Sehemu ya 10: Utawala wa Uzia

Ufalme wa Yuda

Utawala wa Awali wa Uzia na Ustawi Wake

810 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

2 Nyakati 26:1–4

1 Kisha watu wote wa Yuda wakamtwaa Uzia, aliyekuwa na umri wa miaka kumi na sita, nao wakamfanya mfalme mahali pa Amazia baba yake. 2 Ndiye alijenga upya Elathi kuirudisha kwa Yuda baada ya Amazia kulala pamoja na baba zake.

3 Uzia alikuwa na umri wa miaka kumi na sita alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka hamsini na miwili. Mama yake aliitwa Yekolia wa Yerusalemu. 4 Akatenda yaliyo mema machoni pa Bwana, kama Amazia baba yake alivyofanya.

2 Wafalme 15:1

1 Katika mwaka wa ishirini na saba wa utawala wa Yeroboamu mfalme wa Israeli, Azaria mwana wa Amazia mfalme wa Yuda alianza kutawala.

2 Nyakati 26:5–15

5 Akamtafuta Mungu katika siku za Zekaria, aliyemwelekeza kumcha Mungu. Wakati wote alipomtafuta Bwana, Mungu alimfanikisha.

6 Alipigana vita dhidi ya Wafilisti na kubomoa kuta za Gathi, Yabne na Ashdodi. Kisha akajenga upya miji karibu na Ashdodi na mahali pengine katikati ya Wafilisti. 7 Mungu akamsaidia dhidi ya Wafilisti na dhidi ya Waarabu walioishi Gur-Baali na dhidi ya Wameuni. 8 Waamoni wakamletea Uzia ushuru, umaarufu wake ukaenea hadi kwenye mpaka wa Misri, kwa sababu alikuwa amekuwa na nguvu sana.

9 Uzia akajenga minara huko Yerusalemu katika Lango la Pembeni, katika Lango la Bondeni na katika pembe, mahali kuta zikutanapo, kisha akaijengea ngome. 10 Akajenga pia minara jangwani na kuchimba visima vingi vya maji, kwa sababu alikuwa na mifugo mingi chini ya vilimani na kwenye nchi tambarare. Alikuwa na watu wanaofanya kazi katika mashamba yake na kwenye mashamba yake ya mizabibu huko vilimani na katika ardhi zenye rutuba, kwa kuwa aliupenda udongo.

11 Zaidi ya hayo, Uzia alikuwa na jeshi lililofunzwa vizuri, lililokuwa tayari kwenda vitani kwa vikosi kufuatana na idadi yao kama walivyokusanywa na Yeieli mwandishi na Maaseya msimamizi chini ya maelekezo ya Hanania, mmojawapo wa maafisa wa mfalme. 12 Idadi yote ya viongozi wa jamaa waliowaongoza hawa wapiganaji walikuwa 2,600. 13 Chini ya uongozi wao kulikuwa na jeshi la askari 307,500 watu waliofundishwa kwa ajili ya vita, jeshi lenye nguvu la kumsaidia mfalme dhidi ya adui zake. 14 Uzia akalipatia jeshi lote ngao, mikuki, chapeo, dirii, pinde na mawe ya kombeo. 15 Huko Yerusalemu watu wenye utaalamu mkubwa wakatengeneza mitambo iliyotumika katika minara na kwenye pembe za ulinzi ili kurusha mishale na kuvurumisha mawe makubwa. Sifa zake zikaenea mbali sana kwa sababu alisaidiwa mno mpaka akawa na nguvu sana.

Yoeli Anatabiri Kuangushwa kwa Yuda karibu 787 KK

Uzia anapopanua jeshi lake, Yoeli anatabiri kwamba siku moja jeshi la kigeni litaangusha ufalme wa Yuda.

Yoeli 1

1 Neno la Bwana ambalo lilimjia Yoeli mwana wa Pethueli.

2 Sikilizeni hili, enyi wazee;

sikilizeni, ninyi nyote mnaoishi katika nchi.

Je, jambo kama hili lilishawahi kutokea

katika siku zenu au katika siku za babu zenu?

3 Waelezeni watoto wenu,

na watoto wenu wawaambie watoto wao,

na watoto wao kwa kizazi kitakachofuata.

4 Kilichosazwa na kundi la tunutu

nzige wakubwa wamekula,

kilichosazwa na nzige wakubwa

parare wamekula,

kilichosazwa na parare

madumadu wamekula.

5 Amkeni, enyi walevi, mlie!

Pigeni yowe enyi wanywaji wote wa mvinyo,

pigeni yowe kwa sababu ya mvinyo mpya,

kwa kuwa mmenyangʼanywa

kutoka midomoni mwenu.

6 Taifa limevamia nchi yangu,

lenye nguvu tena lisilo na idadi;

lina meno ya simba,

magego ya simba jike.

7 Limeharibu mizabibu yangu

na kuangamiza mitini yangu.

Limebambua magome yake

na kuyatupilia mbali,

likayaacha matawi yake yakiwa meupe.

8 Omboleza kama bikira aliyevaa nguo ya gunia

anayehuzunika kwa ajili ya mume wa ujana wake.

9 Sadaka za nafaka na sadaka za kinywaji

zimekatiliwa mbali kutoka nyumba ya Bwana.

Makuhani wanaomboleza,

wale wanaohudumu mbele za Bwana.

10 Mashamba yameharibiwa,

ardhi imekauka;

nafaka imeharibiwa,

mvinyo mpya umekauka,

mafuta yamekoma.

11 Kateni tamaa, enyi wakulima,

lieni, enyi mlimao mizabibu;

huzunikeni kwa ajili ya ngano na shayiri,

kwa sababu mavuno ya shambani yameharibiwa.

12 Mzabibu umekauka

na mtini umenyauka;

mkomamanga, mtende na mtofaa,

miti yote shambani, imekauka.

Hakika furaha yote ya mwanadamu

imeondoka.

13 Vaeni nguo ya gunia, enyi makuhani, muomboleze;

pigeni yowe, enyi mnaohudumu madhabahuni.

Njooni, vaeni nguo ya gunia usiku kucha,

enyi mnaohudumu mbele za Mungu wangu;

kwa kuwa sadaka za nafaka na sadaka za kinywaji

zimezuiliwa kufika katika nyumba ya Mungu wenu.

14 Tangazeni saumu takatifu;

liiteni kusanyiko takatifu.

Iteni wazee

na wote waishio katika nchi

waende katika nyumba ya Bwana Mungu wenu,

wakamlilie Bwana.

15 Ole kwa siku hiyo!

Kwa kuwa siku ya Bwana iko karibu;

itakuja kama uharibifu

kutoka kwa Mwenyezi.

16 Je, chakula hakikukatiliwa mbali

mbele ya macho yetu:

furaha na shangwe

kutoka nyumba ya Mungu wetu?

17 Mbegu zinakauka

chini ya mabonge ya udongo.

Ghala zimeachwa katika uharibifu,

ghala za nafaka zimebomolewa,

kwa maana hakuna nafaka.

18 Jinsi gani ngʼombe wanavyolia!

Makundi ya mifugo yanahangaika

kwa sababu hawana malisho;

hata makundi ya kondoo yanateseka.

19 Kwako, Ee Bwana, naita,

kwa kuwa moto umeteketeza

malisho ya mbugani

na miali ya moto imeunguza

miti yote shambani.

20 Hata wanyama wa porini wanakuonea shauku;

vijito vya maji vimekauka,

na moto umeteketeza

malisho yote ya mbugani.