Yesu Analipa Kodi ya Hekalu ya Nusu Shekeli

Yesu, Masiya, analipa nusu shekeli kwa ajili ya hekalu.

Kipindi cha kujiondoa kutoka Galilaya sasa kimekwisha. Inaelekea matukio yaliyobaki ya kipindi hiki yalichukua siku chache tu.

Kapernaumu

29 au 28 BK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Mathayo 17:24–27

17:24 Baada ya Yesu na wanafunzi wake kufika Kapernaumu, wakusanya kodi ya Hekalu wakamjia Petro na kumuuliza, “Je, Mwalimu wenu halipi kodi ya Hekalu?”

25 Petro akajibu, “Ndiyo, yeye hulipa.” Petro aliporudi nyumbani, Yesu akawa wa kwanza kulizungumzia, akamuuliza, “Unaonaje Simoni? Wafalme wa dunia hupokea ushuru na kodi kutoka kwa nani? Je, ni kutoka kwa watoto wao au kutoka kwa watu wengine?”

26 Petro akamjibu, “Kutoka kwa watu wengine.” Yesu akamwambia, “Kwa hiyo watoto wao wamesamehewa. 27 Lakini ili tusije tukawaudhi, nenda baharini ukatupe ndoana. Mchukue samaki wa kwanza utakayemvua. Fungua kinywa chake nawe utakuta humo fedha, ichukue ukalipe kodi yako na yangu.”

Wale Kumi na Wawili Wanabishana Kuhusu Nani Aliye Mkuu Zaidi

Wale Kumi na Wawili wanabishana kuhusu nani atakayekuwa mkuu zaidi chini ya utawala wa Masiya. Raia wake lazima wawe kama watoto.

Kapernaumu

Mathayo 18:1–5

18:1 Wakati huo, wanafunzi wakamjia Yesu na kumuuliza, “Je, nani aliye mkuu kuliko wote katika Ufalme wa Mbinguni?”

2 Yesu akamwita mtoto mdogo na kumsimamisha katikati yao. 3 Naye akasema: “Amin, nawaambia, msipookoka na kuwa kama watoto wadogo, kamwe hamtaingia katika Ufalme wa Mbinguni.

4 Kwa hiyo mtu yeyote anyenyekeaye kama huyu mtoto, ndiye aliye mkuu kuliko wote katika Ufalme wa Mbinguni.

5 “Yeyote amkaribishaye mtoto mdogo kama huyu kwa Jina langu, anikaribisha mimi.

Marko 9:33–37

9:33 Basi wakafika Kapernaumu na baada ya kuingia nyumbani akawauliza, “Mlikuwa mnabishana nini kule njiani?” 34 Lakini hawakumjibu, kwa sababu njiani walikuwa wakibishana kuhusu nani miongoni mwao alikuwa mkuu zaidi ya wote.

35 Akaketi chini, akawaita wote kumi na wawili, akawaambia: “Kama mtu yeyote akitaka kuwa wa kwanza, hana budi kuwa wa mwisho na mtumishi wa wote.”

36 Kisha akamchukua mtoto mdogo, akamsimamisha katikati yao. Akamkumbatia, akawaambia,

37 “Mtu yeyote amkaribishaye mmoja wa hawa watoto wadogo kwa Jina langu, anikaribisha mimi. Naye anikaribishaye mimi, amkaribisha Baba yangu aliyenituma.”

Luka 9:46–48

9:46 Kukazuka mabishano miongoni mwa wanafunzi kuhusu ni nani miongoni mwao atakayekuwa mkuu kuliko wote.

47 Lakini Yesu akayatambua mawazo yao, naye akamchukua mtoto mdogo, akamsimamisha kando yake.

48 Kisha akawaambia, “Yeyote amkaribishaye mtoto huyu mdogo kwa Jina langu, anikaribisha mimi, na yeyote atakayenikaribisha mimi, atakuwa amemkaribisha yeye aliyenituma. Kwa maana yeye aliye mdogo miongoni mwenu, ndiye aliye mkuu kuliko wote.”

Yesu Anakemea Bidii ya Yohana Isiyo na Uelewa Sahihi

Yesu anakemea bidii potovu ya mtume Yohana kwa kutumia mifano mwafaka ya kimafumbo.

