Agano la Mungu na Abramu
1912 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Baada ya jambo hili, neno la Bwana likamjia Abramu katika maono:
“Usiogope, Abramu.
Mimi ni ngao yako,
na thawabu yako kubwa sana.”
2 Lakini Abramu akasema, “Ee Bwana Mwenyezi, utanipa nini na mimi sina hata mtoto na atakayerithi nyumba yangu ni huyu Eliezeri Mdameski?” 3 Abramu akasema, “Hukunipa watoto, hivyo mtumishi katika nyumba yangu ndiye atakuwa mrithi wangu.”
4 Ndipo neno la Bwana lilipomjia: “Mtu huyu hatakuwa mrithi wako, bali mwana atakayetoka katika viuno vyako mwenyewe ndiye atakayekuwa mrithi wako.” 5 Akamtoa nje na kusema, “Tazama juu kuelekea mbinguni na uhesabu nyota, kama hakika utaweza kuzihesabu.” Ndipo akamwambia, “Hivyo ndivyo uzao wako utakavyokuwa.”
6 Abramu akamwamini Bwana, naye kwake hili likahesabiwa kuwa haki.
7 Pia akamwambia, “Mimi ndimi Bwana, niliyekutoa toka Uru ya Wakaldayo nikupe nchi hii uimiliki.”
8 Lakini Abramu akasema, “Ee Bwana Mwenyezi, nitawezaje kujua kwamba nitapata kuimiliki?”
9 Ndipo Bwana akamwambia, “Niletee mtamba wa ngʼombe, mbuzi na kondoo dume, kila mmoja wa miaka mitatu, pamoja na hua na kinda la njiwa.”
10 Abramu akamletea hivi vyote, akampasua kila mnyama vipande viwili, akavipanga kila kimoja kuelekea mwenzake, lakini hata hivyo ndege, hakuwapasua vipande viwili. 11 Kisha ndege walao nyama wakatua juu ya mizoga, lakini Abramu akawafukuza.
12 Wakati jua lilipokuwa linatua, Abramu akashikwa na usingizi mzito, giza nene na la kutisha likaja juu yake. 13 Kisha Bwana akamwambia, “Ujue hakika kwamba wazao wako watakuwa wageni kwenye nchi ambayo si yao, nao watafanywa watumwa na kuteswa kwa miaka mia nne. 14 Lakini nitaliadhibu taifa lile watakalolitumikia kama watumwa, na baadaye watatoka huko na mali nyingi. 15 Wewe, hata hivyo utakwenda kwa baba zako kwa amani na kuzikwa katika uzee mwema. 16 Katika kizazi cha nne wazao wako watarudi hapa, kwa maana dhambi ya Waamori bado haijafikia kipimo kilichojaa.”
17 Wakati jua lilipokuwa limezama na giza limeingia, tanuru la moshi na mwali wa moto unaowaka vikatokea na kupita kati ya vile vipande vya nyama. 18 Siku hiyo Bwana akafanya Agano na Abramu, na kumwambia, “Nitawapa wazao wako nchi hii, kuanzia Kijito cha Misri hadi mto ule mkubwa, Frati, 19 yaani nchi ya Wakeni, Wakenizi, Wakadmoni, 20 Wahiti, Waperizi, Warefai, 21 Waamori, Wakanaani, Wagirgashi na Wayebusi.”
Kuzaliwa kwa Ishmaeli
1 Basi Sarai, mkewe Abramu, alikuwa hajamzalia watoto. Lakini alikuwa na mtumishi wa kike Mmisri jina lake Hagari, 2 hivyo Sarai akamwambia Abramu, “Bwana amenizuilia kupata watoto. Nenda, ukakutane kimwili na mtumishi wangu wa kike, huenda nitaweza kupata watoto kupitia kwake.”
Abramu akakubaliana na lile Sarai alilosema. 3 Hivyo baada ya Abramu kuishi katika nchi ya Kanaani miaka kumi, Sarai akamchukua mtumishi wake wa kike wa Kimisri, Hagari na kumpa mumewe awe mke wake. 4 Akakutana kimwili na Hagari, naye akapata mimba.
Hagari alipojua kuwa ana mimba, alianza kumdharau Sarai. 5 Ndipo Sarai akamwambia Abramu, “Unawajibika na manyanyaso ninayoyapata. Nilimweka mtumishi wangu mikononi mwako, sasa kwa vile anajua kwamba ana mimba, ananidharau mimi. Bwana na aamue kati yako na mimi.”
6 Abramu akamwambia, “Mtumishi wako yuko mikononi mwako. Mtendee lolote unalofikiri ni bora zaidi.” Ndipo Sarai akamtesa Hagari, hivyo akamtoroka.
7 Malaika wa Bwana akamkuta Hagari karibu na chemchemi huko jangwani; ilikuwa chemchemi ile iliyokuwa kando ya barabara iendayo Shuri. 8 Malaika akamwambia, “Hagari, mtumishi wa Sarai, umetokea wapi, na unakwenda wapi?”
Akamjibu, “Ninamkimbia bibi yangu Sarai.”
9 Ndipo malaika wa Bwana akamwambia, “Rudi kwa bibi yako ukajishushe chini yake.” 10 Malaika akaendelea akasema, “Nitazidisha wazao wako, hivi kwamba watakuwa wengi mno wasiohesabika.”
11 Pia malaika wa Bwana akamwambia:
“Wewe sasa una mimba
nawe utamzaa mwana.
Utamwita jina lake Ishmaeli,
kwa sababu Bwana amesikia juu ya huzuni yako.
12 Atakuwa punda-mwitu katikati ya wanadamu,
mkono wake utakuwa dhidi ya kila mtu
na mkono wa kila mtu dhidi yake,
naye ataishi kwa uhasama
na ndugu zake wote.”
13 Hagari akampa Bwana aliyezungumza naye jina hili: “Wewe ndiwe Mungu unionaye mimi,” kwa maana alisema, “Sasa nimemwona yeye anayeniona mimi.” 14 Ndiyo sababu kisima kile kikaitwa Beer-Lahai-Roi, ambacho bado kipo huko hata leo kati ya Kadeshi na Beredi.
15 Hivyo Hagari akamzalia Abramu mwana, naye Abramu akamwita huyo mwana Hagari aliyemzalia, Ishmaeli. 16 Abramu alikuwa na umri wa miaka themanini na sita wakati Hagari alipomzalia Ishmaeli.