Msingi wa Hekalu Unawekwa
536 KK
Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)
8 Katika mwezi wa pili wa mwaka wa pili baada ya Waisraeli kufika kwenye nyumba ya Mungu huko Yerusalemu, Zerubabeli mwana wa Shealtieli, Yeshua mwana wa Yosadaki na ndugu zao wengine (makuhani, Walawi na wote waliorejea Yerusalemu kutoka uhamishoni) walianza kazi, wakiteua Walawi wenye umri kuanzia miaka ishirini au zaidi kusimamia ujenzi wa nyumba ya Bwana. 9 Yeshua na wanawe, pamoja na ndugu zake, Kadmieli na wanawe (wazao wa Hodavia), wana wa Henadadi na wana wao na ndugu zao, Walawi wote walijiunga pamoja kusimamia wale waliofanya kazi katika nyumba ya Mungu.
10 Wajenzi walipoweka msingi wa Hekalu la Bwana, makuhani wakiwa wamevalia mavazi yao wakiwa na tarumbeta na Walawi (wana wa Asafu) wakiwa na matoazi, walishika nafasi zao za kumtukuza Bwana, kama ilivyoagizwa na Daudi mfalme wa Israeli. 11 Waliimba nyimbo za sifa na za shukrani kwa Bwana hivi:
“Yeye ni mwema;
upendo wake kwa Israeli
wadumu milele.”
Watu wote wakapaza sauti kubwa za sifa kwa Bwana, kwa sababu msingi wa nyumba ya Bwana ulikuwa umewekwa. 12 Lakini wengi wa makuhani wazee, Walawi na viongozi wa jamaa waliokuwa wameona Hekalu la mwanzoni, walilia kwa sauti walipoona msingi wa Hekalu hili ukiwekwa, huku wengine wengi wakipiga kelele kwa furaha. 13 Hakuna mtu ambaye angeweza kutofautisha sauti hizo za furaha na za kilio, kwa sababu watu walipiga kelele sana. Nayo hiyo sauti ikasikika mbali.
Kwa mwimbishaji. Mtindo wa gitithi. Zaburi ya wana wa Kora.
1 Ee Bwana Mwenye Nguvu Zote,
makao yako yapendeza kama nini!
2 Nafsi yangu inatamani sana,
naam, hata kuona shauku,
kwa ajili ya nyua za Bwana;
moyo wangu na mwili wangu
vinamlilia Mungu Aliye Hai.
3 Hata shomoro amejipatia makao,
mbayuwayu amejipatia kiota
mahali awezapo kuweka makinda yake:
mahali karibu na madhabahu yako,
Ee Bwana Mwenye Nguvu Zote,
Mfalme wangu na Mungu wangu.
4 Heri wale wanaokaa nyumbani mwako,
wanaokusifu wewe daima.
5 Heri wale ambao nguvu zao ziko kwako,
na njia ziendazo Sayuni zimo mioyoni mwao.
6 Wanapopita katika Bonde la Baka,
hulifanya mahali pa chemchemi,
pia mvua za vuli hulijaza kwa madimbwi.
7 Huendelea toka nguvu hadi nguvu,
hadi kila mmoja afikapo
mbele za Mungu huko Sayuni.
8 Ee Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote, sikia maombi yangu;
nisikilize, Ee Mungu wa Yakobo.
9 Ee Mungu, uitazame ngao yetu,
mtazame kwa wema mpakwa mafuta wako.
10 Siku moja katika nyua zako ni bora
kuliko siku elfu mahali pengine;
afadhali ningekuwa bawabu katika nyumba ya Mungu wangu
kuliko kukaa katika mahema ya waovu.
11 Kwa kuwa Bwana ni jua na ngao,
Bwana hutoa wema na heshima;
hakuna kitu chema anachowanyima
wale ambao hawana hatia.
12 Ee Bwana Mwenye Nguvu Zote,
heri ni mtu yule anayekutumaini wewe.
Kwa mwimbishaji. Wimbo. Zaburi.
1 Mpigieni Mungu kelele za shangwe, dunia yote!
2 Imbeni utukufu wa jina lake;
mpeni sifa zake kwa utukufu!
3 Mwambieni Mungu, “Jinsi gani yalivyo ya kutisha matendo yako!
Uwezo wako ni mkuu mno kiasi kwamba
adui wananyenyekea mbele zako.
4 Dunia yote yakusujudia,
wanakuimbia wewe sifa,
wanaliimbia sifa jina lako.”
5 Njooni mwone yale Mungu aliyoyatenda,
mambo ya kutisha aliyoyatenda
miongoni mwa wanadamu!
6 Alifanya bahari kuwa nchi kavu,
wakapita kati ya maji kwa miguu,
njooni, tumshangilie.
7 Yeye hutawala kwa uwezo wake milele,
macho yake huangalia mataifa yote:
waasi wasithubutu kujiinua dhidi yake.
8 Enyi mataifa, msifuni Mungu wetu,
sauti ya sifa yake isikike,
9 ameyahifadhi maisha yetu
na kuizuia miguu yetu kuteleza.
10 Ee Mungu, wewe ulitujaribu,
ukatusafisha kama fedha.
11 Umetuingiza kwenye nyavu
na umetubebesha mizigo mizito
migongoni mwetu.
12 Uliwaruhusu watu watukalie vichwani,
tulipita kwenye moto na kwenye maji,
lakini ulituleta kwenye nchi
iliyojaa utajiri tele.
13 Nitakuja hekaluni mwako na sadaka za kuteketezwa
na kukutimizia nadhiri zangu:
14 nadhiri ambazo midomo yangu iliahidi
na nilizotamka kwa kinywa changu
nilipokuwa katika shida.
15 Nitakutolea dhabihu za wanyama wanono
na sadaka za kondoo dume,
nitakutolea mafahali na mbuzi.
16 Njooni msikilize ninyi nyote mnaomcha Mungu,
nami niwaambie aliyonitendea.
17 Nilimlilia kwa kinywa changu,
sifa zake zilikuwa katika ulimi wangu.
18 Kama ningekuwa nimeyaficha maovu moyoni mwangu,
Bwana asingekuwa amenisikiliza;
19 lakini hakika Mungu amenisikiliza
na amesikia sauti yangu katika maombi.
20 Sifa apewe Mungu,
ambaye hakulikataa ombi langu
wala kunizuilia upendo wake!