Yesu na Yohana Wanahudumu Sambamba
Yesu na Yohana Mbatizaji wanahudumu sambamba, na Yohana anaendelea kuwa mwaminifu kwa Yesu.
27 BK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
Yohana 3:22–36
3:22 Baada ya haya, Yesu na wanafunzi wake walikwenda katika nchi ya Uyahudi, nao wakakaa huko kwa muda na kubatiza. 23 Yohana naye alikuwa akibatiza huko Ainoni karibu na Salimu kwa sababu huko kulikuwa na maji tele. Watu wazima wakamjia huko ili kubatizwa. 24 (Hii ilikuwa kabla Yohana hajatiwa gerezani). 25 Mashindano yakazuka kati ya baadhi ya wanafunzi wa Yohana na Myahudi mmoja kuhusu suala la desturi ya kunawa kwa utakaso. 26 Wakamwendea Yohana wakamwambia, “Rabi, yule mtu aliyekuwa pamoja nawe ngʼambo ya Mto Yordani, yule uliyeshuhudia habari zake, sasa anabatiza na kila mtu anamwendea!”
27 Yohana akawajibu, “Hakuna mtu yeyote awezaye kupata kitu chochote isipokuwa kile tu alichopewa kutoka mbinguni. 28 Ninyi wenyewe ni mashahidi wangu kwamba nilisema, ‘Mimi si Kristo, ila nimetumwa nimtangulie.’ 29 Bibi arusi ni wa bwana arusi. Lakini rafiki yake bwana arusi anayesimama karibu naye na kusikiliza kutoka kwake, hufurahi sana aisikiapo sauti ya bwana arusi. Kwa sababu hii furaha yangu imekamilika. 30 Yeye hana budi kuwa mkuu zaidi na mimi nizidi kuwa mdogo.”
31 “Yeye ajaye kutoka juu yu juu ya yote, yeye aliye wa duniani ni wa dunia, naye huzungumza mambo ya duniani. Yeye aliyekuja kutoka mbinguni, yu juu ya yote. 32 Yeye hushuhudia yale aliyoyaona na kuyasikia, lakini hakuna yeyote anayekubali ushuhuda wake. 33 Lakini yeyote anayekubali huo ushuhuda anathibitisha kwamba, Mungu ni kweli. 34 Yeye aliyetumwa na Mungu husema maneno ya Mungu, kwa kuwa Mungu humtoa Roho pasipo kipimo. 35 Baba anampenda Mwana, naye ametia vitu vyote mikononi mwake. 36 Yeyote anayemwamini Mwana ana uzima wa milele, lakini yeye asiyemwamini Mwana hatauona uzima, bali ghadhabu ya Mungu itakuwa juu yake.”
Kwa Nini Kristo Anaondoka Uyahudi
Mathayo 4:12
4:12 Yesu aliposikia kwamba Yohana Mbatizaji alikuwa ametiwa gerezani, alirudi Galilaya.
Marko 1:14
1:14 Baada ya Yohana kukamatwa na kutiwa gerezani, Yesu aliingia Galilaya akaanza kuhubiri habari njema ya Mungu,
Luka 3:19–20; 4:14
3:19 Lakini Yohana alipomkemea Mfalme Herode kuhusu uhusiano wake na Herodia, mke wa ndugu yake, na maovu mengine aliyokuwa amefanya, 20 Herode aliongezea jambo hili kwa hayo mengine yote: alimfunga Yohana gerezani.
4:14 Kisha Yesu akarudi mpaka Galilaya, akiwa amejaa nguvu za Roho Mtakatifu, nazo habari zake zikaenea katika sehemu zote za nchi za kandokando.
Yohana 4:1–4
4:1 Mafarisayo wakasikia kwamba Yesu alikuwa anapata na kubatiza wanafunzi wengi zaidi kuliko Yohana, 2 ingawa kwa kweli si Yesu mwenyewe aliyekuwa akibatiza, ila ni wanafunzi wake. 3 Bwana alipojua mambo haya, aliondoka Uyahudi akarudi tena Galilaya.
4 Wakati huo ilimlazimu apitie Samaria.