Maono ya Ezekieli ya Hekalu la Pili (continued)
574 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Yule mtu akanirudisha mpaka kwenye ingilio la Hekalu, nami nikaona maji yakitoka chini ya kizingiti cha Hekalu yakitiririkia upande wa mashariki (kwa maana upande wa mbele wa Hekalu ulielekea mashariki). Maji yalikuwa yakitoka chini upande wa kusini wa Hekalu, kusini mwa madhabahu. 2 Ndipo akanitoa nje kupitia lango la kaskazini na kunizungusha mpaka kwenye lango la nje linaloelekea mashariki, nayo maji yalikuwa yakitiririka kutoka upande wa kusini.
3 Mtu yule alipokwenda upande wa mashariki akiwa na kamba ya kupimia mkononi mwake, akapima dhiraa 1,000 kisha akanipitisha kwenye hayo maji ambayo yalifika kwenye vifundo vya miguu. 4 Akapima dhiraa 1,000 nyingine na kunipitisha kwenye hayo maji ambayo yalifika magotini. Akapima dhiraa nyingine 1,000 na kunipitisha kwenye hayo maji ambayo yalifika kiunoni. 5 Akapima tena dhiraa 1,000 nyingine, lakini wakati huu yalikuwa mto ambao sikuweza kuvuka, kwa kuwa maji yalikuwa na kina kirefu ambacho ni cha kuogelea, mto ambao hakuna mtu yeyote ambaye angeweza kuvuka. 6 Akaniuliza, “Je, mwanadamu, unaona hili?”
Kisha akanirudisha mpaka kwenye ukingo wa huo mto. 7 Nilipofika pale, nikaona idadi kubwa ya miti kila upande wa ule mto.
8 Akaniambia, “Haya maji yanatiririka kuelekea nchi ya mashariki na kushuka mpaka Araba, ambapo huingia Baharini. Yanapomwagikia kwenye hiyo Bahari, maji yaliyoko humo huponywa na kuwa safi. 9 Popote mto huu uendapo kila kiumbe hai kinachoyaparamia hayo maji kitaishi, nako kutakuwa na samaki wengi mno, mara maji haya yafikapo huko. Maji hayo yatakuwa hai na kila kitu kitakachoishi kule mto uendako. 10 Wavuvi watasimama kando ya bahari, kuanzia En-Gedi hadi En-Eglaimu huko patakuwa mahali pa kutandaza nyavu za kuvulia samaki. Samaki watakuwa wa aina nyingi, kama samaki wa Bahari Kuu 11 Lakini madimbwi yake na mabwawa yake hayatakuwa na maji yanayofaa kunywa, bali yatabakia kuwa maji ya chumvi. 12 Miti ya matunda ya kila aina itaota kwenye kingo zote mbili za mto huu. Majani yake hayatanyauka wala haitaacha kuwa na matunda katika matawi yake. Kila mwezi kutakuwa na matunda, kwa sababu maji yatokayo patakatifu yanaitiririkia. Matunda yake yatakuwa chakula na majani yake yatakuwa dawa.”
13 Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: “Hii ndiyo mipaka ambayo kwayo mtagawanya hiyo nchi kuwa urithi miongoni mwa hayo makabila kumi na mawili ya Israeli, pamoja na mafungu mawili ya Yosefu. 14 Mtagawa kwa usawa miongoni mwao. Kwa sababu niliapa kwa mkono ulioinuliwa kuwapa baba zenu, nchi hii itakuwa urithi wenu.
15 “Huu ndio utakuwa mpaka wa hiyo nchi:
“Upande wa kaskazini utaanzia Bahari Kuu kwa njia ya Hethloni kupitia Lebo-Hamathi hadi maingilio ya Sedadi. 16 Berotha na Sibraimu (ambao uko kwenye mpaka kati ya Dameski na Hamathi), hadi kufikia Haser-Hatikoni, ambao uko katika mpaka wa Haurani. 17 Hivyo mpaka utaendelea kuanzia Baharini hadi Hasar-Enoni, ukiambaa na mpaka wa kaskazini wa Dameski, pamoja na mpaka wa Hamathi upande wa kaskazini. Huu utakuwa ndio mpaka wa kaskazini.
18 Upande wa mashariki mpaka utapita kati ya Haurani na Dameski, kuambaa Yordani na kati ya Gileadi na nchi ya Israeli, hadi bahari ya mashariki na kufika Tamari. Huu utakuwa ndio mpaka wa mashariki.
