Daudi Anawahesabu Watu (continued)
1017 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
1 Shetani akainuka dhidi ya Israeli na kumshawishi Daudi ahesabu watu wa Israeli. 2 Kwa hiyo Daudi akamwambia Yoabu na majemadari wa jeshi, “Nendeni mkawahesabu Waisraeli kuanzia Beer-Sheba mpaka Dani. Kisha nileteeni taarifa ili kwamba niweze kufahamu wako wangapi.”
3 Yoabu akajibu, “Bwana na aongeze jeshi lake mara mia na zaidi. Mfalme bwana wangu, kwani hawa wote si raiya wa bwana wangu? Kwa nini bwana wangu unataka kufanya hivi? Kwa nini kuleta hatia juu ya Israeli?”
4 Hata hivyo, neno la mfalme likawa na nguvu juu ya Yoabu; kwa hiyo Yoabu akaondoka na kuzunguka Israeli yote kisha akarudi Yerusalemu. 5 Yoabu akampa Daudi jumla ya idadi ya watu wanaoweza kupigana. Katika Israeli kulikuwa na watu 1,100,000 ambao wangeweza kutumia upanga na katika Yuda watu 470,000.
8 Kisha Daudi akamwambia Mungu, “Nimetenda dhambi kubwa kwa kufanya jambo hili. Sasa, ninakusihi, ondoa hatia ya mtumishi wako. Nimefanya jambo la kipumbavu sana.”
9 Bwana akamwambia Gadi, mwonaji wa Daudi, 10 “Nenda ukamwambie Daudi, hivi ndivyo asemavyo Bwana: ‘Ninakupa wewe uchaguzi wa mambo matatu. Nichagulie mojawapo nitakalotenda dhidi yako.’ ”
11 Kwa hiyo Gadi akamwendea Daudi akamwambia, “Hili ndilo Bwana asemalo: ‘Chagua: 12 miaka mitatu ya njaa, au miezi mitatu ya kushindwa na adui zako, ukipatwa na upanga wao, au siku tatu za upanga wa Bwana, yaani, siku tatu za tauni katika nchi na malaika wa Bwana akiangamiza kila mahali katika Israeli.’ Sasa basi, amua jinsi nitakavyomjibu yeye aliyenituma.”
13 Daudi akamwambia Gadi, “Ninayo mahangaiko makubwa. Mimi na nianguke mikononi mwa Bwana kwa maana rehema zake ni kuu mno, lakini usiniache niangukie mikononi mwa wanadamu.”
14 Basi Bwana akatuma tauni katika Israeli, watu 70,000 wa Israeli wakafa.
16 Malaika aliponyoosha mkono wake ili kuangamiza Yerusalemu, Bwana akahuzunika kwa sababu ya maafa, akamwambia yule malaika aliyekuwa anawadhuru watu, “Yatosha! Rudisha mkono wako.” Wakati huo malaika wa Bwana alikuwa kwenye sakafu ya kupuria ya Arauna, Myebusi.
18 Siku hiyo Gadi akamwendea Daudi na kumwambia, “Panda ukamjengee Bwana madhabahu kwenye sakafu ya kupuria ya Arauna Myebusi.” 19 Kwa hiyo Daudi akakwea kama vile Bwana alivyokuwa ameamuru kwa kinywa cha Gadi. 20 Arauna alipotazama na kumwona mfalme na watu wake wakija kumwelekea, alitoka nje na kusujudu mbele ya mfalme kifudifudi, akiuinamisha uso wake ardhini.
21 Arauna akasema, “Mbona bwana wangu mfalme amekuja kwa mtumishi wake?”
Daudi akajibu, “Kununua sakafu yako ya kupuria, ili niweze kumjengea Bwana madhabahu, ili tauni iliyo katika watu iondolewe.”
22 Arauna akamwambia Daudi, “Bwana wangu mfalme na achukue chochote kinachompendeza na akitoe sadaka. Hapa kuna maksai kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, pia kuna miti ya kupuria na nira za ngʼombe kwa ajili ya kuni. 23 Ee mfalme, Arauna anatoa vyote hivi kwa mfalme.” Pia Arauna akamwambia mfalme, “Bwana Mungu wako na akukubali.”
24 Lakini mfalme akamjibu Arauna, “La hasha, nasisitiza kuvilipia. Sitatoa sadaka ya kuteketezwa kwa Bwana Mungu wangu isiyonigharimu chochote.”
