Jinsi ya Kumtendea na Kumsamehe Ndugu Anayetenda Dhambi
Njia sahihi ya kumtendea ndugu aliyekukosea, na wajibu wa kumsamehe ndugu kwa uvumilivu (mfano wa mtumishi asiye na huruma).
29 au 28 BK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
Mathayo 18:15–35
18:15 “Kama ndugu yako akikukosea, nenda ukamwonyeshe kosa lake, kati yenu ninyi wawili peke yenu. Kama akikusikiliza, utakuwa umempata tena ndugu yako. 16 Lakini kama hatakusikiliza, nenda na mtu mwingine mmoja au wawili ili kila neno lithibitishwe kwa ushahidi wa mashahidi wawili au watatu. 17 Kama akikataa kuwasikiliza hao, liambie kanisa. Naye kama akikataa hata kulisikiliza kanisa, basi awe kwenu kama mtu asiyeamini au mtoza ushuru.
18 “Amin, nawaambia, lolote mtakalolifunga duniani litakuwa limefungwa mbinguni, na lolote mtakalolifungua duniani litakuwa limefunguliwa mbinguni.
19 “Tena nawaambia, ikiwa wawili wenu watakubaliana duniani kuhusu jambo lolote watakaloomba, watafanyiwa na Baba yangu aliye mbinguni. 20 Kwa kuwa wanapokusanyika pamoja watu wawili au watatu kwa Jina langu, mimi niko papo hapo pamoja nao.”
21 Ndipo Petro akamjia Yesu na kumuuliza, “Bwana, ndugu yangu anikosee mara ngapi nami nimsamehe? Je, hata mara saba?”
22 Yesu akamjibu, “Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini.
23 “Kwa hiyo Ufalme wa Mbinguni unaweza kufananishwa na mfalme aliyetaka kufanya hesabu zake za fedha na watumishi wake. 24 Alipoanza kufanya hesabu zake, mtu mmoja aliyekuwa anadaiwa talanta 10,000, aliletwa kwake. 25 Kwa kuwa alikuwa hawezi kulipa deni hilo, bwana wake akaamuru kwamba auzwe, yeye, mkewe, watoto wake na vyote alivyokuwa navyo, ili lile deni lipate kulipwa.
26 “Yule mtumishi akampigia magoti, akamsihi yule bwana akisema, ‘Naomba univumilie, nami nitakulipa deni lako lote.’ 27 Yule bwana wa huyo mtumishi akamwonea huruma, akafuta deni lake lote, akamwacha aende zake.
28 “Lakini yule mtumishi alipokuwa anatoka nje, akakutana na mtumishi mwenzake aliyekuwa amemkopesha dinari mia moja. Akamkamata, akamkaba koo akimwambia, ‘Nilipe kile ninachokudai!’
29 “Yule mtumishi mwenzake akapiga magoti akamsihi akisema, ‘Naomba univumilie, nami nitakulipa deni lako lote.’
30 “Lakini akakataa. Badala yake, alienda akamtupa gerezani hata atakapolipa hilo deni. 31 Watumishi wenzake walipoona haya yaliyotukia wakaudhika sana, nao wakaenda na kumwambia bwana wao kila kitu kilichokuwa kimetukia.
32 “Yule bwana akamwita yule mtumishi akamwambia, ‘Wewe mtumishi mwovu! Mimi nilikusamehe deni lako lote uliponisihi. 33 Je, haikukupasa kumhurumia mtumishi mwenzako kama mimi nilivyokuhurumia wewe?’ 34 Kwa hasira, yule bwana wake akamtia yule mtumishi mikononi mwa askari wa gereza ili ateswe mpaka atakapolipa yote aliyokuwa anadaiwa.
35 “Hivi ndivyo Baba yangu wa mbinguni atakavyomfanyia kila mmoja wenu ikiwa hatamsamehe ndugu yake kutoka moyoni mwake.”
