Isaya Anatabiri Kuangamizwa kwa Tiro
715 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Neno kuhusu Tiro:
Ombolezeni, enyi meli za Tarshishi!
Kwa kuwa Tiro imeangamizwa,
imeachwa bila nyumba wala bandari.
Kuanzia nchi ya Kitimu
neno limewajia.
2 Nyamazeni kimya, enyi watu wa kisiwani,
pia ninyi wafanyabiashara wa Sidoni,
ambao mabaharia wamewatajirisha.
3 Kwenye maji makuu
nafaka za Shihori zilikuja;
mavuno ya Naili yalikuwa mapato ya Tiro,
naye akawa soko la mataifa.
4 Uaibishwe ee Sidoni, nawe ee ngome la bahari,
kwa kuwa bahari imesema:
“Sijapata kuwa na uchungu wa kuzaa wala sijapata kuzaa,
wala sijapata kulea wana wala kutunza mabinti.”
5 Habari ifikapo Misri,
watakuwa katika maumivu makuu kwa ajili ya taarifa kutoka Tiro.
6 Vukeni mpaka Tarshishi,
ombolezeni, enyi watu wa kisiwani.
7 Je, huu ndio mji wenu uliojaa sherehe,
mji wa zamani, zamani kabisa
ambao miguu yake imeuchukua
kufanya makao nchi za mbali sana?
8 Ni nani amepanga hili dhidi ya Tiro,
mji utoao mataji,
ambao wafanyabiashara wake ni wana wa mfalme
na wachuuzi wake ni watu mashuhuri wa dunia?
9 Bwana Mwenye Nguvu Zote ndiye alipanga jambo hili,
ili kukishusha kiburi cha utukufu wote
na kuwanyenyekesha wale wote
ambao ni mashuhuri duniani.
10 Ee Binti Tarshishi,
pita katika nchi yako kama vile Mto Naili
kwa kuwa huna tena bandari.
11 Bwana amenyoosha mkono wake juu ya bahari
na kuzifanya falme zake zitetemeke.
Ametoa amri kuhusu Kanaani
kwamba ngome zake ziangamizwe.
12 Alisema, “Usizidi kufurahi,
ee Bikira Binti Sidoni, sasa umepondwa!
“Simama, vuka uende Kitimu;
hata huko hutapata pumziko.”
13 Tazama katika nchi ya Wakaldayo,
watu hawa ambao sasa hawaonekani kama wapo!
Waashuru wameifanya nchi hiyo
kuwa mahali pa viumbe wa jangwani.
Wamesimamisha minara yao ya vita kuuzunguka,
wameziteka ngome zake na kuziacha tupu
na kuufanya kuwa magofu.
14 Ombolezeni, enyi meli za Tarshishi;
ngome yenu imeangamizwa!
15 Wakati huo Tiro utasahauliwa kwa miaka sabini, muda wa maisha ya mfalme. Lakini mwisho wa miaka hiyo sabini, itakuwa kwa Tiro kama ilivyo katika wimbo wa kahaba:
16 “Twaa kinubi, tembea mjini kote,
ewe kahaba uliyesahauliwa;
piga kinubi vizuri, imba nyimbo nyingi,
ili upate kukumbukwa.”
17 Mwishoni mwa miaka sabini, Bwana atashughulika na Tiro. Naye atarudia ajira yake ya ukahaba, na atafanya biashara yake na falme zote juu ya uso wa dunia. 18 Lakini faida na mapato yake yatawekwa wakfu kwa Bwana; hayatahifadhiwa wala kufichwa. Faida zake zitakwenda kwa wale wakaao mbele za Bwana kwa ajili ya chakula tele na mavazi mazuri.
Isaya Anatabiri Uvamizi wa Waashuru
Unabii wa Isaya kuhusu uvamizi wa Palestina uliofanywa na jeshi la Waashuru.
5 “Ole kwa Ashuru, fimbo ya hasira yangu,
ambaye mkononi mwake ana rungu ya ghadhabu yangu!
6 Ninamtuma dhidi ya taifa lisilomjua Mungu,
ninamtuma dhidi ya taifa linalonikasirisha,
kukamata mateka na kunyakua nyara,
pia kuwakanyaga chini kama matope ya barabarani.
7 Lakini hili silo analokusudia,
hili silo alilo nalo akilini;
kusudi lake ni kuangamiza,
kuyakomesha mataifa mengi.
8 Maana asema, ‘Je, wafalme wote
si majemadari wangu?
9 Je, Kalno hakutendwa kama Karkemishi?
Hamathi si kama Arpadi,
nayo Samaria si kama Dameski?