Kwa hiyo Daudi akanunua ile sakafu ya kupuria nafaka na maksai, akazilipia shekeli hamsini za fedha. 25 Kisha Daudi akamjengea Bwana madhabahu mahali hapo, na kutoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani. Kisha Bwana akajibu kwa ajili ya nchi, nayo tauni ikakoma katika Israeli.
Miezi Sita ya Mwisho ya Utawala wa Daudi 1015 KK
Daudi Anajiandaa Kujenga Hekalu
1 Ndipo Daudi akasema, “Nyumba ya Bwana Mungu itakuwa mahali hapa, pia pamoja na madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa kwa ajili ya Israeli.”
2 Kwa hiyo Daudi akatoa amri wakusanyike wageni wote waliokuwa wanaishi Israeli, na kutoka miongoni mwao akaweka waashi ili kuchonga mawe kwa ajili ya kujenga nyumba ya Mungu. 3 Daudi akatoa chuma tele ili kutengenezea misumari kwa ajili ya mafungo ya malango ya nyumba na shaba tele isiyopimika. 4 Pia akatoa magogo ya mierezi yasiyohesabika, kwa kuwa Wasidoni na Watiro walikuwa wamemletea Daudi idadi kubwa ya mierezi.
5 Daudi akasema, “Mwanangu Solomoni bado ni mdogo wa umri na hana uzoefu. Nyumba itakayojengwa kwa ajili ya Bwana inatakiwa iwe yenye uzuri mwingi na sifa na fahari mbele ya mataifa yote. Kwa hiyo nitaifanyia matayarisho.” Daudi akafanya matayarisho makubwa kabla ya kifo chake.
6 Kisha akamwita Solomoni mwanawe akamwagiza kujenga nyumba kwa ajili ya Bwana, Mungu wa Israeli. 7 Daudi akamwambia Solomoni: “Mwanangu, nilikuwa na jambo hili ndani ya moyo wangu kujenga nyumba kwa ajili ya Jina la Bwana Mungu wangu. 8 Lakini neno hili la Bwana likanijia, kusema: ‘Wewe umemwaga damu nyingi na kupigana vita vingi. Wewe hutajenga nyumba kwa ajili ya Jina langu, kwa sababu umemwaga damu nyingi juu ya nchi machoni pangu. 9 Lakini utakuwa na mwana ambaye atakuwa mtu wa amani na utulivu nami nitampa utulivu mbele ya adui zake wote pande zote. Jina lake ataitwa Solomoni, nami nitawapa Israeli amani na utulivu wakati wa utawala wake. 10 Yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa ajili ya Jina langu. Yeye atakuwa mwanangu, nami nitakuwa baba yake. Nami nitakifanya imara kiti chake cha enzi cha utawala wake katika Israeli milele.’
11 “Sasa, mwanangu, Bwana awe pamoja nawe, nawe uwe na mafanikio upate kuijenga nyumba ya Bwana Mungu wako, kama alivyosema utafanya. 12 Bwana na akupe hekima na ufahamu wakati atakuweka juu ya Israeli, ili uweze kuishika sheria ya Bwana Mungu wako. 13 Ndipo utakapofanikiwa, ikiwa utakuwa na bidii kutii amri na sheria Bwana alizompa Mose kwa ajili ya Israeli. Uwe hodari na ushujaa. Usiogope wala usikate tamaa.
14 “Nimejitaabisha sana ili kupata mahitaji kwa ajili ya Hekalu la Bwana: talanta 100,000 za dhahabu, talanta 1,000,000 za fedha na kiasi kisichopimika cha shaba na chuma, pia mbao na mawe. Nawe waweza kuviongeza. 15 Unao wafanyakazi wengi: Wachonga mawe, waashi na maseremala, pamoja na watu walio na ustadi katika kila kazi 16 wa kufua dhahabu, fedha, shaba na chuma, mafundi wasiohesabika. Sasa basi anza kazi hii, naye Bwana awe pamoja nawe.”
17 Kisha Daudi akawaamuru viongozi wote wa Israeli wamsaidie Solomoni mwanawe. 18 Akawaambia, “Je, Bwana Mungu wenu si yuko pamoja na ninyi? Pia si amewapa raha pande zote? Kwa maana amewatia wenyeji wa nchi mkononi mwangu, nayo nchi iko chini ya Bwana na watu wake. 19 Sasa itoeni mioyo yenu na nafsi zenu katika kumtafuta Bwana Mungu wenu. Anzeni kujenga Maskani ya Bwana Mungu, ili mweze kulileta Sanduku la Agano la Bwana na vyombo vitakatifu vya Mungu katika Hekalu litakalojengwa kwa ajili ya Jina la Bwana.”