Wafuasi wa Masiya Lazima Waache Kila Kitu
Wafuasi wa Masiya lazima waache kila kitu ili wamtumikie.
Mathayo 8:19–22
8:19 Kisha mwalimu mmoja wa sheria akamjia Yesu na kumwambia, “Mwalimu, nitakufuata kokote uendako.”
20 Naye Yesu akamjibu, “Mbweha wana mapango, nao ndege wa angani wana viota, lakini Mwana wa Adamu hana mahali pa kulaza kichwa chake.”
21 Mwanafunzi mwingine akamwambia, “Bwana, niruhusu kwanza nikamzike baba yangu.”
22 Lakini Yesu akamwambia, “Nifuate, uwaache wafu wawazike wafu wao.”
Luka 9:57–62
9:57 Walipokuwa njiani wakienda, mtu mmoja akamwambia Yesu, “Nitakufuata kokote uendako.”
58 Yesu akamjibu, “Mbweha wana mapango, nao ndege wa angani wana viota, lakini Mwana wa Adamu hana mahali pa kulaza kichwa chake.”
59 Yesu akamwambia mtu mwingine, “Nifuate.”
Mtu huyo akamjibu, “Bwana, niruhusu kwanza nikamzike baba yangu.”
60 Yesu akamwambia, “Waache wafu wawazike wafu wao, bali wewe nenda ukautangaze Ufalme wa Mungu.”
61 Mtu mwingine akamwambia, “Bwana, nitakufuata lakini naomba kwanza nikawaage jamaa yangu.”
62 Yesu akamwambia, “Mtu yeyote atiaye mkono wake kulima, kisha akatazama nyuma, hafai kwa Ufalme wa Mungu.”
Yesu Anakataa Ushauri wa Ndugu Zake
Ndugu zake Yesu wasioamini wanamsihi ajionyeshe huko Uyahudi, naye anakataa ushauri wao.
Yohana 7:2–9
7:2 Sikukuu ya Vibanda ya Wayahudi ilikuwa imekaribia. 3 Hivyo ndugu zake Yesu wakamwambia, “Ondoka hapa uende Uyahudi ili wanafunzi Wako wapate kuona miujiza unayofanya. 4 Mtu anayetaka kujulikana hafanyi mambo yake kwa siri. Kama unafanya mambo haya, jionyeshe kwa ulimwengu.” 5 Hata ndugu zake mwenyewe hawakumwamini.
6 Yesu akawaambia, “Wakati wangu bado haujawadia, lakini wakati wenu upo siku zote. 7 Ulimwengu hauwezi kuwachukia ninyi, lakini unanichukia mimi kwa sababu ninawashuhudia kwamba matendo yao ni maovu. 8 Ninyi nendeni kwenye Sikukuu, lakini mimi sitahudhuria Sikukuu hii kwa sababu wakati wangu haujawadia.” 9 Akiisha kusema hayo, akabaki Galilaya.
Yesu Anaenda Yerusalemu kwa Siri Kupitia Samaria
Luka 9:51–56
9:51 Wakati ulipokaribia wa yeye kuchukuliwa mbinguni, alikaza uso wake kwenda Yerusalemu. 52 Akatuma watu wamtangulie, nao wakaenda katika kijiji kimoja cha Samaria kumwandalia kila kitu; 53 lakini watu wa kijiji kile hawakumkaribisha kwa sababu alikuwa anakwenda zake Yerusalemu. 54 Wanafunzi wake, yaani Yakobo na Yohana, walipoona hayo, wakasema: “Bwana, unataka tuagize moto kutoka mbinguni ili uwaangamize?” 55 Yesu akageuka na kuwakemea, 56 nao wakaenda kijiji kingine.
Yohana 7:10
7:10 Lakini ndugu zake walipokwisha kuondoka kwenda kwenye Sikukuu, yeye pia alikwenda lakini kwa siri.