Miujiza ya Elisha (continued)

892 KK

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™ (OKCV)

2 Wafalme 5:1–6:23

1 Wakati huu, Naamani alikuwa jemadari wa jeshi la mfalme wa Aramu. Alikuwa mtu mkuu mbele ya bwana wake na aliyeheshimiwa sana, kwa sababu kupitia kwake, Bwana alikuwa amewapa Aramu ushindi. Alikuwa askari shujaa, lakini alikuwa na ukoma.

2 Siku hizo vikosi kutoka Aramu vilikuwa vimekwenda na vikawa vimemteka msichana kutoka Israeli, naye akamtumikia mkewe Naamani. 3 Akamwambia bibi yake, “Kama bwana wangu angelimwona nabii aliyeko Samaria! Angemponya ukoma wake.”

4 Naamani akaenda kwa bwana wake na kumwambia alichosema yule msichana kutoka Israeli. 5 Mfalme wa Aramu akamjibu, “Hakika, nenda. Nitatuma barua kwa mfalme wa Israeli.” Kwa hiyo Naamani akaondoka, akiwa amechukua talanta kumi za fedha, shekeli 6,000 za dhahabu, na mivao kumi ya mavazi. 6 Barua aliyopelekea mfalme wa Israeli iliandikwa hivi: “Pamoja na barua hii ninamtuma mtumishi wangu, Naamani, kwako ili uweze kumponya ukoma wake.”

7 Mara mfalme wa Israeli alipomaliza kuisoma ile barua, akararua mavazi yake na kusema, “Je, mimi ni Mungu? Je, mimi naweza kuua na kufufua tena? Kwa nini huyu mtu anamtuma mtu ili mimi nipate kumponya ukoma wake? Tazama jinsi anavyotafuta kuanzisha ugomvi nami!”

8 Elisha mtu wa Mungu aliposikia kwamba mfalme wa Israeli alikuwa amerarua mavazi yake, akamtumia ujumbe huu: “Kwa nini umerarua mavazi yako? Mwamuru mtu huyo aje kwangu, naye atajua ya kuwa yuko nabii katika Israeli.” 9 Kwa hiyo Naamani akaenda, akiwa na farasi zake na magari yake, na kusimama mlangoni mwa nyumba ya Elisha. 10 Elisha akamtuma mjumbe kumwambia, “Nenda uoge katika Yordani mara saba, na nyama ya mwili wako itapona, nawe utatakasika.”

11 Lakini Naamani akaondoka akiwa amekasirika, akasema, “Hakika nilidhani kwamba angetoka nje, asimame na kuliitia jina la Bwana Mungu wake, na kuweka mkono wake juu ya mahali pagonjwa, aniponye ukoma wangu. 12 Je, Abana na Farpari, mito ya Dameski, si bora zaidi kuliko mito yoyote ya Israeli? Je, nisingeweza kuoga ndani ya hiyo mito na kutakasika?” Basi akageuka na kuondoka kwa hasira kuu.

13 Watumishi wa Naamani wakamwendea na kumwambia, “Baba yangu, kama huyo nabii angekuambia kufanya jambo lililo kubwa, je, usingelifanya? Je, si zaidi sana basi, anapokuambia, ‘Oga na utakasike!’ ” 14 Hivyo akashuka na kujizamisha ndani ya Yordani mara saba, kama vile huyo mtu wa Mungu alivyokuwa amemwambia, nayo nyama ya mwili wake ikapona na kutakasika kama ya mwili wa mvulana mdogo.

15 Kisha Naamani na wahudumu wake wote wakarudi kwa yule mtu wa Mungu. Akasimama mbele yake na kusema, “Sasa najua kwamba hakuna Mungu katika ulimwengu wote isipokuwa katika Israeli. Tafadhali sasa upokee zawadi kutoka kwa mtumishi wako.”

16 Nabii akajibu, “Hakika kama Bwana aishivyo, ambaye ninamtumikia, sitapokea kitu hata kimoja.” Ingawa Naamani alimsihi sana, yeye alikataa.

