Hekalu la Pili Lawekwa Wakfu

515 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Ezra 6:14–22

14 Hivyo wazee wa Wayahudi waliendelea kujenga na kustawi kutokana na mahubiri ya manabii Hagai na Zekaria, mwana wa Ido. Wakakamilisha ujenzi wa Hekalu kulingana na agizo la Mungu wa Israeli na amri ya Koreshi, Dario na Artashasta wafalme wa Uajemi. 15 Hekalu lilikamilika siku ya kumi na mbili ya mwezi wa Adari, ndio mwezi wa tatu, katika mwaka wa sita wa utawala wa Mfalme Dario.

16 Kisha watu wa Israeli: makuhani, Walawi na wengine wote waliohamishwa, wakaadhimisha kule kuwekwa wakfu nyumba ya Mungu kwa shangwe. 17 Kwa ajili ya kuwekwa wakfu nyumba hii ya Mungu walitoa mafahali mia moja, kondoo dume mia mbili, wana-kondoo mia nne, sadaka kwa ajili ya dhambi ya Israeli yote walitoa mbuzi dume kumi na wawili, mmoja kwa ajili ya kila kabila la Israeli. 18 Wakawaweka makuhani katika nafasi zao na Walawi wakawekwa katika makundi yao ya huduma kwa Mungu huko Yerusalemu, kulingana na ilivyoandikwa katika Kitabu cha Mose.

19 Katika siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza, waliorudi kutoka uhamishoni wakaadhimisha Pasaka. 20 Makuhani na Walawi walikuwa wamekwisha kujitakasa nao wamekuwa safi kwa kufuata kawaida za ibada. Walawi wakachinja kondoo wa Pasaka kwa ajili ya wana wa waliorudi kutoka utumwani uhamishoni, kwa ajili ya ndugu zao makuhani na wao wenyewe. 21 Hivyo Waisraeli waliokuwa wamerudi kutoka utumwani uhamishoni wakaila Pasaka, pamoja na wale waliokuwa wamejitenga na matendo ya unajisi wa Mataifa ya jirani ili kumtafuta Bwana, Mungu wa Israeli. 22 Kwa muda wa siku saba waliiadhimisha Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu kwa furaha, kwa sababu Bwana alikuwa amewajaza furaha kwa kubadilisha nia ya mfalme wa Ashuru kwamba awasaidie ujenzi wa nyumba ya Mungu, Mungu wa Israeli.

Zaburi 48

Wimbo. Zaburi ya wana wa Kora.

1 Bwana ni mkuu, anayestahili kusifiwa sana,

katika mji wa Mungu wetu,

mlima wake mtakatifu.

2 Ni mzuri katika kuinuka kwake juu sana,

furaha ya dunia yote.

Kama vilele vya juu sana vya Safoni ni Mlima Sayuni,

mji wa Mfalme Mkuu.

3 Mungu yuko katika ngome zake;

amejionyesha mwenyewe kuwa ngome yake.

4 Wakati wafalme walipounganisha nguvu,

waliposonga mbele pamoja,

5 walimwona nao wakashangaa,

wakakimbia kwa hofu.

6 Kutetemeka kuliwashika huko,

maumivu kama ya mwanamke

mwenye utungu wa kuzaa.

7 Uliwaangamiza kama meli za Tarshishi

zilizovunjwa na upepo wa mashariki.

8 Kama tulivyokuwa tumesikia,

ndivyo tulivyoona

katika mji wa Bwana Mwenye Nguvu Zote,

katika mji wa Mungu wetu:

Mungu ataufanya uwe salama milele.

9 Ee Mungu, hekaluni mwako

tunatafakari upendo wako usiokoma.

10 Ee Mungu, kama jina lako lilivyo,

sifa zako zinafika hadi miisho ya dunia,

mkono wako wa kuume umejazwa na haki.

11 Mlima Sayuni unashangilia,

vijiji vya Yuda vinafurahi

kwa sababu ya hukumu zako.