19 Upande wa kusini utaanzia Tamari hadi kufikia maji ya Meriba-Kadeshi, kisha utaambaa na Kijito cha Misri hadi Bahari Kuu. Huu utakuwa ndio mpaka wa kusini.
20 Upande wa magharibi, Bahari Kuu itakuwa ndio mpaka hadi kwenye sehemu mkabala na Lebo-Hamathi. Huu utakuwa ndio mpaka wa magharibi.
21 “Mtagawanya nchi hii miongoni mwenu kufuatana na makabila ya Israeli. 22 Mtaigawanya kuwa urithi kwa ajili yenu na kwa ajili ya wageni wanaoishi miongoni mwenu na ambao wana watoto. Wao watakuwa kwenu kama wenyeji wazawa wa Israeli, pamoja na ninyi watagawiwa urithi miongoni mwa makabila ya Israeli. 23 Katika kabila lolote mgeni atakapoishi hapo ndipo mtakapompatia urithi wake,” asema Bwana Mwenyezi.
48:1 “Haya ndiyo majina ya makabila na sehemu zao: Kwenye mpaka wa kaskazini, Dani atakuwa na sehemu moja, mpaka huo utafuata barabara ya Hethloni hadi Lebo-Hamathi, Hasar-Enani hata mpaka wa kaskazini wa Dameski karibu na Hamathi utakuwa sehemu ya huo mpaka wake kuanzia upande wa mashariki hadi upande wa magharibi.
2 “Asheri atakuwa na sehemu moja, itapakana na nchi ya Dani kuanzia mashariki hadi upande wa magharibi.
3 “Naftali atakuwa na sehemu moja, itapakana na nchi ya Asheri kuanzia mashariki hadi magharibi.
4 “Manase atakuwa na sehemu moja, itapakana na nchi ya Naftali kuanzia mashariki hadi magharibi.
5 “Efraimu atakuwa na sehemu moja, itapakana na nchi ya Manase kuanzia mashariki hadi magharibi.
6 “Reubeni atakuwa na sehemu moja, itapakana na nchi ya Efraimu kuanzia mashariki hadi magharibi.
7 “Yuda atakuwa na sehemu moja, itapakana na nchi ya Reubeni kuanzia mashariki hadi magharibi.
8 “Kupakana na nchi ya Yuda kuanzia mashariki mpaka magharibi itakuwa ndiyo sehemu utakayoitoa ili kuwa toleo maalum. Itakuwa na upana wa dhiraa 25,000 na urefu wake kuanzia mashariki mpaka magharibi utakuwa ule ule wa sehemu moja ya kabila, mahali patakatifu patakuwa katikati ya eneo hilo.
9 “Hiyo sehemu maalum mtakayotoa kwa Bwana itakuwa na urefu wa dhiraa 25,000 na upana wa dhiraa 10,000 10 Hii itakuwa ni sehemu takatifu kwa ajili ya makuhani. Itakuwa na urefu wa dhiraa 25,000 upande wa kaskazini, upana wa dhiraa 10,000 upande wa magharibi, dhiraa 10,000 upande wa mashariki na urefu wa dhiraa 25,000 upande wa kusini. Katikati yake patakuwa mahali patakatifu pa Bwana. 11 Hii itakuwa kwa ajili ya makuhani waliowekwa wakfu, Wasadoki, waliokuwa waaminifu katika kunitumikia nao hawakupotoka kama Walawi walivyofanya wakati Waisraeli walipopotoka. 12 Itakuwa toleo maalum kwao kutoka sehemu takatifu ya nchi, yaani, sehemu takatifu sana, inayopakana na nchi ya Walawi.
13 “Kando ya nchi ya makuhani, Walawi watakuwa na mgawo wa urefu wa dhiraa 25,000 na upana wa dhiraa 10,000. Urefu wake utakuwa jumla dhiraa 25,000 na upana wa dhiraa 10,000. 14 Hawataruhusiwa kuuza wala kuibadilisha hata mojawapo. Hii ndiyo sehemu nzuri ya nchi kuliko nyingine zote, hivyo haitakuwa mikononi mwa watu wengine, kwa sababu ni takatifu kwa Bwana.
