Daudi Anakimbilia kwa Ahimeleki huko Nobu
1060 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Daudi akaenda Nobu, kwa Ahimeleki kuhani. Ahimeleki akatetemeka alipokutana naye, akamuuliza, “Kwa nini uko peke yako? Kwa nini hukufuatana na mtu yeyote?”
2 Daudi akamjibu Ahimeleki kuhani, akisema, “Mfalme ameniagiza shughuli fulani na kuniambia, ‘Mtu yeyote asijue chochote kuhusu kazi yako wala maagizo yako!’ Kuhusu watu wangu, nimewaambia tukutane mahali fulani. 3 Sasa basi, una nini mkononi? Nipatie mikate mitano au chochote unachoweza kupata.”
4 Lakini kuhani akamjibu Daudi, “Sina mkate wowote wa kawaida kwa sasa. Hata hivyo, ipo hapa mikate iliyowekwa wakfu, iwapo watu wamejitenga na wanawake.”
5 Daudi akajibu, “Hakika tumejitenga na wanawake kwa siku hizi chache kama kawaida ya ninapotoka kwenda kwenye shughuli. Navyo vyombo vya wale vijana huwa ni vitakatifu hata kwenye safari ya kawaida, si zaidi sana leo vyombo vyao vitakuwa ni vitakatifu?” 6 Hivyo kuhani akampa ile mikate iliyowekwa wakfu, kwa kuwa hapakuwepo mikate mingine isipokuwa hiyo ya Wonyesho iliyokuwa imeondolewa hapo mbele za Bwana na kubadilishwa na mingine yenye moto siku ile ilipoondolewa.
7 Basi siku hiyo palikuwepo na mmoja wa watumishi wa Sauli, aliyezuiliwa mbele za Bwana; alikuwa Doegi Mwedomu, kiongozi wa wachunga wanyama wa Sauli.
8 Daudi akamuuliza Ahimeleki, “Je, unao mkuki au upanga hapa? Sikuleta upanga wala silaha nyingine yoyote, kwa sababu shughuli ya mfalme ilikuwa ya haraka.”
9 Kuhani akajibu, “Upanga wa Goliathi Mfilisti, ambaye ulimuua katika Bonde la Ela, upo hapa, umefungiwa katika kitambaa nyuma ya kisibau. Kama unauhitaji, uchukue, hakuna upanga mwingine hapa ila huo tu.”
Daudi akasema, “Hakuna upanga mwingine kama huo. Nipatie huo.”
Daudi Anakimbilia kwa Akishi, Mfalme wa Gathi
10 Siku ile Daudi akamkimbia Sauli na kwenda kwa Akishi mfalme wa Gathi. 11 Lakini watumishi wa Akishi wakamwambia, “Je, huyu si ndiye Daudi mfalme wa nchi? Je, huyu si ndiye yule ambaye wanaimba katika ngoma zao wakisema:
“ ‘Sauli amewaua elfu zake,
naye Daudi makumi elfu yake’?”
12 Daudi akayaweka maneno haya moyoni naye akamwogopa sana Akishi mfalme wa Gathi. 13 Basi akajifanya mwendawazimu mbele yao; naye alipokuwa mikononi mwao, alitenda kama kichaa, akikwaruza kwa kutia alama juu ya milango ya lango na kuachia udelele kutiririka kwenye ndevu zake.
14 Akishi akawaambia watumishi wake, “Tazameni mtu huyu! Ana wazimu! Kwa nini mnamleta kwangu? 15 Je, mimi nimepungukiwa na wenda wazimu kiasi kwamba mmeniletea mtu huyo hapa aendelee kufanya hivi mbele yangu? Je, ilikuwa ni lazima mtu huyo aje nyumbani kwangu?”
Kwa mwimbishaji. Mtindo wa “Njiwa mkimya wa mbali.” Utenzi wa Daudi. Baada ya kukamatwa na Wafilisti huko Gathi.
1 Ee Mungu unihurumie, maana watu wananifuatia vikali;
mchana kutwa wanazidisha mashambulizi yao.
