Sehemu ya 6: Utawala wa Ahazia

Ufalme wa Yuda

884 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

2 Wafalme 8:25

25 Katika mwaka wa kumi na mbili wa utawala wa Yoramu mwana wa Ahabu mfalme wa Israeli, Ahazia mwana wa Yehoramu mfalme wa Yuda alianza kutawala.

2 Nyakati 22:1–7

1 Watu wa Yerusalemu wakamfanya Ahazia, mdogo wa wote wa wana wa Yerohamu, kuwa mfalme mahali pa baba yake, kwa sababu washambuliaji wa ghafula waliokuwa wameingia kambini pamoja na Waarabu, walikuwa wamewaua wana wakubwa wote wa Yehoramu. Kwa hiyo Ahazia mwana wa Yehoramu mfalme wa Yuda akaanza kutawala.

2 Ahazia alikuwa na umri wa miaka ishirini na miwili alipoanza kutawala, naye akatawala katika Yerusalemu kwa mwaka mmoja. Mama yake aliitwa Athalia, mjukuu wa Omri.

3 Ahazia naye akaenenda katika njia za nyumba ya Ahabu, kwa sababu mama yake alimshawishi katika kutenda maovu. 4 Akafanya yaliyo maovu machoni pa Bwana kama walivyokuwa wamefanya nyumba ya Ahabu, kwa kuwa baada ya kufa kwa baba yake nyumba ya Ahabu ndio waliokuwa washauri wake, kwa uangamivu wake. 5 Pia akafuata shauri lao alipokwenda pamoja na Yoramu mwana wa Ahabu mfalme wa Israeli kupigana na Hazaeli mfalme wa Aramu huko Ramoth-Gileadi. Waaramu wakamjeruhi Yoramu. 6 Hivyo akarudi Yezreeli ili apate kuuguza majeraha aliyojeruhiwa huko Ramothi alipopigana na Hazaeli mfalme wa Aramu.

Ndipo Ahazia mwana wa Yehoramu, mfalme wa Yuda, akashuka kwenda Yezreeli kumtazama Yoramu mwana wa Ahabu, kwa sababu alikuwa amejeruhiwa.

7 Mungu alikuwa ameamuru kwamba kuanguka kwa Ahazia kungetokea atakapokwenda kumwona Yoramu. Ahazia alipowasili, wakatoka pamoja na Yoramu ili kwenda kukutana na Yehu mwana wa Nimshi, ambaye Bwana alikuwa amemtia mafuta kuangamiza nyumba ya Ahabu.

2 Wafalme 9:27

27 Wakati Ahazia mfalme wa Yuda alipoona kilichotokea, akakimbia kupitia barabara ya Beth-Hagani. Yehu akamkimbiza akipaza sauti na kusema, “Muue naye pia!” Wakamjeruhi katika gari lake kwenye njia ielekeayo Guri karibu na Ibleamu, lakini akatorokea Megido na akafia huko.

2 Nyakati 22:8–9

8 Yehu alipokuwa anatekeleza hukumu juu ya nyumba ya Ahabu, akawakuta wakuu wa Yuda na wana wa jamaa ya Ahazia waliokuwa wanamhudumia Ahazia, naye akawaua. 9 Ndipo akaenda kumsaka Ahazia, nao watu wake wakamkamata alipokuwa amejificha huko Samaria. Akaletwa kwa Yehu, naye Yehu akamuua. Wakamzika kwani walisema, “Alikuwa mwana wa Yehoshafati, ambaye alimtafuta Bwana kwa moyo wake wote.” Hivyo hapakuwa na mtu mwenye uwezo katika nyumba ya Ahazia aliyeweza kushika ufalme.

2 Wafalme 9:28–29

28 Watumishi wake wakambeba kwa gari la vita na kumpeleka Yerusalemu, wakamzika pamoja na baba zake kwenye kaburi lake katika Mji wa Daudi. 29 (Katika mwaka wa kumi na moja wa Yoramu mwana wa Ahabu, Ahazia alianza kutawala katika Yuda.)

2 Wafalme 8:26–29

26 Ahazia alikuwa na umri wa miaka ishirini na miwili alipoanza kutawala, naye akatawala katika Yerusalemu kwa mwaka mmoja. Mama yake aliitwa Athalia, mjukuu wa Omri mfalme wa Israeli. 27 Akaenenda katika njia za nyumba ya Ahabu, na kutenda maovu machoni pa Bwana, kama nyumba ya Ahabu ilivyokuwa imefanya, kwa kuwa alikuwa ameoa kutoka nyumba ya Ahabu.

28 Ahazia akaenda vitani na Yoramu mwana wa Ahabu kupigana na Hazaeli mfalme wa Aramu huko Ramoth-Gileadi. Waaramu wakamjeruhi Yoramu. 29 Hivyo Mfalme Yoramu akarudi Yezreeli ili apate kuuguza majeraha aliyojeruhiwa na Waaramu huko Ramothi alipopigana na Hazaeli mfalme wa Aramu.

Ndipo Ahazia mwana wa Yehoramu mfalme wa Yuda akashuka kwenda Yezreeli kumtazama Yoramu mwana wa Ahabu, kwa sababu alikuwa amejeruhiwa.

Ufalme wa Israeli 885 KK

Utawala wa Yehoramu Juu ya Israeli Wakamilika

Njama ya Hazaeli

2 Wafalme 8:7–15

7 Elisha akaenda Dameski, naye Ben-Hadadi mfalme wa Aramu alikuwa mgonjwa. Mfalme alipoambiwa, “Mtu wa Mungu ametoka mbali akapanda hadi hapa,” 8 mfalme akamwambia Hazaeli. “Chukua zawadi na uende kumlaki huyo mtu wa Mungu. Muulize Bwana kupitia yeye, kwamba, ‘Je, nitapona ugonjwa huu?’ ”

9 Hazaeli akaenda kumlaki Elisha, akiwa amechukua zawadi ya kila kitu kizuri kilichopatikana Dameski, mizigo iliyobebwa na ngamia arobaini. Akaingia ndani na kusimama mbele yake, akasema, “Mwanao Ben-Hadadi mfalme wa Aramu amenituma niulize, ‘Je, nitapona ugonjwa huu?’ ”

10 Elisha akajibu, “Nenda ukamwambie, ‘Hakika utapona’; lakini Bwana amenifunulia kwamba kweli atakufa.” 11 Elisha akamkazia Hazaeli macho kwa nguvu mpaka akaona aibu. Kisha mtu wa Mungu akaanza kulia.

12 Hazaeli akauliza “Kwa nini bwana wangu analia?”

Elisha akajibu, “Kwa sababu najua mabaya utakayowatendea Waisraeli. Utachoma moto ngome zao, utawaua vijana wao kwa upanga, kuwatupa chini kwa nguvu watoto wachanga, na kuwatumbua wanawake wenye mimba.”

13 Hazaeli akasema, “Itawezekanaje mtumishi wako, aliye mbwa tu, kufanya tendo la ajabu namna hiyo?”

Elisha akamjibu, “Bwana amenionyesha kuwa utakuwa mfalme wa Aramu.”

14 Kisha Hazaeli akamwacha Elisha na kumrudia bwana wake. Ben-Hadadi akamuuliza, “Elisha alikuambia nini?” Hazaeli akajibu, “Aliniambia kwamba hakika utapona.” 15 Lakini kesho yake Hazaeli akachukua nguo nzito, akailoweka ndani ya maji, akaitandaza juu ya uso wa mfalme, hivyo akafa. Kisha Hazaeli akaingia mahali pake kuwa mfalme wa Aramu.