Yesu Anahojiwa Kwanza na Anasi

Yesu anahojiwa kwanza na Anasi, aliyekuwa kuhani mkuu.

Ijumaa kabla ya mapambazuko

Kesi ya Kiyahudi, na matukio yaliyoizunguka.

30 au 29 BK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Yohana 18:13–14, 19–23

18:13 Kwanza wakampeleka kwa Anasi, mkwewe Kayafa, aliyekuwa kuhani mkuu mwaka ule. 14 Kayafa ndiye alikuwa amewashauri Wayahudi kwamba imempasa mtu mmoja kufa kwa ajili ya watu.

19 Wakati huo kuhani mkuu akawa anamuuliza Yesu kuhusu wanafunzi wake na mafundisho yake.

20 Yesu akamjibu, “Nimekuwa nikizungumza waziwazi mbele ya watu wote. Siku zote nimefundisha katika masinagogi na Hekaluni, mahali ambapo Wayahudi wote hukusanyika. Sikusema jambo lolote kwa siri. 21 Mbona unaniuliza mimi maswali? Waulize wale walionisikia yale niliyowaambia. Wao wanajua niliyosema.”

22 Alipomaliza kusema hayo, mmoja wa askari aliyekuwa amesimama karibu naye, akampiga Yesu kofi usoni, kisha akasema, “Je, hivyo ndivyo unavyomjibu kuhani mkuu?”

23 Yesu akamjibu akasema, “Kama nimesema jambo baya, shuhudia huo ubaya niliousema. Lakini kama nimesema yaliyo kweli, mbona umenipiga?”

Kayafa na Baraza la Wayahudi Wanamhukumu Yesu

Yesu anashtakiwa na kuhukumiwa kwa haraka na Kayafa na Baraza la Wayahudi, ambao wanamdhihaki na kumpiga.

Makazi ya kuhani mkuu Kayafa. Kabla ya mapambazuko ya Ijumaa

Mathayo 26:57, 59–68

26:57 Wale waliokuwa wamemkamata Yesu wakampeleka kwa Kayafa, kuhani mkuu, mahali ambapo walimu wa sheria pamoja na wazee walikuwa wamekusanyika.

59 Viongozi wa makuhani na Baraza la Wayahudi lote wakatafuta ushahidi wa uongo dhidi ya Yesu ili wapate kumuua.

60 Lakini hawakupata jambo lolote, ingawa mashahidi wengi wa uongo walijitokeza.

Hatimaye wakajitokeza mashahidi wawili wa uongo

61 na kusema, “Huyu mtu alisema, ‘Ninaweza kulivunja Hekalu la Mungu na kulijenga tena kwa siku tatu.’ ”

62 Kisha kuhani mkuu akasimama na kumwambia Yesu, “Je, wewe hutajibu? Ni ushahidi gani hawa watu wanauleta dhidi yako?”

63 Lakini Yesu akakaa kimya.

Ndipo kuhani mkuu akamwambia, “Nakuapisha mbele za Mungu aliye hai. Tuambie kama wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu.”

64 Yesu akajibu, “Wewe umenena. Lakini ninawaambia nyote: Siku za baadaye, mtamwona Mwana wa Adamu akiwa ameketi mkono wa kuume wa Mwenye Nguvu, na akija juu ya mawingu ya mbinguni.”

65 Ndipo kuhani mkuu akararua mavazi yake na kusema, “Amekufuru! Tuna haja gani tena ya mashahidi zaidi? Tazama, sasa ninyi mmesikia hayo makufuru.

66 Uamuzi wenu ni gani?”

Wakajibu, “Anastahili kufa.”

67 Kisha wakamtemea mate usoni na wengine wakampiga ngumi. Wengine wakampiga makofi

68 na kusema, “Tutabirie, wewe Kristo! Ni nani aliyekupiga?”

Marko 14:53, 55–65

14:53 Wakampeleka Yesu kwa kuhani mkuu, nao viongozi wa makuhani wote, na wazee na walimu wa sheria wote wakakusanyika pamoja.

55 Viongozi wa makuhani na Baraza la Wayahudi lote wakatafuta ushahidi dhidi ya Yesu ili wapate kumuua. Lakini hawakupata jambo lolote.

56 Wengi walitoa ushahidi wa uongo dhidi yake, lakini maelezo yao hayakukubaliana.

57 Ndipo wengine wakasimama wakatoa ushahidi wa uongo dhidi yake, wakisema:

58 “Sisi tulimsikia akisema, ‘Mimi nitalibomoa Hekalu hili lililojengwa na wanadamu, na katika siku tatu nitajenga jingine ambalo halikujengwa na wanadamu.’ ” 59 Lakini hata hivyo, ushahidi wao haukukubaliana.

60 Basi kuhani mkuu akasimama mbele yao, akamuuliza Yesu, “Je, wewe hutajibu? Ni ushahidi gani hawa watu wanauleta dhidi yako?”

61 Lakini Yesu akakaa kimya, hakusema neno lolote.

Kuhani mkuu akamuuliza tena, “Je, wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu Aliyebarikiwa?”

62 Yesu akajibu, “Mimi ndimi. Nanyi mtamwona Mwana wa Adamu akiwa ameketi mkono wa kuume wa Mwenye Nguvu, na akija juu ya mawingu ya mbinguni.”

63 Kuhani mkuu akararua mavazi yake, akasema, “Tuna haja gani tena ya mashahidi zaidi? 64 Ninyi mmesikia hayo makufuru. Uamuzi wenu ni gani?”

Wote wakamhukumu kwamba anastahili kifo.

65 Kisha baadhi ya watu wakaanza kumtemea mate; wakamfunga kitambaa machoni, wakampiga kwa ngumi na kumwambia, “Tabiri!” Walinzi wakamchukua na kumpiga makofi.

Luka 22:54, 63–65

22:54 Kisha wakamkamata Yesu, wakamchukua, wakaenda naye mpaka nyumbani kwa kuhani mkuu. Lakini Petro akafuata kwa mbali.

63 Watu waliokuwa wanamlinda Yesu wakaanza kumdhihaki na kumpiga.

64 Wakamfunga kitambaa machoni na kumuuliza, “Tabiri! Tuambie ni nani aliyekupiga?”

65 Wakaendelea kumtukana kwa matusi mengi.

Yohana 18:24

18:24 Ndipo Anasi akampeleka Yesu kwa kuhani mkuu Kayafa, akiwa bado amefungwa.