Sehemu ya 4: Utawala wa Yehoshafati

Ufalme wa Yuda

Kuingia kwa Yehoshafati Madarakani na Utawala Wake Mwema

914 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

1 Wafalme 22:41–44

41 Yehoshafati mwana wa Asa akawa mfalme wa Yuda katika mwaka wa nne wa Ahabu mfalme wa Israeli. 42 Yehoshafati alikuwa na umri wa miaka thelathini na mitano alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka ishirini na mitano. Jina la mama yake aliitwa Azuba binti Shilhi. 43 Katika kila jambo alitembea katika njia za Asa baba yake wala hakwenda kinyume chake. Alifanya yaliyo mema machoni pa Bwana. Hata hivyo mahali pa juu pa kuabudia hapakuondolewa. Watu waliendelea kutoa kafara na kufukiza uvumba huko. 44 Yehoshafati pia alikuwa na amani na mfalme wa Israeli.

1 Wafalme 22:46–47

46 Aliondolea mbali katika nchi mahanithi wa mahali pa kuabudia miungu waliobaki huko hata baada ya utawala wa baba yake Asa. 47 Tangu hapo hapakuwepo na mfalme katika Edomu, naibu ndiye alitawala.

2 Nyakati 17:2–19

2 Akaweka jeshi katika miji yote ya Yuda yenye ngome na kuweka askari walinzi katika Yuda na katika miji ya Efraimu ile ambayo baba yake Asa alikuwa ameiteka.

3 Bwana Mungu alikuwa na Yehoshafati kwa sababu katika miaka yake ya mwanzoni alienenda katika njia za Daudi baba yake. Hakutafuta Mabaali 4 bali alimtafuta Mungu wa baba yake na kuzifuata amri zake badala ya kufuata desturi za watu wa Israeli. 5 Kwa hiyo Bwana akauimarisha ufalme chini ya uongozi wake, nao Yuda wote wakamletea Yehoshafati zawadi, hivyo akawa na utajiri mwingi na heshima. 6 Moyo wake ukawa hodari katika njia za Bwana na zaidi ya yote, akaondoa mahali pa juu pa kuabudia miungu na nguzo za Maashera katika Yuda.

7 Katika mwaka wa tatu wa utawala wa akatuma maafisa wake ambao ni: Ben-Haili, Obadia, Zekaria, Nethaneli na Mikaya ili kufundisha katika miji ya Yuda. 8 Pamoja nao walikuwepo Walawi fulani nao ni: Shemaya, Nethania, Zebadia, Asaheli, Shemiramothi, Yehonathani, Adoniya, Tobia, Tob-Adonia, pamoja nao walikuwepo makuhani Elishama na Yehoramu. 9 Wakafundisha Yuda yote, wakiwa wamechukua Kitabu cha Sheria ya Bwana wakazunguka miji yote ya Yuda na kufundisha watu.

10 Hofu ya Bwana ikawa juu ya falme zote za nchi zilizozunguka Yuda, hivyo hawakufanya vita na Yehoshafati. 11 Baadhi ya Wafilisti wakamletea Yehoshafati zawadi na fedha kama ushuru, nao Waarabu wakamletea mifugo: kondoo dume 7,700 na mbuzi 7,700.

12 Yehoshafati akaendelea kupata nguvu zaidi na zaidi, akajenga ngome na miji ya hazina katika Yuda 13 na akawa na wingi mkubwa wa vitu katika miji ya Yuda. Pia aliweka askari wa vita wenye uzoefu huko Yerusalemu. 14 Wakaandikishwa katika jamaa zao kama ifuatavyo:

Kutoka Yuda, majemadari wa vikosi vya elfu:

Jemadari Adna akiwa na askari wa vita 300,000;

15 aliyefuata ni jemadari Yehohanani, akiwa na askari 280,000 walio tayari kwa vita;

16 aliyefuata ni Amasia mwana wa Zikri, ambaye alijitolea kwa ajili ya kazi ya Bwana, akiwa na askari 200,000.

17 Kutoka Benyamini:

Eliada, askari shujaa akiwa na watu 200,000 wenye silaha za nyuta na ngao;

18 aliyefuata ni Yehozabadi, akiwa na askari 180,000 wenye silaha za vita.