15 “Eneo linalobaki lenye upana wa dhiraa 5,000 na urefu wa dhiraa 25,000, litakuwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida ya mji, kwa ajili ya ujenzi wa nyumba na malisho. Mji utakuwa katikati yake 16 nao utakuwa na vipimo hivi: upande wa kaskazini dhiraa 4,500, upande wa kusini dhiraa 4,500, upande wa mashariki dhiraa 4,500 na upande wa magharibi dhiraa 4,500. 17 Sehemu ya malisho kwa ajili ya mji itakuwa na eneo la dhiraa 250 upande wa kaskazini, dhiraa 250 upande wa kusini, dhiraa 250 upande wa mashariki na dhiraa 250 upande wa magharibi. 18 Eneo linalobaki, linalopakana na sehemu takatifu likiwa na urefu sawa nalo, litakuwa dhiraa 10,000 upande wa mashariki na dhiraa 10,000 upande wa magharibi. Mazao yake yatawapa watumishi wa mji chakula. 19 Watumishi wa mji wanaolima shamba hili watatoka katika makabila yote ya Israeli. 20 Eneo lote la hiyo sehemu litakuwa mraba, yaani, dhiraa 25,000 kila upande. Kama toleo maalum mtatenga sehemu takatifu, pamoja na milki ya mji.
21 “Eneo linalobaki pande zote za eneo linalofanya sehemu takatifu na milki ya mji litakuwa mali ya mkuu atawalaye. Eneo hili litaenea upande wa mashariki kuanzia kwenye dhiraa 25,000 za sehemu takatifu hadi mpaka wa mashariki na kuelekea upande wa magharibi kuanzia kwenye dhiraa 25,000 hadi mpaka wa magharibi. Maeneo yote haya mawili yanayoenda sambamba na urefu wa sehemu za makabila yatakuwa ya mkuu anayetawala, na sehemu ile takatifu pamoja na mahali patakatifu pa Hekalu itakuwa katikati yake. 22 Kwa hiyo milki ya Walawi na milki ya mji vitakuwa katikati ya eneo lile ambalo ni mali ya mkuu anayetawala. Eneo la mkuu anayetawala litakuwa kati ya mpaka wa Yuda na mpaka wa Benyamini.
23 “Kuhusu makabila yaliyobaki: Benyamini atakuwa na sehemu moja, itakayoanzia upande wa mashariki hadi upande wa magharibi.
24 “Simeoni atakuwa na sehemu moja, itakayopakana na nchi ya Benyamini kuanzia mashariki hadi magharibi.
25 “Isakari atakuwa na sehemu moja, itakayopakana na nchi ya Simeoni kuanzia mashariki hadi magharibi.
26 “Zabuloni atakuwa na sehemu moja, itakayopakana na nchi ya Isakari kuanzia mashariki hadi magharibi.
27 “Gadi atakuwa na sehemu moja, itakayopakana na nchi ya Zabuloni kuanzia mashariki hadi magharibi.
28 “Mpaka wa kusini wa Gadi utapita kusini kuanzia Tamari hadi maji ya Meriba-Kadeshi, kisha kupitia upande wa Kijito cha Misri hadi Bahari Kuu.
29 “Hii ndiyo nchi mtakayogawanya kuwa urithi kwa makabila ya Israeli, nazo zitakuwa sehemu zao,” asema Bwana Mwenyezi.
30 “Haya yatakuwa ndiyo malango ya mji ya kutokea: Kuanzia upande wa kaskazini, ambayo urefu wake ni dhiraa 4,500, utakuwa na malango matatu, 31 malango hayo ya mji yatapewa majina ya makabila ya Israeli. Malango hayo matatu ya upande wa kaskazini moja litakuwa lango la Reubeni, lango la Yuda na lango la Lawi.
32 “Upande wa mashariki, wenye urefu wa dhiraa 4,500, utakuwa na malango matatu: lango la Yosefu, lango la Benyamini na lango la Dani.
33 “Upande wa kusini, wenye urefu wa dhiraa 4,500, utakuwa na malango matatu: lango la Simeoni, lango la Isakari na lango la Zabuloni.
34 “Upande wa magharibi, wenye urefu wa dhiraa 4,500, utakuwa na malango matatu: lango la Gadi, lango la Asheri na lango la Naftali.
35 “Urefu wote kuzunguka utakuwa dhiraa 18,000.
“Nalo jina la mji huo kuanzia wakati huo na kuendelea litakuwa:
Bwana yupo hapa.”