Yeremia Anatoa Wito wa Toba na Anaomboleza (continued)
Yeremia anawasihi watu watubu, na kuombolezea mateso yao kadiri utumwa unavyokaribia.
612 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Laiti kichwa changu kingekuwa chemchemi ya maji
na macho yangu yangekuwa kisima cha machozi!
Ningelia usiku na mchana
kwa kuuawa kwa watu wangu.
2 Laiti ningekuwa na nyumba
ya kukaa wasafiri jangwani,
ningewaacha watu wangu
na kwenda mbali nao,
kwa kuwa wote ni wazinzi,
kundi la watu wadanganyifu.
3 “Huweka tayari ndimi zao kama upinde,
ili kurusha uongo;
wamekuwa na nguvu katika nchi
lakini si katika ukweli.
Wanatoka dhambi moja hadi nyingine,
hawanitambui mimi,”
asema Bwana.
4 “Jihadhari na rafiki zako;
usiwaamini ndugu zako.
Kwa kuwa kila ndugu ni mdanganyifu,
na kila rafiki ni msingiziaji.
5 Rafiki humdanganya rafiki,
hakuna yeyote asemaye kweli.
Wamefundisha ndimi zao kudanganya,
wanajichosha wenyewe katika kutenda dhambi.
6 Unakaa katikati ya udanganyifu;
katika udanganyifu wao wanakataa kunitambua mimi,”
asema Bwana.
7 Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote:
“Tazama, nitawasafisha na kuwajaribu,
kwani ni nini kingine niwezacho kufanya
kwa sababu ya dhambi ya watu wangu?
8 Ndimi zao ni mshale wenye sumu,
hunena kwa udanganyifu.
Kwa kinywa chake kila mmoja huzungumza maneno mazuri na jirani yake,
lakini moyoni mwake humtegea mtego.
9 Je, nisiwaadhibu kwa ajili ya jambo hili?”
asema Bwana.
“Je, nisijilipizie kisasi
kwa taifa kama hili?”
10 Nitalia na kuomboleza kwa ajili ya milima
na kuomboleza kuhusu malisho ya jangwani.
Yamekuwa ukiwa, wala hakuna apitaye humo,
milio ya ngʼombe haisikiki.
Ndege wa angani wametoroka
na wanyama wamekimbia.
11 “Nitaifanya Yerusalemu lundo la magofu,
makao ya mbweha;
nami nitaifanya miji ya Yuda kuwa ukiwa
ili asiwepo atakayeishi humo.”
12 Ni mtu yupi aliye na hekima ya kutosha ayaelewe haya? Ni nani aliyefundishwa na Bwana awezaye kuyaeleza haya? Kwa nini nchi imeharibiwa na kufanywa ukiwa kama jangwa ambapo hakuna awezaye kupita?
13 Bwana akasema, “Ni kwa sababu wameiacha sheria yangu, niliyoiweka mbele yao: hawajaniheshimu mimi wala kufuata sheria yangu. 14 Badala yake wamefuata ukaidi wa mioyo yao, wamefuata Mabaali, kama vile baba zao walivyowafundisha.” 15 Kwa hiyo, hivi ndivyo asemavyo Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli: “Tazama, nitawafanya watu hawa wale chakula kichungu na kunywa maji yenye sumu. 16 Nitawatawanya katika mataifa ambayo wao wala baba zao hawakuwajua, nikiwafuata kwa upanga mpaka niwe nimewaangamiza kabisa.”
17 Hivi ndivyo asemavyo Bwana Mwenye Nguvu Zote:
“Fikiri sasa! Waite wanawake waombolezao waje,
waite wale walio na ustadi kuliko wote.
18 Nao waje upesi
na kutuombolezea,
mpaka macho yetu yafurike machozi
na vijito vya maji vitoke kwenye kope zetu.
19 Sauti ya kuomboleza imesikika kutoka Sayuni:
‘Tazama jinsi tulivyoangamizwa!
Tazama jinsi aibu yetu ilivyo kubwa!
Ni lazima tuihame nchi yetu
kwa sababu nyumba zetu zimekuwa magofu.’ ”
20 Basi, enyi wanawake, sikieni neno la Bwana;
fungueni masikio yenu msikie maneno ya kinywa chake.
Wafundisheni binti zenu kuomboleza;
fundishaneni kila mmoja na mwenzake maombolezo.
21 Mauti imeingia ndani kupitia madirishani,
imeingia kwenye majumba yetu ya fahari;
imewakatilia mbali watoto katika barabara
na vijana waume kutoka viwanja vya miji.
22 Sema, “Hili ndilo asemalo Bwana:
“ ‘Maiti za wanaume zitalala
kama mavi katika mashamba,
kama malundo ya nafaka nyuma ya mvunaji,
wala hakuna anayekusanya.’ ”
23 Hili ndilo asemalo Bwana:
“Mwenye hekima asijisifu katika hekima yake,
au mwenye nguvu ajisifu katika nguvu zake,
wala tajiri ajisifu katika utajiri wake,
24 lakini yeye ajisifuye, na ajisifu kwa sababu hili:
kwamba ananifahamu na kunijua mimi,
kwamba mimi ndimi Bwana, nitendaye wema,
hukumu na haki duniani,
kwa kuwa napendezwa na haya,”
asema Bwana.