17 Naamani akasema, “Ikiwa hutapokea, tafadhali mtumishi wako na apewe udongo kiasi cha mzigo wa kuweza kubebwa na punda wawili, kwa sababu mtumishi wako hatatoa tena sadaka ya kuteketezwa na dhabihu kwa mungu mwingine isipokuwa Bwana. 18 Lakini Bwana na amsamehe mtumishi wake kwa kitu hiki kimoja: Wakati bwana wangu atakapoingia kwenye hekalu la Rimoni ili kusujudu, naye akiwa anauegemea mkono wangu, nami nikasujudu huko pia, wakati nitakaposujudu ndani ya hekalu la Rimoni, Bwana na amsamehe mtumishi wako kwa ajili ya jambo hili.”

19 Elisha akamwambia, “Nenda kwa amani.”

Baada ya Naamani kusafiri umbali fulani, 20 Gehazi, mtumishi wa Elisha mtu wa Mungu, akajiambia mwenyewe, “Bwana wangu amemwachia kirahisi sana Naamani, huyu Mwaramu, kwa kutokupokea kutoka kwake vile alivyovileta. Hakika kama Bwana aishivyo, nitamkimbilia na kupata kitu kutoka kwake.”

21 Hivyo Gehazi akaharakisha kumfuatilia Naamani. Naamani alipomwona akikimbia kumwelekea, akashuka chini kutoka kwenye gari lake na kwenda kumlaki. Akauliza, “Je, mambo yote ni sawa?”

22 Gehazi akajibu, “Mambo yote ni sawa. Bwana wangu amenituma nikuambie, ‘Vijana wawili kutoka kwa wana wa manabii wamenijia kutoka nchi ya vilima ya Efraimu. Tafadhali wape talanta ya fedha na mivao miwili ya mavazi.’ ”

23 Naamani akasema, “Hakika, chukua talanta mbili za fedha.” Akamsihi Gehazi azipokee, kisha akafunga talanta mbili za fedha katika mifuko miwili pamoja na mivao miwili ya mavazi. Akawapa watumishi wake wawili mizigo hiyo, nao wakaibeba wakitangulia mbele ya Gehazi. 24 Gehazi alipofika kwenye kilima, akavichukua vile vitu kutoka kwa wale watumishi na kuvificha ndani ya nyumba. Akawaaga wale watu, nao wakaondoka. 25 Kisha akaingia ndani na kusimama mbele ya Elisha bwana wake.

Elisha akamuuliza, “Gehazi, ulikuwa wapi?”

Gehazi akajibu, “Mtumishi wako hakwenda popote.”

26 Lakini Elisha akamwambia, “Je, roho yangu haikuwa pamoja nawe wakati yule mtu aliposhuka kutoka kwenye gari lake ili kukulaki? Je, huu ni wakati wa kupokea fedha au kupokea nguo, mashamba ya mizeituni, mashamba ya mizabibu, makundi ya kondoo na mbuzi, makundi ya ngʼombe, au watumishi wa kiume na wa kike? 27 Ukoma wa Naamani utakushika wewe na wazao wako milele.” Kisha Gehazi akaondoka mbele ya Elisha, mwenye ukoma, mweupe kama theluji.

6:1 Wana wa manabii wakamwambia Elisha, “Tazama, mahali hapa tunapokutana nawe ni padogo sana kwetu. 2 Twendeni Yordani, mahali ambapo kila mmoja wetu anaweza kupata nguzo moja, nasi tujenge huko mahali petu pa kuishi.”

Naye akawaambia, “Nendeni.”

3 Kisha mmoja wao akasema, “Je, tafadhali, huwezi kufuatana na watumishi wako?”

Elisha akajibu, “Nitakuja.” 4 Naye akaenda pamoja nao.

Basi wakaenda Yordani, nao wakaanza kukata miti. 5 Mmoja wao alipokuwa anakata mti, shoka lilitumbukia kwenye maji. Akalia, “Ee bwana wangu, shoka lilikuwa la kuazima!”