19 Hawa ndio waliomtumikia mfalme, mbali na wale mfalme aliweka katika miji yenye ngome huko Yuda yote.

Vita vya Yehoshafati na Utawala Bora 897 KK

2 Nyakati 18:1–2

1 Basi, Yehoshafati alikuwa na mali nyingi sana na heshima. Naye akafanya urafiki na Ahabu kwa mwanawe kumwoa binti wa Ahabu. 2 Baada ya miaka kadhaa akashuka kumtembelea Ahabu huko Samaria. Ahabu akachinja ngʼombe na kondoo wengi kwa ajili yake na watu aliokuwa amefuatana nao. Kisha Ahabu akamshawishi Yehoshafati kukwea pamoja naye ili kuishambulia Ramoth-Gileadi.

2 Nyakati 19:1–7

1 Mfalme Yehoshafati wa Yuda akarudi salama kwenye jumba lake la kifalme huko Yerusalemu. 2 Yehu mwonaji, mwana wa Hanani, akapanda kwenda kuonana naye akamwambia Mfalme Yehoshafati, “Je, utawasaidia waovu na kuwapenda wale wanaomchukia Bwana? Kwa sababu ya jambo hili, ghadhabu ya Bwana iko juu yako. 3 Hata hivyo, kuna mema yaliyoonekana kwako, kwa kuwa umeondoa katika nchi nguzo za Ashera na umeukaza moyo wako katika kumtafuta Mungu.”

4 Yehoshafati aliishi huko Yerusalemu, naye akatoka akaenda tena miongoni mwa watu, kuanzia Beer-Sheba hadi nchi ya vilima ya Efraimu na kuwageuza wakamrudia Bwana, Mungu wa baba zao. 5 Akawaweka waamuzi katika nchi, kwenye miji yote ya Yuda yenye maboma. 6 Akawaambia, “Angalieni kwa makini yale mtendayo, kwa kuwa hamkuhukumu kwa ajili ya mwanadamu bali kwa ajili ya Bwana ambaye yu pamoja nanyi kila mtoapo hukumu. 7 Basi sasa hofu ya Bwana na iwe juu yenu. Hukumuni kwa uangalifu, kwa kuwa kwa Bwana Mungu wetu hakuna jambo lisilo la haki, upendeleo, wala rushwa.”

Zaburi 82

Zaburi ya Asafu.

1 Mungu anaongoza kusanyiko kuu,

anatoa hukumu miongoni mwa “miungu”:

2 “Hata lini utaendelea kuwatetea wasio haki

na kuonyesha upendeleo kwa waovu?

3 Teteeni wanyonge na yatima,

tunzeni haki za maskini na walioonewa.

4 Mwokoeni mnyonge na mhitaji,

wakomboeni kutoka mkononi mwa mwovu.

5 “Hawajui lolote, hawaelewi lolote.

Wanatembea gizani;

misingi yote ya dunia imetikisika.

6 “Nilisema, ‘Ninyi ni “miungu”;

ninyi nyote ni wana wa Aliye Juu Sana.’

7 Lakini mtakufa kama wanadamu wa kawaida;

mtaanguka kama mtawala mwingine yeyote.”

8 Ee Mungu, inuka uihukumu nchi,

kwa kuwa mataifa yote ni urithi wako.

2 Nyakati 19:8–11

8 Pia huko Yerusalemu, Yehoshafati akaweka baadhi ya Walawi, makuhani na viongozi wa jamaa za Waisraeli ili kutoa hukumu kwa ajili ya Bwana na kuamua magomvi. Nao waliishi huko Yerusalemu. 9 Akawapa maagizo haya: “Ni lazima mtumike kwa uaminifu na kwa moyo wote katika kicho cha Bwana. 10 Katika kila shauri lifikalo mbele yenu kutoka kwa ndugu zenu wale waishio katika miji, ikiwa ni la umwagaji wa damu au mambo mengine yahusuyo sheria, amri, hukumu au maagizo, inawapasa ninyi kuwaonya kwamba wasiingie katika hatia dhidi ya Bwana, la sivyo ghadhabu yake itakuja juu yenu na ndugu zenu. Tendeni hivyo, nanyi hamtatenda dhambi.

11 “Amaria kuhani mkuu atakuwa juu yenu katika jambo lolote linalomhusu Bwana naye Zebadia mwana wa Ishmaeli, kiongozi wa kabila la Yuda, atakuwa juu yenu kwa jambo lolote linalomhusu mfalme, nao Walawi watatumika kama maafisa mbele yenu. Tendeni kwa ujasiri, naye Bwana atakuwa pamoja na wale watendao vyema.”