Ufalme wa Israeli

Hitimisho la Utawala wa Yeroboamu wa Pili

809 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

2 Wafalme 14:25–27

25 Ndiye alirudishia mipaka ya Israeli kuanzia Lebo-Hamathi hadi Bahari ya Araba, sawasawa na neno la Bwana, Mungu wa Israeli, lililosemwa kupitia mtumishi wake Yona mwana wa Amitai, nabii kutoka Gath-Heferi.

26 Bwana alikuwa ameona jinsi kila mmoja katika Israeli, awe mtumwa au aliye huru, alivyoteseka kwa uchungu; hapakuwepo na yeyote wa kuwasaidia. 27 Kwa kuwa Bwana alikuwa hajasema kuwa atafuta jina la Israeli chini ya mbingu, akawaokoa kwa mkono wa Yeroboamu mwana wa Yehoashi.

Hosea Anawatolea Israeli Unabii 801 KK

Wito wa kwanza wa Hosea kwa makabila kumi.

Hosea 1–3

1 Neno la Bwana lililomjia Hosea mwana wa Beeri wakati wa utawala wa Uzia, Yothamu, Ahazi na Hezekia, wafalme wa Yuda, na wakati wa utawala wa Yeroboamu mwana wa Yehoashi, mfalme wa Israeli.

2 Wakati Bwana alipoanza kuzungumza kupitia Hosea, Bwana alimwambia, “Nenda ukajitwalie mwanamke wa uzinzi na watoto wa uzinzi, kwa sababu nchi ina hatia ya uzinzi wa kupindukia kwa kumwacha Bwana.” 3 Kwa hiyo alimwoa Gomeri binti Diblaimu, naye akachukua mimba na kumzalia Hosea mwana.

4 Kisha Bwana akamwambia Hosea, “Mwite Yezreeli, kwa kuwa kitambo kidogo nitaiadhibu nyumba ya Yehu kwa ajili ya mauaji ya kule Yezreeli, nami nitaukomesha ufalme wa Israeli. 5 Katika siku ile nitavunja upinde wa Israeli katika Bonde la Yezreeli.”

6 Gomeri akachukua tena mimba akamzaa binti. Kisha Bwana akamwambia Hosea, “Mwite Lo-Ruhama, kwa maana sitaonyesha tena upendo kwa nyumba ya Israeli, kwamba nisije kabisa nikawasamehe. 7 Hata hivyo nitaonyesha upendo kwa nyumba ya Yuda, nami nitawaokoa si kwa upinde, upanga au vita, wala kwa farasi na wapanda farasi, bali kwa njia ya Bwana Mungu wao.”

8 Baada ya Gomeri kumwachisha Lo-Ruhama kunyonya, Gomeri alipata mwana mwingine. 9 Kisha Bwana akasema, “Mwite Lo-Ami kwa maana ninyi si watu wangu, nami si Mungu wenu.

10 “Hata hivyo Waisraeli watakuwa kama mchanga kando ya bahari, ambao hauwezi kupimika wala kuhesabiwa. Mahali pale walipoambiwa, ‘Ninyi si watu wangu,’ wao wataitwa ‘wana wa Mungu aliye hai.’ 11 Watu wa Yuda na watu wa Israeli wataunganishwa tena, nao watamchagua kiongozi mmoja nao watakwea watoke katika nchi, kwa kuwa siku ya Yezreeli itakuwa kuu sana.

2:1 “Waambie ndugu zako, ‘Watu wangu,’ na pia waambie dada zako, ‘Wapendwa wangu.’

2 “Mkemeeni mama yenu, mkemeeni,

kwa maana yeye si mke wangu,

nami si mume wake.

Aondoe sura ya uzinzi katika uso wake

na uzinzi kati ya matiti yake.

3 Kama sivyo nitamvua nguo zake awe uchi

na kumwacha uchi kama siku ile aliyozaliwa.

Nitamfanya kama jangwa,

nitamgeuza awe nchi ya kiu,

nami nitamuua kwa kiu.

4 Sitaonyesha upendo wangu kwa watoto wake,

kwa sababu ni watoto wa uzinzi.

5 Mama yao amekosa uaminifu

na amewachukua mimba katika aibu.

Gomeri alisema, ‘Nitawaendea wapenzi wangu,

ambao hunipa chakula changu

na maji yangu,

sufu yangu na kitani yangu, mafuta yangu

na kinywaji changu.’

6 Kwa hiyo mimi Mungu nitaizuia njia yake

kwa vichaka vya miiba,

nitamjengea ukuta ili kwamba

asiweze kutoka.