6 Mtu wa Mungu akauliza, “Je, liliangukia wapi?” Alipomwonyesha mahali penyewe, Elisha akakata kijiti na kukitupa mahali pale, nalo shoka likaelea. 7 Akasema, “Lichukue.” Kisha yule mtu akanyoosha mkono wake, akalichukua.

8 Wakati huo mfalme wa Aramu alikuwa akipigana vita na Israeli. Baada ya kukubaliana na maafisa wake, akasema, “Nitapiga kambi yangu mahali fulani na fulani.”

9 Mtu wa Mungu akatuma ujumbe kwa mfalme wa Israeli: “Jihadhari usije ukapita mahali pale, kwa sababu Waaramu wanashuka huko.” 10 Kwa hiyo mfalme wa Israeli akatuma neno la tahadhari mahali pale alikokuwa ameelekezwa na mtu wa Mungu. Mara kwa mara Elisha alimwonya mfalme kwamba watu wawe macho kwenye maeneo kama hayo.

11 Hili lilimfadhaisha sana mfalme wa Aramu. Akawaita maafisa wake, akawauliza, “Je, hamtaniambia ni nani miongoni mwenu aliye upande wa mfalme wa Israeli?”

12 Mmoja wa maafisa wake akasema, “Mfalme bwana wangu, hakuna hata mmoja wetu. Lakini Elisha, yule nabii aliye Israeli, humwambia mfalme wa Israeli hata yale maneno unayozungumza katika chumba chako cha kulala.”

13 Mfalme akaagiza akisema, “Nendeni, mkatafute aliko, ili niweze kutuma watu kumkamata.” Taarifa ikarudi kwamba, “Yuko Dothani.” 14 Ndipo akatuma farasi na magari ya vita na jeshi lenye nguvu huko. Walikwenda usiku na kuuzunguka mji.

15 Kesho yake asubuhi na mapema, mtumishi wa mtu wa Mungu alipoamka na kutoka nje, jeshi, pamoja na farasi na magari ya vita, likawa limeuzunguka mji. Mtumishi wake akasema, “Ole wetu, bwana wangu! Tutafanya nini?”

16 Nabii akajibu, “Usiogope. Wale walio pamoja nasi ni wengi zaidi kuliko wale walio pamoja nao.”

17 Kisha Elisha akaomba, “Ee Bwana, mfumbue macho huyu mtumishi ili apate kuona.” Ndipo Bwana akayafumbua macho ya yule mtumishi, naye akatazama na kuona vilima vimejaa farasi na magari ya moto, yamemzunguka Elisha pande zote.

18 Wakati adui waliposhuka kumwelekea, Elisha akamwomba Bwana: “Wapige watu hawa kwa upofu.” Basi Mungu akawapiga kwa upofu, kama Elisha alivyoomba.

19 Elisha akawaambia, “Hii sio njia yenyewe, na huu sio huo mji. Nifuateni mimi, nami nitawapeleka kwa huyo mtu mnayemtafuta.” Naye akawapeleka Samaria.

20 Baada ya kuingia mjini, Elisha akasema, “Bwana, yafungue macho ya watu hawa ili wapate kuona.” Ndipo Bwana akayafungua macho yao, na walipotazama, kumbe hapo ndipo walipojikuta, ndani ya Samaria.

21 Wakati mfalme wa Israeli alipowaona, akamuuliza Elisha, “Je, baba yangu, niwaue?”

22 Naye akajibu, “Usiwaue. Je, utawaua watu uliowateka kwa upanga wako mwenyewe na upinde wako? Wape chakula na maji ili wapate kula na kunywa, na kisha wamrudie bwana wao.” 23 Basi akawaandalia karamu kubwa, na baada ya kula na kunywa, akawaaga nao wakarudi kwa bwana wao. Hivyo, vikosi kutoka Aramu vikakoma kuvamia nchi ya Israeli.