Daudi Anawahesabu Watu
1017 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Hasira ya Bwana ikawaka tena dhidi ya Israeli, naye akamchochea Daudi dhidi yao, akisema, “Nenda ukawahesabu Israeli na Yuda.”
2 Kwa hiyo mfalme akamwambia Yoabu, pamoja na majemadari wa jeshi aliokuwa nao, “Nendeni kwa makabila yote ya Israeli kuanzia Dani hadi Beer-Sheba na mwandikishe watu wapiganaji, ili niweze kujua idadi yao.”
3 Lakini Yoabu akamjibu mfalme, “Bwana Mungu wako na azidishe jeshi mara mia, nayo macho ya bwana wangu mfalme na yaone hili. Lakini kwa nini bwana wangu mfalme anataka kufanya kitu cha namna hii?”
4 Hata hivyo, neno la mfalme likawa na nguvu juu ya Yoabu pamoja na majemadari wa jeshi, kwa hiyo wakaondoka mbele ya mfalme kuandikisha wapiganaji wa Israeli.
5 Baada ya kuvuka Yordani, walipiga kambi karibu na Aroeri, kusini ya mji ulioko kwenye bonde jembamba, ndipo wakipitia Gadi, wakaenda hadi Yazeri. 6 Walikwenda hadi Gileadi na pia eneo la Tahtimu-Hodshi, wakaendelea hadi Dani-Yaani na kuzunguka kuelekea Sidoni. 7 Kisha wakaenda kuelekea ngome ya Tiro pamoja na miji yote ya Wahivi na ya Wakanaani. Mwishoni, walikwenda mpaka Beer-Sheba katika Negebu ya Yuda.
8 Baada ya kupita katika nchi nzima, walirudi Yerusalemu baada ya miezi tisa na siku ishirini.
9 Yoabu akatoa hesabu ya wapiganaji kwa mfalme: Katika Israeli kulikuwako watu 800,000 wenye uwezo wa kupigana, na katika Yuda watu 500,000.
6 Lakini Yoabu hakuwahesabu Walawi na Wabenyamini, kwa sababu alichukizwa sana na amri ya mfalme. 7 Amri hii ilikuwa mbaya machoni pa Mungu pia; hivyo akaiadhibu Israeli.
23 Daudi hakuwahesabu watu waliokuwa chini ya miaka ishirini, kwa sababu Bwana alikuwa ameahidi kuwafanya Israeli kuwa wengi kama nyota za angani. 24 Yoabu mwana wa Seruya alianza kuwahesabu watu lakini hakumaliza. Kwa sababu ya kuwahesabu watu, hasira ya Mungu iliwaka juu ya Israeli, nayo hiyo hesabu yao haikuingizwa katika kitabu cha kumbukumbu za Mfalme Daudi.
10 Dhamiri ya Daudi ilishtuka baada ya kuwahesabu wapiganaji, naye akamwambia Bwana, “Nimefanya dhambi kubwa kwa kufanya jambo hili. Ee Bwana, sasa ninakusihi, ondoa hatia ya mtumishi wako. Nimefanya jambo la kipumbavu sana.”
11 Kabla Daudi hajaamka kesho yake asubuhi, neno la Bwana lilikuwa limemjia Gadi nabii, aliyekuwa mwonaji wa Daudi, kusema: 12 “Nenda ukamwambie Daudi, ‘Hivi ndivyo asemavyo Bwana: Ninakupa wewe uchaguzi wa mambo matatu. Nichagulie mojawapo nitakalotenda dhidi yako.’ ”
13 Basi Gadi akaenda kwa Daudi na kumwambia, “Je, ije njaa ya miaka mitatu katika nchi yako? Au miezi mitatu ya kukimbia adui zako wakikufuatia? Au siku tatu za tauni katika nchi yako? Basi sasa, fikiri juu ya hilo na uamue jinsi nitakavyomjibu huyo aliyenituma.”
14 Daudi akamjibu Gadi, “Nitataabika sana. Afadhali tuangukie mikononi mwa Bwana, kwa maana rehema zake ni kuu, lakini usiniache nianguke mikononi mwa wanadamu.”
15 Basi Bwana akatuma tauni katika Israeli kuanzia asubuhi mpaka mwisho wa muda ulioamriwa, wakafa watu 70,000 kuanzia Dani hadi Beer-Sheba.
15 Mungu akapeleka malaika kuangamiza Yerusalemu. Lakini malaika alipokuwa akifanya hivyo, Bwana akaona na akahuzunika kwa sababu ya maafa, akamwambia yule malaika aliyekuwa anaangamiza watu, “Yatosha! Rudisha mkono wako.” Wakati huo malaika wa Bwana alikuwa amesimama katika sakafu ya kupuria nafaka ya Arauna Myebusi.
16 Daudi akayainua macho yake akamwona huyo malaika wa Bwana akiwa amesimama katikati ya mbingu na dunia, naye ameunyoosha upanga wake juu ya Yerusalemu tayari kuangamiza. Kisha Daudi na wazee, waliokuwa wamevaa nguo za gunia, wakaanguka kifudifudi.