10 Kama vile mkono wangu ulivyotwaa falme za sanamu,
falme ambazo vinyago vyao vilizidi vile vya Yerusalemu na Samaria:
11 je, nisiishughulikie Yerusalemu na sanamu zake
kama nilivyoshughulikia Samaria na vinyago vyake?’ ”
12 Bwana atakapokuwa amemaliza kazi yake yote dhidi ya Mlima Sayuni na Yerusalemu, atasema, “Nitamwadhibu mfalme wa Ashuru kwa ajili ya majivuno ya ukaidi wa moyo wake na kutazama kwa macho yenye dharau.” 13 Kwa kuwa anasema:
“ ‘Kwa nguvu za mkono wangu nimefanya hili,
kwa hekima yangu, kwa sababu nina ufahamu.
Niliondoa mipaka ya mataifa,
niliteka nyara hazina zao,
kama yeye aliye shujaa
niliwatiisha wafalme wao.
14 Kama mtu atiavyo mkono kwenye kiota,
ndivyo mkono wangu ulivyochukua utajiri wa mataifa;
kama watu wakusanyavyo mayai yaliyoachwa,
ndivyo nilivyokusanya nchi zote;
wala hakuna hata mmoja aliyepiga bawa
au kufungua kinywa chake kutoa mlio.’ ”
15 Je, shoka laweza kujigamba kuwa na nguvu zaidi
kuliko yule anayelitumia,
au msumeno kujisifu
dhidi ya yule anayeutumia?
Ni kana kwamba fimbo ingeweza kumwinua yeye aichukuaye,
au mkongojo ungemwinua mwenye kuutumia!
16 Kwa hiyo Bwana, Bwana Mwenye Nguvu Zote,
atatuma ugonjwa wa kudhoofisha kwa askari wake walio hodari,
katika fahari yake moto utawaka
kama mwali wa moto.
17 Nuru ya Israeli itakuwa moto,
Aliye Mtakatifu wao mwali wa moto;
katika siku moja utaunguza na kuteketeza miiba
na michongoma yake.
18 Fahari ya misitu yake na mashamba yenye rutuba
utateketeza kabisa,
kama vile mtu mgonjwa adhoofikavyo.
19 Nayo miti inayobaki katika misitu yake itakuwa michache sana
hata mtoto mdogo angeweza kuihesabu.
20 Katika siku ile, mabaki ya Israeli,
walionusurika wa nyumba ya Yakobo,
hawatamtegemea tena yeye aliyewapiga,
lakini watamtegemea kwa kweli
Bwana Aliye Mtakatifu wa Israeli.
21 Mabaki watarudi, mabaki wa Yakobo
watamrudia Mungu Mwenye Nguvu.
22 Ingawa watu wako, ee Israeli, ni wengi kama mchanga wa pwani,
ni mabaki yao tu watakaorudi.
Maangamizi yamekwisha amriwa,
ni mengi tena ni haki.
23 Bwana, Bwana Mwenye Nguvu Zote, atatekeleza
maangamizi yaliyoamriwa juu ya nchi yote.
24 Kwa hiyo, hili ndilo Bwana, Bwana Mwenye Nguvu Zote asemalo:
“Enyi watu wangu mkaao Sayuni,
msiwaogope Waashuru,
wanaowapiga ninyi kwa fimbo
na kuinua rungu dhidi yenu, kama Misri ilivyofanya.
25 Bado kitambo kidogo sana hasira yangu dhidi yenu itakoma,
na ghadhabu yangu itaelekezwa kwenye maangamizi yao.”
26 Bwana Mwenye Nguvu Zote atawachapa kwa mjeledi,
kama alivyowapiga Wamidiani katika mwamba wa Orebu,
naye atainua fimbo yake juu ya maji,
kama alivyofanya huko Misri.
27 Katika siku hiyo mzigo wao utainuliwa kutoka mabegani mwenu,
na nira yao kutoka shingoni mwenu;
nira itavunjwa
kwa sababu ya kutiwa mafuta.
28 Wanaingia Ayathi,
wanapita katikati ya Migroni,
wanahifadhi mahitaji huko Mikmashi.
29 Wanavuka kivukoni, nao wanasema,
“Tutapiga kambi huko Geba usiku kucha.”
Rama inatetemeka;
Gibea ya Sauli inakimbia.
30 Piga kelele, ee Binti Galimu!
Sikiliza, ee Laisha!
Maskini Anathothi!
31 Madmena inakimbia;
watu wa Gebimu wanajificha.
32 Siku hii ya leo watasimama Nobu;
watatikisa ngumi zao
kwa mlima wa Binti Sayuni,
kwa kilima cha Yerusalemu.
33 Tazama, Bwana, Bwana Mwenye Nguvu Zote,
atayakata matawi kwa nguvu kuu.
Miti mirefu sana itaangushwa,
ile mirefu itashushwa chini.
34 Atakata vichaka vya msitu kwa shoka;
Lebanoni itaanguka mbele zake yeye Mwenye Nguvu.