7 Gomeri atawafuatia wapenzi wake lakini hatawapata;

atawatafuta lakini hatawapata.

Kisha atasema,

‘Nitarudi kwa mume wangu kama kwanza,

kwa maana nilikuwa na hali njema zaidi

kuliko sasa.’

8 Gomeri hajakubali kuwa mimi ndiye

niliyempa nafaka, divai mpya na mafuta,

niliyemwongezea fedha na dhahabu waliyoitumia

kwa kumtumikia Baali.

9 “Kwa hiyo nitachukua nafaka yangu wakati itakapokomaa

na divai yangu mpya wakati itakapokuwa tayari.

Nitamnyangʼanya sufu yangu na kitani yangu

iliyokusudiwa kufunika uchi wake.

10 Basi sasa nitaufunua ufisadi wake

mbele ya wapenzi wake;

hakuna yeyote atakayemtoa

mikononi mwangu.

11 Nitakomesha furaha na macheko yake yote:

sikukuu zake za mwaka,

sikukuu za Miandamo ya Mwezi,

siku zake za Sabato,

sikukuu zake zote zilizoamriwa.

12 Nitaiharibu mizabibu yake na mitini yake,

ambayo alisema yalikuwa malipo yake

kutoka kwa wapenzi wake;

nitaifanya kuwa kichaka,

nao wanyama pori wataila.

13 Nitamwadhibu kwa ajili ya siku

alizowafukizia uvumba Mabaali;

alipojipamba kwa pete

na kwa vito vya thamani,

na kuwaendea wapenzi wake,

lakini mimi alinisahau,”

asema Bwana.

14 “Kwa hiyo sasa nitamshawishi;

nitamwongoza hadi jangwani

na kuzungumza naye kwa upole.

15 Huko nitamrudishia mashamba yake ya mizabibu,

nami nitalifanya Bonde la Akori

mlango wa matumaini.

Huko ataimba kama alivyofanya katika siku za ujana wake,

kama siku zile alizotoka Misri.

16 “Katika siku ile,” asema Bwana,

“utaniita mimi ‘Mume wangu’;

hutaniita tena mimi ‘Bwana wangu.’

17 Nitaondoa majina ya Mabaali kutoka midomoni mwake,

wala hataomba tena kwa majina yao.

18 Katika siku ile nitafanya Agano kwa ajili yao

na wanyama wa kondeni, na ndege wa angani,

na viumbe vile vitambaavyo ardhini.

Upinde, upanga na vita,

nitaondolea mbali katika nchi,

ili kwamba wote waweze kukaa salama.

19 Nitakuposa uwe wangu milele;

nitakuposa kwa uadilifu na haki,

kwa upendo na huruma.

20 Nitakuposa kwa uaminifu,

nawe utamkubali Bwana.

21 “Katika siku ile nitajibu,”

asema Bwana,

“nitajibu kwa anga,

nazo anga zitajibu kwa nchi;

22 nayo nchi itajibu kwa nafaka,

divai mpya na mafuta,

navyo vitajibu kwa Yezreeli.

23 Nitampanda katika nchi kwa ajili yangu mwenyewe;

nami nitaonyesha pendo langu kwake

yule ambaye nilimwita, ‘Si mpenzi wangu.’

Nitawaambia wale walioitwa, ‘Sio watu wangu,’

‘Ninyi ni watu wangu’;

nao watasema, ‘Wewe ndiwe Mungu wangu.’ ”

3:1 Bwana akaniambia, “Nenda, ukaonyeshe upendo wako kwa mke wako tena, ingawa amependwa na mwingine naye ni mzinzi. Mpende kama Bwana apendavyo Waisraeli, ingawa wanageukia miungu mingine na kupenda mikate mitamu ya zabibu kavu iliyowekwa wakfu.”

2 Basi nilimnunua huyo mwanamke kwa shekeli kumi na tano za fedha, pia kwa kiasi kama cha homeri moja na nusu ya shayiri. 3 Kisha nilimwambia, “Utaishi nami kwa siku nyingi, hupaswi kuwa kahaba au kuwa na uhusiano wa karibu na mtu yeyote, nami nitaishi na wewe.”

4 Kwa maana Waisraeli wataishi siku nyingi bila kuwa na mfalme wala mkuu, bila kuwa na dhabihu wala mawe matakatifu, bila kisibau wala sanamu. 5 Baadaye Waisraeli watarudi na kumtafuta Bwana Mungu wao na Daudi mfalme wao. Watakuja wakitetemeka kwa Bwana na kwa baraka zake katika siku za mwisho.