Ayubu Anasisitiza Tena Uadilifu Wake (continued)

Ayubu anasisitiza tena uadilifu wake, na kulinganisha ustawi wake wa zamani na dhiki yake ya sasa.

2130 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Ayubu 28–29

1 “Kuna machimbo ya fedha,

na mahali dhahabu isafishwapo.

2 Chuma hupatikana ardhini,

nayo shaba huyeyushwa kutoka mawe ya madini.

3 Mwanadamu hukomesha giza;

huyatafuta hadi sehemu iliyo mbali,

kwa ajili ya kuchimbua mawe yenye madini

katika giza jeusi sana.

4 Huchimba shimo jembamba mbali na makao ya watu,

mahali paliposahaulika na nyayo za wanadamu;

mbali na wanadamu huningʼinia na kupembea kwa kamba.

5 Ardhi, ambako chakula hutoka,

chini hugeuzwa kwa moto;

6 yakuti samawi hutoka katika miamba yake,

nalo vumbi lake lina vipande vya dhahabu.

7 Hakuna ndege awindaye aijuaye njia ile iliyofichika,

wala hakuna jicho la mwewe lililoiona.

8 Wanyama wa porini wanaotamba hawajawahi kupakanyaga,

wala simba azungukaye huko.

9 Mikono ya mwanadamu hushambulia miamba migumu sana,

na kuiacha wazi mizizi ya milima.

10 Hutoboa shimo refu la kupenya chini kwa chini kwenye miamba;

macho yake huona hazina zake zote.

11 Hutafuta vyanzo vya mito

na kuvileta vitu vilivyofichika katika nuru.

12 “Lakini hekima inaweza kupatikana wapi?

Ufahamu unakaa wapi?

13 Mwanadamu hatambui thamani yake;

haiwezi kupatikana katika nchi ya walio hai.

14 Kilindi husema, ‘Haiko ndani yangu’;

bahari nayo husema, ‘Haiko pamoja nami.’

15 Haiwezi kununuliwa kwa dhahabu safi kuliko zote,

wala thamani yake haiwezi kupimwa kwa fedha.

16 Haiwezi kununuliwa kwa dhahabu ya Ofiri,

kwa shohamu ya thamani kubwa au yakuti samawi ya thamani kubwa.

17 Dhahabu wala mawe maangavu haviwezi kulinganishwa nayo,

wala haiwezi hubadilishwa na vito vya dhahabu.

18 Marijani na yaspi hazistahili kutajwa;

thamani ya hekima ni zaidi ya akiki nyekundu.

19 Yakuti manjano ipatikanayo Kushi haiwezi kulinganishwa nayo,

wala haiwezi kununuliwa kwa dhahabu safi.

20 “Ni wapi basi hekima itokako?

Ufahamu hukaa wapi?

21 Imefichika machoni pa kila kitu kilicho hai,

imesitiriwa hata kwa ndege wa angani.

22 Uharibifu na Mauti husema,

‘Ni uvumi wake tu uliotufikia masikioni mwetu.’

23 Mungu anaifahamu njia ya kuiendea hekima

na ndiye peke yake anayefahamu inakokaa,

24 kwa maana yeye huitazama miisho ya dunia

na huona kila kitu chini ya mbingu.

25 Alipofanyiza nguvu za upepo

na kuyapima maji,

26 alipofanya maagizo kwa ajili ya mvua

na njia kwa ajili ya umeme wa radi,

27 ndipo alipoitazama hekima na kuikadiria thamani yake,

akaithibitisha na kuihakikisha.

28 Naye Mungu akamwambia mwanadamu,

‘Kumcha Bwana: hiyo ndiyo hekima,

nako kujitenga na uovu ndio ufahamu.’ ”

29:1 Ayubu akaendelea na hoja yake, akasema:

2 “Tazama jinsi ninavyoitamani miezi iliyopita,

zile siku ambazo Mungu alikuwa akinilinda,

3 wakati taa yake iliniangazia kichwani changu,

na kwa mwanga wake Mungu nikapita katikati ya giza!

4 Natamani siku zile nilizokuwa katika ustawi wangu,

wakati urafiki wa Mungu wa ndani ulipoibariki nyumba yangu,

5 wakati Mwenyezi alikuwa pamoja nami,

nao watoto wangu walikuwa wamenizunguka,

6 wakati njia yangu ilikuwa imenyweshewa siagi,

nao mwamba ukanimiminia vijito vya mafuta ya zeituni.

7 “Wakati nilipokwenda kwenye lango la mji

na kuketi katika kiwanja,

8 vijana waliniona wakakaa kando,

nao wazee walioketi wakasimama;

9 wakuu wakaacha kuzungumza

na kuziba vinywa vyao kwa mikono yao;

10 wenye vyeo wakanyamazishwa,

nazo ndimi zao zikagandamana na makaakaa ya vinywa vyao.

11 Yeyote aliyenisikia alinena mema juu yangu,

nao walioniona walinisifu,

12 kwa sababu nilimwokoa maskini aliyeomba msaada,

naye yatima aliyekuwa hana wa kumsaidia.

13 Mtu aliyekuwa karibu kufa alinibariki,

nami niliufanya moyo wa mjane kuimba.

14 Niliivaa haki kama vazi langu;

uadilifu ulikuwa joho langu na kilemba changu.

15 Nilikuwa macho ya kipofu

na miguu kwa kiwete.

16 Nilikuwa baba kwa mhitaji;

nilimtetea mgeni.

17 Niliyavunja meno makali ya waovu,

na kuwapokonya wahanga kwenye meno yao.

18 “Nikafikiri, ‘Nitafia katika nyumba yangu mwenyewe,

nazo siku zangu zitakuwa nyingi kama chembechembe za mchanga.

19 Mizizi yangu itafika mpaka kwenye maji,

nao umande utakaa juu ya matawi yangu usiku kucha.

20 Utukufu wangu utabakia kuwa mpya ndani yangu,

upinde wangu daima utaendelea kuwa mpya mkononi mwangu.’

21 “Watu walinisikiliza kwa tumaini,

wakingojea ushauri wangu kwa utulivu.

22 Baada ya mimi kuzungumza, hawakusema zaidi;

maneno yangu yaliingia masikioni mwao kwa makini.

23 Waliningojea kama manyunyu ya mvua

na kuyapokea maneno yangu

kama ardhi inyonyavyo mvua ya vuli.

24 Walipokata tamaa niliwaonyesha uso wa furaha;

nuru ya uso wangu ilikuwa ya thamani kwao.

25 Niliwachagulia njia na kukaa kama mkuu wao;

niliishi kama mfalme katikati ya majeshi yake;

nikawa kama yeye anayewafariji waombolezaji.