25 “Siku zinakuja, nitakapowaadhibu wale wote ambao wametahiriwa kimwili tu, asema Bwana, 26 yaani Misri, Yuda, Edomu, Amoni, Moabu na wote wanaoishi jangwani sehemu za mbali. Kwa maana mataifa haya yote hayakutahiriwa mioyo yao, nayo nyumba yote ya Israeli haikutahiriwa.”
10:1 Sikieni lile ambalo Bwana, anena nanyi ee nyumba ya Israeli. 2 Hili ndilo asemalo Bwana:
“Usijifunze njia za mataifa
wala usitishwe na ishara katika anga,
ingawa mataifa yanatishwa nazo.
3 Kwa maana desturi za mataifa hazina maana,
wanakata mti msituni,
na fundi anauchonga kwa patasi.
4 Wanaparemba kwa fedha na dhahabu,
wanakikaza kwa nyundo na misumari ili kisitikisike.
5 Sanamu zao ni kama sanamu
iliyowekwa shambani la matango kutishia ndege
nazo haziwezi kuongea;
sharti zibebwe
sababu haziwezi kutembea.
Usiziogope; haziwezi kudhuru,
wala kutenda lolote jema.”
6 Hakuna aliye kama wewe, Ee Bwana;
wewe ni mkuu,
jina lako ni lenye nguvu katika uweza.
7 Ni nani ambaye haimpasi kukuheshimu wewe,
Ee Mfalme wa mataifa?
Hii ni stahili yako.
Miongoni mwa watu wote wenye hekima
katika mataifa na katika falme zao zote,
hakuna aliye kama wewe.
8 Wote hawana akili, tena ni wapumbavu,
wanafundishwa na sanamu za miti zisizofaa lolote.
9 Huleta fedha iliyofuliwa kutoka Tarshishi
na dhahabu kutoka Ufazi.
Kile ambacho fundi na sonara wametengeneza
huvikwa mavazi ya rangi ya samawi na urujuani:
vyote vikiwa vimetengenezwa
na mafundi stadi.
10 Lakini Bwana ni Mungu wa kweli,
yeye ndiye Mungu aliye hai, Mfalme wa milele.
Anapokasirika, dunia hutetemeka,
mataifa hayawezi kustahimili hasira yake.
11 “Waambie hivi: ‘Miungu hii, ambayo haikuumba mbingu na dunia, itaangamia kutoka dunia na kutoka chini ya mbingu.’ ”
12 Lakini Mungu aliiumba dunia kwa uweza wake,
akaweka misingi ya ulimwengu kwa hekima yake,
na akazitandaza mbingu kwa ufahamu wake.
13 Atoapo sauti yake, maji yaliyo katika mbingu hunguruma;
huyafanya mawingu yainuke kutoka miisho ya dunia.
Hupeleka umeme wa radi pamoja na mvua,
naye huuleta upepo kutoka ghala zake.
14 Kila mmoja ni mjinga na hana maarifa,
kila sonara ameaibishwa na sanamu zake.
Vinyago vyake ni vya udanganyifu,
havina pumzi ndani yavyo.
15 Havifai kitu, ni vitu vya kufanyia mzaha tu,
hukumu yavyo itakapowadia, vitaangamia.
16 Yeye aliye Fungu la Yakobo sivyo alivyo,
kwani ndiye Muumba wa vitu vyote,
pamoja na Israeli, kabila la urithi wake:
Bwana Mwenye Nguvu Zote ndilo jina lake.
17 Kusanyeni mali na vitu vyenu mwondoke nchi hii,
enyi mnaoishi katika hali ya kuzingirwa na jeshi.
18 Kwa kuwa hili ndilo asemalo Bwana:
“Wakati huu, nitawatupa nje kwa nguvu
wote waishio katika nchi hii;
nitawataabisha
ili waweze kutekwa.”
19 Ole wangu mimi kwa ajili ya kuumia kwangu!
Jeraha langu ni kubwa!
Lakini nilisema,
“Kweli hii ni adhabu yangu,
nami sharti niistahimili.”
20 Hema langu limeangamizwa;
kamba zake zote zimekatwa.
Wana wangu wametekwa na hawapo tena;
hakuna hata mmoja aliyebaki wa kusimamisha hema langu
wala wa kusimamisha kibanda changu.
21 Wachungaji hawana akili
wala hawamuulizi Bwana,
hivyo hawastawi
na kundi lao lote la kondoo limetawanyika.
22 Sikilizeni! Taarifa inakuja:
ghasia kubwa kutoka nchi ya kaskazini!
Hii itafanya miji ya Yuda ukiwa,
makao ya mbweha.
23 Ninajua, Ee Bwana, kwamba maisha ya mwanadamu si yake mwenyewe;
hawezi kuziongoza hatua zake mwenyewe.
24 Unirudi, Ee Bwana, lakini kwa kipimo cha haki:
si katika hasira yako,
usije ukaniangamiza.
25 Umwage ghadhabu yako juu ya mataifa
wasiokujua wewe,
juu ya mataifa wasioliitia jina lako.
Kwa kuwa wamemwangamiza Yakobo;
wamemwangamiza kabisa
na kuiharibu nchi yake.