Unabii wa Mwisho wa Ezekieli Dhidi ya Misri

Utabiri wa mwisho dhidi ya Misri.

572 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Ezekieli 29:17–30:19

17 Katika mwaka wa ishirini na saba, mwezi wa kwanza, siku ya kwanza, neno la Bwana likanijia, kusema: 18 “Mwanadamu, Nebukadneza mfalme wa Babeli aliongoza jeshi lake kufanya kazi ngumu dhidi ya Tiro; kila kichwa kilipata upaa na kila bega likachunika. Lakini yeye na jeshi lake hawakupata malipo yoyote kutokana na muda wote aliongoza hiyo vita dhidi ya Tiro. 19 Kwa hiyo hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Nitaitia Misri mikononi mwa Nebukadneza mfalme wa Babeli, naye atachukua utajiri wa Misri. Atateka mateka na kuchukua nyara mali za Misri kama ujira kwa ajili ya jeshi lake. 20 Nimempa mfalme wa Babeli nchi ya Misri kuwa ujira kwa juhudi zake kwa sababu yeye na jeshi lake walifanya kwa ajili yangu, asema Bwana Mwenyezi.

21 “Katika siku hiyo nitaifanya nyumba ya Israeli iwe na nguvu nami nitakifungua kinywa chako miongoni mwao. Ndipo watakapojua kwamba Mimi ndimi Bwana.”

30:1 Neno la Bwana likanijia kusema: 2 “Mwanadamu, toa unabii na useme: ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo:

“ ‘Ombolezeni ninyi na mseme,

“Ole wa siku ile!”

3 Kwa kuwa siku ile imekaribia,

siku ya Bwana imekaribia,

siku ya mawingu,

siku ya maangamizi kwa mataifa.

4 Upanga utakuja dhidi ya Misri,

nayo maumivu makuu yataijia Ethiopia.

Mauaji yatakapoangukia Misri,

utajiri wake utachukuliwa

na misingi yake itabomolewa.

5 Kushi na Putu, Ludi na Arabia yote, Libya na watu wa nchi ya Agano watauawa kwa upanga pamoja na Misri.

6 “ ‘Hili ndilo Bwana asemalo:

“ ‘Wale walioungana na Misri wataanguka

na kiburi cha nguvu zake kitashindwa.

Kutoka Migdoli hadi Aswani,

watauawa ndani yake kwa upanga,

asema Bwana Mwenyezi.

7 “ ‘Hizo nchi zitakua ukiwa

miongoni mwa nchi zilizo ukiwa,

nayo miji yao itakuwa magofu

miongoni mwa miji iliyo magofu.

8 Ndipo watakapojua kwamba mimi ndimi Bwana,

nitakapoiwasha Misri moto

na wote wamsaidiao watapondwa.

9 “ ‘Siku hiyo wajumbe watatoka kwangu kwa merikebu, ili kuwatia hofu Ethiopia, wakiwa katika hali yao ya kuridhika. Maumivu makali yatawapata siku ya maangamizi ya Misri, kwa kuwa hakika itakuja.

10 “ ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo:

“ ‘Nitakomesha makundi ya wajeuri ya Misri

kwa mkono wa Nebukadneza mfalme wa Babeli.

11 Yeye na jeshi lake, taifa lililo katili kuliko mataifa yote,

litaletwa ili kuangamiza nchi.

Watafuta panga zao dhidi ya Misri

na kuijaza nchi kwa waliouawa.

12 Nitakausha vijito vya Naili

na nitaiuza nchi kwa watu waovu,

kwa mkono wa wageni,

nitaifanya nchi ukiwa na kila kitu

kilichomo ndani yake.

Mimi Bwana nimenena haya.

13 “ ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo:

“ ‘Nitaangamiza sanamu

na kukomesha vinyago katika Memfisi

Hapatakuwepo tena na mkuu katika nchi ya Misri,

nami nitaeneza hofu katika nchi nzima.

14 Nitaifanya Pathrosi kuwa ukiwa

na kuitia moto Soani,

nami nitaipiga kwa adhabu Thebesi

15 Nitaimwaga ghadhabu yangu juu ya Pelusiumu,

ngome ya Misri,

nami nitakatilia mbali

makundi ya wajeuri wa Thebesi.

16 Nitaitia moto nchi ya Misri;

Pelusiumu itagaagaa kwa maumivu makuu.

Thebesi itachukuliwa na tufani,

Memfisi itakuwa katika taabu daima.

17 Wanaume vijana wa Oni na wa Pi-Besethi

wataanguka kwa upanga

nayo hiyo miji itatekwa.

18 Huko Tahpanhesi mchana utatiwa giza

nitakapovunja kongwa la Misri;

hapo kiburi cha nguvu zake kitakoma.

Atafunikwa na mawingu

na vijiji vyake vitatekwa.

19 Kwa hiyo nitaipiga Misri kwa adhabu,

nao watajua kuwa Mimi ndimi Bwana.’ ”