Kukaa kwa Yesu Kapernaumu kwa Mara ya Kwanza
Yesu anakaa Kapernaumu kwa mara ya kwanza, pamoja na familia yake na wanafunzi wake wa mwanzo.
(Baadaye Kapernaumu itakuwa makao yake.)
26 BK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
Yohana 2:12
2:12 Baada ya hayo, Yesu pamoja na mama yake, ndugu zake na wanafunzi wake, walishuka mpaka Kapernaumu, wakakaa huko siku chache.
Yesu Analitakasa Hekalu kwa Mara ya Kwanza Wakati wa Pasaka 27 BK
Yerusalemu. Yaelekea mwaka wa 27 BK
Yohana 2:13–22
2:13 Ilipokaribia wakati wa Pasaka ya Wayahudi, Yesu alipanda kwenda Yerusalemu. 14 Huko Hekaluni aliwakuta watu wakiuza ngʼombe, kondoo na njiwa, nao wengine walikuwa wameketi mezani wakibadili fedha. 15 Akatengeneza mjeledi kutokana na kamba, akawafukuza wote kutoka kwenye eneo la Hekalu, pamoja na kondoo na ngʼombe. Akazipindua meza za wale wabadili fedha na kuzimwaga fedha zao. 16 Akawaambia wale waliokuwa wakiuza njiwa, “Waondoeni hapa! Mnathubutuje kuifanya nyumba ya Baba yangu kuwa mahali pa biashara?”
17 Wanafunzi wake wakakumbuka kuwa imeandikwa: “Wivu wa nyumba yako utanila.”
18 Ndipo Wayahudi wakamuuliza, “Unaweza kutuonyesha ishara gani ili kuthibitisha mamlaka uliyo nayo ya kufanya mambo haya?”
19 Yesu akawajibu, “Libomoeni hili Hekalu, nami nitalijenga tena kwa siku tatu!”
20 Wale Wayahudi wakamjibu, “Hekalu hili lilijengwa kwa muda wa miaka arobaini na sita, nawe wasema utalijenga kwa siku tatu?” 21 Lakini yeye Hekalu alilozungumzia ni mwili wake. 22 Baada ya kufufuliwa kutoka kwa wafu, wanafunzi wake wakakumbuka yale aliyokuwa amesema. Ndipo wakayaamini Maandiko na yale maneno Yesu aliyokuwa amesema.
Nikodemo Anakutana na Yesu
Huko Yerusalemu wakati wa Pasaka
Yohana 2:23–3:21
2:23 Ikawa Yesu alipokuwa Yerusalemu kwenye Sikukuu ya Pasaka, watu wengi waliona ishara na miujiza aliyokuwa akifanya, wakaamini katika jina lake. 24 Lakini Yesu hakujiaminisha kwao kwa sababu aliwajua wanadamu wote. 25 Hakuhitaji ushuhuda wa mtu yeyote kuhusu mtu, kwa kuwa alijua yote yaliyokuwa moyoni mwa mtu.
3:1 Basi palikuwa na mtu mmoja Farisayo, jina lake Nikodemo, mmoja wa Baraza la Wayahudi lililotawala. 2 Huyu alimjia Yesu usiku akamwambia, “Rabi, tunajua kuwa wewe ni mwalimu uliyetumwa na Mungu, kwa maana hakuna mtu awezaye kufanya miujiza hii uifanyayo wewe, kama Mungu hayuko pamoja naye.”
3 Yesu akamjibu, “Amin, amin nakuambia, hakuna mtu anayeweza kuuona Ufalme wa Mungu kama hajazaliwa mara ya pili.”
4 Nikodemo akauliza, “Awezaje mtu kuzaliwa wakati akiwa mzee? Hakika hawezi kuingia mara ya pili kwenye tumbo la mama yake ili azaliwe!”
5 Yesu akamwambia, “Amin, amin nakuambia, hakuna mtu yeyote anayeweza kuingia Ufalme wa Mungu kama hajazaliwa kwa maji na kwa Roho. 6 Mwili huzaa mwili, lakini Roho huzaa roho. 7 Kwa hiyo usishangae ninapokuambia huna budi ‘kuzaliwa mara ya pili.’ 8 Upepo huvuma popote upendapo. Mvumo wake unausikia lakini huwezi ukafahamu utokako wala uendako. Ndivyo ilivyo kwa kila mtu aliyezaliwa na Roho.”
9 Nikodemo akamuuliza, “Mambo haya yanawezekanaje?”
10 Yesu akamwambia, “Wewe ni mwalimu mashuhuri wa Waisraeli, nawe huelewi mambo haya? 11 Amin, amin ninakuambia, sisi tunazungumza lile tunalolijua na tunashuhudia lile tuliloliona. Lakini ninyi watu hamkubali ushuhuda wetu. 12 Nimewaambia mambo ya duniani, nanyi hamkuniamini, mtaniaminije basi nitakapowaambia mambo ya mbinguni? 13 Hakuna mtu yeyote aliyekwenda mbinguni isipokuwa yeye aliyeshuka kutoka mbinguni, yaani, Mwana wa Adamu. 14 Kama vile Mose alivyomwinua yule nyoka kule jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa juu. 15 Ili kila mtu amwaminiye awe na uzima wa milele.
16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. 17 Kwa maana Mungu hakumtuma Mwanawe kuuhukumu ulimwengu, bali kupitia kwake ulimwengu upate kuokolewa. 18 Yeyote amwaminiye hahukumiwi, lakini asiyeamini amekwisha kuhukumiwa, kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu. 19 Hii ndiyo hukumu kwamba: Nuru imekuja ulimwenguni, nao watu wakapenda giza kuliko nuru kwa sababu matendo yao ni maovu. 20 Kwa kuwa kila atendaye maovu huchukia nuru, wala haji kwenye nuru ili matendo yake maovu yasifichuliwe. 21 Lakini yule aishiye kwa ukweli huja kwenye nuru, ili ionekane wazi kwamba matendo yake yametendeka katika Mungu.”