Mfano wa Mchungaji Mwema

Katika mfano (istiara) wa mchungaji mwema, Yesu anawaonyesha Mafarisayo wenye uhasama na kudokeza kwamba atakufa kwa ajili ya kundi lake na kufufuka tena.

Yerusalemu

29 au 28 BK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

Yohana 10:1–21

10:1 “Amin, amin nawaambia, yeye asiyeingia katika zizi la kondoo kwa kupitia kwenye lango, lakini akwea kuingia ndani kwa njia nyingine, ni mwizi na mnyangʼanyi. 2 Yeye anayeingia kwa kupitia kwenye lango ndiye mchungaji wa kondoo. 3 Mlinzi humfungulia lango na kondoo huisikia sauti yake. Huwaita kondoo wake kwa majina yao na kuwatoa nje ya zizi. 4 Akiisha kuwatoa wote nje, hutangulia mbele yao na kondoo humfuata kwa kuwa wanaijua sauti yake. 5 Lakini kondoo hawatamfuata mgeni bali watamkimbia, kwa sababu hawaijui sauti ya mgeni.” 6 Yesu alitumia mfano huu, lakini wao hawakuelewa hayo aliyokuwa akiwaambia.

7 Kwa hiyo Yesu akasema nao tena akawaambia, “Amin, amin nawaambia, mimi ndimi lango la kondoo. 8 Wote walionitangulia ni wevi na wanyangʼanyi, lakini kondoo hawakuwasikia. 9 Mimi ndimi lango, yeyote anayeingia zizini kwa kupitia kwangu ataokoka, ataingia na kutoka, naye atapata malisho. 10 Mwizi huja ili aibe, kuua na kuangamiza. Mimi nimekuja ili wapate uzima kisha wawe nao tele.

11 “Mimi ndimi mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo. 12 Mtu wa kuajiriwa sio mchungaji mwenye kondoo. Amwonapo mbwa mwitu akija, yeye hukimbia na kuwaacha kondoo. Naye mbwa mwitu hulishambulia kundi na kulitawanya. 13 Yeye hukimbia kwa sababu ameajiriwa wala hawajali kondoo.

14 “Mimi ndimi mchungaji mwema. Ninawajua kondoo wangu nao kondoo wangu wananijua. 15 Kama vile Baba anavyonijua mimi, nami ninavyomjua Baba, nami nautoa uhai wangu kwa ajili ya kondoo. 16 Ninao kondoo wengine ambao si wa zizi hili, inanipasa kuwaleta, nao wataisikia sauti yangu, hivyo patakuwa na kundi moja na mchungaji mmoja. 17 Baba yangu ananipenda kwa kuwa ninautoa uhai wangu ili niupate tena. 18 Hakuna mtu aniondoleaye uhai wangu, bali ninautoa kwa hiari yangu mwenyewe. Ninao uwezo wa kuutoa uhai wangu na pia ninao uwezo wa kuutwaa tena. Amri hii nimepewa na Baba yangu.”

19 Kwa maneno haya Wayahudi waligawanyika. 20 Wengi wao wakasema, “Huyu amepagawa na pepo mchafu, naye amechanganyikiwa.”

21 Wengine wakasema, “Haya si maneno ya mtu aliyepagawa na pepo mchafu. Je, pepo mchafu aweza kufungua macho ya kipofu?”

Utume wa Wale Sabini

Utume wa wale Sabini, na furaha ya Kristo kwa kazi yao wanaporudi.

Hapa tuna mambo ambayo ni Luka pekee anayeyasimulia, ambayo yaelekea yalitokea Uyahudi. Baadhi yake yanafanana na matukio na mafundisho ya wakati wa huduma huko Galilaya ambayo Mathayo na Marko wanasimulia.

Inaelekea huko Uyahudi

(Linganisha na utume wa wale Kumi na Wawili.)