12 Tembeeni katika Sayuni,

uzungukeni mji,

hesabuni minara yake;

13 yatafakarini vyema maboma yake,

angalieni ngome zake,

ili mpate kusimulia habari zake

kwa kizazi kijacho.

14 Kwa kuwa huyu Mungu ni Mungu wetu milele na milele;

atakuwa kiongozi wetu hata mwisho.

Zaburi 81

Kwa mwimbishaji. Mtindo wa gitithi. Zaburi ya Asafu.

1 Mwimbieni kwa furaha, Mungu aliye nguvu yetu;

mpigieni kelele za shangwe Mungu wa Yakobo!

2 Anzeni wimbo, pigeni matari,

pigeni kinubi na zeze kwa sauti nzuri.

3 Pigeni baragumu za pembe za kondoo dume

wakati wa Mwandamo wa Mwezi,

na wakati wa mwezi mpevu,

katika siku ya Sikukuu yetu;

4 hii ni amri kwa Israeli,

agizo la Mungu wa Yakobo.

5 Aliiweka iwe kama sheria kwa Yosefu

alipotoka dhidi ya Misri,

huko tulikosikia lugha ambayo hatukuielewa.

6 Asema, “Nimeondoa mzigo mabegani mwao;

mikono yao iliwekwa huru kutoka kwenye kikapu.

7 Katika shida yako uliniita nami nikakuokoa,

nilikujibu katika mawingu yenye ngurumo;

nilikujaribu katika maji ya Meriba.

8 “Enyi watu wangu, sikieni, nami nitawaonya:

laiti kama mngenisikiliza, ee Israeli!

9 Hamtakuwa na mungu mgeni miongoni mwenu;

msimsujudie mungu wa kigeni.

10 Mimi ni Bwana Mungu wako,

niliyekutoa nchi ya Misri.

Panua sana kinywa chako

nami nitakijaza.

11 “Lakini watu wangu hawakutaka kunisikiliza;

Israeli hakutaka kunitii.

12 Basi niliwaacha katika ukaidi wa mioyo yao

wafuate mashauri yao wenyewe.

13 “Laiti kama watu wangu wangalinisikiliza,

kama Israeli wangalifuata njia zangu,

14 ningaliwatiisha adui zao kwa haraka,

na kuugeuza mkono wangu dhidi ya watesi wao!

15 Wale wanaomchukia Bwana wangalinyenyekea mbele zake,

na adhabu yao ingedumu milele.

16 Bali ninyi mngalilishwa ngano iliyo bora,

na kuwatosheleza kwa asali itokayo kwenye mwamba.”

Zaburi 146

1 Msifuni Bwana!

Ee nafsi yangu, umsifu Bwana,

2 Nitamsifu Bwana maisha yangu yote;

nitamwimbia Mungu wangu sifa

wakati wote niishipo.

3 Usiweke tumaini lako kwa wakuu,

kwa wanadamu ambao hufa,

ambao hawawezi kuokoa.

4 Roho yao itokapo hurudi mavumbini,

siku hiyo hiyo mipango yao yote hukoma.

5 Heri yeye ambaye Mungu wa Yakobo ni msaada wake,

ambaye tumaini lake ni katika Bwana, Mungu wake,

6 Muumba wa mbingu na nchi,

na bahari na vyote vilivyomo ndani yake:

Bwana anayedumu kuwa mwaminifu

milele na milele.

7 Naye huwapatia haki walioonewa

na kuwapa wenye njaa chakula.

Bwana huwaweka wafungwa huru,

8 Bwana huwafumbua vipofu macho,

Bwana huwainua waliolemewa na mizigo yao,

Bwana huwapenda wenye haki.

9 Bwana huwalinda wageni

na kuwategemeza yatima na wajane,

lakini hupinga njia za waovu.

10 Bwana atamiliki milele,

Mungu wako, ee Sayuni,

kwa vizazi vyote.

Msifuni Bwana.