Daudi Anakimbilia Pango la Adulamu
1060 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Daudi akaondoka Gathi na kukimbilia kwenye pango la Adulamu. Ndugu zake na watu wa nyumba ya baba yake waliposikia habari hiyo, wakamwendea huko.
Utenzi wa Daudi. Alipokuwa pangoni. Maombi.
1 Namlilia Bwana kwa sauti,
nainua sauti yangu kwa Bwana anihurumie.
2 Namimina malalamiko yangu mbele zake,
mbele zake naeleza shida zangu.
3 Wakati roho yangu inapozimia ndani yangu,
wewe ndiwe unajua njia zangu.
Katika njia ninayopita
watu wameniwekea mtego.
4 Tazama kuume kwangu na uone,
hakuna hata mmoja anayejihusisha nami.
Sina kimbilio,
hakuna anayejali maisha yangu.
5 Ee Bwana, nakulilia wewe,
nasema, “Wewe ni kimbilio langu,
fungu langu katika nchi ya walio hai.”
6 Sikiliza kilio changu,
kwa sababu mimi ni mhitaji sana;
niokoe na wale wanaonifuatilia,
kwa kuwa wamenizidi nguvu.
7 Nifungue kutoka kifungo changu,
ili niweze kulisifu jina lako.
Ndipo wenye haki watanizunguka,
kwa sababu ya wema wako kwangu.
2 Wale wote waliokuwa katika dhiki au waliokuwa na madeni au wale ambao hawakuridhika wakamkusanyikia Daudi, naye akawa kiongozi wao. Watu wapatao 400 walikuwa pamoja naye.
8 Baadhi ya Wagadi wakajitenga na kujiunga na Daudi katika ngome yake huko jangwani. Walikuwa mashujaa hodari, waliokuwa tayari kwa vita na wenye uwezo wa kutumia ngao na mkuki. Nyuso zao zilikuwa nyuso za simba na walikuwa na wepesi kama paa milimani.
9 Ezeri alikuwa mkuu wao,
Obadia alikuwa wa pili katika uongozi, Eliabu wa tatu,
10 Mishmana wa nne, Yeremia wa tano,
11 Atai wa sita, Elieli wa saba,
12 Yohanani wa nane, Elzabadi wa tisa,
13 Yeremia wa kumi, na Makbanai wa kumi na moja.
14 Hawa Wagadi walikuwa majemadari. Aliyekuwa wa mwisho kuliko wote aliweza kuongoza askari 100, na aliyekuwa na uweza zaidi ya wote aliongoza 1,000. 15 Wao ndio walivuka Mto Yordani katika mwezi wa kwanza ukiwa umefurika hadi kwenye kingo zake zote na kusababisha watu wote waliokuwa wanaishi kwenye mabonde kukimbilia mashariki na wengine magharibi.
16 Wabenyamini wengine na baadhi ya watu kutoka Yuda pia walikuja kwa Daudi katika ngome yake. 17 Daudi akatoka nje kuwalaki na akawaambia, “Kama mmekuja kwangu kwa amani, kunisaidia, mimi niko tayari kuwaruhusu ninyi kuungana nami. Lakini kama mmekuja ili kunisaliti kwa adui zangu wakati mimi mikono yangu haina hatia, basi Mungu wa baba zetu aone na awahukumu.”
18 Kisha Roho akaja juu ya Amasai, mkuu wa wale Thelathini, naye akasema:
“Sisi tu watu wako, ee Daudi!
Nasi tuko pamoja na wewe, ee mwana wa Yese!
Ushindi, naam, ushindi uwe kwako,
pia ushindi kwa wale walio upande wako,
kwa kuwa Mungu wako atakusaidia.”
Kwa hiyo Daudi akawapokea na kuwafanya viongozi wa vikosi vyake vya uvamizi.
13 Wakati wa mavuno, viongozi watatu kati ya viongozi thelathini walishuka, wakamwendea Daudi katika pango la Adulamu, wakati kikundi cha Wafilisti kilikuwa kimepiga kambi katika Bonde la Warefai. 14 Wakati huo Daudi alikuwa katika ngome, na kambi ya Wafilisti ilikuwa huko Bethlehemu. 15 Daudi akatamani maji, akasema, “Laiti mtu angenipatia maji ya kunywa kutoka kisima kilicho karibu na lango la Bethlehemu!” 16 Basi mashujaa hao watatu wakapenya katikati ya Wafilisti, wakaenda kuchota maji kutoka kwa kisima kilicho karibu na lango la Bethlehemu, wakamletea Daudi. Lakini Daudi akakataa kuyanywa. Badala yake, aliyamimina mbele za Bwana. 17 Akasema, “Iwe mbali nami, Ee Bwana, kufanya kitu hiki. Je, hii si damu ya watu ambao walikwenda kwa kuhatarisha maisha yao?” Naye Daudi hakuyanywa.
Haya yalifanywa na hao mashujaa watatu.
15 Wakuu watatu miongoni mwa wale thelathini, walimwendea Daudi katika mwamba huko kwenye pango la Adulamu, wakati kikundi cha Wafilisti kilikuwa kimepiga kambi katika Bonde la Warefai. 16 Wakati huo Daudi alikuwa katika ngome, na kambi ya Wafilisti ilikuwa huko Bethlehemu. 17 Daudi akatamani maji, akasema, “Laiti mtu angenipatia maji ya kunywa kutoka kisima kilichoko karibu na lango la Bethlehemu!” 18 Kwa hivyo wale watatu, wakapita katikati ya safu za Wafilisti, wakachota maji kutoka kwa kisima kilicho karibu na lango la Bethlehemu, wakamletea Daudi. Lakini yeye akakataa kuyanywa. Badala yake, aliyamimina mbele za Bwana. 19 Akasema, “Mungu apishie mbali kwamba nifanye hivi! Je kweli, niinywe damu ya watu hawa waliohatarisha maisha yao?” Kwa sababu walihatarisha maisha yao kuyaleta yale maji, Daudi hakukubali kuyanywa.
Huo ndio uliokuwa ujasiri wa wale mashujaa watatu.