Vita vya Yehoshafati na Utawala Bora (continued)
897 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Ikawa baada ya jambo hili, Wamoabu na Waamoni, pamoja na baadhi ya Wameuni wakaja ili wapigane vita na Yehoshafati.
2 Watu fulani wakaja wakamwambia Yehoshafati, “Jeshi kubwa linakuja dhidi yako kutoka Edomu tokea ngʼambo ile nyingine ya Bahari. Tayari liko Hasason-Tamari” (yaani En-Gedi). 3 Yehoshafati akaogopa, akaazimu kumtafuta Bwana, na akatangaza kwa Yuda wote kufunga. 4 Watu wa Yuda wakakusanyika pamoja ili kutafuta msaada kutoka kwa Bwana. Wakaja kutoka kila mji wa Yuda ili kumtafuta.
5 Kisha Yehoshafati akasimama katika kusanyiko la Yuda na Yerusalemu katika Hekalu la Bwana, mbele ya ua mpya, 6 akasema:
“Ee Bwana, Mungu wa baba zetu, si wewe ndiwe uliye Mungu mbinguni? Si wewe ndiwe utawalaye juu ya falme zote za mataifa? Uweza na nguvu viko mkononi mwako, wala hakuna yeyote awezaye kushindana nawe. 7 Je, si wewe, Ee Mungu wetu, uliyewafukuza wenyeji wa nchi hii mbele ya watu wako Israeli, ukawapa wazao wa Abrahamu, rafiki yako, hata milele? 8 Wameishi ndani yake na humo wamekujengea mahali patakatifu kwa ajili ya Jina lako, wakisema: 9 ‘Kama maafa yakitujia, ikiwa ni upanga, hukumu, tauni, au njaa, tutasimama mbele zako, mbele ya Hekalu hili ambalo limeitwa kwa Jina lako na kukulilia katika shida yetu, nawe utatusikia na kutuokoa.’
10 “Lakini sasa hawa watu wa kutoka Amoni, Moabu na Mlima Seiri, ambao hukuwaruhusu Israeli wazivamie nchi zao wakati walitoka Misri, hivyo wakageukia mbali nao na hawakuwaangamiza, 11 tazama jinsi wanavyotulipa kwa kuja kututupa nje ya milki uliyotupa sisi kuwa urithi. 12 Ee Mungu wetu, je, wewe hutawahukumu? Kwa kuwa sisi hatuna uwezo wa kukabiliana na jeshi hili kubwa linalokuja kutushambulia. Sisi hatujui la kufanya, bali macho yetu yanakutazama wewe.”
13 Watu wote wa Yuda pamoja na wake zao, watoto wao na wadogo wao wakasimama pale mbele za Bwana.
14 Ndipo Roho wa Bwana akaja juu ya mtu mmoja jina lake Yahazieli mwana wa Zekaria, mwana wa Benaya, Mwana wa Yeieli, mwana wa Matania, Mlawi mzao wa Asafu alipokuwa amesimama katika kusanyiko.
15 Akasema: “Sikilizeni, enyi Yuda wote nanyi nyote mkaao Yerusalemu, nawe Mfalme Yehoshafati! Hili ndilo Bwana asemalo kwenu, ‘Msiogope wala msifadhaike kwa sababu ya jeshi hili kubwa. Kwa maana vita hivi si vyenu, bali ni vya Mungu. 16 Kesho shukeni kukabiliana nao. Watakwea kwa kupandia Genge la Sisi, nanyi mtawakuta mwisho wa bonde, kabla ya Jangwa la Yerueli. 17 Hamtahitaji kupigana vita hivi. Kaeni kwenye nafasi zenu, simameni imara na mkaone wokovu Bwana atakaowapatia, enyi Yuda na Yerusalemu. Msiogope, wala msifadhaike. Kesho tokeni mwende mkawakabili, naye Bwana atakuwa pamoja nanyi.’ ”
18 Yehoshafati akainamisha uso wake chini, nao watu wote wa Yuda na Yerusalemu wakaanguka chini ili kuabudu mbele za Bwana. 19 Ndipo baadhi ya Walawi kutoka kwa Wakohathi na kwa wana wa Kora wakasimama na kumsifu Bwana, Mungu wa Israeli, kwa sauti kuu sana.
20 Asubuhi na mapema wakaondoka kuelekea Jangwa la Tekoa. Walipoanza safari, Yehoshafati akasimama akasema, “Nisikilizeni, enyi Yuda, na watu wa Yerusalemu! Mwaminini Bwana Mungu wenu, hivyo mtathibitika, wasadikini manabii wake nanyi mtafanikiwa. 21 Alipomaliza kushauriana na watu, Yehoshafati akawaweka watu wa kumwimbia Bwana na kumsifu katika utukufu wa utakatifu wake walipokuwa wametangulia mbele ya jeshi, wakisema:
“Mshukuruni Bwana
kwa kuwa upendo wake wadumu milele.”
22 Walipoanza kuimba na kusifu, Bwana akaweka waviziao dhidi ya watu wa Amoni, Moabu na wale wa Mlima Seiri waliokuwa wamekuja kuishambulia Yuda, nao wakashindwa. 23 Watu wa Amoni na Moabu wakawainukia watu wa Mlima Seiri ili kuwaua na kuwaangamiza kabisa. Baada ya kumaliza kuwachinja watu wa Seiri, wakaangamizana wao kwa wao.
