Sehemu ya 10: Huduma ya Baadaye Huko Perea
Yamkini kuanzia Sikukuu ya Kuwekwa Wakfu mwaka wa 29 BK hadi safari ya mwisho mwaka wa 30 BK (karibu miezi mitatu na nusu)
Yesu Anajiondoa Kwenda Bethania Ng'ambo ya Yordani
Yesu anajiondoa Yerusalemu kwenda Bethania ng'ambo ya Yordani.
Pereya
29 hadi 30 BK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
Yohana 10:40–42
10:40 Akaenda tena ngʼambo ya Mto Yordani mpaka mahali pale ambapo Yohana alikuwa akibatiza hapo awali, naye akakaa huko. 41 Watu wengi wakamjia, nao wakawa wakisema, “Yohana hakufanya muujiza wowote, lakini kila jambo alilosema kumhusu huyu mtu ni kweli.” 42 Nao wengi wakamwamini Yesu huko.
Yesu Anafundisha Perea na Anaonywa Kuhusu Herode
Yesu anafundisha huko Perea, akiwa safarini kuelekea Yerusalemu, na anaonywa kuhusu Herode Antipa.
Luka 13:22–35
13:22 Yesu akapita katika miji na vijiji, akifundisha wakati alisafiri kwenda Yerusalemu. 23 Mtu mmoja akamuuliza, “Bwana, ni watu wachache tu watakaookolewa?”
24 Yesu akawaambia, “Jitahidini sana kuingia kupitia mlango mwembamba, kwa maana nawaambia wengi watajaribu kuingia, lakini hawataweza. 25 Wakati mwenye nyumba atakapoondoka na kufunga mlango, mtasimama nje mkibisha mlango na kusema, ‘Bwana! Tufungulie mlango!’
“Lakini yeye atawajibu, ‘Siwajui ninyi, wala mtokako.’
26 “Ndipo mtamjibu, ‘Tulikula na kunywa pamoja nawe, tena ulifundisha katika mitaa yetu.’
27 “Lakini yeye atawajibu, ‘Siwajui ninyi, wala mtokako. Ondokeni kwangu, ninyi watenda maovu!’
28 “Ndipo kutakuwako kilio na kusaga meno, mtakapowaona Abrahamu, Isaki, Yakobo na manabii wote wakiwa katika Ufalme wa Mungu, lakini ninyi mkiwa mmetupwa nje. 29 Watu watatoka mashariki na magharibi, kaskazini na kusini, nao wataketi kwenye sehemu walizoandaliwa karamuni katika Ufalme wa Mungu. 30 Tazama, kunao walio wa mwisho watakaokuwa wa kwanza, nao wa kwanza watakaokuwa wa mwisho.”
31 Wakati huo huo baadhi ya Mafarisayo wakamwendea Yesu na kumwambia, “Ondoka hapa uende mahali pengine kwa maana Herode anataka kukuua.”
32 Yesu akawajibu, “Nendeni mkamwambie yule mbweha, ‘Ninafukuza pepo wachafu na kuponya wagonjwa leo na kesho, nami siku ya tatu nitaikamilisha kazi yangu.’ 33 Sina budi kuendelea na safari yangu leo, kesho na kesho kutwa: kwa maana haiwezekani nabii kufa mahali pengine isipokuwa Yerusalemu.
34 “Ee Yerusalemu, Yerusalemu, uwauaye manabii na kuwapiga mawe wale waliotumwa kwako! Mara ngapi nimetamani kuwakusanya watoto wako pamoja, kama vile kuku akusanyavyo vifaranga wake chini ya mabawa yake, lakini hukutaka! 35 Tazama nyumba yenu imeachwa ukiwa. Ninawaambia, hamtaniona tena mpaka wakati ule mtakaposema, ‘Amebarikiwa yeye ajaye kwa jina la Bwana.’ ”
Akiwa Anakula na Farisayo Mwenye Cheo, Yesu Anaponya Tena
Akiwa anakula (chakula cha asubuhi) na Farisayo mwenye cheo, Yesu anaponya tena siku ya Sabato na kujitetea. Tukio hilo linampa nafasi ya kutoa mifano mitatu.