Luka 10:1–24

10:1 Baada ya hayo, Bwana akawachagua wengine sabini na wawili, akawatuma wawili wawili katika kila mji na kila sehemu aliyokusudia kwenda baadaye. 2 Akawaambia, “Mavuno ni mengi, lakini watendakazi ni wachache. Kwa hiyo mwombeni Bwana wa mavuno, ili apeleke watendakazi katika shamba lake la mavuno. 3 Haya! nendeni. Ninawatuma kama wana-kondoo katikati ya mbwa mwitu. 4 Msichukue mkoba, wala mfuko, wala viatu, na msimsalimu mtu yeyote njiani.

5 “Mkiingia katika nyumba yoyote, kwanza semeni, ‘Amani iwe kwenu.’ 6 Kama kuna mtu wa amani humo, basi amani yenu itakuwa juu yake. La sivyo, itawarudia. 7 Kaeni katika nyumba hiyo, mkila na kunywa kile watakachowapa, kwa sababu kila mtendakazi anastahili malipo yake. Msihamehame kutoka nyumba hadi nyumba.

8 “Mkienda katika mji na watu wake wakawakaribisha, kuleni chochote kiwekwacho mbele yenu, 9 waponyeni wagonjwa waliomo na waambieni: ‘Ufalme wa Mungu umekaribia.’ 10 Lakini mkiingia katika mji, nao hawakuwakaribisha, tokeni mwende katika barabara zake mkaseme: 11 ‘Hata mavumbi ya mji wenu yaliyoshikamana na miguu yetu, tunayakungʼuta dhidi yenu. Lakini mjue kwamba Ufalme wa Mungu umekaribia.’ 12 Ninawaambia, itakuwa rahisi zaidi kwa Sodoma kustahimili katika siku ile kuliko mji ule.

13 “Ole wako Korazini! Ole wako Bethsaida! Kwa kuwa kama miujiza iliyofanyika kwenu ingefanyika Tiro na Sidoni, miji hiyo ingekuwa imetubu zamani, kwa kuvaa magunia na kujipaka majivu. 14 Lakini itakuwa rahisi zaidi kwa Tiro na Sidoni kustahimili katika siku ya hukumu, kuliko ninyi. 15 Nawe, Kapernaumu, je, utainuliwa hadi mbinguni? La hasha, utashushwa mpaka kuzimu.”

16 “Yeye awasikilizaye ninyi anisikiliza mimi; naye awakataaye ninyi amenikataa mimi. Lakini yeye anikataaye mimi amkataa yeye aliyenituma.”

17 Wale sabini na wawili wakarudi kwa furaha, na kusema, “Bwana, hata pepo wachafu wanatutii kwa jina lako.”

18 Yesu akawaambia, “Nilimwona Shetani akianguka kutoka mbinguni kama umeme wa radi. 19 Tazama nimewapa mamlaka ya kukanyaga nyoka na nge na juu ya nguvu zote za adui; wala hakuna kitu chochote kitakachowadhuru. 20 Basi, msifurahi kwa kuwa pepo wachafu wanawatii, bali furahini kwa kuwa majina yenu yameandikwa mbinguni.”

21 Wakati huo Yesu akashangilia katika Roho Mtakatifu, akasema, “Nakuhimidi Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa umewaficha mambo haya wenye hekima na wenye elimu, nawe ukawafunulia watoto wadogo. Naam, Baba, kwa kuwa hivyo ndivyo ilivyokupendeza.

22 “Nimekabidhiwa vitu vyote na Baba yangu. Hakuna mtu amjuaye Mwana ni nani ila Baba, wala hakuna amjuaye Baba ni nani ila Mwana na yeyote ambaye Mwana anapenda kumfunulia.”

23 Basi Yesu akawageukia wanafunzi wake akanena nao faraghani, akawaambia, “Heri macho yanayoona yale mambo mnayoyaona. 24 Kwa maana nawaambia, manabii wengi na wafalme walitamani kuona yale mnayoyaona lakini hawakuyaona, na walitamani kusikia yale mnayoyasikia lakini hawakuyasikia.”