Yeremia Anatoa Wito wa Toba na Anaomboleza

Yeremia anawasihi watu watubu, na kuombolezea mateso yao kadiri utumwa unavyokaribia.

612 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Yeremia 7–8

1 Hili ndilo neno lililomjia Yeremia kutoka kwa Bwana: 2 “Simama kwenye lango la nyumba ya Bwana, na huko upige mbiu ya ujumbe huu:

“ ‘Sikieni neno la Bwana, enyi watu wote wa Yuda mliokuja kupitia malango haya ili kumwabudu Bwana. 3 Hili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli: Tengenezeni njia zenu na matendo yenu, nami nitawaacha mkae mahali hapa. 4 Msitumainie maneno ya udanganyifu na kusema, “Hili ni Hekalu la Bwana, Hekalu la Bwana, Hekalu la Bwana!” 5 Kama kweli mkibadili njia zenu na matendo yenu, mkatendeana haki kila mmoja na mwenzake, 6 kama msipomwonea mgeni, yatima wala mjane, na kumwaga damu isiyo na hatia mahali hapa, nanyi kama msipofuata miungu mingine kwa madhara yenu wenyewe, 7 ndipo nitawaacha mkae mahali hapa, katika nchi niliyowapa baba zenu milele na milele. 8 Lakini tazama, mnatumainia maneno ya udanganyifu yasiyo na maana.

9 “ ‘Je, mtaiba na kuua, mtazini na kuapa kwa uongo, na kufukiza uvumba kwa Baali, na kufuata miungu mingine ambayo hamkuijua, 10 kisha mje na kusimama mbele yangu katika nyumba hii inayoitwa kwa Jina langu, mkisema, “Tuko salama.” Salama kwa kufanya mambo haya yote ya kuchukiza? 11 Je, nyumba hii, iitwayo kwa Jina langu, imekuwa pango la wanyangʼanyi kwenu? Lakini nimekuwa nikiona yanayotendeka! asema Bwana.

12 “ ‘Nendeni sasa mahali pangu palipokuwa huko Shilo, mahali ambapo nilipafanya pa kwanza kuwa makao ya Jina langu, nanyi mwone lile nililopafanyia kwa ajili ya uovu wa watu wangu Israeli. 13 Mlipokuwa mnafanya yote haya, asema Bwana, nilisema nanyi tena na tena, lakini hamkusikiliza; niliwaita, lakini hamkujibu. 14 Kwa hiyo, nililolifanyia Shilo, nitalifanya sasa kwa nyumba hii iitwayo kwa Jina langu, Hekalu mnalolitumainia, mahali nilipowapa ninyi na baba zenu. 15 Nitawafukuza mbele yangu, kama nilivyowafanyia ndugu zenu, watu wa Efraimu.’

16 “Kwa hiyo usiombe kwa ajili ya watu hawa, wala usinililie, na usifanye maombi kwa ajili yao; usinisihi, kwa sababu sitakusikiliza. 17 Je, huyaoni hayo wanayoyatenda katika miji ya Yuda na katika barabara za Yerusalemu? 18 Watoto wanakusanya kuni, baba zao wanawasha moto, na wanawake wanakanda unga na kuoka mikate kwa ajili ya Malkia wa Mbinguni. Wanamimina sadaka za vinywaji kwa miungu mingine ili kunikasirisha. 19 Lakini je, mimi ndiye wanayenikasirisha? asema Bwana. Je, hawajiumizi wenyewe na kujiaibisha?

20 “ ‘Kwa hiyo hivi ndivyo asemavyo Bwana Mwenyezi: Hasira yangu na ghadhabu yangu itamwagwa mahali hapa, juu ya mwanadamu na mnyama, juu ya miti ya shambani na juu ya matunda ya ardhini, nayo itaungua pasipo kuzimwa.

21 “ ‘Hivi ndivyo asemavyo Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli: Endeleeni, ongezeni sadaka zenu za kuteketezwa juu ya dhabihu zenu nyingine, mle nyama hiyo wenyewe! 22 Kwa kuwa nilipowaleta baba zenu kutoka Misri na kusema nao, sikuwapa amri kuhusu sadaka za kuteketezwa na dhabihu tu, 23 lakini niliwapa amri hii nikisema: Nitiini mimi, nami nitakuwa Mungu wenu nanyi mtakuwa watu wangu. Enendeni katika njia zote ninazowaamuru ili mpate kufanikiwa. 24 Lakini hawakusikiliza wala kujali. Badala yake, walifuata ukaidi wa mioyo yao miovu. Walirudi nyuma badala ya kusonga mbele. 25 Tangu wakati ule baba zenu walipotoka Misri hadi sasa, siku baada ya siku, tena na tena nimewatumia watumishi wangu manabii. 26 Lakini hawakunisikiliza wala hawakujali. Walikuwa na shingo ngumu na kufanya maovu kuliko baba zao.’

27 “Utakapowaambia haya yote, hawatakusikiliza; utakapowaita, hawatajibu. 28 Kwa hiyo waambie, ‘Hili ni taifa ambalo halimtii Bwana, Mungu wao, wala kukubali maonyo. Kweli imekufa, imetoweka midomoni mwao. 29 Nyoeni nywele zenu na kuzitupa, ombolezeni katika miinuko iliyo kame, kwa kuwa Bwana amekikataa na kukiacha kizazi hiki kilichomkasirisha.