17 Ikawa Daudi alipomwona huyo malaika aliyekuwa akiwaua watu, akamwambia Bwana, “Mimi ndiye niliyetenda dhambi na kukosa. Hawa ni kondoo tu. Wamefanya nini? Mkono wako uwe juu yangu na nyumba yangu.”
17 Daudi akamwambia Mungu, “Je, si mimi ndiye niliyeamuru watu wahesabiwe? Mimi ndiye niliyetenda dhambi na kukosa. Hawa ni kondoo tu. Wamefanya nini? Ee Bwana, Mungu wangu, mkono wako na uwe juu yangu mimi na jamaa yangu, lakini usiache tauni hii iendelee juu ya watu wako.”
18 Kisha malaika wa Bwana akamwamuru Gadi amwambie Daudi apande na kumjengea Bwana madhabahu kwenye sakafu ya kupuria nafaka ya Arauna Myebusi. 19 Kwa hiyo Daudi akakwea, akalitii lile neno ambalo Gadi alikuwa amelisema katika jina la Bwana.
20 Arauna alipokuwa akipura ngano, akageuka akamwona yule malaika. Wanawe wanne waliokuwa pamoja naye wakajificha, yeye akaendelea kupura ngano. 21 Kisha Daudi akakaribia, Arauna alipotazama na kumwona, akaondoka kwenye uwanja wa kupuria nafaka akamsujudia Daudi akiuinamisha uso wake ardhini.
22 Daudi akamwambia, “Nipatie huu uwanja wako wa kupuria nafaka ili niweze kujenga madhabahu ya Bwana tauni ipate kukomeshwa katika watu. Niuzie kwa bei yake kamili.”
23 Arauna akamwambia Daudi, “Uchukue huo uwanja. Mfalme bwana wangu na afanye lolote analopenda. Tazama, nitatoa maksai kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa, vifaa vya kupuria kuwa kuni, pamoja na ngano kwa ajili ya dhabihu ya nafaka. Natoa hivi vyote.”
24 Lakini Mfalme Daudi akamjibu Arauna, “La hasha! Lakini ninasisitiza kwamba nitalipa bei yake kamili. Sitachukua kilicho chako kwa ajili ya Bwana au kutoa sadaka ya kuteketezwa ambayo hainigharimu chochote.”
25 Basi Daudi akamlipa Arauna shekeli za dhahabu 600 kwa ajili ya ule uwanja. 26 Kisha Daudi akamjengea Bwana madhabahu mahali hapo, na kutoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani. Akamwita Bwana naye Bwana akajibu maombi yake kwa moto toka mbinguni juu ya madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa.
27 Kisha Bwana akanena na yule malaika, naye akarudisha upanga wake katika ala yake. 28 Wakati huo, Daudi alipoona kwamba Bwana amemjibu kule kwenye uwanja wa kupuria nafaka wa Arauna Myebusi, akatoa dhabihu huko. 29 Maskani ya Bwana ambayo Mose aliitengeneza kule jangwani, pamoja na madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa kwa wakati huo vilikuwa viko mahali pa juu pa kuabudia huko Gibeoni. 30 Lakini Daudi hakuthubutu kuisogelea ili kumuuliza Mungu, kwa sababu aliuogopa upanga wa yule malaika wa Bwana.
Utenzi wa kuweka wakfu hekalu. Zaburi ya Daudi.
1 Nitakutukuza wewe, Ee Bwana,
kwa kuwa umeniinua kutoka vilindi,
na hukuacha adui zangu
washangilie juu yangu.
2 Ee Bwana, Mungu wangu, nilikuita unisaidie
na wewe umeniponya.
3 Ee Bwana, umenitoa Kuzimu,
umeniokoa nisishuke kwenye shimo la mauti.
4 Mwimbieni Bwana, enyi watakatifu wake;
lisifuni jina lake takatifu.
5 Kwa maana hasira yake ni ya muda mfupi,
bali upendo wake hudumu siku zote.
Inawezekana kilio kiwepo usiku kucha,
lakini asubuhi kukawa na furaha.
6 Nilipofanikiwa nilisema,
“Sitatikiswa kamwe.”
7 Ee Bwana, uliponijalia,
uliuimarisha mlima wangu,
lakini ulipouficha uso wako
nilifadhaika.
8 Kwako wewe, Ee Bwana, niliita,
kwa Bwana niliomba rehema:
9 “Kuna faida gani katika kuangamia kwangu?
Katika kushuka kwangu shimoni?
Je, mavumbi yatakusifu?
Je, yatatangaza uaminifu wako?
10 Ee Bwana, unisikie na kunihurumia,
Ee Bwana, uwe msaada wangu.”
11 Uligeuza maombolezo yangu kuwa kucheza,
ulinivua nguo za gunia ukanivika shangwe,
12 ili moyo wangu uweze kukusifu na usikae kimya.
Ee Bwana Mungu wangu, nitakushukuru milele.