Bildadi Anaendeleza Hoja Tena

2130 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Ayubu 25

1 Ndipo Bildadi Mshuhi akajibu:

2 “Mamlaka na kuheshimiwa ni vyake Mungu;

yeye huthibitisha amani katika mbingu juu.

3 Je, majeshi yake yaweza kuhesabika?

Ni nani asiyeangaziwa na nuru yake?

4 Mtu awezaje kuwa mwadilifu mbele za Mungu?

Awezaje mtu aliyezaliwa na mwanamke kuwa safi?

5 Ikiwa hata mwezi sio mwangavu

nazo nyota si safi machoni pake,

6 sembuse mtu ambaye ni funza:

mwanadamu ambaye ni buu tu!”

Ayubu Anasisitiza Tena Uadilifu Wake

Ayubu anasisitiza tena uadilifu wake, na kulinganisha ustawi wake wa zamani na dhiki yake ya sasa.

Ayubu 26–27

1 Kisha Ayubu akajibu:

2 “Tazama jinsi ulivyomsaidia mtu asiye na uwezo!

Jinsi ulivyouokoa mkono ulio dhaifu!

3 Ni shauri gani ulilompa yeye asiye na hekima?

Nayo ni busara gani kubwa uliyoonyesha!

4 Ni nani aliyekusaidia kutamka maneno hayo?

Nayo ni roho ya nani iliyosema kutoka kinywani mwako?

5 “Wafu wako katika maumivu makuu,

wale walio chini ya maji na wale waishio ndani yake.

6 Mauti iko wazi mbele za Mungu;

Uharibifu haukufunikwa.

7 Hutandaza anga la kaskazini mahali patupu;

naye huiningʼiniza dunia mahali pasipo na kitu.

8 Huyafungia maji kwenye mawingu yake,

hata hivyo mawingu hayapasuki kwa uzito wake.

9 Huufunika uso wa mwezi mpevu,

akitandaza mawingu juu yake.

10 Amechora mstari wa upeo juu ya uso wa maji,

ameweka mpaka wa nuru na giza.

11 Nguzo za mbingu nazo zatetemeka,

zinatishika anapozikemea.

12 Kwa nguvu zake aliisukasuka bahari;

kwa hekima yake alimkata Rahabu vipande vipande.

13 Aliisafisha anga kwa pumzi yake;

kwa mkono wake alimchoma joka aendaye mbio.

14 Haya ni mambo madogo tu katika matendo yake;

tazama jinsi ulivyo mdogo mnongʼono tunaousikia kumhusu!

Ni nani basi awezaye kuelewa

ngurumo za nguvu zake?”

27:1 Ndipo Ayubu akaendelea na hoja yake, akasema:

2 “Hakika kama Mungu aishivyo, aliyeninyima haki yangu,

Mwenyezi ambaye amenifanya

nionje uchungu wa nafsi,

3 kwa muda wote nitakaokuwa na uhai ndani yangu,

nayo pumzi ya Mungu ikiwa puani mwangu,

4 midomo yangu haitanena uovu,

wala ulimi wangu hautatamka udanganyifu.

5 Sitakubaliana nanyi kabisa kuwa mko sahihi;

hadi nife, sitakana uadilifu wangu.

6 Nitadumisha haki yangu wala sitaiacha;

dhamiri yangu haitanisuta muda wote ninaoishi.

7 “Watesi wangu wawe kama waovu,

nao adui zangu wawe kama wasio haki!

8 Kwa maana mtu asiyemcha Mungu

analo tegemeo gani anapokatiliwa mbali,

Mungu anapouondoa uhai wake?

9 Je, Mungu husikiliza kilio chake,

shida zimjiapo?

10 Je, anaweza kumfurahia Mwenyezi?

Je, atamwita Mungu nyakati zote?

11 “Nitawafundisha juu ya uweza wa Mungu;

njia za Mwenyezi sitazificha.

12 Ninyi nyote mmeona hili wenyewe.

Ni ya nini basi mazungumzo haya yasiyo na maana?

13 “Hili ndilo fungu ambalo Mungu humpa mtu mwovu,

urithi ule mtu mdhalimu anapokea kutoka kwa Mwenyezi:

14 Hata kama watoto wake watakuwa wengi kiasi gani,

fungu lao ni kuuawa kwa upanga;

wazao wake hawatakuwa kamwe

na chakula cha kuwatosha.

15 Tauni itawazika wale watakaonusurika miongoni mwao,

nao wajane wao hawatawaombolezea.

16 Ajapokusanya fedha nyingi kama mavumbi,

na mavazi kama malundo ya udongo wa mfinyanzi,

17 yale yote mtu mwovu aliyojiwekea akiba, mwenye haki atayavaa,

naye asiye na hatia ataigawanya fedha yake.

18 Nyumba aijengayo ni kama utando wa buibui,

kama kibanda alichotengeneza mlinzi.

19 Yeye hulala akiwa tajiri, lakini ndiyo mara ya mwisho;

afunguapo macho yake, yote yametoweka.

20 Vitisho humjia kama mafuriko;

dhoruba humkumba ghafula usiku.

21 Upepo mkali wa mashariki humchukua, naye hutoweka;

humzoa kutoka mahali pake.

22 Humvurumisha bila huruma,

huku akikimbia kasi kukwepa nguvu zake.

23 Upepo humpigia makofi kwa dharau,

na kumfukuza atoke mahali pake.