Isaya Anatabiri Uvamizi wa Waashuru (continued)
Unabii wa Isaya kuhusu uvamizi wa Palestina uliofanywa na jeshi la Waashuru.
715 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Chipukizi litatokea kutoka shina la Yese,
kutoka mizizi yake Tawi litazaa tunda.
2 Roho wa Bwana atakaa juu yake,
Roho wa hekima na wa ufahamu,
Roho wa shauri na wa uweza,
Roho wa maarifa na wa kumcha Bwana
3 naye atafurahia kumcha Bwana.
Hatahukumu kwa yale ayaonayo kwa macho yake,
wala kuamua kwa yale ayasikiayo kwa masikio yake,
4 bali kwa uadilifu atahukumu wahitaji,
kwa haki ataamua wanyenyekevu wa dunia.
Ataipiga dunia kwa fimbo ya kinywa chake,
kwa pumzi ya midomo yake atawaua waovu.
5 Haki itakuwa mkanda wake
na uaminifu utakuwa mshipi kiunoni mwake.
6 Mbwa mwitu ataishi pamoja na mwana-kondoo,
naye chui atalala pamoja na mbuzi,
ndama, mwana simba na ngʼombe wa mwaka mmoja watakaa pamoja,
naye mtoto mdogo atawaongoza.
7 Ngʼombe na dubu watalisha pamoja,
watoto wao watalala pamoja,
na simba atakula majani makavu kama maksai.
8 Mtoto mchanga atacheza karibu na shimo la nyoka,
naye mtoto mdogo ataweka mkono wake
kwenye kiota cha fira.
9 Hawatadhuru wala kuharibu
juu ya mlima wangu mtakatifu wote,
kwa kuwa dunia itajawa na kumjua Bwana
kama maji yajazavyo bahari.
10 Katika siku hiyo, Shina la Yese atasimama kama bendera kwa ajili ya mataifa. Mataifa yatakusanyika kwake, na mahali pake pa kupumzikia patakuwa utukufu. 11 Katika siku hiyo Bwana atanyoosha mkono wake mara ya pili kurudisha mabaki ya watu wake waliosalia kutoka Ashuru, Misri, Pathrosi, Kushi, Elamu, Babeli, Hamathi na kutoka visiwa vya baharini.
12 Atainua bendera kwa mataifa
na kuwakusanya Waisraeli walioko uhamishoni;
atawakusanya watu wa Yuda waliotawanyika
kutoka pembe nne za dunia.
13 Wivu wa Efraimu utatoweka,
na adui wa Yuda watakatiliwa mbali;
Efraimu hatamwonea Yuda wivu,
wala Yuda hatakuwa na uadui na Efraimu.
14 Watawashukia katika miteremko ya Wafilisti
hadi upande wa magharibi,
kwa pamoja watawateka watu nyara
hadi upande wa mashariki.
Watawapiga Edomu na Moabu,
na Waamoni watatawaliwa nao.
15 Bwana atakausha
ghuba ya bahari ya Misri;
kwa upepo mkavu ataupeleka mkono wake
juu ya Mto Frati.
Ataugawanya katika vijito saba
ili watu waweze kuuvuka wakiwa wamevaa viatu.
16 Itakuwepo njia kuu kwa mabaki ya watu wake
wale waliosalia kutoka Ashuru,
kama ilivyokuwa kwa Israeli
walipopanda kutoka Misri.
12:1 Katika siku ile utasema:
“Nitakusifu wewe, Ee Bwana.
Ingawa ulinikasirikia,
hasira yako imegeukia mbali
nawe umenifariji.
2 Hakika Mungu ni wokovu wangu;
nitamtumaini wala sitaogopa.
Bwana, Bwana, ni nguvu zangu na wimbo wangu;
amekuwa wokovu wangu.”
3 Kwa furaha mtachota maji
kutoka visima vya wokovu.
4 Katika siku hiyo mtasema:
“Mshukuruni Bwana, mliitie jina lake;
julisheni miongoni mwa mataifa yale aliyoyafanya,
tangazeni kuwa jina lake limetukuka.
5 Mwimbieni Bwana, kwa kuwa ametenda mambo makuu,
hili na lijulikane duniani kote.