30 “ ‘Watu wa Yuda wamefanya maovu machoni pangu, asema Bwana. Wameziweka sanamu zao za machukizo ndani ya nyumba iitwayo kwa Jina langu, na wameitia unajisi. 31 Wamejenga mahali pa juu pa kuabudia sanamu pa Tofethi kwenye Bonde la Ben-Hinomu ili kuwateketeza wana wao na binti zao kwenye moto, kitu ambacho sikuamuru, wala hakikuingia akilini mwangu. 32 Kwa hiyo mjihadhari, siku zinakuja, asema Bwana, wakati watu watakapokuwa hawapaiti Tofethi au Bonde la Ben-Hinomu, lakini watapaita Bonde la Machinjo, kwa sababu watawazika wafu huko Tofethi mpaka pasiwe tena nafasi. 33 Ndipo mizoga ya watu hawa itakuwa chakula cha ndege wa angani na wanyama wa nchi, wala hapatakuwepo na yeyote wa kuwafukuza. 34 Nitazikomesha sauti za shangwe na furaha, na sauti za bwana arusi na bibi arusi katikati ya miji ya Yuda na barabara za Yerusalemu, kwa sababu nchi itakuwa ukiwa.

8:1 “ ‘Wakati huo, asema Bwana, mifupa ya wafalme na maafisa wa Yuda, mifupa ya makuhani na manabii, na mifupa ya watu wa Yerusalemu itaondolewa kutoka makaburi yao. 2 Itawekwa wazi kwa jua, na mwezi, na nyota zote za mbingu, ambazo walizipenda na kuzitumikia, na ambazo wamezifuata kutafuta ushauri na kuziabudu. Hawatakusanywa pamoja au kuzikwa, lakini watakuwa kama mavi yaliyotapakaa juu ya ardhi. 3 Popote nitakapowafukuzia, mabaki wote wa kizazi hiki kiovu watatamani kufa kuliko kuishi, asema Bwana Mwenye Nguvu Zote.’

4 “Waambie, ‘Hivi ndivyo asemavyo Bwana:

“ ‘Je, watu wanapoanguka hawainuki?

Je, mtu anapopotea harudi?

5 Kwa nini basi watu hawa walipotea?

Kwa nini Yerusalemu inapotea kila mara?

Wanangʼangʼania udanganyifu

na wanakataa kurudi.

6 Nimewasikiliza kwa makini,

lakini hawataki kusema lililo sawa.

Hakuna anayetubia makosa yake

akisema, “Nimefanya nini?”

Kila mmoja hufuata njia yake mwenyewe

kama farasi anayekwenda vitani.

7 Hata korongo aliyeko angani

anayajua majira yake yaliyoamriwa,

nao njiwa, mbayuwayu na koikoi

hufuata majira yao ya kurudi.

Lakini watu wangu hawajui

Bwana anachotaka kwao.

8 “ ‘Mwawezaje kusema, “Sisi tuna busara

kwa sababu tunayo sheria ya Bwana,”

wakati ambapo kwa hakika kalamu ya uongo ya waandishi

imeandika kwa udanganyifu?

9 Wenye hekima wataaibika,

watafadhaika na kunaswa.

Kwa kuwa wamelikataa neno la Bwana,

hiyo hekima waliyo nayo ni ya namna gani?

10 Kwa hiyo nitawapa watu wengine wake zao,

na mashamba yao kwa wamiliki wengine.

Kuanzia aliye mdogo kabisa hadi aliye mkubwa kabisa,

wote wana tamaa ya kupata zaidi;

manabii na makuhani wanafanana,

wote wanafanya udanganyifu.

11 Wanafunga majeraha ya watu wangu

bila uangalifu.

Wanasema, “Amani, amani,”

wakati hakuna amani.

12 Je, wanaona aibu kwa ajili ya tabia yao inayochukiza mno?

Hapana, hawana aibu hata kidogo,

hawajui hata kuona haya.

Kwa hiyo wataanguka miongoni mwa hao walioanguka,

watashushwa chini watakapoadhibiwa,

asema Bwana.

13 “ ‘Nitayaondoa mavuno yao,

asema Bwana.

Hapatakuwepo zabibu kwenye mzabibu.

Hapatakuwepo na tini kwenye mtini,

majani yake yatanyauka.

Kile nilichowapa

watanyangʼanywa.’ ”

14 “Kwa nini tunaketi hapa?

Kusanyikeni pamoja!

Tukimbilie kwenye miji yenye maboma,

tukaangamie huko!

Kwa kuwa Bwana, Mungu wetu

ametuhukumu kuangamia,

na kutupa maji yenye sumu tunywe,

kwa sababu tumemtenda dhambi.

15 Tulitegemea amani,

lakini hakuna jema lililokuja,

tulitegemea wakati wa kupona,

lakini kulikuwa hofu tu.

16 Mkoromo wa farasi za adui

umesikika kuanzia Dani,

kwa mlio wa madume yao ya farasi,

nchi yote inatetemeka.

Wamekuja kuangamiza nchi na vyote vilivyomo,

mji na wote waishio ndani yake.”

17 “Tazama, nitatuma nyoka wenye sumu kali katikati yenu,

fira ambao hawawezi kulogwa,

nao watawauma,”

asema Bwana.

18 Ee Mfariji wangu katika huzuni,

moyo wangu umezimia ndani yangu.

19 Sikia kilio cha watu wangu

kutoka nchi ya mbali:

“Je, Bwana hayuko Sayuni?

Je, Mfalme wake hayuko tena huko?”

“Kwa nini wamenikasirisha kwa vinyago vyao,

kwa sanamu zao za kigeni zisizofaa?”

20 “Mavuno yamepita,

kiangazi kimekwisha,

nasi hatujaokolewa.”

21 Kwa kuwa watu wangu wamepondwa, nami nimepondeka pia;

ninaomboleza, nayo hofu kuu imenishika.

22 Je, hakuna zeri ya kuponya katika Gileadi?

Je, hakuna tabibu huko?

Kwa nini basi hakuna uponyaji

wa majeraha ya watu wangu?