24 Yuda walipofika katika mnara wa ulinzi wa jangwani, wakaliangalia lile jeshi kubwa, wakaona ni maiti tupu zimetapakaa ardhini, wala hakuna yeyote aliyenusurika. 25 Hivyo Yehoshafati na watu wake wakaenda kujitwalia nyara kutoka kwao, nao wakakuta humo wingi wa mifugo, mali, nguo na vitu vya thamani, ambavyo vilikuwa vingi zaidi ya vile walivyoweza kuchukua. Wakakusanya nyara kwa siku tatu kwa sababu zilikuwa nyingi mno. 26 Siku ya nne wakakusanyika katika Bonde la Beraka kwa maana huko ndiko walikomsifu Bwana. Ndiyo sababu linaitwa Bonde la Beraka mpaka leo.
1 Sio kwetu sisi, Ee Bwana, sio kwetu sisi,
bali utukufu ni kwa jina lako,
kwa sababu ya upendo
na uaminifu wako.
2 Kwa nini mataifa waseme,
“Yuko wapi Mungu wao?”
3 Mungu wetu yuko mbinguni,
naye hufanya lolote limpendezalo.
4 Lakini sanamu zao ni za fedha na dhahabu,
zilizotengenezwa kwa mikono ya wanadamu.
5 Zina vinywa, lakini haziwezi kusema,
zina macho, lakini haziwezi kuona;
6 zina masikio, lakini haziwezi kusikia,
zina pua, lakini haziwezi kunusa;
7 zina mikono, lakini haziwezi kupapasa,
zina miguu, lakini haziwezi kutembea;
wala koo zao haziwezi kutoa sauti.
8 Wale wanaozitengeneza watafanana nazo,
vivyo hivyo wale wote wanaozitumainia.
9 Ee nyumba ya Israeli, mtumainini Bwana,
yeye ni msaada na ngao yao.
10 Ee nyumba ya Aroni, mtumainini Bwana,
yeye ni msaada na ngao yao.
11 Ninyi mnaomcha, mtumainini Bwana,
yeye ni msaada na ngao yao.
12 Bwana anatukumbuka na atatubariki:
ataibariki nyumba ya Israeli,
ataibariki nyumba ya Aroni,
13 atawabariki wale wanaomcha Bwana,
wadogo kwa wakubwa.
14 Bwana na awawezeshe kuongezeka,
ninyi na watoto wenu.
15 Mbarikiwe na Bwana
Muumba wa mbingu na dunia.
16 Mbingu zilizo juu sana ni mali ya Bwana,
lakini dunia amempa mwanadamu.
17 Sio wafu wanaomsifu Bwana,
wale washukao mahali pa kimya,
18 bali ni sisi tunaomtukuza Bwana,
sasa na hata milele.
Msifuni Bwana.
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya wana wa Kora. Mtindo wa alamothi.
1 Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu,
msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso.
2 Kwa hiyo hatutaogopa, hata kama dunia ikiondolewa
nayo milima ikiangukia moyoni mwa bahari.
3 Hata kama maji yake yatanguruma na kuumuka,
milima nayo ikitetemeka kwa mawimbi yake.
4 Kuna mto ambao vijito vyake vinaufurahisha mji wa Mungu,
mahali patakatifu ambako Aliye Juu Sana anaishi.
5 Mungu yuko katikati yake, hautaanguka,
Mungu atausaidia asubuhi na mapema.
6 Mataifa yanafanya ghasia, falme zinaanguka,
Yeye huinua sauti yake, dunia ikayeyuka.
7 Bwana Mwenye Nguvu Zote yu pamoja nasi,
Mungu wa Yakobo ni ngome yetu.
8 Njooni mkaone kazi za Bwana
jinsi alivyofanya ukiwa katika nchi.
9 Anakomesha vita hata miisho ya dunia,
anakata upinde na kuvunjavunja mkuki,
anateketeza ngao kwa moto.
10 “Tulieni, mjue ya kwamba mimi ndimi Mungu;
nitatukuzwa katikati ya mataifa,
nitatukuzwa katika dunia.”
11 Bwana Mwenye Nguvu Zote yu pamoja nasi;
Mungu wa Yakobo ni ngome yetu.
27 Kisha watu wote wa Yuda na Yerusalemu, wakiongozwa na Yehoshafati, wakarudi Yerusalemu wakiwa na furaha kwa kuwa Bwana alikuwa amewasababisha wafurahi juu ya adui zao. 28 Wakaingia Yerusalemu na kwenda hekaluni mwa Bwana wakiwa na vinubi, zeze na tarumbeta.
29 Hofu ya Mungu ikazipata falme zote za nchi waliposikia jinsi Bwana alivyokuwa amepigana dhidi ya adui za Israeli. 30 Ufalme wa Yehoshafati ukawa na amani, kwa kuwa Mungu wake alikuwa amemstarehesha pande zote.
35 Hatimaye Yehoshafati mfalme wa Yuda akafanya urafiki na Ahazia mfalme wa Israeli ambaye alifanya maovu sana. 36 Akaungana naye kutengeneza meli nyingi za kwenda Tarshishi, nazo zilitengenezwa huko Esion-Geberi. 37 Ndipo Eliezeri mwana wa Dodavahu wa Maresha akatoa unabii dhidi ya Yehoshafati, akasema, “Kwa kuwa umeungana na Ahazia, Bwana ataangamiza vile mlivyotengeneza.” Zile meli zikavunjika na hazikuweza kungʼoa nanga ili kwenda Tarshishi.
49 Wakati ule, Ahazia mwana wa Ahabu akamwambia Yehoshafati, “Waache watu wangu wasafiri baharini pamoja na watu wako,” lakini Yehoshafati akakataa.
16 Katika mwaka wa tano wa Yoramu mwana wa Ahabu mfalme wa Israeli, wakati huo Yehoshafati akiwa mfalme wa Yuda, Yehoramu mwana wa Yehoshafati akaanza kutawala kama mfalme wa Yuda.