6 Pazeni sauti mwimbe kwa furaha, watu wa Sayuni,
kwa maana mkuu ni yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli miongoni mwenu.”
13:1 Neno kuhusu Babeli ambalo Isaya mwana wa Amozi aliliona:
2 Twekeni bendera juu ya mlima usio na kitu,
wapazieni sauti,
wapungieni mkono waingie
katika malango ya wenye heshima.
3 Nimewaamuru watakatifu wangu;
nimewaita mashujaa wangu waitimize hasira yangu:
wale wanaoshangilia ushindi wangu.
4 Sikilizeni kelele juu ya milima,
kama ile ya umati mkubwa wa watu!
Sikilizeni, makelele katikati ya falme,
kama mataifa yanayokusanyika pamoja!
Bwana Mwenye Nguvu Zote anakusanya
jeshi kwa ajili ya vita.
5 Wanakuja kutoka nchi za mbali sana,
kutoka miisho ya mbingu,
Bwana na silaha za ghadhabu yake,
kuangamiza nchi yote.
6 Ombolezeni, kwa maana siku ya Bwana i karibu,
itakuja kama uharibifu kutoka kwa Mwenyezi.
7 Kwa sababu ya hili, mikono yote italegea,
moyo wa kila mtu utayeyuka.
8 Hofu itawakamata,
uchungu na maumivu makali yatawashika,
watagaagaa kama mwanamke aliye na utungu wa kuzaa.
Watatazamana kwa hofu kila mtu na mwenzake,
nyuso zao zikiwaka kama moto.
9 Tazameni, siku ya Bwana inakuja,
siku katili, yenye ghadhabu na hasira kali,
kuifanya nchi kuwa ukiwa
na kuwaangamiza wenye dhambi waliomo ndani yake.
10 Nyota za mbinguni na makundi ya nyota
havitatoa mwanga wake.
Jua linalochomoza litatiwa giza
na mwezi hautatoa nuru yake.
11 Nitauadhibu ulimwengu kwa ajili ya uovu wake,
waovu kwa ajili ya dhambi zao.
Nitakomesha majivuno ya wenye kiburi,
na nitakishusha kiburi cha watu wakatili.
12 Nitawafanya wanadamu kuwa adimu kuliko dhahabu safi,
watakuwa wachache sana kuliko dhahabu ya Ofiri.
13 Kwa hiyo nitazifanya mbingu zitetemeke,
nayo dunia itatikisika kutoka mahali pake
katika ghadhabu ya Bwana Mwenye Nguvu Zote,
katika siku ya hasira yake iwakayo.
14 Kama swala awindwaye,
kama kondoo wasio na mchungaji,
kila mmoja atarudi kwa watu wake mwenyewe,
kila mmoja atakimbilia nchi yake ya kuzaliwa.
15 Yeyote atakayetekwa atapasuliwa tumbo,
wote watakaokamatwa watauawa kwa upanga.
16 Watoto wao wachanga watavunjwa vipande vipande
mbele ya macho yao;
nyumba zao zitatekwa
na wake zao watatendwa jeuri.
17 Tazama, nitawachochea Wamedi dhidi yao,
ambao hawajali fedha
wala hawafurahii dhahabu.
18 Mishale yao itawaangusha vijana,
hawatakuwa na huruma kwa watoto wachanga
wala hawataangalia watoto kwa huruma.
19 Babeli, johari ya falme,
utukufu wa kiburi cha Wababeli,
itaangushwa na Mungu
kama Sodoma na Gomora.
20 Hautakaliwa na watu kamwe
wala watu hawataishi humo kwa vizazi vyote.
Hakuna Mwarabu atakayepiga hema lake huko,
hakuna mchungaji atakayepumzisha makundi yake huko.
21 Lakini viumbe wa jangwani watalala huko,
mbweha watajaza nyumba zake,
bundi wataishi humo
nao mbuzi-mwitu watarukaruka humo.
22 Fisi watalia ndani ya ngome zake,
mbweha ndani ya majumba yake ya kifahari.
Wakati wake umewadia,
na siku zake hazitaongezwa.