2 Wasingiziaji wangu wananifuatia mchana kutwa,
wengi wananishambulia kwa kiburi chao.
3 Wakati ninapoogopa,
nitakutumaini wewe.
4 Katika Mungu, ambaye neno lake ninalisifu,
katika Mungu ninatumaini; sitaogopa.
Mwanadamu apatikanaye na kufa,
atanitenda nini?
5 Mchana kutwa wanayageuza maneno yangu,
siku zote wanapanga shauri la kunidhuru.
6 Wananifanyia hila, wanajificha,
wanatazama hatua zangu,
wakiwa na shauku ya kuutoa uhai wangu.
7 Wasiepuke kwa vyovyote,
Ee Mungu, katika hasira yako yaangushe mataifa.
8 Andika maombolezo yangu,
orodhesha machozi yangu katika gombo lako:
je, haya hayapo katika kumbukumbu zako?
9 Ndipo adui zangu watarudi nyuma
ninapoita msaada.
Kwa hili nitajua kwamba Mungu
yuko upande wangu.
10 Katika Mungu, ambaye neno lake ninalisifu,
katika Bwana, ambaye neno lake ninalisifu,
11 katika Mungu ninatumaini, sitaogopa.
Mwanadamu anaweza kunitenda nini?
12 Ee Mungu, nina nadhiri kwako,
nitakutolea wewe sadaka zangu za shukrani.
13 Kwa kuwa umeniokoa toka kwenye mauti
na miguu yangu kwenye kujikwaa,
ili niweze kuenenda mbele za Mungu
katika nuru ya uzima.
Zaburi ya Daudi, alipojifanya mwendawazimu mbele ya Abimeleki, ambaye alimfukuza, naye akaondoka.
1 Nitamtukuza Bwana nyakati zote,
sifa zake zitakuwa midomoni mwangu siku zote.
2 Nafsi yangu itajisifu katika Bwana,
walioonewa watasikia na wafurahi.
3 Mtukuzeni Bwana pamoja nami,
naam, na tulitukuze jina lake pamoja.
4 Nilimtafuta Bwana naye akanijibu,
akaniokoa kwenye hofu zangu zote.
5 Wale wamtazamao hutiwa nuru,
nyuso zao hazifunikwi na aibu kamwe.
6 Maskini huyu alimwita Bwana, naye akamsikia,
akamwokoa katika taabu zake zote.
7 Malaika wa Bwana hufanya kituo
akiwazunguka wale wamchao,
naye huwaokoa.
8 Onjeni mwone kwamba Bwana ni mwema,
heri mtu yule anayemkimbilia.
9 Mcheni Bwana enyi watakatifu wake,
kwa maana wale wamchao
hawapungukiwi na chochote.
10 Wana simba wenye nguvu
hutindikiwa na kuona njaa,
bali wale wamtafutao Bwana
hawatakosa kitu chochote kilicho chema.
11 Njooni, watoto wangu, mnisikilize,
nitawafundisha kumcha Bwana.
12 Yeyote kati yenu anayependa uzima
na kutamani kuziona siku nyingi njema,
13 basi auzuie ulimi wake na mabaya,
na midomo yake kutokana na kusema uongo.
14 Aache uovu, atende mema,
aitafute amani na kuifuatilia.
15 Macho ya Bwana huwaelekea wenye haki,
na masikio yake yako makini kusikiliza kilio chao.
16 Uso wa Bwana uko kinyume na watendao maovu,
ili kufuta kumbukumbu lao duniani.
17 Wenye haki hulia, naye Bwana huwasikia,
huwaokoa katika taabu zao zote.
18 Bwana yu karibu na waliovunjika moyo,
na huwaokoa waliopondeka roho.
19 Mwenye haki ana mateso mengi,
lakini Bwana humwokoa nayo yote,
20 huhifadhi mifupa yake yote,
hata mmoja hautavunjika.
21 Ubaya utamuua mtu mwovu,
nao adui za mwenye haki watahukumiwa.
22 Bwana huwakomboa watumishi wake,
yeyote anayemkimbilia yeye
hatahukumiwa kamwe.