabaya,

hawajui kutenda yaliyo mema.”

23 Niliitazama dunia,

nayo haikuwa na umbo tena ni tupu;

niliziangalia mbingu,

mianga ilikuwa imetoweka.

24 Niliitazama milima, nayo ilikuwa ikitetemeka,

vilima vyote vilikuwa vikiyumbayumba.

25 Nilitazama, wala watu hawakuwepo;

kila ndege wa angani alikuwa ameruka zake.

26 Nilitazama, hata nchi iliyokuwa imestawi vizuri imekuwa jangwa,

miji yake yote ilikuwa magofu

mbele za Bwana,

mbele ya hasira yake kali.

27 Hivi ndivyo Bwana asemavyo:

“Nchi yote itaharibiwa,

ingawa sitaiangamiza kabisa.

28 Kwa hiyo dunia itaomboleza

na mbingu zilizo juu zitakuwa giza,

kwa sababu nimesema nami sitarudi nyuma,

nimeamua na wala sitageuka.”

29 Kwa sauti ya wapanda farasi na wapiga upinde

kila mji unakimbia.

Baadhi wanakimbilia vichakani,

baadhi wanapanda juu ya miamba.

Miji yote imeachwa,

hakuna aishiye ndani yake.

30 Unafanya nini, ewe uliyeharibiwa?

Kwa nini unajivika vazi jekundu

na kuvaa vito vya dhahabu?

Kwa nini unapaka macho yako rangi?

Unajipamba bure.

Wapenzi wako wanakudharau,

wanautafuta uhai wako.

31 Nasikia kilio kama cha mwanamke

katika utungu wa kuzaa,

kilio cha uchungu kama cha anayemzaa

mtoto wake wa kwanza:

kilio cha Binti Sayuni akitweta ili aweze kupumua,

akiinua mikono yake, akisema,

“Ole wangu! Ninazimia;

maisha yangu yamekabidhiwa kwa wauaji.”