Kapernaumu

Mathayo 18:6–14

18:6 Lakini kama mtu yeyote akimsababisha mmojawapo wa hawa wadogo wanaoniamini kutenda dhambi, ingekuwa bora kwake afungiwe jiwe kubwa la kusagia shingoni mwake, na kutoswa katika kilindi cha bahari.

7 “Ole kwa ulimwengu kwa sababu ya yale mambo yanayosababisha watu kutenda dhambi! Mambo hayo lazima yawepo, lakini ole wake mtu yule ambaye huyasababisha.

8 Ikiwa mkono wako au mguu wako unakusababisha utende dhambi, ukate na uutupe mbali. Ni afadhali kwako kuingia katika uzima ukiwa huna mkono mmoja au mguu mmoja, kuliko kuwa na mikono miwili au miguu miwili, na kutupwa katika moto wa milele.

9 Nalo jicho lako likikusababisha kutenda dhambi, lingʼoe, ulitupe mbali. Ni afadhali kwako kuingia katika uzima ukiwa na jicho moja, kuliko kuwa na macho mawili lakini ukatupwa katika moto wa jehanamu.

10 “Angalia ili usimdharau mmojawapo wa hawa wadogo, kwa maana nawaambia, malaika wao mbinguni daima wanauona uso wa Baba yangu aliye mbinguni. [ 11 Kwa maana Mwana wa Adamu alikuja kuokoa kile kilichopotea.]

12 “Mwaonaje? Ikiwa mtu ana kondoo mia moja, na mmoja wao akapotea, je, hatawaacha wale tisini na tisa vilimani na kwenda kumtafuta huyo mmoja aliyepotea? 13 Naye akishampata, amin, nawaambia, hufurahi zaidi kwa ajili ya huyo kondoo mmoja kuliko wale tisini na tisa ambao hawakupotea. 14 Vivyo hivyo, Baba yenu wa mbinguni hapendi hata mmojawapo wa hawa wadogo apotee.

Marko 9:38–50

9:38 Yohana akamwambia, “Mwalimu, tumemwona mtu akitoa pepo wachafu kwa jina lako, nasi tukamkataza, kwa sababu yeye si mmoja wetu.”

39 Yesu akasema, “Msimkataze, kwa kuwa hakuna yeyote atendaye miujiza kwa Jina langu ambaye baada ya kitambo kidogo aweza kunena lolote baya dhidi yangu. 40 Kwa maana yeyote asiye kinyume chetu, yuko upande wetu. 41 Amin, nawaambia, yeyote awapaye ninyi kikombe cha maji kwa Jina langu kwa sababu ninyi ni mali ya Kristo, hakika hataikosa thawabu yake.”

42 “Kama mtu yeyote akimsababisha mmojawapo wa wadogo hawa wanaoniamini kutenda dhambi, ingekuwa bora kwake afungiwe jiwe kubwa la kusagia shingoni mwake, na kutoswa baharini.

43 Kama mkono wako ukikusababisha kutenda dhambi, ukate. Ni afadhali kwako kuingia katika uzima ukiwa na mkono mmoja, kuliko kuwa na mikono miwili lakini ukaingia jehanamu, mahali ambako moto hauzimiki. [ 44 Mahali ambako funza wake hawafi wala moto wake hauzimiki.] 45 Kama mguu wako ukikusababisha kutenda dhambi, ukate. Ni afadhali kwako kuingia katika uzima ukiwa kiwete, kuliko kuwa na miguu miwili lakini ukaingia jehanamu. [ 46 Mahali ambako funza wake hawafi wala moto hauzimiki.]

47 Nalo jicho lako likikusababisha kutenda dhambi, lingʼoe. Ni afadhali kwako kuingia katika Ufalme wa Mungu ukiwa na jicho moja, kuliko kuwa na macho mawili lakini ukatupwa jehanamu,

48 mahali ambako

“ ‘funza wake hawafi,

wala moto wake hauzimiki.’

49 Kila mmoja atatiwa chumvi kwa moto.

50 “Chumvi ni nzuri, lakini ikipoteza ladha yake utaifanyaje ili iweze kukolea tena? Mwe na chumvi ndani yenu, mkaishi kwa amani, kila mmoja na mwenzake.”

Luka 9:49–50

9:49 Yohana akasema, “Bwana, tumemwona mtu akitoa pepo wachafu kwa jina lako, nasi tukamzuia, kwa sababu yeye si mmoja wetu.”

50 Yesu akasema, “Msimzuie, kwa sababu yeyote ambaye si kinyume nanyi, yu upande wenu.”