Wote Lazima Watubu au Waangamie
Wote lazima watubu au waangamie (misiba miwili ya wakati huo). Mfano wa mtini usiozaa matunda.
Inaelekea huko Uyahudi
29 au 28 BK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
Luka 13:1–9
13:1 Wakati huo huo, kulikuwa na watu waliomwambia Yesu habari za Wagalilaya ambao Pilato aliwaua, na damu ya hao watu akaichanganya na dhabihu yao waliyokuwa wanatoa. 2 Yesu akawauliza, “Mnadhani kwamba hawa Wagalilaya ambao walikufa kifo cha namna hiyo walikuwa na dhambi kuwazidi Wagalilaya wengine wote? 3 La hasha! Ninyi nanyi msipotubu, mtaangamia vivyo hivyo. 4 Au wale watu kumi na wanane waliokufa walipoangukiwa na mnara huko Siloamu: mnadhani wao walikuwa waovu kuliko watu wote waliokuwa wanaishi Yerusalemu? 5 Nawaambia, la hasha! Ninyi nanyi msipotubu, wote mtaangamia vivyo hivyo.”
6 Kisha Yesu akawaambia mfano huu: “Mtu mmoja alikuwa na mtini uliopandwa katika shamba lake la mizabibu, akaja ili kutafuta tini kwenye mti huo, lakini hakupata hata moja. 7 Hivyo akamwambia mtunza shamba: ‘Tazama, kwa muda wa miaka mitatu sasa nimekuwa nikija kutafuta matunda kwenye mtini huu, nami sikupata hata moja. Ukate! Kwa nini uendelee kuharibu ardhi?’
8 “Yule mtunza shamba akamjibu, ‘Bwana, uache tena kwa mwaka mmoja zaidi, nami nitaupalilia na kuuwekea mbolea. 9 Kama ukizaa matunda mwaka ujao, vyema, la sivyo uukate.’ ”
Yesu Anamponya Mwanamke Kilema Siku ya Sabato
Yesu anamponya mwanamke kilema siku ya Sabato na kujitetea dhidi ya mkuu wa sinagogi. Anarudia mifano ya mbegu ya haradali na ya chachu.
Luka 13:10–21
13:10 Basi Yesu alikuwa akifundisha katika sinagogi mojawapo siku ya Sabato. 11 Wakati huo huo akaja mwanamke mmoja aliyekuwa na pepo mchafu, naye alikuwa amepinda mgongo kwa muda wa miaka kumi na minane, wala alikuwa hawezi kunyooka wima. 12 Yesu alipomwona, akamwita, akamwambia, “Mwanamke, uwe huru, umepona ugonjwa wako.” 13 Yesu alipomwekea mikono yake, mara akasimama wima akaanza kumtukuza Mungu.
14 Lakini kiongozi wa sinagogi akakasirika kwa sababu Yesu alikuwa ameponya mtu siku ya Sabato. Akaambia ule umati wa watu, “Kuna siku sita ambazo watu wanapaswa kufanya kazi. Katika siku hizo, njooni mponywe, lakini si katika siku ya Sabato.”
15 Lakini Bwana akamjibu, “Enyi wanafiki! Je, kila mmoja wenu hamfungulii ngʼombe wake au punda wake kutoka zizini akampeleka kumnywesha maji siku ya Sabato? 16 Je, huyu mwanamke, ambaye ni binti wa Abrahamu, aliyeteswa na Shetani akiwa amemfunga kwa miaka yote hii kumi na minane, hakustahili kufunguliwa kutoka kifungo hicho siku ya Sabato?”
17 Aliposema haya, wapinzani wake wakaaibika, lakini watu wakafurahi kwa ajili ya mambo ya ajabu aliyoyafanya.
18 Kisha Yesu akauliza, “Ufalme wa Mungu unafanana na nini? Nitaufananisha na nini? 19 Umefanana na punje ya haradali ambayo mtu aliichukua na kuipanda katika shamba lake. Nayo ikakua, ikawa mti nao ndege wa angani wakatengeneza viota vyao kwenye matawi yake.”
20 Yesu akauliza tena, “Nitaufananisha Ufalme wa Mungu na nini? 21 Unafanana na chachu ambayo mwanamke aliichukua akaichanganya katika kiasi kikubwa cha unga mpaka wote ukaumuka.”
Katika Sikukuu ya Kuwekwa Wakfu, Wayahudi Wanajaribu Kumpiga Yesu Mawe
Katika Sikukuu ya Kuwekwa Wakfu, Yesu bado hataki kusema wazi kwamba yeye ndiye Masiya. Wayahudi wanajaribu kumpiga mawe.
Hapa Injili ya Yohana inaendelea tena na simulizi, ikitupeleka Yerusalemu, kisha Perea.
Yerusalemu
Yohana 10:22–39
10:22 Wakati huo ilikuwa Sikukuu ya Kuwekwa wakfu kwa Hekalu huko Yerusalemu, nao ulikuwa wakati wa majira ya baridi. 23 Naye Yesu alikuwa akitembea ndani ya Hekalu katika ukumbi wa Solomoni. 24 Wayahudi wakamkusanyikia wakamuuliza, “Utatuweka katika hali ya mashaka mpaka lini? Kama wewe ndiye Kristo tuambie waziwazi.”
25 Yesu akawajibu, “Nimewaambia, lakini hamwamini. Mambo ninayoyatenda kwa jina la Baba yangu yananishuhudia. 26 Lakini hamwamini, kwa sababu ninyi si wa kundi la kondoo wangu. 27 Kondoo wangu huisikia sauti yangu nami nawajua, nao hunifuata, 28 nami ninawapa uzima wa milele, hawataangamia kamwe wala hakuna mtu atakayewapokonya kutoka mikono yangu. 29 Baba yangu aliyenipa hawa ni mkuu kuliko wote na hakuna awezaye kuwapokonya kutoka mikononi mwake. 30 Mimi na Baba yangu tu umoja.”
31 Kwa mara nyingine Wayahudi wakainua mawe ili wampige nayo, 32 lakini Yesu akawaambia, “Nimewaonyesha miujiza mingi mikubwa kutoka kwa Baba yangu. Ni ipi katika hiyo mnataka kunipiga mawe?”
33 Wayahudi wakamjibu, “Hatukupigi mawe kwa sababu ya mambo mema uliyotenda, bali ni kwa kuwa umekufuru. Wewe ingawa ni mwanadamu unajifanya kuwa Mungu.”
34 Yesu akawajibu, “Je, haikuandikwa katika Sheria ya kwamba, ‘Nimesema kuwa, ninyi ni miungu?’ 35 Kama aliwaita ‘miungu,’ wale ambao neno la Mungu liliwafikia, nayo Maandiko hayawezi kutanguka, 36 je, mwawezaje kusema kwamba yule ambaye Baba amemweka wakfu na kumtuma ulimwenguni anakufuru, kwa sababu nilisema, ‘Mimi ni Mwana wa Mungu?’ 37 Ikiwa sifanyi kazi za Baba yangu, basi msiniamini, 38 lakini ikiwa nazifanya kazi za Mungu, hata kama hamniamini mimi ziaminini hizo kazi, ili mpate kujua na kuelewa kwamba Baba yu ndani yangu, nami ndani yake.” 39 Ndipo wakajaribu kumkamata kwa mara nyingine, lakini akaponyoka kutoka mikononi mwao.