Yamkini huko Perea
Luka 14:1–24
14:1 Ikawa siku moja Yesu alipokuwa amekwenda kula chakula kwa mmoja wa viongozi wa Mafarisayo siku ya Sabato, watu walikuwa wakimchunguza kwa bidii. 2 Papo hapo mbele yake palikuwa na mtu mmoja mwenye ugonjwa wa kuvimba mwili. 3 Yesu akawauliza wale Mafarisayo na walimu wa sheria, “Je, ni halali kuponya watu siku ya Sabato au la?” 4 Wakakaa kimya. Hivyo Yesu akamshika yule mgonjwa mkono na kumponya, akamruhusu aende zake.
5 Kisha akawauliza, “Kama mmoja wenu angekuwa na mtoto au ngʼombe wake aliyetumbukia katika kisima siku ya Sabato, je, hamtamvuta mara moja na kumtoa?” 6 Nao hawakuwa na la kusema.
7 Alipoona jinsi wageni walivyokuwa wanachagua mahali pa heshima wakati wa kula, akawaambia mfano huu: 8 “Mtu akikualika arusini, usikae mahali pa mgeni wa heshima kwa kuwa inawezekana amealikwa mtu mheshimiwa kuliko wewe. 9 Kama mkifanya hivyo yule aliyewaalika ninyi wawili atakuja na kukuambia, ‘Mpishe huyu mtu kiti chako.’ Ndipo kwa aibu utalazimika kukaa katika nafasi ya chini kabisa. 10 Badala yake, unapoalikwa, chagua nafasi ya chini, ili yule mwenyeji wako atakapokuona atakuja na kukuambia, ‘Rafiki yangu, nenda kwenye nafasi iliyo bora zaidi.’ Kwa jinsi hii utakuwa umepewa heshima mbele ya wageni wenzako wote. 11 Kwa maana kila mtu ajikwezaye atashushwa, naye ajishushaye atakwezwa.”
12 Kisha Yesu akamwambia yule aliyewaalika, “Uandaapo karamu ya chakula cha mchana au cha jioni, usialike rafiki zako au ndugu zako au jamaa zako au majirani zako walio matajiri tu. Ukifanya hivyo, wao nao wanaweza kukualika kwao, nawe ukawa umelipwa kile ulichofanya na kupata thawabu yako. 13 Bali ufanyapo karamu, waalike maskini, vilema na vipofu, 14 nawe utabarikiwa kwa sababu hawa hawana uwezo wa kukulipa. Mungu atakulipa wakati wa ufufuo wa wenye haki.”
15 Mmoja wa wale waliokuwa pamoja naye mezani aliposikia hivi akamwambia Yesu, “Amebarikiwa mtu yule atakayekula katika karamu ya Ufalme wa Mungu!”
16 Yesu akamjibu, “Mtu mmoja alikuwa anaandaa karamu kubwa, akaalika watu wengi. 17 Wakati wa karamu ulipofika, akamtuma mtumishi wake akawaambie wale walioalikwa, ‘Karibuni, kila kitu ki tayari sasa.’
18 “Lakini wote, kila mmoja, wakaanza kutoa udhuru: Wa kwanza akasema, ‘Nimenunua shamba, lazima niende kuliona. Tafadhali niwie radhi.’
19 “Mwingine akasema, ‘Ndipo tu nimenunua jozi tano za ngʼombe wa kulimia, nami ninakwenda kuwajaribu, tafadhali niwie radhi.’ 20 Naye mwingine akasema, ‘Nimeoa mke, kwa hiyo siwezi kuja.’
21 “Yule mtumishi akarudi, akampa bwana wake taarifa. Ndipo yule mwenye nyumba akakasirika, akamwagiza yule mtumishi wake, akisema, ‘Nenda upesi kwenye mitaa na vichochoro vya mjini uwalete maskini, vilema, vipofu na viwete.’
22 “Yule mtumishi akamwambia, ‘Bwana, yale uliyoniagiza nimefanya, lakini bado ipo nafasi.’
23 “Ndipo yule bwana akamwambia mtumishi wake, ‘Nenda kwenye barabara na vijia vilivyoko nje ya mji na uwalazimishe watu waingie ili nyumba yangu ipate kujaa. 24 Kwa maana nawaambia, hakuna hata mmoja wa wale walioalikwa atakayeionja karamu yangu.’ ”