Abramu na Loti Wanatengana
1996 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
5 Basi Loti, ambaye alikuwa anafuatana na Abramu, alikuwa pia na makundi ya mbuzi, kondoo, ngʼombe na mahema. 6 Lakini nchi haikuwatosha kukaa pamoja kwa ajili ya wingi wa mali zao. 7 Ukazuka ugomvi kati ya wachunga mifugo wa Abramu na wale wa Loti. Wakati huo, Wakanaani na Waperizi ndio waliokuwa wenyeji wa nchi hiyo.
8 Hivyo Abramu akamwambia Loti, “Pasiwe na ugomvi wowote kati yangu na wewe, wala kati ya wachungaji wangu na wako, kwa kuwa sisi ni ndugu. 9 Je, nchi yote haiko mbele yako? Tutengane. Kama ukielekea kushoto, nitakwenda kulia; kama ukielekea kulia, mimi nitakwenda kushoto.”
10 Loti akatazama akaona lile bonde lote la Yordani kuwa lilikuwa na maji tele, kama bustani ya Bwana, kama nchi ya Misri, kuelekea Soari. (Hii ilikuwa kabla Bwana hajaharibu Sodoma na Gomora.) 11 Hivyo Loti akajichagulia bonde lote la Yordani, akaelekea upande wa mashariki. Watu hao wawili wakatengana: 12 Abramu akaishi katika nchi ya Kanaani, wakati Loti aliishi miongoni mwa miji ya lile bonde na kupiga mahema yake karibu na Sodoma. 13 Basi watu wa Sodoma walikuwa waovu, wakifanya sana dhambi dhidi ya Bwana.
Ahadi kwa Abramu Inafanywa Upya 1920 KK
14 Baada ya Loti kuondoka Bwana akamwambia Abramu, “Ukiwa hapo ulipo, inua macho yako utazame kaskazini na kusini, mashariki na magharibi. 15 Nchi yote unayoiona nitakupa wewe na uzao wako hata milele. 16 Nitaufanya uzao wako uwe mwingi kama mavumbi ya nchi, hivyo kama kuna yeyote awezaye kuhesabu mavumbi, basi uzao wako utahesabika. 17 Ondoka, tembea katika marefu na mapana ya nchi, kwa maana ninakupa wewe.”
18 Basi Abramu akaondoa mahema yake, akaenda kuishi karibu na mialoni ya Mamre huko Hebroni, huko akamjengea Bwana madhabahu.
Vita na Wafalme Watano 1912 KK
1 Wakati huu Amrafeli mfalme wa Shinari, Arioko mfalme wa Elasari, Kedorlaoma mfalme wa Elamu, na Tidali mfalme wa Goimu 2 kwa pamoja walikwenda kupigana vita dhidi ya Bera mfalme wa Sodoma, Birsha mfalme wa Gomora, Shinabu mfalme wa Adma, Shemeberi mfalme wa Seboimu, na mfalme wa Bela (yaani Soari). 3 Hawa wote waliotajwa mwishoni waliunganisha majeshi yao kutoka Bonde la Sidimu (yaani Bahari ya Chumvi). 4 Walikuwa wametawaliwa na Mfalme Kedorlaoma kwa miaka kumi na miwili, lakini mwaka wa kumi na tatu waliasi.
5 Mnamo mwaka wa kumi na nne, Mfalme Kedorlaoma na wafalme waliojiunga naye walikwenda kupigana na kuwashinda Warefai katika Ashtaroth-Kanaimu, Wazuzi katika Hamu, Waemi katika Shawe-Kiriathaimu, 6 na Wahori katika nchi ya kilima cha Seiri, hadi El-Parani karibu na jangwa. 7 Kisha wakarudi wakaenda En-Misfati (yaani Kadeshi), wakashinda nchi yote ya Waamaleki, pamoja na Waamori waliokuwa wakiishi Hasason-Tamari.
8 Ndipo mfalme wa Sodoma, mfalme wa Gomora, mfalme wa Adma, mfalme wa Seboimu, na mfalme wa Bela (yaani Soari) wakatoka kupanga majeshi yao kwenye Bonde la Sidimu 9 dhidi ya Kedorlaoma, mfalme wa Elamu, Tidali mfalme wa Goimu, Amrafeli mfalme wa Shinari, na Arioko mfalme wa Elasari, yaani wafalme wanne dhidi ya wafalme watano. 10 Basi Bonde la Sidimu lilikuwa limejaa mashimo ya lami, nao wafalme wa Sodoma na wa Gomora walipokimbia, baadhi ya watu walitumbukia huko na wengine wakakimbilia vilimani. 11 Wale wafalme wanne wakateka mali yote ya Sodoma na Gomora pamoja na vyakula vyao vyote, kisha wakaenda zao. 12 Pia walimteka Loti mwana wa ndugu yake Abramu pamoja na mali zake, kwa kuwa alikuwa akiishi Sodoma.
13 Mtu mmoja aliyekuwa ametoroka akaja kumpa Abramu Mwebrania taarifa. Wakati huu Abramu alikuwa anaishi karibu na mialoni ya Mamre Mwamori, aliyekuwa ndugu yake Eshkoli na Aneri, ambao wote walikuwa wameungana na Abramu. 14 Abramu alipopata habari kwamba jamaa yake amechukuliwa mateka, akawaita watu 318 wa nyumbani mwake waliokuwa wamefunzwa kupigana vita, wakawafuatilia hadi Dani. 15 Wakati wa usiku Abramu aliwagawa watu wake katika vikosi ili awashambulie, na akawafuatilia, akawafukuza hadi Hoba, kaskazini ya Dameski. 16 Akarudisha mali zote, na akamrudisha Loti jamaa yake na mali zake, pamoja na wanawake na watu wengine.
17 Abramu aliporudi baada ya kumshinda Mfalme Kedorlaoma na wale wafalme waliojiunga naye, mfalme wa Sodoma akatoka kwenda kumlaki katika Bonde la Shawe (yaani Bonde la Mfalme).
Melkizedeki Anambariki Abramu
18 Ndipo Melkizedeki mfalme wa Salemu alipoleta mkate na divai. Alikuwa kuhani wa Mungu Aliye Juu Sana. 19 Naye akambariki Abramu, akisema,
“Abarikiwe Abramu na Mungu Aliye Juu Sana,
Muumba wa mbingu na nchi.
20 Abarikiwe Mungu Aliye Juu Sana,
ambaye amewaweka adui zako mkononi mwako.”
Ndipo Abramu akampa Melkizedeki sehemu ya kumi ya kila kitu.
21 Mfalme wa Sodoma akamwambia Abramu, “Nipe hao watu na hizo mali uchukue wewe mwenyewe.”
22 Lakini Abramu akamwambia mfalme wa Sodoma, “Nimeinua mkono wangu kwa Bwana, Mungu Aliye Juu Sana, Muumba wa mbingu na dunia, na nimeapa 23 kwamba sitapokea kitu chochote kilicho chako, hata kama ni uzi au gidamu ya kiatu, ili kamwe usije ukasema, ‘Nimemtajirisha Abramu.’ 24 Sitapokea chochote, ila kile tu watu wangu walichokula na sehemu ambayo ni fungu la watu waliokwenda pamoja nami, ambao ni Aneri, Eshkoli na Mamre. Wao na wapewe fungu lao.”