Sehemu ya 13: Kukamatwa, Kushtakiwa, Kusulubiwa na Kuzikwa kwa Yesu
Usiku wa Alhamisi, Ijumaa, na Jumamosi ya Wiki ya Mateso ya Yesu (siku za giza kwa ufalme wa Mungu)
Yesu Anasalitiwa, Anakamatwa na Kuachwa
Bustani ya Gethsemane. Ijumaa, muda mrefu kabla ya mapambazuko
30 au 29 BK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
Mathayo 26:47–56
26:47 Alipokuwa bado anazungumza, Yuda, mmoja wa wale Kumi na Wawili, akafika. Alikuwa amefuatana na umati mkubwa wa watu wenye panga na marungu, waliokuwa wametumwa na viongozi wa makuhani na wazee wa watu.
48 Basi msaliti alikuwa amewapa hao watu ishara, kwamba: “Yule nitakayembusu ndiye. Mkamateni.”
49 Mara Yuda akamjia Yesu na kumsalimu, “Salamu, Rabi!” Akambusu.
50 Yesu akamwambia, “Rafiki, fanya kile ulichokuja kufanya hapa.”
Kisha wale watu wakasogea mbele, wakamkamata Yesu.
51 Ghafula mmoja wa wale waliokuwa na Yesu alipoona hivyo, akaushika upanga wake, akauchomoa na kumpiga mtumishi wa kuhani mkuu, akamkata sikio.
52 Ndipo Yesu akamwambia, “Rudisha upanga wako mahali pake, kwa maana wote watumiao upanga watakufa kwa upanga.
53 Je, unadhani siwezi kumwomba Baba yangu naye mara moja akaniletea zaidi ya majeshi kumi na mawili ya malaika? 54 Lakini je, yale Maandiko yanayotabiri kwamba ni lazima itendeke hivi yatatimiaje?”
55 Wakati huo, Yesu akawaambia ule umati wa watu, “Je, mmekuja na panga na marungu kunikamata kana kwamba mimi ni mnyangʼanyi? Siku kwa siku niliketi Hekaluni nikifundisha, mbona hamkunikamata?
56 Lakini haya yote yametukia ili maandiko ya manabii yapate kutimia.” Ndipo wanafunzi wake wote wakamwacha na kukimbia.
Marko 14:43–52
14:43 Yesu alipokuwa bado anazungumza, Yuda, mmoja wa wale wanafunzi Kumi na Wawili, akatokea. Alikuwa amefuatana na umati wa watu wenye panga na marungu, waliokuwa wametumwa na viongozi wa makuhani, walimu wa sheria, na wazee.
44 Basi msaliti alikuwa amewapa hao watu ishara, kwamba: “Yule nitakayembusu ndiye. Mkamateni, mkamchukue chini ya ulinzi.”
45 Mara Yuda akamjia Yesu na kusema, “Rabi.” Akambusu.
46 Wale watu wakamkamata Yesu, wakamweka chini ya ulinzi.
47 Ndipo mmoja wa wale waliokuwa wamesimama karibu aliuchomoa upanga wake na kumpiga mtumishi wa kuhani mkuu, akamkata sikio.
48 Kisha Yesu akawaambia, “Mmekuja na panga na marungu kunikamata kana kwamba mimi ni mnyangʼanyi?
49 Siku kwa siku nilikuwa pamoja nanyi nikifundisha Hekaluni, wala hamkunikamata. Lakini Maandiko sharti yatimie.” 50 Ndipo wanafunzi wake wote wakamwacha, wakakimbia.
51 Kijana mmoja, ambaye hakuwa amevaa kitu isipokuwa alijitanda nguo ya kitani, alikuwa akimfuata Yesu. Walipomkamata, 52 alikimbia uchi, akaliacha vazi lake.
Luka 22:47–53
22:47 Yesu alipokuwa bado anazungumza, umati mkubwa wa watu ukaja. Uliongozwa na Yuda, ambaye alikuwa mmoja wa wale wanafunzi Kumi na Wawili. Akamkaribia Yesu ili ambusu.
48 Lakini Yesu akamwambia, “Yuda, je, unamsaliti Mwana wa Adamu kwa busu?”
49 Wafuasi wa Yesu walipoona yale yaliyokuwa yanakaribia kutokea, wakasema, “Bwana, tuwakatekate kwa panga zetu?”
50 Mmoja wao akampiga mtumishi wa kuhani mkuu kwa upanga, akamkata sikio la kuume.
51 Lakini Yesu akasema, “Acheni!” Akaligusa lile sikio la yule mtu na kumponya.
52 Kisha Yesu akawaambia wale viongozi wa makuhani, maafisa wa walinzi wa Hekalu, pamoja na wazee waliokuwa wamekuja kumkamata, “Mmekuja na panga na marungu, kana kwamba mimi ni mnyangʼanyi?
53 Siku kwa siku nilikuwa pamoja nanyi Hekaluni lakini hamkunikamata. Lakini hii ni saa yenu, wakati giza linatawala!”
Yohana 18:2–12
18:2 Basi Yuda, yule aliyemsaliti alipafahamu mahali hapo kwani Yesu alikuwa akikutana humo na wanafunzi wake mara kwa mara.
3 Hivyo Yuda akaja bustanini. Aliongoza kikosi cha askari wa Kirumi, na baadhi ya maafisa kutoka kwa viongozi wa makuhani na Mafarisayo. Nao walikuwa wamechukua taa, mienge na silaha.
4 Yesu akijua yale yote yatakayompata, akajitokeza mbele yao akawauliza, “Mnamtafuta nani?”
5 Wao wakamjibu, “Yesu wa Nazareti.”
Yesu akawajibu, “Mimi ndiye.” Yuda, yule aliyemsaliti alikuwa amesimama pamoja nao. 6 Yesu alipowaambia, “Mimi ndiye,” walirudi nyuma na kuanguka chini!
7 Akawauliza tena, “Mnamtafuta nani?”
Nao wakamjibu, “Yesu wa Nazareti.”
8 Yesu akawaambia, “Nimekwisha kuwaambia kuwa, mimi ndiye; kwa hiyo kama mnanitafuta mimi, waacheni hawa watu waende zao.” 9 Hii ilikuwa ili litimie lile neno alilosema, “Sikumpoteza hata mmoja miongoni mwa wale ulionipa.”
10 Simoni Petro, aliyekuwa na upanga, akaufuta na kumkata sikio la kuume mtumishi wa kuhani mkuu. Jina la mtumishi huyo aliitwa Malko.
11 Yesu akamwambia Petro, “Rudisha upanga wako kwenye ala yake. Je, hainipasi kukinywea kikombe alichonipa Baba?”
12 Hivyo wale askari, wakiwa pamoja na majemadari wao na maafisa wa Wayahudi, wakamkamata Yesu na kumfunga.